Chama cha Wafanyakazi Vyuo Vikuu (THTU) chajitosa Mgogoro wa Mafao ya Pensheni

pefhana

Senior Member
Mar 26, 2017
158
105
THTU YATAKA SULUHISHO KUHUSU TAHARUKI YA KIKOKOTOO CHA MAFAO YA KUSTAAF

Utangulizi

Hivi karibuni, umeibuka mjadala mkali juu ya mafao ya watumishi wanaostaafu ajira baada ya mfuko mpya wa PSSSF kuanza kufanya kazi. Mjadala huo unajikita kwenye kikokotoo cha mafao ambacho kinapunguza mafao yanayolipwa kwa mtumishi aliyestaafu. Mjadala huu ambao umetawaliwa na hisia kali umepelekea kurushiana lawama kwa taasisi na wadau wote wanaohusika na sekta ya hifadhi ya jamii. Ni wazi kabisa kwamba Vyama vya wafanyakazi vimelaumiwa, Bunge limelaumiwa, Serikali imelaumiwa na Mamlaka ya hifadhi ya jamii (SSRA) imelaumiwa. THTU tunaamini kwamba kuacha hili jambo liishe bila muafaka ni kutojitendea haki sisi kama Taifa lenye watu wakomavu na waliostaarabika. Kimsingi, mjadala wa mafao ya kustaafu limekuwa likijirudia mara kwa mara bila muafaka wa pande zote na hivyo kuendelea kuacha hisia za kurushiana lawama.

THTU tunaamini kwamba jambo hili liko ndani ya uwezo wetu kama Taifa kulipatia muafaka na ufumbuzi wa kudumu. Kwa msingi huo, tunapenda kuungana na wafanyakazi wote nchini na umma wa Tanzania kutoa maoni yetu machache kama kichocheo cha kuhamisha mjadala kutoka kulaumiana kwenda kwenye suluhisho ili hatimae hali ya utulivu irejee.

Awali ya yote, tunakiri kwamba tulishiriki kikamilifu kutoa maoni yetu wakati wa kuandikwa sheria iliyounda mfuko wa PSSSF. Tunaishukuru na kuipongeza Serikali pamoja na Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Kamati ya Huduma za Jamii kwa kutumia zaidi ya masaa matatu kusikiliza maoni yetu (wakati huo). Maoni mengi tuliyotoa kama chama cha Wafanyakazi wa Taasisi za Elimu ya Juu yalizingatiwa kwenye sheria husika. Tunathubutu kusema kwamba tunaikubali sheria iliyounganisha mifuko. Ni bahati mbaya sana kwamba uundaji wa kanuni ambazo ndizo zenye vikokotoo haukuwa shirikishi kwa upande wetu sisi THTU. Hata hivyo, tunaamini bado muda upo wa sisi kutoa maoni yetu kwa lengo la kuboresha
Mjadala mkubwa ulioibuka baada ya mfuko wa PSSSF kuanza kazi umejikita katika vikokotoo vinavyoshusha mafao ya mkupuo kwa wastaafu hasa kwenye kipengele cha asilimia sihirini na tano (25%).
Ieleweke kwamba ni kweli Serikali kupitia Mamlaka ya Udhibiti wa Mifuko ya Hifadhi ya Jamii (SSRA) imejitahidi sana kuboresha mafao hasa kwa Mifuko ya PPF na NSSF ambayo ndiyo ilikuwa inalipa mafao kidogo sana kuliko mifuko mingine kabla ya kuunganishwa
Mfano mzuri ni kikokotoo cha PPF ambacho awali kilikuwa 1/960; baada ya majadiliano na SSRA na mfuko husika ikawa 1/600 na mwaka 2014 SSRA ilisawazisha kikokotoo kwa mifuko yote ikawa 1/580 isipokuwa kwa watumishi wa mifuko ya LAPF na PSPF kabla ya Julai 2014 ambao walibaki na 1/540. Ndio maana wakati huo Profesa aliyefanya kazi kwa zaidi ya miaka 30 akichangia mfuko wa PPF alilipwa fao la mkupuo la milioni isiyozidi ishirini na tano (25,000,000) wakati mtumishi aliyestaafu akiwa PSPF/LAPF alipokea milioni sitini mpaka mia moja. Mfano huu pekee utupe faraja kwamba majadiliano ya pamoja huleta suluhisho lenye manufaa kwa pande zote
Baada ya vikokotoo kusawazishwa mwaka 2014, wale watumishi waliokuwa wakichangia mifuko ya PSPF na LAPF kabla ya Julai 2014 waliruhusiwa kubaki na kikokotoo chao kilichokuwepo ambacho ni 1/540, miaka 15.5 na 50% ya fao la mkupuo. Kikokotoo kilichosawazishwa ni 1/580, miaka 12.5 na 25% ya fao la mkupuo. Hii ina maana ilitengenezwa makundi mawili katika ulipaji wa mafao ya kustaafu.
Baada ya mfuko wa PSSSF kuanzishwa, kikokotoo kilichosawazishwa na ambacho kilianza kutumika mwaka 2014 kimeondoa yale makundi mawili yaliyokuwepo hasa kwenye vipengele vya asilimia na miaka. Hii ina maana kwamba wastaafu wote wanaanza kutumia kikokotoo cha 1/580, miaka 12.5; 25% ya fao la mkupuo na 75% ya pensheni ya kila mwezi. Kwa msingi huu, walioathiriwa zaidi na kikokotoo kipya ni wale waliokuwepo kwenye mifuko ya PSPF na LAPF kabla ya Julai 2014. Kundi hili lililoathiriwa limesaidia kutoa picha halisi ya mafao ya hifadhi ya jamii baada ya mtumishi kustaafu
Sisi THTU tunaamini ukweli huu uliodhihirika au uliojidhihiri wenyewe unapaswa kuangaliwa kwa jicho la pekee na kurekebishwa kwa mjadala wa pamoja. Wizara husika kupitia SSRA inaweza kuratibu zoezi la kupokea maoni ya wadau wote kwa lengo la kurekebisha kikokotoo kilicholeta taharuki na hivyo kutuliza wafanyakazi. SSRA imeshafanya mikutano mingi na wadau hasa wafanyakazi kupitia vyama vyao tangu ilipoanzishwa. Majadiliano ya pamoja itapelekea uwepo wa muafaka wa pamoja na kuacha kulaumiana.
Sisi THTU tunatoa pendekezo la kuanzia kuelekea mjadala wa pamoja kwamba kikokotoo KIBORESHWE ili kuondoa makundi yaliyopo sasa. Pendekezo letu la kuboresha kikokotoo ni 1/540, miaka 15.5 na 50% ya fao la mkupuo na 50% inayobaki iwe pensheni ya kila mwezi. Bahati nzuri SSRA imetoa ufafanuzi mzuri kabisa kwamba kwa kikokotoo cha sasahivi, mstaafu atalipwa pesa zake zote kwa utaratibu wa 25% mkupuo na 75% kila mwezi. Kumbe mwisho wa siku mstaafu atalipwa pesa zake zote. Mjadala wa pamoja ujikite kwenye swali hili; Je! Tunaweza kuboresha kikokotoo kikawa 50% ya mkupuo na 50% iliyobaki ikaingia kwenye pensheni ya kila mwezi? Maeneo mengine yanayolalamikiwa yatajadiliwa kwenye mjadala wa pamoja.

