Chadema: Wabunge 19 wa viti maalumu waondolewe Bungeni kabla ya mwezi Novemba, 2022

Roving Journalist

JF Roving Journalist
Apr 18, 2017
2,801
11,961
Mzungumzaji kuu ni Mhe. Salimu Mwalimu, Naibu Katibu Mkuu wa Chama hicho ambaye anaelezea maamuzi ya kamati kuu iliyoketi Septemba 17-18, 2022
  • Kamati kuu imeitaka Serikali kupeleka muswada wa kufuta sheria mpya ya tozo ambayo imekuwa mzigo mkubwa kwa watanzania.
  • Serikali ije na mpango madhubuti wa kuhakikisha chakula kinapatikana kwa uhakika na kudhibiti kupanda kwa gharama zake.
  • Serikali ipunguze utitiri wa kodi na tozo kwenye mafuta ili bei yake ipungue nchini.
  • Kamati kuu imemtaka CAG kufanya ukaguzi maalumu kwenye mfuko wa bima ya Taifa (NHIF) ili aje na majibu kwa Umma juu ya mwenendo wa michango ya wanachama. Serikali itoe muda wa kutosha kwa wananchi kujadili sheria mpya ya bima kwa afya kwa wote, CHADEMA inapinga mchakato unaopanga kuipitisha sheria hii kwa hati ya dharura.
  • Ripoti ya CAG upande wa Zanzibar imebaini matumizi mabaya ya fedha za umma. Kamati kuu inataka hatua stahiki kwa wahusika zichukuliwe dhidi yao.
  • Vyombo vya ulinzi vya Zanzibar vimekuwa vinapewa kandarasi bila uwazi. Mikataba lazima iwekwe wazi kwa umma.
  • Mazungumzo ya maridhiano ya kisiasa nchini yaendelee. Ili mazungumzo haya yaendelee pasipo kukwama, Kamati kuu imeitaka Serikali kuondoa haraka zuio haramu kwa vyama vya siasa juu ya uhuru wao wa kufanya mikutano bila masharti yoyote. Muswada wa sheria unaofufua mchakato wa katiba mpya upelekwe bungeni kabla ya mwezi novemba. Aidha, Serikali iwaondoe bungeni wabunge 19 wa viti maalumu kabla ya mwezi novemba.
  • Kamati za vyama nchi nzima zianze kujipanga kuanza kwa mikutano ya hadhara.
  • Kamati kuu inalaani uondolewaji wa wamasai Loliondo pamoja na kuhamishwa kwa fedha zao za miradi ya maendeleo, pia inaitaka Serikali kusitisha zoezi hili pamoja na kuwalipa fidia waathirika wote.
Pamoja na hayo, Kamati kuu ilipokea taarifa za uchaguzi wa Kenya ambapo imeona moja kati ya jambo kubwa ambalo watanzania tunaweza kujifunza ni kuwa na katiba imara inayoweza kutoa nafasi ya kuwa na uchaguzi wa huru, haki na wazi.

Akijibu swali la mwandishi wa habari aliyetaka kufahamu juu ya sharti la kuwatoa wabunge 19 Bungeni huku kesi ikiwa mahakamani, Mhe. Mwalimu amesema Serikali na Chama cha mapinduzi wanajua ni jinsi gani wabunge hao waliwaruhusu waingie bungeni hivyo wao wenyewe wataona namna gani wafanye ili kuwatoa.

Kuhusu kikosi kazi, wao kama CHADEMA bado hawakitambui na hawahusiki kwa namna yoyote na mambo wanayofanya.

======

CHAMA CHA DEMOKRASIA NA MAENDELEO (CHADEMA)

MAAZIMIO YA KIKAO CHA KAMATI KUU YA CHAMA KILICHOFANYIKA SEPTEMBA 17-18, 2022 JIJINI DAR ES SALAAM.

Kamati Kuu ya Chadema ilikutana kwa siku mbili Jijini Dare es salaam katika kikao chake cha kawaida kilichoongozwa na Mwenyekiti wa Chama Taifa, Mheshimiwa Freeman Mbowe.

Kamati Kuu ilikuwa na ajenda kadhaa zikiwemo kupokea na kuijadili taarifa ya hali ya Siasa na Uchumi nchini, pia ilihusisha taarifa ya hali ya siasa Zanzibar, Mwenendo wa mazungumzo ya Maridhiano baina ya Chadema, CCM na Serikali, Bajeti ya Serikali ya mwaka 2022/23 na madhara yake kwa wananchi, Hatari ya Mfuko wa Bima ya Afya kufilisika na kutungwa Kwa sheria Mpya ya bima ya Afya kwa wote. Hali ya upatikanaji na bei kubwa ya chakula nchini. Bei kubwa ya Mafuta na nyinginezo kadhaa.

