Chakachua CCM maandamano kila sehemu | JamiiForums | The Home of Great Thinkers

Dismiss Notice
You are browsing this site as a guest. It takes 2 minutes to CREATE AN ACCOUNT and less than 1 minute to LOGIN

Chakachua CCM maandamano kila sehemu

Discussion in 'Uchaguzi Tanzania' started by Moseley, Aug 11, 2010.

 1. Moseley

  Moseley Senior Member

  #1
  Aug 11, 2010
  Joined: Jul 10, 2010
  Messages: 184
  Likes Received: 10
  Trophy Points: 35
  MAANDAMANO, urudishwaji wa kadi na vurugu zimeendelea kutawala maeneo mbalimbali nchini kutokana na wanachama kupata taarifa kutoka ndani ya vikao vya kamati za siasa za mikoa za CCM zinazoonyesha kuwa baadhi ya wagombea walioibuka washindi wamewekewa alama za chini au kuondolewa na kurejeshwa wale walioshindwa.

  Kamati hizo zinachambua washindi wa kura za maoni za ubunge na udiwani na kuweka alama kwa wagombea ili kuiwezesha kamati kuu ya CCM kutoa orodha ya mwisho ya wagombea ambao hawatakuwa na matatizo wakati Tume ya Uchaguzi itakapotoa orodha ya majina ya waliopitishwa kugombea nafasi hizo.

  Lakini uchambuzi huo wa kamati za siasa unaonekana kukera wanachama, hasa waliowapigia kura baadhi ya wagombea walioibuka kidedea kwenye kura za maoni, ambao sasa wanaendelea kuandamana na kuzingira ofisi za CCM kupinga maamuzi hayo.

  Tayari katibu wa itikadi na uenezi wa CCM, John Chiligati ameshatetea maamuzi hayo ya kamati za siasa akisema kuwa wale watakaobainika kucheza rafu wataenguliwa, huku makamu mwenyekiti wa chama hicho kwa upande wa Bara, Pius Msekwa akisema kuwa watakaobainika kusababisha kukithiri kwa vitendo vya rushwa hawatapona.

  Rushwa iliripotiwa kwa wingi wakati wa kampeni huku ukiukwaji wa taratibu ukijitokeza wakati wa kupiga kura, ikiwa ni pamoja na kuibuka kwa wanachama wapya, kutokuwepo kwa leja za wanachama na vurugu zilizosababisha baadhi ya vituo kutokuwa na upigaji kura.

  Kwa mujibu wa taarifa zilizokusanywa kutoka maeneo mbalimbali nchini, wanachama hao wakiwa katika makundi waliandamana maeneo mbalimbali, kurudisha kadi, kutishia kuwapigia kura wagombea wa vyama vya upinzani na wengine kutishia kuhamia upinzani.

  Kwenye jimbo la Temeke, Nora Damian anaripoti kuwa wanachama wa CCM waliandamana hadi ofisi za wilaya za chama kupinga kile walichodai kuwa ni kuchezewa rafu kwa mgombea wao katika kura za maoni.

  Tukio hilo lilitokea jana majira ya saa 4:00 asubuhi wakati wanachama hao walipoanzia maandamano yao maeneo ya Temeke Wailes kwenda hadi ofisi za wilaya ambazo ziko karibu na Hospitali ya Wilaya ya Temeke na hivyo kusababisha usumbufu mkubwa kwenye barabara iendayo kituo cha Temeke Mwisho.

  Wanachama hao, wakiwa na mabango yaliyoandikwa ujumbe tofauti na wakisindikizwa kwa ngoma maalumu ya mdundiko walikuwa wamekusanya kadi za chama hicho na kuandamana hadi makao makuu ya ofisi za chama hicho kupinga mgombea wao wa udiwani katika Kata ya Miburani, Mkenga Rajabu kuchezewa rafu katika kura za maoni.

  Mmoja wa wanachama hao, Abdallah Ajili alisema kuwa kwenye kura za maoni mgombea wao, Mkenga alipata kura 703 lakini wamepata taarifa kwamba chama kinataka kumpitisha diwani anayemaliza muda wake, Mang'wela Fortunatus aliyepata kura 518.

  "Chama kinaelekea wapi kama sisi tunapiga kura kumchagua mtu tunayemtaka halafu wanatuchezea rafu," alihoji Ajili. "Jina la mgombea wetu wamelikata kwa madai kwamba amepiga teke masanduku ya kura na kukimbia nayo."

