Chai na Comrade Robert Mugabe/Raia Mwema, Septemba 12, 2019

Rubawa

JF-Expert Member
Dec 25, 2015
2,055
3,239
BARAZANI

Chai na Comrade Robert Mugabe

Na Ahmed Rajab

ROBERT Mugabe, Rais wa zamani wa Zimbabwe, aliyefariki dunia Ijumaa Singapore alikokuwa akitibiwa, atatambuliwa na historia kuwa baba wa taifa huru la Zimbabwe. Lakini historia pia haitosahau kwamba Mugabe alikuwa mtawala wa kimabavu ambaye katika miaka ya mwisho ya enzi yake aliwaumiza wananchi wengi wenzake.

Hali kadhalika, historia itakumbusha kwamba Mugabe aliingia madarakani kwa mguu mwema aliposhika hatamu za nchi yake baada ya uchaguzi mkuu wa kwanza wa kidemokrasia ulioifanya nchi hiyo iwe huru 1980 . Ataendelea kusifika kwa mifumo bora ya elimu na afya aliyoianzisha miaka ya mwanzo ya utawala wake.

Ingawa alikuwa na itikadi ya Kimarx lakini sera zake za kiuchumi zilikuwa ni za kimuhafidhina, za kibepari. Asingeweza kufanya vingine ila kuwa na sera kama hizo. Na angefanya vingine kwa kujaribu kuibirua misingi ya uchumi wa nchi yake angezidi kujipalilia makaa.

Muhimu zaidi atakumbukwa kwa kuwarejeshea Waafrika ardhi zao zilizokuwa zimeporwa na walowezi wa kizungu. Kuna wenye kumlaumu kwa hatua hiyo.

Kwa hakika, suala la kuyachukua mashamba ya wazungu na kuwagaia Waafrika limepotoshwa na wengi hasa wa nchi za Magharibi. Mugabe hakuwa na hila ila alibidi afanye mageuzi ya umiliki wa ardhi. Tusisahau kwamba msingi wa vita vya ukombozi wa Zimbabwe ulikuwa suala hilo la ardhi.

Mambo yalimchachia Mugabe pale wakongwe wa mapinduzi, wenyewe wanajiita “maveterani”, walipomiminika kwenye uwanja wa Ikulu, Harare, wakidai ardhi. Walivitia najisi viwanja hivyo kwa kwenda haja ndogo humo.

Mpango huo wa ugawaji wa ardhi ulikuwa wa sehemu mbili. Sehemu ya kwanza ilitekelezwa kwa mafanikio licha ya shida walizokuwa nazo wakulima wadogo kwa upande wa nyenzo za kulimia. Lakini sehemu ya pili ndiyo iliyokuwa na ukorofi. Katika sehemu hiyo ya pili ardhi iligaiwa kwa waliokuwa karibu na Mugabe, ama kisiasa au kidamu.

Mugabe pia analaumiwa kwa kuufuja uchumi. Wenye kumlaumu kwa hilo wanasahau kwamba mwanzoni uchumi uliharibika Mugabe alivyokuwa akizitekeleza sera za Benki ya Dunia na Shirika la Fedha la Mataifa (IMF). Dada hao wawili wa Washington walimrandia Mugabe na mwisho walifanikiwa kumshawishi aifuate miongozo yao ya kuurekebisha uchumi.

Badala ya kurekebishika, uchumi huo ukaanza kudidimia. Hapo ndipo hali za maisha za Wazimbabwe zilipoanza kuporomoka.

Jambo jengine linalomfanya Mugabe alaaniwe ni mauaji ya Gukurahundi ambapo watu wasiopungua 20,000, wengine wanasema waliokaribia 80,000, waliuliwa na kikosi cha mgambo cha Mugabe, Brigedi ya Tano. Mauaji hayo yalitokea baina ya 1983 na 1987.

Ni vigumu kumtetea Mugabe kwa mauaji hayo. Hata hivyo, wapo wenye kumkingia kifua na wenye kukumbusha kwamba hata Joshua Nkomo, ambaye ni Mdebele, hatimaye alimsamehe.

Mugabe alipotea njia dira yake ya uadilifu ilipomponyoka. Aligeuka na kuwa mtawala wa kimabavu wakati uchumi wa nchi yake ulipokuwa umezidi kuporomoka. Vyombo vya usalama vya utawala wake vikizikandamiza haki za binadamu hasa za wapinzani na wakosoaji wake.

Mugabe alikuwa akiithamini historia na akiitegemea alipokuwa akikata maamuzi yake. Jambo lenye kustaajabisha na kusikitisha ni kuiona historia hiyo hiyo ikianza kuthubutu kumhukumu vibaya.