Hitimisho

Ni pendekezo letu THTU kwamba sasa tatizo limeshafahamika. Tuhamishe mjadala kutoka kulaumiana kwenda kwenye suluhisho. Sasa tuunganishe nguvu na akili zetu kutafuta suluhisho. Mwalimu Nyerere anatuasa kwamba tujisahihishe. Tusiogope kujisahihisha. Sisi tumeanza na pendekezo. Tunawaalika wadau wote kuelekea kwenye mjadala wa pamoja kupata muafaka wa pamoja. Hakuna linaloshindikana, tutimize wajibu wetu.

Muhimu:

THTU itakutanisha wataalamu wa sekta ya hifadhi ya jamii ili kuandaa mapendekezo ya kina na kuwasilisha SSRA na Wizara husika kwa ajili ya mjadala na ufumbuzi. Tunaamini mapendekezo yetu yanaendana na malengo ya kulinda afya za muda mrefu ya mifuko na pia kutimiza malengo ya hifadhi ya jamii.
 
Nmeelewa kuwa ninyi pia mlishirikishwa kwa ukaribu, lakini kwenye kikokotoo nachelea kusema mlifahamu ila mlipoona baadhi ya mifuko ni kama imebebwa, basi hamkujishughulisha kwa kuona walio PSPF na LAPF ndio wameminywa.
Anyway, kelele nyingi nadhani zinaweza mkataza ng'ombe kunywa maji walau kwa mda, ila kwa nionacho bila jitihada kufanyika, upande wa utetezi wa kikokotoo kipya una cover media kwa kasi. Amkeni watumishi.
 
Ushauri wangu; ni vema manung'uniko ya watumishi yatafutiwe majibu au majawabu. pia suala la madai mbalimbali ya watumishi yafanyiwe kazi sasa yaani bajeti ya 2019/2020 . nje ya hapo ITAKUWA TOO LATE. nadhani nimeleweka !
 
Jiwe mtamfanya aache kujisifia kwa kufanya shughuli za maendeleo kwa kutumia fedha zandani huku akiacha waliohangaika kulijenga taifa lao kutembea mpaka miguu kuota matege na kuwawaisha kufa haraka kisa kutaka masifa
 
Kumbe kuna THTU na Vyama vya wafanyakazi!
Oneni sasa DHAMBI ya uroho wa madaraka inavyo watafuna. Mngekuwa kitu kimoja saizi mngezungumza lugha moja.
 
1 Reactions
Reply
Back
Top Bottom