  Mwanachama mwingine, Juliana Magogo alilalamikia kuwepo kwa tawi la Chuo Kikuu Kishiriki cha Elimu (Duce) katika mchakato wa kura za maoni kwa kile alichodai kuwa matawi yanayojulikana ni sita na kwamba hilo la Duce limetengenezwa kwa njama za kuwaongezea kura wagombea wengine.

  Alisema matawi yanayotambulika ni Miburani, Uwanja wa Taifa, Wailes, Keko Machungwa A na B na Keko Juu.

  Baada ya kufika ofisi za wilaya chama hicho walianza kuimba nyimbo na kucheza huku wakionyesha mabango yao ambayo yalikuwa na ujumbe tofauti, ukiwemo uliosomeka ‘CCM sio Yanga wala Simba'.

  Baada ya fujo kuzidi polisi zaidi ya sita walifika katika eneo hilo na kufanikiwa kuwatuliza wanachama hao.

  Akizungumza baada ya tafrani hiyo, katibu wa CCM wa wilaya, Saad Kusilawe alisema kushinda kwenye kura za maoni si kigezo cha kupitishwa kuwania uongozi kwani kuna mambo mbalimbali yanayoangaliwa yakiwemo idadi ya kura, tabia ya mgombea na mwenendo wake.

  "Mgombea anaweza akapata kura nyingi lakini akawa na kashfa mbalimbali au alishawahi kushitakiwa, hivyo vyote vinaangaliwa katika mchakato wa uteuzi wa wagombea," alisema Kusilawe.

  Alisema orodha kamili ya walioteuliwa kugombea udiwani itatolewa leo baada ya kikao cha watendaji wa wilaya zote tatu kukaa.

  Katibu huyo alisema wataendelea kujadili malalamiko mbalimbali yanayoletwa na wanachama na kama itabainika mgombea alipata ushindi kwa hila, uteuzi utatenguliwa.

  Akizungumzia madai ya kuwepo tawi la Duce katika kura za maoni, katibu huyo alisema tawi hilo lilifunguliwa hivi karibuni na Rais Jakaya Kikwete, lakini walisahau kuliingiza kwenye orodha ya matawi.
  Hata hivyo, alisema siku ya kupiga kura za maoni alilifunga tawi hilo na kuchoma moto karatasi za kupigia kura, baada ya kutokea mtafaruku kati ya katibu wa tawi hilo na mgombea udiwani wa Miburani.
  Wanachama wavamia tawi Kimara

  Naye Fidelis Butahe anaripoti kuwa zaidi ya wanachama 150 wa Kata ya Kimara jijini Dar es Salaam walivamia ofisi za wilaya za chama hicho huku wakitishia kuhamia Chadema kama kutakuwa na mabadiliko ya matokeo ya kura za maoni za udiwani.

  Wanachama hao waliamua kuzivamia ofisi za CCM wilaya ya Kinondoni wakiwa ndani ya mabasi mawili baada ya kusikia tetesi kuwa aliyekuwa diwani wa kata hiyo, Mahmoud Mringo amepitishwa na chama hicho kutetea nafasi yake licha ya kushindwa katika kura za maoni.

  Matokeo ya kura za maoni za udiwani katika Kata hiyo yanaonyesha kuwa Gama Gama alishinda kwa kupata kura 608, akifuatiwa na Mahmoud Mringo (552), Amri Mganga (93), Godfrey Mheluka (86), Boniface Kobelo (37) na Shedrack Kombe (31).

  "Leo (jana) asubuhi Mringo alikuwa akipiga simu ofisi za CCM na kueleza kuwa jina lake limepitishwa kwa hiyo yeye ndio diwani, sisi hatukubaliani na jambo hili hata kidogo," alisema mmoja wa wanachama hao.
  "Ndio maana hata kura za maoni alishindwa kwa kuwa ametuchosha; Kimara hakuna maendeleo yoyote... kila siku ni bora ya jana. Hatukubali kuongozwa na mtu ambaye hatukumchagua,".

  Kabla ya kupanda magari hayo, kundi la wanachama hao lilikuwa limekusanyika mita chache kutoka ofisi za CCM Kimara na kusababisha zaidi ya polisi 20 kufika eneo hilo.

  Hata hivyo, polisi hao walitawanyika mara baada ya kuelezwa na wanachama hao kuwa mkusanyiko huo hakuwa na lengo la kufanya vurugu bali walikuwa katika harakati za kutafuta usafiri kuelekea ofisi za CCM.

  Kwenye ofisi za CCM wilayani Kinondoni, wanachama hao walionana na katibu wa wilaya na kumueleza malalamiko yao na hasa ya Mringo.