Yote hayo yanatokea kwa sababu Mugabe alikuwa na sura mbili mithili ya sarafu ya shilingi. Upande mmoja ulikuwa na sura iliyokuwa iking’ara lakini sura ya upande wa pili ilisawijika. Ilikuwa chafu.

Siku moja mwishoni mwa Oktoba 1997 nilibahatika kuwa naye Mugabe kwa takriban siku nzima. Nilikuwa naibu mwenyekiti wa kamati maalum iliyoundwa London kuandaa mkutano uliopewa jina la “Africa At 40 Committee”.

Lengo la mkutano lilikuwa kulitathmini bara la Afrika miaka 40 baada ya Ghana kupata uhuru. Ghana, iliyokuwa zamani ikiitwa Gold Coast, ilikuwa nchi ya mwanzo barani Afrika kupewa uhuru na wakoloni.

Tuliupanga mkutano huo uwe vile vile unaangalia mbele kwa kuiangazia dhana ya maendeleo na ushirikiano wa kikanda barani Afrika.

Mwenyekiti wetu alikuwa Ad’Obe Obe, mwandishi maarufu wa Kinigeria aliyekuwa mhariri wa gazeti la West Africa na ambaye baadaye alikuwa mshauri muhtasi wa Rais Olusegun Obasanjo wa Nigeria. Obe na mimi tulihangaika kwa muda wa miezi kadhaa kuufanikisha mkutano huo.

Bahati nzuri wakati huo kulikuwa kunafanywa mkutano mkuu wa viongozi wa nchi zanachama za Jumuiya ya Madola huko Edinburgh, Uskochi. Tuliwaalika viongozi wa Kiafrika waliokuwa wakihudhuria mkutano wa Edinburgh na tukawasihi wasirudi makwao moja kwa moja ila wasalie na kuuhudhuria mkutano wetu.

Baadhi yao walikubali na tulikuwa tumeshampanga Mugabe atoe hotuba ya ufunguzi. Waziri Mkuu wa zamani wa Uingereza James Callaghan alikuwa amekwishatukubalia ombi letu la kumtaka awe mwenyeji wa mkutano huo.

Maudhui ya hotuba ya Mugabe, iliyokuwa ya kusisimua, yalikuwa juu ya swali hili: nini maana ya uhuru? Kwame Nkrumah, waziri mkuu wa kwanza na Rais wa kwanza wa Ghana, alikwishasema nchi yake ilipopata uhuru 1957 kwamba uhuru huo hautokuwa na maana endapo hautofungamanishwa na ukombozi kamili wa bara zima la Afrika.

Mugabe, ujanani mwake, alihamasishwa kwa kiwango kikubwa na nadharia pamoja na harakati za Nkrumah. Alimpenda Nkrumah kiasi cha kumfanya akimbilie Ghana huru kwenda kufanya kazi ya ualimu kwa miaka mitatu. Huko ndiko alikompata mkewe wa kwanza, Sarah, ambaye anajulikana zaidi kwa jina la Sally. Mugabe aliwahi vile vile kusomesha Zambia, nchi hiyo ilipokuwa koloni iliyokuwa ikiitwa Rhodesia ya Kaskazini.

Wakati huohuo alipokuwa anasomesha skuli Ghana, Mugabe akihudhuria darasa katika Taasisi ya Itikadi ya Kwame Nkrumah huko Winneba, mji ulio kusini kama kilomita 52 kutoka Accra. Huko Ghana ndiko alikoanza kuikumbatia itikadi ya Umarx.

Mugabe aliipenda Ghana na alimpenda zaidi Nkrumah. Lakini si Nkrumah pekee aliyemvutia Mugabe.

Siku hizo Mugabe alikuwa pia akivutiwa na Elvis Presley, mwimbaji wa Kimarekani aliyejulikana kama “Mfalme” wa muziki wa “Rock and Roll” pamoja na Bing Crosby, mwimbaji mwengine wa Kimarekani ambaye wakati mwingine alikuwa akiimba kama vile hataki.

Wote wawili walikuwa pia waigizaji wa sinema na wote walijaa moyoni mwa Mugabe. Waliokuwa naye siku za ujana wake wanasema kwamba Mugabe alikuwa mwepesi wa kuzungumza habari za waimbaji hao kwa kina kama alivyokuwa mwepesi wa kuzichambua siasa.

Kwenye mkutano wetu wakati wa kipindi cha mapumziko baina ya vikao nilimchukua Mugabe na viongozi wengine kwenda kwenye chumba cha kupumzikia. Viongozi hao walikuwa ni pamoja na Sam Nujoma, aliyekuwa Rais wa Namibia, na Dk. Salim Ahmed Salim, aliyekuwa katibu mkuu wa Umoja wa Nchi Huru za Kiafrika (OAU).

