CHADEMA - Tume Huru ya Uchaguzi na Uchaguzi wa Haki

BAVICHA Taifa

Senior Member
Jul 25, 2013
117
661
1. UTANGULIZI
Mipango ya nchi nyingi dunia inaendelea au inaparaganyika kutokana na uimara wa Katiba zinazoongoza nchi hizo. Katiba imara inatokana na kuwa na Chombo imara kinachosimamia uchaguzi wa kupata viongozi wake kwa kuanzia ngazi ya chini hadi ya juu.

Chaguzi nyingi duniani zinagubikwa na ghilba mbalimbali na baadae kutangazwa matokeo ya uongo na mifumo ya chaguzi inayohusika na hivyo kuwa ndio chanzo cha machafuko ya uharibifu wa miundombinu mikubwa, vita na umwagaji damu. Chadema mara zote imekuwa ikisisitiza umuhimu wa kuwa na Tume huru ya Uchaguzi kwa chaguzi zote zinazofanyika ili kuwa na mfumo imara na ulio na uhalali kwa wananchi wote.

Uchaguzi ni mchakato unaoanzia kwenye kutambua wapigakura na kuwaandikisha kwenye daftari la wapigakura, na ili uchaguzi uheshimike, sharti mchakato wake ufanyike kwa usahihi, weledi, bila upendeleo na uwazi, aidha ni muhimu kuwa wapiga kura wawe na imani nao. Hii inahitaji chombo na watendaji wake wenye uhuru kamili kwa matendo yao. Hicho chombo (Tume) kina wajibu wa kuhakikisha kuwa uchaguzi unaonekana kuwa huru na haki. Tume ihakikishe walioandikishwa kupiga kura, waliopiga kura na kura zilizopigwa vinahesabiwa kwa usahihi na haraka na karatasi au mfumo wa kidigitali vya kupigia kura siku zote vichukuliwe kama nyaraka muhimu.

Uhuru wa chombo cha kusimamia uchaguzi (Tume ya Uchaguzi) unatakiwa kuanzia katika upatikanaji wa watendaji wake wakuu na upatikaji wa rasilimali za kufanyia kazi sambamba na sheria na kanuni vinavyoongoza mchakato mzima wa chaguzi husika.

2. HISTORIA YA TUME HURU ZA UCHAGUZI
Wasilisho hili ni matokeo ya utafiti uliofanywa na Chama cha Demokrasia na Maenceleo (Chadema) kwa madhumuni ya kupata Tume ya Uchaguzi ya Taifa Tanzania ambayo ni huru ili iweze kusimamia kwa uhuru na haki chaguzi za urais, ubunge, udiwani na nafasi nyingine muhimu katika serikali za mitaa. Utafiti umefanya mapitio ya katiba, sheria na kanuni za uchaguzi za nchi zenye sifa ya chaguzi huru na haki duniani kama vile Marekani, India, Uingereza, Ghana, Kenya, Zambia, Australia na Afrika Kusini. Aidha imerejea makala muhimu, taarifa na tafiti zinazoainisha matatizo ya mifumo ya chaguzi na mapendekezo ya kuboresha ili kupata matokeo ya haki yatakayoepusha vita, migogoro na mitafaruku duniani. Mkazo umewekwa katika muundo wa Tume za uchaguzi zenyewe hususan wenyeviti na wajumbe wake, wakurugenzi, wasimamizi wa uchaguzi, wasajili na maafisa wengine muhimu katika mifumo ya uchaguzi. Aidha imezingatia sifa za wajumbe hao, muhula wa kazi na usalama wao, na fedha za kulipia shughuli za chaguzi kuhakikisha uhuru halisi wa mifumo hiyo ya uchaguzi.

3. HALI ILIVYO DUNIANI

Chaguzi nyingi duniani zinagubikwa na machafuko kama vita na umwagaji damu baada ya kutangazwa matokeo ya uongo na mifumo ya chaguzi inayohusika. Kwa mfano baada ya kupinduliwa kwa Rais wa kwanza wa Ghana Dr. Kwame Nkrumah kulifuatia tawala za kijeshi kwa miongo mingi kabla ya kurejea katika chaguzi za vyama vingi.

Hivyo katika jitihada za kuboresha mfumo wa uchaguzi nchi hiyo iliandaa Mpango Mkakati wa Tume ya Uchaguzi ya Ghana (Electoral Commission Ghana Strategic Plan) wenye madhumuni ya kuhakikisha chaguzi huru za kidemokrasia zenye kuaminika kwa viwango vya kimataifa. Lengo kuu ni kuwa na viwango vya juu vya weledi na uadilifu muda wote kuhakikisha kuwa mfumo wa uchaguzi hauingiliwi na yeyote na kwamba chaguzi zenyewe zinakuwa huru na haki. Aidha kutengeneza muamana na raia na wadau wengine.

