Chadema yamshinikiza Kikwete kutekeleza ahadi | JamiiForums | The Home of Great Thinkers

Dismiss Notice
You are browsing this site as a guest. It takes 2 minutes to CREATE AN ACCOUNT and less than 1 minute to LOGIN

Chadema yamshinikiza Kikwete kutekeleza ahadi

Discussion in 'Habari na Hoja mchanganyiko' started by Henry Kilewo, May 14, 2011.

 1. Henry Kilewo

  Henry Kilewo Verified User

  #1
  May 14, 2011
  Joined: Feb 9, 2010
  Messages: 889
  Likes Received: 63
  Trophy Points: 45
  KATIKA kile kinachoonekana kuwa ni kumshinikiza Rais Jakaya Kikwete kutekeleza ahadi alizotoa wakati wa kampeni za urais mwaka jana, Chadema kimesema kitatumia kura za maoni kumwajibisha ikiwa atashindwa kuzitekeleza.Katibu Mkuu wa Chadema, Dk Willibrod Slaa aliwaambia maelfu ya wakazi wa Mji wa Songea mkoani Ruvuma kuwa wamegundua kwamba katika nchi nyingine, akitolea mfano, Japan, kama waziri mkuu wao akishindwa kutimiza ahadi zake, wananchi hupiga kura za maoni.

  Akihutubia mkutano wa hadhara katika Uwanja wa Shule ya Msingi Kibulangoma, Dk Slaa alisema chama chake kilipoanza kuandamana, Rais Kikwete alisema kuwa wanapanga njama za kumwondoa madarakani na kutokana na hilo, kiliamua kuchunguza sababu za Rais kutoa kauli hiyo.

  "Serikali ikichaguliwa si lazima akae miaka mitano ikiwa ni kama hajatekeleza ahadi za wananchi na kama hatupi elimu bora na bure kushusha bei ya sukari na mabati. Kama ameshindwa hilo tutamwondoa kwa kura za maoni," alisema Dk Slaa."Tutaandamana na kupiga mchakamchaka ili hoja zetu tulizoahidiwa zitekelezwe kupitia Bunge kwa kuwa nchi itakalika kama wananchi wana amani na maisha mazuri," alisema Dk Slaa.

  Alidai kuwa Rais Kikwete amekuwa hawajali wananchi ikiwa ni pamoja na kutokuwashukuru kwa kumpigia kura, akidai kwamba tangu aingie madarakani katika awamu hii, amekuwa akisafiri nje ya nchi badala ya kuwatembelea wananchi wake."Kikwete atueleze alichaguliwa na Ulaya au Tanzania, anasafiri nje kila mwezi badala ya kuwashukuru wananchi waliomchagua," alisema Dk Slaa.

  Katika hatua nyingine, Dk Slaa alisema kuwa CCM kimekuwa kikiishambulia Chadema kuwa kinafanya ufisadi kwa kununua magari yaliyotumika, akisema walishasema kwamba watanunua malori ya Mwenyekiti wa chama hicho, Freeman Mbowe kwa kuwa wamekuwa wakiyatumia tangu yakiwa mapya.

  "Tutayanunua magari haya ya Mbowe kwani ndiyo yaliyotuzungusha nchi nzima katika uchaguzi na yalikuwa mapya hivyo yatanunuliwa na chama na hakuna mjadala mwingine," alisema Dk Slaa.

  Akizungumza katika mkutano huo, Mbowe alisema wataendelea kuandamana na kumshtaki Rais Kikwete kwa wananchi mpaka kieleweke."Haiwezekani tukaendelea kunyanyasika wakati kila mtu amepigika, maisha ni magumu na tunahitaji ahadi zitekelezwe," alisema na kuongeza kuwa Chadema kinapenda amani, lakini kufanya hivyo inatumika kama giza kukaa kimya. "Haiwezekani kila siku gharama za maisha zinapanda halafu tukakaa kimya."

