CHADEMA yaiumbua CCM | JamiiForums | The Home of Great Thinkers

Dismiss Notice
You are browsing this site as a guest. It takes 2 minutes to CREATE AN ACCOUNT and less than 1 minute to LOGIN

CHADEMA yaiumbua CCM

Discussion in 'Jukwaa la Siasa' started by Serayamajimbo, Aug 20, 2009.

 1. S

  Serayamajimbo Senior Member

  #1
  Aug 20, 2009
  Joined: Apr 15, 2009
  Messages: 191
  Likes Received: 0
  Trophy Points: 0
  WAKATI Chama Cha Mapinduzi (CCM), kikijaribu mara kwa mara kujinasua kutoka kwenye tuhuma za ufisadi zinazoelekezwa kwake, Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), kimeibuka na kuanika hadharani nyaraka za siri kutoka kwenye vikao vya ndani vya CCM, zinazoonyesha jinsi chama hicho kinavyozidi kukumbatia vitendo vya ufisadi nchini.
  Akihutubia wananchi kwenye viwanja vya Manzese Bakhressa, jijini Dar es Salaam mwishoni mwa wiki, Mkurugenzi wa Mambo ya Nje wa CHADEMA, John Mnyika, alisema ushahidi wa nyaraka za siri alizozipata hivi karibuni kutoka kwenye kikao cha ndani cha CCM Wilaya ya Kinondoni, unaonyesha jinsi kinavyolinda ufisadi unaofanywa na viongozi mbalimbali wa chama hicho na serikali yake.
  Akitumia taarifa ya kikao cha Kamati ya Siasa ya CCM ya Halmashauri ya Wilaya ya Kinondoni, kilichoketi hivi karibuni, alisema chama hicho kiliamua kubariki ufisadi wa Meya wa Manispaa ya Kinondoni, Salum Londa, wa kujipatia fedha za umma, zaidi ya sh milioni 100, kwa kuamua kumuonya badala ya kumfukuza uanachama na kumfungulia mashitaka.
  Mnyika ambaye aligombea ubunge Jimbo la Ubungo kupitia CHADEMA mwaka 2005, alisema Londa alijipatia fedha hizo baada ya kupandisha bei za kulipia matrela ya kuzolea taka kutoka kwenye bei halisi iliyopaswa kulipwa kwa kazi hiyo, lakini licha ya kamati ya siasa ya chama chake kuutambua ufisadi huo, haikuamua kumchukulia hatua kali, zaidi ya kukubaliana aonywe.
  “Nina taarifa ya siri hapa. Ni taarifa ya kikao cha Kamati ya Siasa ya CCM ya Halmashauri ya Wilaya ya Kinondoni, juu ya ubadhirifu wa fedha za umma na uongozi mbovu wa Manispaa ya Kinondoni.
  “Taarifa hii inaonyesha kuwa CCM inajua na inakiri kuwa kulifanyika ufisadi wa kujipatia fedha za umma zaidi ya sh milioni 100, kwa njia ya udanganyifu, uliofanywa na kina Londa,” alisema Mnyika.
  Alisema fedha zilizotafunwa ni za wananchi na inasikitisha kuona CCM imechukua hatua dhaifu kwa Londa na wenzake ambao walipaswa wafukuzwe uanachama na wafikishwe mahakamani kwa kosa hilo.
  “Mnataka kitokee nini tena ndani ya nchi hii ili muamini kuwa CCM ni chama cha mafisadi? Kama ufisadi wa fedha za EPA, Richmond hamkuuelewa vizuri, je hata huu nao ulio karibu kabisa na ninyi hauonyeshi jinsi CCM inavyolinda mafisadi?” alihoji Mnyika.
  Aliongeza kuwa, CCM ni chama cha mafisadi, CHADEMA ni chama kinachopigania uwazi, ukweli na uwajibikaji kama rangi nyeupe iliyomo kwenye bendera yake.
  Alibainisha kuwa kutokana na taarifa hiyo, ni dhahiri uchafu wa mazingira uliokithiri katika mitaa mbalimbali ndani ya Wilaya ya Kinondoni, unasababishwa zaidi na ufisadi wa kutoa zabuni za uzoaji taka kwa kampuni zisizo na uwezo ili viongozi wajichotee fedha za umma kwa njia za udanganyifu.
  “Kwa hiyo, mkiona katika maeneo yenu, katika mitaa yenu kuna uchafu, mazingira ni machafu, hali hiyo inasababishwa na ufisadi uliokithiri ndani ya uongozi wa Manispaa ya Kinondoni. Fedha nyingi zinazopaswa kutumika kwa shughuli za uzoaji taka zinaliwa. Zabuni za uzoaji taka zinatolewa kwa kampuni zisizo na uwezo wala vifaa vya kutosha. Ufisadi huu pia ulibarikiwa na CCM katika kikao cha Kamati yake ya Siasa cha Wilaya ya Kinondoni. CCM ni chama cha mafisadi,” alisema Mnyika.