  "Tumepata taarifa kuwa Mringo kapita katika kura za maoni... kwa kifupi sisi hatukubali; kama akipita na tuko tayari kumchagua mgombea wa Chadema na kuihama CCM. Pamoja na kuwa mshindi hajatangazwa kichama, lakini huo ndio msimamo wetu," alisema mmoja wa wanachama hao aliyefahamika kwa jina moja la Ibrahim
  Baadaye wanachama hao walikwenda ofisi za mkoa ambako walionana na uongozi na kueleza malalamiko hayo.

  "Inawezekana kukawa na kamchezo ka kushusha majina ya wagombea udiwani walioshinda kwenye kura za maoni na kupandisha walioshika nafasi ya pili au ya tatu. Huu si utaratibu mzuri na kwa hali hii wengi tutahamia Chadema," alisema mwanachama mwingine kwenye kundi hilo.

  Alipoulizwa kuhusu madai hayo, Mringo alisema: " Wewe ndio unanieleza habari hizo hivi sasa. Kifupi siwezi kuzungumza lolote; wanaoweza kuzungumza ni makao makuu ya CCM... sisi wagombea tulishamaliza kazi yetu, sina la kusema ndugu yangu."

  Kwenye jimbo la Korogwe, Raisa Said anaripoti kuwa wanachama zaidi ya 300 wa CCM wa matawi ya chama hicho yaliyopo Kata ya Lutindi, Tarafa ya Bungu wametishia kujiengua uanachama baada ya kupata taarifa kuwa mshindi wa kura za maoni ameenguliwa.

  Wakizungumza nje ya ofisi ya wilaya baada ya kufanya maandamano, wanachama hao ambao walikuwa pamoja na baadhi ya viongozi wao wa matawi , walisema wataihama CCM na kwenda upinzani endapo hawatasikilizwa.

  Wanachama hao wapatao 28 waliiambia Mwananchi kuwa hawaridhishwi na uamuzi wa kamati ya siasa ya kumuengua Jafari Ngoda ambaye alishinda.

  Chalange Yusuph, ambaye ni katibu wa tawi la Lewa, alisema hawaridhiki na uamuzi wa kumuengua mshindi kwenye kura za maoni na kwamba wao kama viongozi pamoja na wanachama zaidi ya 300 wa matawi yao watarudisha kadi zao za CCM.

  Mwenyekiti wa tawi la Kwebago, Alihud Chalema alisema hata wakibakia CCM hawatamsaidia mgombea atakayepitishwa wakati wa uchaguzi, huku katibu wa tawi la Kizumba akisema wanachama 308 waliompa kura Ngoda wameporwa ushindi wao kwa nguvu za fedha.

  Hata hivyo, katibu wa chama hicho wilayani Korogwe, Lucy Mwiru alisema kamati inafuata alama zilizowekwa na kamati ya siasa ya kata, hivyo wao kata ndio wamemuengua mshindi huyo ambaye alipambana na wenzake sita na kuwabwaga.

  Mwiru alisema kuwa wamefikia uamuzi huo kutokana na taarifa kutoka kwenye kata yake kuwa Ngoda alikuwa anazuia maendeleo kwa kukataa shule ya sekondari isijengwe shambani kwake mwaka 2002 wakati huo akiwa diwani.

  "Lakini pia tumeambiwa ameshitakiwa Mahakama ya Ardhi Tanga kwa ajili hiyo hiyo," alisema katibu huyo.

  "Sisi tunaangalia chama kwanza mtu baadae, nami nitawashangaa kama watahama chama na kurudisha kadi eti kwa sababu tu mtu wao hakupita. Vikao vinafanyika kwa maslahi ya chama... kama tutang'ang'ania mtu wao apite, anaweza kuwekewa pingamizi tukaikosa kata."

  Katibu wa kata ya Lutindi alikiri kumuwekea alama za kumuengua Ngoda akidai kuwa hapendi maendeleo, ameshitakiwa na pia kuishitaki Serikali ya Kijiji cha Lewa. Alidai walikuwa wanaujua udhaifu wote huo, lakini walimuacha atoe fedha ya fomu Sh 10,000 na Sh 50,000 za mchango ili kutunisha fedha za chama.

  Ngoda alisema yote hayo yamepandikizwa ili kumuharibia na si kweli kwamba kamati ya siasa ya kata ilikaa na kukubaliana hayo na kudai kuwa muhtasari wa kikao hicho uliandikiwa hoteli ya Travellers mjini Korogwe.

  Uchaguzi kurudiwa Simanjiro
  Joseph Lyimo anaripoti kutoka Simanjiro mkoani Manyara kuwa baada ya kuvurugika kwa upigaji kura za maoni kwenye baadhi ya matawi, mchakato huo unarudiwa kesho baada ya ujumbe kutoka makao makuu ya chama mkoani Dodoma kumaliza vikao vyao na uongozi wa wilaya.

