Erythrocyte
JF-Expert Member
- Nov 6, 2012
- 117,601
- 217,993
Taarifa hii imetolewa leo na Naibu Katibu Mkuu wa Chama hicho upande wa Zanzibar Mh. Salum Mwalimu Mjini Zanzibar alipokuwa akiongea na Waandishi wa Habari.
=====
TAMKO LA KUTANGAZA NIA KUWANIA NAFASI YA RAIS WA ZANZIBAR KUPITIA CHAMA CHA DEMOKRASIA NA MAENDELEO (CHADEMA)
Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kinatangaza kusudio la kusimamisha mgombea katika nafasi ya Rais wa Zanzibar katika uchaguzi Mkuu wa Oktoba mwaka huu na hivyo inafungua milango kwa wanachama wake wenye sifa kutangaza nia.
Hii ni mara ya kwanza kwa CHADEMA kutangaza rasmi kuweka mgombea katika nafasi hiyo ya juu ya nchi kwa upande wa Zanzibar.
Naibu Katibu Mkuu wa Chadema Zanzibar Salum Mwalim ametoa tangazo hilo katika mkutano na waandishi wa Habari uliofanyika leo Jumamosi June 06, 2020 katika Ofisi Kuu ya Chadema , Kisiwandui Zanzibar.
“Tunawatangazia rasmi wanachama wetu wenye sifa na ambao wana nia ya kugombea nafasi ya Urais wa Zanzibar waandike kwa Katibu Mkuu wa chama na kuwasilisha barua hizo ofisi ya Makao Makuu Zanzibar wakati wowote kuanzia leo hadi Juni 15, 2020 Saa Kumi na Nusu Alasiri”
“Chama kimejipima na kutafakari kwa kina na kimeona kwamba sasa ni wakati mufaka kuwapa nafasi wanachama wake wenye ndoto na uwezo wa kugombea nafasi hiyo kutimiza ndoto zao”
Kwa sasa ni kutanga nia zao kwa chama na kwamba baada ya hapo utafuata mchakato wa uchukuaji wa Fomu za ndani ya chama ambapo maelekezo yake pamoja na utaratibu mzima utakaofuata utatolewa baadae. Kwa watakaowasilisha taarifa zao wataruhusiwa kutangaza kusudio lao hilo kwa Umma kupitia vyombo vya habari.
Chama kinawahimiza wanachama wote wenye Sifa, Vigezo na Maadili kama ilivyoanishwa kwenye Kanuni za chama Sura ya Kumi (10) katika Katiba ya Chama ya Mwaka 2006 Toleo la 2016 na matakwa ya Katiba ya Zanzibar kujitokeza.
”Niwatake wanachama wetu wote kufuguliwa kwa mlango huu usiwe chanzo cha kuvuruga umoja na mshikamano ambao umekuwa thabiti ndani ya chama chetu Zanzibar.”
Pamoja na tangazo hili, chama chetu kipo tayari kuendeleza ushirikiano na vyama na kulinda nia na shabaha ya ushirikiano huo bila kuathiri malengo ya vyama vyetu kwa masilahi ya kila M-Zanzibari katika uchaguzi Mkuu wa Oktoba.
Aidha, tunaendelea kuwasisitiza wanachama wetu walioonesha nia ya kugombea nafasi za Udiwani, Uwakilishi na Ubunge kwa Unguja na Pemba kuendelea na taratibu za chama na kwamba milango bado ipo wazi kwa ambao bado hawajafanya hivyo.
Chama kinawatakia kheri wanachama wake, pamoja na wafuasi na wapenzi na kwa pamoja tunawataka kuendelea kujipanga kukiletea chama ushindi katika uchuguzi Mkuu wa Oktoba .
Imetolewa na:
Ofisi ya Naibu Katibu Mkuu
Zanzibar