CHADEMA wilaya ya Rombo yashinda kesi Mahakama Kuu

Mwanahabari Huru

JF-Expert Member
Mar 9, 2015
14,243
34,899
Chama Cha Demokrasia na Maendeleo-CHADEMA Wilaya ya Rombo, imeshinda kesi ya rufaa katika Mahakama Kuu Kanda ya Moshi iliyokuwa imekatwa na diwani wa Kata ya Mengwe, Mwenyekiti wa Kijiji cha Mengwe Juu na wajumbe wengine 12 wa Serikali ya kijiji cha Mengwe juu.

Rufaa hiyo namba 52 ya mwaka 2017 imetokana na kesi ya jinai iliyofunguliwa na Jamhuri ambapo mlalamikaji ndugu Damas Kyauke alidai kuwa viongozi hao walikata miti 42 ya mbao, miti 34 ya kahawa na miti 108 ya matunda wakati wa upanuzi wa barabara katika kitongoji cha Kinangura kinachoongozwa na Mama Manka kutoka CHADEMA

Katika hukumu iliyotolewa na Mahakama ya Hakimu Mkazi Wilaya ya Rombo, washtakiwa wote walikutwa na hatia na kuhukumiwa kwenda jela mwaka 1 au kulipa faini ya shilingi laki 4 kila mmoja na mshtakiwa mmoja alifungwa mwaka 1 bila mbadala wa faini. Lakini pia Mahakama ya Wilaya ilielekeza washtakiwa kumlipa ndugu Damas Kyauke fidia ya Shilingi za Kitanzania Milioni 57 kama fidia ya uharibifu wa mali zake ambapo kila mshtakiwa alitakiwa kutoa kiasi cha shilingi milioni 4 na laki 3 kila mmoja.

Katika hukumu hiyo iliyotolewa leo na Mahakama Kuu Kanda ya Moshi, Jaji aliyekuwa akisikiliza kesi hiyo Mhe. Fikirini, alitengua hukumu iliyokuwa imetolewa na Mahakama ya Wilaya ya Rombo, na kuamuru faini zilizolipwa na wakata rufaa kurejeshwa na pia kuachiliwa mara moja kwa mkata rufaa mmoja ndugu "Yapuu" aliyekuwa akitumikia kifungo katika gereza la Ibukoni Wilayani Rombo.

Hukumu hiyo ya Mahakama Kuu iliyosomwa leo Aprili 20, 2018, imeibua furaha na nderemo kwa wananchi wa tarafa ya Mengwe ambao walikuwa wakikosa huduma kikamilifu kutokana na Viongozi wao kutumia muda mwingi kushughulikia kesi yao iliyokuwa ikiwakabili.

Akizungumzia hukumu hiyo iliyosomwa leo , Mwenyekiti wa CHADEMA Wilaya ya Rombo ambaye pia ni Diwani wa Kata ya Ngoyoni na Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Rombo, Mhe. Evarist Silayo, aliishukuru Mahakama Kuu kwa kutenda Haki na kusema kwamba kwa sasa wanajipanga kufungua kesi ya madai ili haki iweze kutendeka zaidi lakini pia kuwafanya wale wote wenye dhamira ya kuwazuia viongozi waliochaguliwa na wananchi kutimiza majukumu yao bila sababu za msingi kuacha mara mmoja.

Pia Diwani wa Kata ya Mengwe Mhe. Romana Lyakurwa ambaye alikuwa mmoja wa wakata rufaa alisema kuwa "Ninaishukuru Mahakama Kuu kwa kutenda Haki na kufuta hukumu iliyotolewa na Mahakama ya Wilaya ya Rombo na ninaahidi kuongeza bidii katika kuwatumikia wananchi wangu wa Kata ya Megwe" alisema Diwani huyo
 
Mahakama Ziko huru
Hatari
FB_IMG_1494788493080-1.jpg
 
Back
Top Bottom