Mugabe ni mtu aliyekuwa akipenda kupiga masuti. Nimeambiwa kwamba hata alipokuwa katika kambi zao za wakombozi huko Msumbiji akipenda kuvaa suti. Ni mara mbili au tatu tu, tena kwa kushikiliwa na wenzake, ndipo alipovaa magwanda ya kijeshi. Wapiganaji aliokuwa nao Msumbiji wanasema kwamba hakuwa na ujuzi wa kutumia silaha. Hakujifunza hata kupiga bastola.

Siku ya mkutano wetu wa London Mugabe, kama kawaida yake, alipiga suti na tai. Alikuwa akiyumbayumba kidogo alipokuwa akenda akinifuata kwenye chumba cha mapumziko. Alikuwa mpole, mnyenyekevu kama aliyekuwa na haya ingawa haya hizo hazikuigubika haiba yake. Mabega yake kidogo yalipinda.

Nilipomuuliza kama akitaka kahawa au chai alinijibu kwamba angependa chai. Na chai ndiyo niliyomfanyia na kumpa pamoja na vitafunio vya haja.

Wakati Nujoma na Salim pamoja na wengine walipokuwa wakipiga soga na kuangua vicheko, Mugabe, kikombe cha chai mkononi, alikuwa kimya, macho chini, kama mwanamwari aliyezongwa na fikra.

Nasikia tabia hiyo alikuwa nayo tangu utotoni mwake. Alikuwa akipenda kujibanza mwenyewe kwa wenyewe akisoma na kutalii masomo yake badala ya kwenda kucheza na wenzake. Hata baadhi ya wenzake walianza kumchokoza na kumfanyia tashtiti kwa kumwita mwoga na “mtoto wa mama”.

Hadi leo ninamkumbuka Mugabe kuwa ni mtu niliyeona kwake uungwana wa roho na fikira. Alizungumza kwa ufasaha mkubwa na kwa upole ingawa hoja zake zilikuwa na nguvu ya mantiki. Hamna shaka kwamba alikuwa msomi wa aina yake.

Alijitambua kwamba aliwashinda wenzake wengi miongoni mwa viongozi, si wa Kiafrika tu bali wa duniani nzima, kwa elimu aliyokuwa nayo. Alisomea na kuhitimu shahada saba. Shahada ya mwanzo aliyoitia kwapani alitunukiwa na Chuo Kikuu cha Fort Hare cha Afrika Kusini alikosomea historia na Kiingereza. Halafu akapata shahada nyingine za sheria, elimu, uchumi na utawala.

Alipojitumbukiza katika siasa baada ya kurudi kutoka Ghana, Mugabe hakuonesha ishara yoyote ya kuwa na uchu wa madaraka ndani ya vyama vya ukombozi. Nadhani sababu kubwa ni nidhamu ya hali ya juu aliyokuwa nayo. Hatimaye lakini aliwapiku akina Mchungaji Ndabaningi Sithole, Joshua Nkomo na Nathan Shamuyarira.

Tukisema kwamba Mugabe aliikomboa Zimbabwe tutakuwa tunaizungumzia historia kwa mkato. Hatutoitendei haki wala hatutowatendea haki Wazimbabwe, kwa jumla.

Zimbabwe haikukombolewa na mtu mmoja. Hakuna taifa lolote lililokombolewa na mtu mmoja na awe shujaa wa aina gani. Zimbabwe ilikombolewa na Wazimbabwe wenyewe waliopigana na utawala wa walowezi wachache wakiongozwa na Ian Smith. Wazalendo hao, bila ya shaka, walikuwa na kiongozi wao na alama yao. Naye, kwa kipindi cha miaka mitano, alikuwa Robert Gabriel Mugabe.

Mugabe ameondoka na siri nyingi alizokuwa amezificha, au zilizojificha, alipokuwa hai. Kuna mengi ambayo hatutoyajua. Kwa mfano, hatutojua ni nini hasa kilichomfanya akawa alivyokuwa katika miaka 22 ya mwisho ya utawala wake uliodumu kwa miaka 37. Nini kilichomfanya akapoteza dira na akapotea njia miaka kama 15 baada ya kuushika uongozi wa nchi na kuonyesha ujasiri wa kuzinyanyua haki za wanyonge.