  Zoezi hilo linarudiwa kwa maagizo ya katibu mkuu wa CCM, Yusuph Makamba baada ya mmoja kati ya wagombea wa nafasi ya ubunge kulalamikia jinsi kura za maoni zilivyoendeshwa na kukata rufaa kupinga matokeo hayo.

  Akizungumza na Mwananchi kwa njia ya simu, katibu wa chama wilaya ya Kiteto na ambaye ni mjumbe kutoka makao makuu ya chama, Othman Dunga alisema hadi sasa bado wanaendelea na mchakato wa kubaini sehemu zinazolalamikiwa ili watoe maamuzi ya kurudiwa kwa kura hizo.

  "Nadhani mpaka Alhamisi tutakuwa tumeshapata muafaka wa sehemu zitakazorudiwa na kuwatangazia ili uchaguzi huo ufanyike mara moja na pia kurekebisha makosa yaliyojitokeza mwanzoni," alisema Dunga.

  Miongoni mwa kata zilizolalamikiwa ni Terrati, Kijiji cha Engonongoi ambako masanduku ya kura yalichomwa moto, na kata ya Naberera, Kijiji cha Landanai ambako daftari la orodha ya wapigakura lilichukuliwa na kukimbiziwa porini na morani wa kimasai.

  Pia kwenye kata ya Msitu wa Tembo, Kijiji cha Magadini na Korongo, masanduku ya kupigia kura yaliibwa wakati kura zikiwa zimeshapigwa hivyo kusababisha vurugu, hali kadhalika matawi ya kata ya Ruvu Remit.

  Katika uchaguzi huo, mbunge aliyemaliza muda wake, Christopher Ole Sendeka aliongoza kwa kupata kura 18,069 na kufuatiwa na Lenganasa Soipey aliyepata kura 6,598 na James Ole Millya aliyepata kura 4,907.

  Rungwe Mashariki bado hakujatulia
  Amanyisye Ambindwile anaripoti kutoka Tukuyu wilayani Rungwe kwamba hali haijatulia kutokana na baadhi ya wanachama kuandamana wakipinga ushindi Profesa David Mwakyusa.

  Katibu tawala wa Wilaya ya Rungwe, Moses Mwidete alisema jana kwamba polisi wamemkamata Jeremia Mwambete kwa tuhuma za kuhamasisha maandamano kwenye Kata ya Masukulu kupinga matokeo.

  Hali kadhalika, mwenyekiti wa tawi la chama hicho la Ngujuwaje lililo Kata ya Ilima, Kenedy Gwankipya alisema wanachama wengi wanarudisha kadi wakipinga matokeo hayo.

  Habari zaidi zilisema kuwa hali kama hiyo pia imetawala kata za Ikuti na Kyimo ambako wanachama wanatishia kuwapa kura wagombea wa upinzani.

  Chiligati asema washindi wataenguliwa
  Kutoka jijini Dar es salaam, Exuper Kachenje anaripoti kuwa katibu wa itikadi na uenezi wa CCM, John Chiligati amesema chama hicho kinafanyia kazi malalamiko yote kwa kuyachunguza na kwamba si ajabu matokeo katika baadhi ya majimbo yakabadilishwa.

  Chiligati alisema hayo jana alipozungumza na gazeti hili na alikiri pia kuwepo kwa kasoro katika upigaji kura za maoni kwenye baadhi ya majimbo.

  "Malalamiko yapo; chama kinayachunguza. Watu wasishangae matokeo katika baadhi ya majimbo kubadilishwa kwa kuwa tukigundua makosa, hilo si ajabu kutokea," alisema Chiligati.

  "Tukichunguza na kubaini ukiukwaji wa taratibu ni sawa na kufunga goli la mkono. Katika mchezo wa soka, goli la mkono halikubaliki. Watu wasishangae tutalikataa."

  Hata hivyo, Chiligati alisema CCM imeridhika na uendeshaji zoezi hilo kwa jumla kwa kuwa kila mgombea alipewa fursa ya kuweka wakala katika kila kituo cha kupigia kura.

  Naye Leon Bahati anaripoti kuwa makamu mwenyekiti wa CCM-Bara, Pius Msekwa aliungana na Chiligati kueleza kuwa chama hicho kitawaengua wote waliosababisha kukithiri kwa vitendo vya rushwa wakati wa kura za maoni.