Katika kikao hicho Wajumbe walijadili kwa kina taarifa hizo na kufikia maamuzi mbalimbali kama ifuatavyo;

1. Bajeti ya Serikali ya mwaka 2022/23 na tozo za miamala ya kieletroniki.

Kamati Kuu imeitaka Serikali kupeleka Muswada wa marekebisho ya sheria ya fedha ya mwaka 2022/23 kufuta kifungu kilichoingiza tozo kwenye miamala ya kieletroniki nchini kutokana na tozo hizo kuwa mzigo mkubwa kwa Mwananchi.

Kamati Kuu imetaka Muswada huo wa marekebisho ya sheria ufute kifungu cha Sheria ya fedha ya mwaka 2022/23 kilichoanzisha Tozo Mpya ya Vingamuzi ambayo bado haijaanza kutozwa ili kumpunguzia mwananchi gharama kubwa za maisha.

2. Gharama kubwa za chakula nchini.

Kamati Kuu imeitaka Serikali kuja na mpango madhubuti wa uhakika wa upatikanaji wa chakula na kuthibiti kasi ya ukuaji wa bei za chakula nchini.

3. Bei ya Mafuta Nchini.

Kamati Kuu imeitaka Serikali kupunguza msururu wa Kodi na Tozo kwenye Mafuta ili kupunguza bei kubwa ya mafuta nchini.

4. Kufilisika kwa Mfuko wa Bima ya Afya ya Taifa (NHIF) na kutungwa kwa Sheria Mpya ya Bima ya Afya kwa Wote.

Kamati Kuu inamtaka Mkaguzi na Mdhibiti wa Hesabu za Serikali (CAG) kufanya ukaguzi maalum kwenye mfuko wa Bima ya Afya nchini na kutoa taarifa yake kwa Umma kuhusu mwenendo wa hali ya Fedha za wanachama wa mfuko huo ikiwa ni pamoja na madeni yake.

Kamati Kuu imeitaka Serikali kutoa Muda wa kutosha kwa wananchi kuijadili Sheria Mpya ya Bima ya Afya Kwa Wote badala ya kutumia utaratibu wa Hati ya Dharura kuwasilisha Muswada Bungeni. Serikali itumie utaratibu wa kawaida katika kutunga sheria hiyo.

5. Ripoti ya Ukaguzi wa Hesabu za Serikali Zanzibar

Ripoti ya mkaguzi na mdhibiti wa Hesabu za Serikali ya Mapinduzi Zanzibar kwa mwaka wa fedha 2020/21 kama ilivyo kwa miaka iliyotangulia zimebainisha Ubadhirifu, Ufisadi, Uzembe na matumizi mabaya kwa ujumla ya Fedha za Umma.

Chadema haijaridhishwa na hatua ambazo zimechukuliwa na SMZ mpaka hivi sasa hivyo inataka hatua zaidi zichukuliwe kwa wahusika na taarifa ya hatua hizo iwekwe wazi kwa umma. Hatua hizo ziambatane pia kwa upande mwingine kuweka wazi kandarasi zilizopewa vyombo vya usalama na kushughulikia walioshindwa kutekeleza matakwa ya kandarasi hizo."

6. Kuhusu Maridhiano

Kamati Kuu inaazimia kwamba mazungumzo kati ya Chadema na Serikali/CCM kuhusu Maridhiano ya Kisiasa nchini yaendelee kwa kuzingatia mambo yafuatayo:

Kuondolewa haraka iwezekanavyo na bila masharti yoyote zuio haramu la mikutano ya hadhara kwa vyama vya siasa vya upinzani nchini.

Ratiba ya mchakato wa upatikanaji wa Katiba Mpya na hatua zake zote inakubaliwa kwa pamoja na pande zote na kuandaliwa kwa muswada wa sheria ya utekelezaji wake kabla ya kikao cha Bunge cha mwezi Novemba mwaka huu.

Kamati ya Pamoja ya Wataalamu wa Sheria yenye Wajumbe wa pande zote mbili iundwe kwa lengo la kuandaa mapendekezo ya marekebisho ya Sheria mbalimbali yanayohitajika ili kutengeneza mazingira bora ya kupatikana kwa Katiba Mpya. Kamati hiyo iundwe na kuanza kazi kabla ya kikao cha Bunge cha Novemba mwaka huu.

Serikali/CCM inachukua hatua za kuwaondoa Bungeni wale wanaoitwa “Wabunge wa Viti Maalum wa Chadema” kabla ya kikao cha Bunge cha mwezi Novemba mwaka huu.

7. Maandalizi ya Mikutano ya Hadhara

Kamati Kuu inaazimia kwamba Chama, katika ngazi zake zote, kianze maandalizi ya kuanza kwa mikutano ya hadhara nchi nzima kwa wakati na muda utakaoelekezwa na uongozi wa Chama kwa kufuata Katiba, sheria na Kanuni za nchi.

8. Kuhusu kufukuzwa kwa Wananchi wa Wilaya ya Ngorongoro.

Kamati Kuu inapinga na kulaani vikali vitendo vya Serikali ya CCM kuwaondoa kwa nguvu na kinyume cha Katiba, Sheria na Mikataba ya Kimataifa ya Haki za Binadamu wananchi wanaoishi maeneo ya Hifadhi ya Ngorongoro hususani Tarafa ya Loliondo.