Wala hatutojua akili yake ikimwambia nini alipoviruhusu vyombo vyake vya usalama viwakamate, viwatumbukize jela na kuwatesa wapinzani na wakosoaji wake. Tuseme alisahau yaliyomfika yeye utawala wa Smith ulipomfunga jela alikoselelea kwa miaka 11?

Ni muhimu tuyajue hayo ili tuweze kuzitambua dalili za yaliyomsibu katika miaka ya mwisho ya utawala wake. Ni muhimu ili tukiziona dalili hizo zinaibuka kwa viongozi wengine wa Kiafrika tuweze kuchukua hadhari. Angalau umma utaweza ama kuwatanabahisha viongozi wa aina hiyo au kuandaa mikakati ya kuwaangusha kama alivyoangushwa yeye Mugabe licha ya mchango wake adhimu katika ukombozi wa Zimbabwe.

Baruapepe: aamahmedrajab@icloud.com; Twitter: @ahmedrajab
 
Mugabe alikua kiongozi mzuri kilichomponza in kuamini historia ya nyuma itambeba milele, japo alileta uhuru na maendeleo lakini pia alileta maumivu makubwa kwa Wazimbabwe.
 
Siku zote huwa nahisi Ahmed Rajab ni mtu wa system. Mngazija wa Kizanzibari huyu amepata fursa za kuwa karibu na viongozi wengi sana wa ki Afrika kwa mwamvuli wake wa uandishi wa habari

Ukisoma makala zake nyingi(mimi nakiri kusoma makala zake nyingi) waweza dhani ni waziri wa mambo ya nje au mwanadiplomasia aliyetumwa na nchi maana ukaribu wake kwa viongozi wakuu wa nchi mbalimbali sio wa kawaida

Kwa wasioelewa, katika watu waliokua wamemzowea marehemu Mwalimu Nyerere kufikia hata kuweza kumtania na kumfanyia masihara ni huyu jamaa

Kuna wakati alisema walikutana na Mwalimu London wakaongea meengi. Na akasema siku hiyo Mwalimu alifunguka hasa kwa namna ambayo hajawahi kumsika na ilimshangaza lakini kwa vile walikubaliana iwe siri basi na yeye anaheshimu wosia huo na hawezi kuyaweka wazi!

Ni.mtu anyoandika historia aliyoiishi na sio kuhadithiwa. Mtaalamu wa siasa za kiafrika hasa ile ya baada ya uhuru
 
Simulizi zake zinafanana kiasi na za marehemu Ali Nabwa, jamaa was a very good story teller.
Namkumbuka marehemu Ali Nabwa, naye pia alikua Mgazija wa Kizanzibari. Katika moja wapo ya simulizi zake kumuhusu Dr Omar Ali Juma alisema jamaa alikua muungwana na mcha Mungu sana

Nabwa alisema Dr Omar akiwa Makamu wa Rais hakufurahishwa jinsi serikali ilivokuwa inam harass Profesa Anna Tibaijuka wakati huo akiwa ni mwenyekiti wa Baraza La Wanawake Tanzania (BAWATA). Na alifurahi sana alipoteuliwa na UN kua mkuu wa UNFPA

Akasema, Dr Omar akamwambia yeye Nabwa kwamba, "huyu mama tumemsumbua, tumenyanyasa bila sababu ona sasa dunia imejua umuhimu wake"

Nabwa kwa wakati fulani alikua mwandishi wa Makamu wa Rais na aliwahi kufanyakazi na Dr Omari
 
Ni muhimu tuyajue hayo ili tuweze kuzitambua dalili za yaliyomsibu katika miaka ya mwisho ya utawala wake. Ni muhimu ili tukiziona dalili hizo zinaibuka kwa viongozi wengine wa Kiafrika tuweze kuchukua hadhari. Angalau umma utaweza ama kuwatanabahisha viongozi wa aina hiyo au kuandaa mikakati ya kuwaangusha kama alivyoangushwa yeye Mugabe licha ya mchango wake adhimu katika ukombozi wa Zimbabwe.
Tatizo linaanzia pale "GUCCI" Grace alipoanza kutamani kuwa kiongozi wa Zimbabwe.
 
Chupa ya chai imejaa vikombe 12,hii chupa balaaa
Ila chai tamu sana hii maana inatufunza jambo wazee watarajiwa
 
Mugabe alitaka kuacha urais aliposhindwa uchaguzi na Morgan Tsvangirai.

Tatizo likawa, vyombo vya usalama vikakataa, kwa sababu viliona Tsvangirai angeshika urais, angevilipizia kisasi.

Vikamuambia Mugabe kaa hapo hapo kwenye urais, tutakubadikishia mambo.

Wakapindua matokeo.

Mugabe akapeta.
 
Back
Top Bottom