  Msekwa, ambaye alikuwa akihojiwa na kituo cha redio cha Uhuru FM kinachomilikiwa na chama hicho, alisema kwamba kabla ya kufikia mwisho wa mwezi huu, baadhi ya waliohusika na kukithiri kwa vitendo vya rushwa kwenye kura za maoni zilizopigwa siku 10 zilizopita, watakuwa wameanza kufahamika.

  Alisema wamepokea malalamiko mengi kuhusu ukiukwaji huo wa maadili na tayari wameanza kuyajadili hatua kwa hatua ili ifikapo mwishoni mwa wiki hii wawe wamewapata wagombea ambao majina yao watayawasilisha Tume ya Uchaguzi na wahalifu wapelekwe mahakamani.

  "Tunawajadili kwenye sekretarieti ya kamati ndogo ya maadili ambayo mimi ni mwenyekiti wake. Tunachofanya ni kupendekeza maoni yetu ambayo yatajadiliwa na halmashauri kuu ya taifa," alisema Msekwa ambaye aliwahi kuwa spika wa Bunge.

  Lengo la kamati hiyo ndogo, alisema ni kubaini walioshinda kinyume cha sheria ili waondolewe na haki itendeke.

  CCM yailalamikia rasmi Chadema
  Katika hatua nyingine Sadick Mtulya anaripoti kuwa
  Naye Sadick Mtulya anaripoti kuwa CCM jana iliwasilisha rasmi malalamiko ya maandishi kwa Tume ya Uchaguzi (Nec), ikidai kuwa Chadema imeanza kampeni kabla ya muda.

  Hatua hiyo, imefikiwa baada ya timu ya wanasheria wa CCM juzi usiku, kukamilisha kuandaa malalamiko hayo.

  Malalamiko hayo yaliyawasilishwa na ofisi ya katibu mkuu wa CCM, kitengo cha mwanasheria wa chama hicho.

  Kwa mujibu wa chanzo chetu, katika malalamiko hayo, CCM imesema Chadema imevunja maadili ya uchaguzi yaliyotolewa na Nec kwa ajili ya uchaguzi wa rais, wabunge na madiwani kwa mwaka huu, yaliyotiwa saini na vyama vyote 18 vya siasa.

  CCM inadai katika malalamiko hayo kuwa Chadema imetumia mwanya wa kutafuta wadhamini nchini kote, kufanya kampeni jambo ambalo ni ukiukwaji wa maadili katika uchaguzi mkuu wa Oktoba mwaka huu.

  "Pamoja na mambo mengine, malalamiko ya CCM ni kuwa Chadema imetumia mwanya wa kutafuta wadhamini nchini kote, kufanya kampeni jambo ambalo ni ukiukwaji wa maadili katika uchaguzi mkuu wa mwaka huu,'' kilisema chanzo chetu.

  Kwa mujibu wa Nec, maadili ya uchaguzi yaliyotiwa saini na vyama vya siasa hivi karibuni, yataanza kutumika rasmi kuanzia siku ya kwanza ya kampeni, Agosti 20 hadi kutangazwa kwa matokeo.

  Akijibu tuhuma hizo juzi jijini Dar es Salaam mara baada ya kuchukua fomu ya kuwania urais, Dk Willbrod Slaa alisema umbumbumbu wa CCM wa kuelewa mambo ndio uliowafanya watoe malalamiko hayo .

  "CCM tumewazoea. Hawasomi sheria. Hawasomi sera za vyama vingine," alisema Dk Slaa akifafanua kwamba ilifanya kampeni kwa mabango sehemu mbalimbali za nchi ikiwa ni pamoja na Zanzibar, lakini anashangaa wanavyozungumza juu ya madai hayo.

  Hata hivyo, Dk Slaa alikiri kuwa alipokuwa mikoani kutafuta wadhamini, umati mkubwa wa watu ulimfuata na ilibidi aueleze sababu zilizomfanya aamue kuwania nafasi hiyo.

  Alifafanua kwamba wao hawakuwa na mabango wala hawakuwalazimisha watu waende kuwasikiliza, ila ile hali ya wananchi kuwa na shauku ya kumsikiliza ndiyo iliyomfanya aonekane kama anafanya kampeni.

  "Isitoshe, CCM hawajui sheria kwa maana kwamba sisi kama vyama vya siasa tuna wajibu wa kukutana na wananchi ili kuwaeleza sera zetu,'' alisema Dk Slaa.

  Katika hatua nyingine, CCM imesema Rais Jakaya Kikwete atarejesha fomu za kutetea kiti chake Agosti 19, siku moja kabla ya kuanza rasmi kwa kampeni, zitakazomalizika Oktoba 30.

  Source: Mwananchi
  [/B]
   
Loading...