Tangu kupotea kwa masanduku ya kura mwaka 2013 nchini Australia, Tume ya Uchaguzi ya Australia imejizatiti kuondoa udanganyifu na kuhakikisha uadilifu katika mfumo wake wa uchaguzi.

Tume hiyo ikasisitiza kuwa:

“Ili chaguzi ziheshimike, sharti zifanyike kwa usahihi, weledi, bila upendeleo na uwazi, aidha ni muhimu kuwa wapiga kura wawe na imani nao. Hii inahitaji wataalamu wenye uhuru kamili wa matendo yao. Tume ina wajibu kuhakikisha kuwa uchaguzi unaonekana kuwa huru na haki. Tume ihakikishe kura zilizopigwa zinahesabiwa kwa usahihi na haraka na karatasi za kupigia kura siku zote zichukuliwe kama nyaraka muhimu."

Tume ikasisitiza zaidi kuwa uadilifu una tafsiri pana zaidi inayojumuisha usimamizi wote wa mfumo wa uchaguzi.

Ikahitimisha kuwa:
“Matukio ya karibuni duniani kote yanadhihirisha jinsi gani dhana ya uadilifu katika uchaguzi ilivyo pana ... sharti iwe roho ya taratibu zote za chaguzi na ionyeshwe wakati wa uchaguzi.”

Mwaka 2015 Tume ya Uchaguzi ya India nayo ilichukua hatua za kuboresha mfumo wake wa uchaguzi.

Ibara ya 324(2) ya Katiba ya India inaeleza kuwa Tume ya uchaguzi ya India itakuwa na Mwenyekiti na idadi nyingine ya Makamishna wa Uchaguzi kama ambavyo Rais anaweza kuamua kadri inavyohitajika. Kwa amri aliyoitoa tarehe 10 Octoba 1993 Rais aliamua idadi ya makamishna kuwa wawili tu. Hoja ya kuwa na idadi ndogo ya makamishna nikuhakikisha utendaji rahisi na bora. Ilihofiwa idadi kubwa ingezuia utekelezaji wa chaguzi huru na haki.

Taarifa ya Tume hiyo ikasema kuwa kutokana na haja ya Tume kuwa haipendelei na kuwakinga Makamishna wa Tume kuingiliwa na serikali ni muhimu kuwa uteuzi wa maafisa wa uchaguzi unafanyika kwa ushauriano.

“Kwanza, uteuzi wa Makamishna wa Uchaguzi wote (pamoja na Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi) ufanywe na Rais kwa kushauriana na jopo la watu watatu au Kamati ya Uteuzi yenye Waziri Mkuu, Mkuu wa Upinzani au viongozi wa Chama Kikuu cha upinzani na Jaji Mkuu wa India.”

Lakini serikali ya India imesita kuyatelekeleza mapendekezo hayo.
Sifa za kuteuliwa makamishna wa uchaguzi hazijaainishwa na Katiba ya India wala Sheria ya Uwakilishi wa watu (Representation of the People Act) 1951. Masharti na muundo wa kazi wa Makamishna wa Uchaguzi vitaamuliwa na Rais.

Tume ya Uchaguzi ya Marekani (Federal Election Commission) inaundwa na Katibu wa Baraza la Senate na Karani wa Baraza la Wawakilishi (Congress) au wateule wao ambao watakuwa hawana haki ya kupiga kura, na wajumbe sita (6) walioteuliwa na Rais kwa kushauriana na kuridhiwa na Baraza la Senate. Chama kimoja hakiruhusiwi kuwa na zaidi ya wajumbe watatu (3).

Muhula wa kazi wa wajumbe wa Tume hiyo ya uchaguzi ni miaka sita (6) tu.

Sifa ya kuwa mjumbe wa Tume ni uadilifu, kutopendelea na kuwa na uamuzi makini. Tena wakati wa uteuzi wao hawatakiwi kuwa walikuwa maafisa wateule au wafanyakazi wa serikali, bunge au mahakama.

Pia wajumbe hawatakiwi kujihusisha na kazi au biashara nyingine yoyote baada ya kuchaguliwa. Masharti haya yanalenga kuhakikisha wajumbe wa Tume wanakuwa huru katika utendaji wao wa kazi.

Mwenyekiti na Makamu wa Tume watachaguliwa na wajumbe wa Tume yenyewe. Viongozi hao wakuu hawaruhusiwi kuhusiana na chama kimoja.

