Chadema watoa masharti, CUF wakataa

nickname

JF-Expert Member
Dec 20, 2009
544
147
CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kimetoa masharti kwa Chama cha Wananchi (CUF) kuweka wazi msimamo wake kuhusu suala la Katiba mpya, kabla ya kukishirikisha katika uundwaji wa Kambi ya Upinzani bungeni.

Aidha chama hicho kimesema hakitokubaliana na taarifa za kuwapo uwezekano wa kuunda Kambi Ndogo ya Upinzani Bungeni kwa madai kuwa ni kinyume na Kanuni za Mabunge ya Jumuiya ya Madola (CPA) na kwamba iwapo kambi hiyo itaundwa, Chadema itaiomba jumuiya hiyo ilivue Bunge la Tanzania uanachama wake.


Hata hivyo CUF imeendelea kusisitiza msimamo wake kuwa haitambui masharti hayo ya Chadema kwa kuwa hayamo ndani ya kanuni za Kambi ya Upinzani na kuweka wazi kuwa kimemuandikia barua Spika wa Bunge, Anne Makinda, kuomba fursa ya kuunda kambi hiyo ndogo.


Akizungumza na waandishi wa habari jana Dar es Salaam, Mkurugenzi wa Sheria, Katiba na Haki za Binadamu wa Chadema, Tundu Lissu alisema chama hicho kiko tayari kusahau makovu ya uchaguzi yaliyotokana na msuguano baina yake na vyama vingine vya upinzani, lakini kuhusu maridhiano ya Zanzibar baina ya CUF na CCM, lazima lipatiwe ufafanuzi.


Aliyataja kwa kifupi makovu hayo kuwa ni kukwaruzana kwa Mwenyekiti wa CUF, Profesa Ibrahim Lipumba na Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe wakati wa kampeni na mgogoro wa Mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi, James Mbatia na Mbunge wa Kawe, Halima Mdee ambapo alidai majeraha hayo ni madogo na yanasahaulika.


"Maridhiano ya Zanzibar kwanza yamefanyika kinyume na Katiba ya Muungano, lakini pia makubaliano ya Muungano, kutokana na maridhiano hayo na kuundwa kwa Katiba mpya ya Zanzibar sasa Zanzibar ni nchi, tutashirikiana vipi na watu wenye nchi yao, serikali na mipaka? Lazima hili lijadiliwe kabla ya kupeana vyeo bungeni," alisisitiza Lissu.


Alisema, makubaliano ya Muungano yaliyofanyika mwaka 1964 yalifuta nchi mbili za Zanzibar na Tanganyika na kuunda Tanzania, lakini baada ya maridhiano hayo ya CCM na CUF Zanzibar, kumeundwa Katiba mpya na Zanzibar sasa inatambulika kama nchi yenye eneo lenye mipaka, bahari na hata Mahakama.


"Kabla ya kuundwa kwa katiba hiyo, kesi zote za rufani za Zanzibar zilikuwa zinasikilizwa katika Mahakama ya Rufani Tanzania, lakini Katiba hiyo mpya inafuta hilo, maana yake ni kwamba Zanzibar imejikamilisha kama nchi, ina Rais, mipaka, eneo la bahari, vikosi vya jeshi, Bunge na Mahakama," alisema.


Lissu alisema, mabadiliko hayo yana athari kwa uhai wa Muungano wa Tanzania na kwamba vifungu vilivyopo ndani ya Katiba hiyo mpya vinakiuka Katiba ya Tanzania ya mwaka 1977 na kutokana na hali hiyo, ni lazima ijulikane wazi kwamba maridhiano hayo yana ajenda gani na Tanzania Bara.


"Ndio maana tunataka msimamo wa CUF kuhusu hili kwani baada ya kuunda Kambi ya Upinzani, tuna mpango wa kuunda kamati kuchunguza walioharibu Katiba yetu, ndio tunataka msimamo wao kwa kuwa wao wanafaidika na kuchakachuliwa kwa Katiba," alisema.


Pia alisema chama hicho hakitoona shida kuunda Kambi ya Upinzani chenyewe, bila kushirikisha chama chochote cha upinzani kwani hata CUF mwaka 1995 iliunda kambi yake kwa kushirikiana na UDP bila kushirikisha wabunge wa NCCR-Mageuzi.


Kuhusu tetesi za kuunda kwa kanuni mpya, zitakazoruhusu kuundwa kwa Kambi Ndogo ya Upinzani, alikiri kuzisikia na kuongeza kuwa, "Chadema tunasubiri kambi hiyo iundwe, tutapeleka kilio chetu CPA kwa kuwa kufanya hivyo ni kinyume na kanuni za mabunge hayo na tutaomba Bunge la Tanzania livuliwe uanachama."


Akizungumza na gazeti hili kuhusu tamko hilo la Chadema, aliyekuwa Kiongozi wa Kambi ya Upinzani na Mbunge wa Wawi (CUF), Hamad Rashid Mohammed, alisema masharti hayo ya Chadema, hawayatambui.


"Tulitengeneza kanuni za Kambi ya Upinzani tena tukiwa na Dk. Willibrod Slaa (aliyekuwa Mbunge wa Karatu na mgombea urais Chadema), zikapitishwa na wabunge na zikakabidhiwa kwa Spika, na masharti haya hayamo kwenye kanuni hizo kwa hiyo hatuyatambui," alisema.


Kuhusu suala la Katiba Hamad alisema, CUF ilishalilia na kuandamana hadi watu wakapoteza maisha na matokeo yake ndiyo maridhiano ya Zanzibar na kusisitiza kuwa si kweli kuwa yanaifanya Zanzibar kuwa nchi bali ni ‘state' (dola) kama ilivyo California.


Kuhusu suala la kuudwa kwa Kambi Ndogo ya Upinzani, alikiri kwamba yeye ndiye aliyeandika barua kwa Spika wa Bunge, kuomba kuundwa kwa kanuni zinazoitambua kambi hiyo na kwamba suala hilo pia limo kwenye kanuni za CPA na zipo nchi zenye kambi ndogo za upinzani na kutoa mfano Marekani na Uingereza.


"Suala hili linafahamika hata kwenye kanuni za CPA ila kwa bahati mbaya sisi hatukuwa na kanuni hizo, ndio maana nimeandika barua kwa Spika ili kuona uwezekano wa kuunda kambi hiyo, hilo linawezekana kabisa," alisema.


Source : HabariLeo 29/11/2010
 
Back
Top Bottom