Mpaka Kieleweke
JF-Expert Member
- Feb 27, 2007
- 4,132
- 1,571
Naona wandugu hapa kwetu bongo siasa zinaelekea kuwashinda watatwala wetu kwani sasa hawajibu hoja badala yake wanajibu vioja.
Pili nimeshangazwa na CCM kujibu tamko lililoelekezwa kwa rais na CHADEMA badala ya habari maelezo kufanya hivyo je?hii ni kulinda mzee asiumbuliwe?
Naweka tamko la CHADEMA hapa na mwenye la CCM tafadhali aliweke hapa pia ili tuweze kujadili kwa kina.
Pili nimeshangazwa na CCM kujibu tamko lililoelekezwa kwa rais na CHADEMA badala ya habari maelezo kufanya hivyo je?hii ni kulinda mzee asiumbuliwe?
Naweka tamko la CHADEMA hapa na mwenye la CCM tafadhali aliweke hapa pia ili tuweze kujadili kwa kina.
TAMKO LA KAMATI KUU YA CHAMA CHA DEMOKRASIA NA MAENDELEO (CHADEMA) KUHUSU KUUNDWA KWA KAMATI YA RAIS YA UCHUNGUZI WA SHERIA NA MIKATABA YA MADINI.
Kamati Kuu ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) katika Kikao chake cha Dharura kilichofanyika Keys Hotel, Dar es Salaam leo hii tarehe 24 Novemba 2007, imejadili na kutafakari kwa kina uamuzi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wa kuunda Kamati ya Rais ya Uchunguzi wa Sheria na Mikataba ya Madini na uteuzi wa Mheshimiwa Zitto Zuberi Kabwe(Mbunge) kama mjumbe wa kamati hiyo na kufikia maazimio yafuatayo:
1. Kamati Kuu inamtaka Rais asitishe na/au kufuta uteuzi wa wajumbe wa Kamati hiyo ambao wanatuhumiwa kwa ufisadi na/au kwa kuwa na mgongano wa maslahi;
2. Kamati Kuu inamtaka Rais atimize ahadi yake ya kuipa Kamati "uwakilishi mpana zaidi" kwa kuteua wawakilishi wa taasisi zisizokuwa za kiserikali ,mashirika ya dini na taasisi za kitaaluma kama wajumbe katika kamati hiyo;
3. Kamati Kuu inamshauri Rais aongeze masuala yafuatayo kwa ajili ya kuchunguzwa na Kamati katika hadidu za rejea za Kamati:
(i) Tuhuma za ukiukwaji mkubwa wa haki za binadamu dhidi wa wananchi waishio katika maeneo yenye migodi mikubwa ya madini;
(ii) Tuhuma za kuwepo kwa uchafuzi wa mazingira unaotishia afya za wananchi, viumbe hai na rasilimali za maeneo yenye migodi mikubwa ya madini kutokana na shughuli za uchimbaji unaofanywa na makampuni makubwa ya madini nchini;
(iii) Tuhuma za ufisadi na/au rushwa zinazohusiana na uandaaji na/au upitishwaji wa mikataba ya madini kati ya makampuni makubwa ya madini na viongozi na/au watendaji wa ngazi za juu wa serikali;
(iv) Mchango wa sekta ya madini kwa uchumi na maendeleo ya jamii ya wananchi waishio kwenye maeneo yenye migodi mikubwa ya madini.
4. Kamati Kuu inamtaka Rais kutoa hadharani na/au kwa wawakilishi wa kuchaguliwa wa wananchi Ripoti za Kamati za Uchunguzi zilizokwisha kuundwa na serikali kuchunguza matatizo mbalimbali ya madini ikiwemo Kamati ya Jenerali Mboma (2001), Kamati ya Brigedia Jenerali Mang'enya (2003), Kamati ya Dr. Kipokola (2004) na Kamati ya Masha (2006), ili wananchi wafahamu matokeo na mapendekezo ya Kamati hizo;
5. Kamati kuu inamtaka rais kuelekeza kwamba mikataba yote ya madini iliyoingiwa kati ya serikali na makampuni ya madini itolewe hadharani ili wananchi na wawakilishi wao wa kuchaguliwa waweze kufahamu yaliyomo katika mikataba hiyo;
6. Kamati Kuu inaridhia uteuzi na ushiriki wa Mheshimiwa Zitto Zuberi Kabwe katika Kamati ya Rais ya Uchunguzi wa Sheria na Mikataba ya Madini na inaahidi kufuatilia kwa karibu utekelezaji wa majukumu ya kamati hiyo;
7. Kamati Kuu inamtaka Rais atoe ahadi kwa Watanzania kwamba serikali yake itaitoa Ripoti ya Kamati ya Rais ya Uchunguzi wa Sheria na Mikataba ya Madini na kuyafanyia kazi mapendekezo yake;
8. Kamati Kuu inaagiza Sekretariati ya Makao Makuu ya Chama Taifa kuhakikisha kwamba Tamko hili linasambazwa kwa wananchi wa Tanzania kupitia vyombo vya habari na nakala zake kusambazwa katika ngazi zote za chama.
TAMKO HILI limetolewa kwa pamoja na Wajumbe wa Kamati Kuu na kusainiwa na Mwenyekiti wa Chama Taifa na Katibu Mkuu hapa Dar es Salaam leo hii tarehe 24 Novemba , 2007.
------------------------------------------------- ----------------------------------------
Freeman Aikaeli Mbowe
MWENYEKITI