  Alisema taarifa ya kikao hicho cha CCM pia inaonyesha kuwa meya huyo pamoja na madiwani wa halmashauri hiyo, ambao wote ni wa CCM, wamekuwa wakijipatia fedha kifisadi kwa kuuza kinyemela viwanja na maeneo ya umma na kisha kugawana, hali iliyosababisha kuwapo kwa migogoro mbalimbali ya ardhi ndani ya Wilaya ya Kinondoni.
  Mnyika alisema taarifa ya kikao hicho cha ndani cha CCM inaeleza kuwa diwani mmoja wa Wilaya ya Kinondoni, alikula sehemu ya fedha za rambirambi zilizochangwa na watu mbalimbali mwaka 2005 wakati kampeni za uchaguzi zikiendelea, kumsaidia mwanachama mmoja wa CCM aliyemtaja kwa jina la Mwajuma Nyanza, ambaye nyumba yake iliungua moto.
  Alisema jumla ya fedha za rambirambi zilizochangwa kwa ajili ya kumsaidia mwanachama huyo ni sh 350,000 lakini diwani huyo wakati huo akiwa kiongozi wa kawaida wa CCM, hakufikisha fedha zote, alizotumwa kuwasilisha kwa familia iliyofikwa na tukio hilo.
  Mnyika aliwataka wakazi hao wa Manzese na wa jijini Dar es Salaam, kufanya mabadiliko makubwa ya uongozi kwani ufisadi wote unaoendelea ndani ya Manispaa ya Kinondoni umesababishwa na manispaa hiyo kuwa na madiwani wote kutoka CCM.
  Aliwataka kuanza kufanya mabadiliko hayo kwa kuanza kujiandaa kushiriki kikamilifu kwenye uchaguzi wa serikali za mitaa utakaofanyika Oktoba 25 na kuchagua viongozi wa serikali za mitaa kutoka CHADEMA.
  Alisema matokeo ya chaguzi ndogo za ubunge katika majimbo ya Kiteto, Tarime, Busanda na Biharamulo, yameonyesha kuwa CHADEMA ndiyo chama pekee cha upinzani chenye nguvu Tanzania Bara, hivyo ni vema wananchi wote wakaunganisha nguvu zao na kukiunga mkono ili kiing’oe CCM kwa kuanzia na uchaguzi wa serikali za mitaa.
  Katika hatua nyingine, Mnyika alimtaka Waziri Mkuu, Mizengo Pinda kutangaza kanuni za uchaguzi wa serikali za mitaa kwa mwaka 2009 haraka ili vyama vyote vianze kujiandaa.
  Alisema katika kikao cha Bunge lililopita, Pinda, aliahidi kuwa kanuni hizo zingetangazwa mwazoni mwa mwezi huu, lakini mpaka sasa bado hazijatangazwa rasmi wala kuwekwa wazi kwa vyama vya siasa.
  Mnyika alisema kuna taarifa za kuaminika kuwa CCM imeshaanza kugawa fomu za wagombea wake kabla hata kanuni za uchaguzi huo kutangazwa, hali inayoashiria kuwa tayari chama hicho kimeshaanza kupendelewa kwa kupewa taarifa za kanuni zitakazotumika kwenye uchaguzi huo ili kijiandae mapema kabla ya vyama vingine.
  Aidha, alisema amekamata waraka wa CCM kutoka ngazi za juu za chama hicho unaowaelekeza viongozi wake wa chini jinsi ya kurubuni wananchi katika kampeni za uchaguzi wa serikali za mitaa ili kishinde uchaguzi huo.
  Alisema moja ya mambo ambayo waraka huo imewaagiza viongozi wa CCM, ni kuwarubuni wananchi kuwa chama hicho ni chama cha amani na utulivu na vyama vya upinzani ni vyama vya vurugu.
  Mnyika alisema wananchi wasiikubali propaganda hiyo kwani CCM ndicho chama kinachohatarisha amani nchini kwa kuiingiza nchi kwenye mijadala ya udini, kusababisha kukua kwa pengo kati ya tajiri na masikini, na kuwapa vijana mafunzo ili wafanye vurugu wakati wa uchaguzi kama walivyofanya Tarime, Busanda na Biharamulo. Mkutano huo wa juzi ni sehemu ya mikutano ya hadhara ya CHADEMA jimbo la Ubungo, inayofanyika kwa muda wa siku 11 mfululizo, kuwahamasisha wakazi wa jimbo hilo na Mkoa wa Dar es Salaam kwa ujumla kushiriki kikamilifu kwenye uchaguzi ujao wa serikali za mitaa na kukichagua chama hicho.
   
Loading...