Kamati Kuu inapinga na kulaani vikali vitendo vya Serikali ya CCM vya kuhamisha fedha za maendeleo na huduma za jamii zilizotengwa na Bunge kwa ajili ya wananchi wa Wilaya ya Ngorongoro na kuzipeleka Wilaya ya Handeni kama njia ya kuwashinikiza wananchi hao kuondoka katika ardhi na maeneo yao ya jadi na wanayoyamiliki kwa mujibu wa sheria za nchi yetu.

Kamati Kuu inaitaka Serikali ya CCM kusitisha vitendo hivi haramu dhidi ya wananchi wa Ngorongoro pamoja na kuwafidia wale wote ambao wameathiriwa kwa namna mbali mbali na vitendo hivyo.

9. Uchaguzi Mkuu wa Kenya

Kamati Kuu imepokea taarifa ya Uchaguzi Mkuu wa Kenya na imepongeza uwepo wa Katiba Imara ya Kenya Kwa kuweka mifumo na taasisi imara za kusimamia na kuendesha Chaguzi zilizo Wazi na Huru na kuwataka Watanzania kuendelea kupigania upatikanaji wa Katiba Mpya nchini ambayo pamoja na mambo mengine itaweka bayana Mifumo na Taasisi imara za kusimamia na kuendesha Chaguzi Huru, Wazi na za Haki nchini mwetu.
 
Wakikujibu uniambie hasa Hilo la ofisi utaona namna wanavyotafuta kichaka Cha kujificha

Dunia ya sasa ya kidigitali inaondoa ulazima wa kuwa na liofisi likubwa. Wazee ndio wanaamini kuwa na ofisi. Matokeo ya kuwa na maofisi mengi kama CCM, hizo ofisi zimegeuka kuwa sehemu ya majobless, wapika majungu, washirikina, kupanga mipango haramu ya kudhuru wapinzani nk.
 
Dunia ya sasa ya kidigitali inaondoa ulazima wa kuwa na liofisi likubwa. Wazee ndio wanaamini kuwa na ofisi. Matokeo ya kuwa na maofisi mengi kama CCM, hizo ofisi zimegeuka kuwa sehemu ya majobless, wapika majungu, washirikina, kupanga mipango haramu ya kudhuru wapinzani nk.
Kwa hiyo wananchi wakiwa na shida watakuwa wanakuja nyumbani kwenu? Au ndio Yale mliyowaambiaga watanzania wakasome ilani mtandaoni? Yaani nyie wanachadema hamjaanza ubabaishaji Leo Wala Jana, mmeanza muda Sana ubabaishaji Hadi Sasa watanzania wamewashitukia na kuamua kuwapuuza mambo yenu.
 
Rais Samia Suluhu alisema lengo lake ni "KUMUINUA MWANANCHI NA SIO KUMDIDIMIZA"
Nini sasa cha ajabu alichofanya,,, Yaani ANAWADIDIMIZA mwenyewe, halafu baadae ANAWAINUA mwenyewe, then wewe unakuja kumsifia,,,unamsifia kwa Lipi sasa mtu aliyetengeneza tatizo mwenyewe halafu analitatua mwenyewe?

JPM aliwahi kusema "Vijana wa namna yako wana Mchango mdogo sana katika maendeleo ya taifa"
 
Kwa hiyo hayo ndio walikaa wakawa wanajadili kwa siku mbili? Ndio maana nikasema Hawa wamebaki wanakusanyika kupiga soga tu kupoteza muda, Ndio sababu ya kupuuzwa na watanzania.

Sasa hayo ndo manini waliyojadili? Kwani kipi kipya na kisichofanyiwa kazi na serikali hii pendwa ya mh mama Samia suluhu Hassani? Ndio maana watanzania wameendelea kuwa na matumaini na serikali hii ya mama was nguvu
 
Kuagiza Wabunge 19 wa Chadema akina Halima Mdee waondolewe bungeni kabla ya November ni kuingilia Uhuru wa Mahakama, CC ya Chadema lazima ikemewe

Chadema kuagiza Serikali ifute Tozo wakati Kamati kuu ya CCM imeshatoa agizo hilo ni dhahiri Chadema ni tawi la CCM

Nategemea Wakili msomi Kibatala atawaomba radhi akina Halima Mdee kwa niaba ya mteja wake( Chadema)
 
Kuagiza Wabunge 19 wa Chadema akina Halima Mdee waondolewe bungeni kabla ya November ni kuingilia Uhuru wa Mahakama, CC ya Chadema lazima ikemewe

Chadema kuagiza Serikali ifute Tozo wakati Kamati kuu ya CCM imeshatoa agizo hilo ni dhahiri Chadema ni tawi la CCM

Nategemea Wakili msomi Kibatala atawaomba radhi akina Halima Mdee kwa niaba ya mteja wake( Chadema)
Wameagiza? Au ni mtazamo?
 
Back
Top Bottom