  Kwa upande wake, Mbunge wa Mbeya Mjini (Chadema), Joseph Mbilinyi aliwaambia wananchi wa Songea Mjini kuwa walifanya makosa kumchagua Dk Emmanuel Nchimbi kwani licha ya kupewa uwaziri wa sehemu nyeti ambayo inawagusa vijana, hawasaidii chochote."Mmefanya makosa kumchagua Nchimbi kwa kuwa amepewa wizara nyeti ambayo inawagusa vijana wote nchini, lakini ninyi hakuna mnachofaidika," alisema
  Hotuba hizo za viongozi hao zilikuja baada ya maandamano makubwa yaliyoanzia Msalama hadi Viwanja vya Shule ya Kibulangoma.

  Zitto amsakama Mkullo
  Naibu Katibu Mkuu wa Chadema, Zitto Kabwe ameendelea na vita yake ya maneno na Waziri wa Fedha na Uchumi, Mustafa Mkulo safari hii akidai kuwa amekuwa akiibebesha nchi madeni na ndiyo maana deni la taifa linakua kila siku na kufikia Sh16 trilioni, kiasi ambacho ni zaidi ya Bajeti ya Tanzania kwa mwaka.

  Zitto alisema kwa mujibu wa Ripoti ya Mapitio ya Uchumi ya Machi, mwaka huu ya Benki Kuu ya Tanzania (BoT), deni hilo limefikia Dola za Marekani 11.2 bilioni ambazo ni sawa na Sh16 trilioni. Alisema kwa mujibu wa ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), ya mwaka 2009/10 hali hiyo ni ya kutisha kama haitaendana na ukuaji wa hali ya uchumi wa nchi."Hiyo ya BoT ni taarifa ambayo imetoka Machi na hii ya CAG ni ya mwaka ulioishia Juni 30 mwaka jana, inamaanisha deni linazidi kupanda kwa kasi ya ajabu."

  Zitto ambaye alikuwa akiwahutubia wananchi wa Songea Mjini jana, alisema tangu Mkulo ashike wizara hiyo, deni la taifa limekuwa likipanda kila mwaka, kitu ambacho alisema ni mzigo kwa wananchi ambao alisema itabidi watozwe kodi ya juu ili kufanikishwa kupunguzwa au kulipa kwa deni hilo.

  "Huu ni mzigo mkubwa kwa wananchi kwa kuwa sisi tunapambana kutaka kodi ipunguzwe lakini ili Serikali ilipe deni hilo itabidi ipandishe kodi, kitu ambacho ni manyanyaso kwa wananchi hawa maskini," alisema Zitto.
  Alisema kuwa deni hilo ni mzigo kwa Taifa kwa kuwa kama kila mwananchi akitakiwa kuchangia kulipwa kwa deni hilo hivi sasa atachangia zaidi ya Sh300,000 tofauti na mwaka wa fedha uliopita ambao angelipa Sh290,000.

  Zitto alisema ripoti ya CAG imeeleza kulikuwa na ongezeko kubwa la deni la Taifa mwishoni mwa mwaka ulioishia Juni 30, mwaka jana kwa kiasi cha Sh2.8 trilioni kwa kuwa deni hilo kwa mwaka wa fedha 2008/09 lilikuwa Sh7.6 trilioni lakini sasa limefikia Sh10 trilioni."Deni hilo ni sawa na asilimia 38 zaidi ya deni la mwaka uliopita kwa mujibu wa CAG. Kama hali itaendelea kuwa hivi tutaumia sana hasa wananchi wengi walio maskini," alisema Zitto.

  Zitto ambaye ni Waziri Kivuli wa Wizara hiyo, hivi karibuni alidai kuwa Serikali imefilisika kwa kushindwa kulipa wafanyakazi wake mishahara, hivyo kuamua kukopa katika benki za biashara nchini.Kitendo hicho kilimfanya Waziri Mkulo kumjibu, akisema Mbunge huyo wa Kigoma Kaskazini ni mwongo kwa kuwa Serikali haijakopa kama alivyodai.

  Hata hivyo, Zitto alisema kuwa atamthibitishia bungeni Waziri Mkulo jinsi Serikali ilivyokopa fedha benki ili aweze kuwajibika kutokana na kauli yake ya kukataa kusema ukweli.Zitto alisema ni kweli Serikali haina fedha kwa kuwa, kwa mujibu wa taarifa BoT ya mapitio ya uchumi ya Machi, mwaka huu imeshindwa kukusanya kodi kwa asilimia 15.
   
Loading...