Tume ya Uchaguzi ya Zambia ina wajumbe watano ambao huteuliwa na Rais na kuidhinishwa na Bunge. Nao ni Mwenyekiti na Makamu wake na wajumbe wengine watatu.

Sifa ya kuwa mjumbe ni kuwahi kushika wadhifa wa ujaji au kuweza kuwa jaji wa Mahakama Kuu au ya juu. Itaonekana hapa kuwa idhini ya bunge itatolewa kutokana na wingi wa idadi ya wabunge. Kwa nchi nyingi za Afrika, kama Tanzania, Chama Tawala kitakuwa na uamuzi wa mwisho mintarafu wajumbe wa Tume ya Uchaguzi.

Pia kuna dhana potofu kuwa maafisa wa mahakama ndiyo wanastahili kuwa wajumbe wa Tume ya Uchaguzi kutokana na uadilifu wao.

Zambia pia ina Afisa Mkuu wa Uchaguzi ambaye atateuliwa na Tume ya Uchaguzi yenyewe. Wadhifa huu ni sawa na Mkurugenzi wa Uchaguzi Tanzania. Uzuri wa Zambia ni kuwa Tume ina mamlaka ya kumteua Afisa Mkuu wa Uchaguzi kinyume na Tanzania ambapo Mkurugenzi wa Uchaguzi huteuliwa na Rais. Afisa Mkuu wa Uchaguzi ndiye Afisa Mkuu Mtendaji wa Tume ambaye pamoja na majukumu mengine muhimu, atasimamia shughuli za kila siku za Tume.

Nchini Afrika Kusini, Tume Huru ya Uchaguzi ina wajumbe watano mmoja wapo akiwa Jaji wanaoteuliwa na Rais baada ya kupendekezwa na Bunge kufuatia uteuzi wa Kamati ya Vyama ya Bunge. Kamati hii ya vyama ya Bunge hupelekewa orodha ya wagombea wasiopungua nane baada ya kupendekezwa na Kamati ya Uteuzi yenye wajumbe wanne ambao ni Rais wa Mahakama ya Katiba, muwakilishi wa Tume ya Haki za Binadamu, mwakilishi wa Tume ya Jinsia na Usawa na Mkurugenzi wa Mashtaka.

Tukigeukia Canada, Mkuu wa Uchaguzi anateuliwa na azimio la Bunge la Makabwela (House of Commons) kwa muhula wa miaka kumi ambao hauwezi kuongezwa. Na ili kumpa uhuru, anawajibika moja kwa moja kwa Bunge, sio Serikali. Kutokana na uwiano wa wabunge wa vyama mbalimbali ndani ya Bunge lao, utaratibu huu ni mzuri kuliko ambako hakuna uwiano huo kama Tanzania.

Ushahidi nchini Uingereza unaonyesha kuwa hawana tatizo la wizi wa kura katika chaguzi zao. Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar ina wajumbe ambao ni

(a) Mwenyekiti atakayeteuliwa na Rais kwa utaratibu atakaoona uunafaa

(b) Wajumbe wawili watakaoteuliwa na Rais kufuatana na mapendekezo ya

Kiongozi wa shughuli za serikali kwenye Baraza la wawakilishi;

(c) Wajumbe wawili watakaoteuliwa na Rais kufuatana na mapendekezo ya Kiongozi wa Upinzani katika Baraza la Wawakilishi au iwapo hakuna kiongozi wa upinzani basi kwa kushauriana na vyama vya siasa;

(d) Mjumbe mmoja atakayeteuliwa na Rais kutokana miongoni mwa majaji wa Mahakama Kuu;

(e) Mjumbe mmoja atakayeteuliwa na Rais kama Rais atakavyoona inafaa.

Ibara hii inaonyesha kuwa wajumbe wote wa Tume pamoja na Mwenyekiti wake ni wateule wa Rais. Na ukiachia wajumbe walioteuliwa katika aya ya (b) na (c) wengine wote huteuliwa kadiri ambavyo Rais anavyoona inafaa. Baya zaidi ni kuwa kati ya wajumbe hao saba (7) upinzani unashirikishwa katika uteuzi wa wajumbe wawili(2) tu. Kwa kifupi Tume hii inawajibika zaidi kwa Rais kwa hiyo sio huru.

Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi atakuwa mtu aliyekuwa mwenye sifa za kuwa jaji wa Mahakama Kuu au Mahakama ya Rufaa katika nchi yoyote iliyo mwanachama wa Jumuiya ya Madola au mtu anayeheshimika katika jamii. Makamu wa Mwenyekiti atateuliwa na wajumbe wenzake. Tume itasimamia uchaguzi wa Rais, wajumbe wa Baraza la wawakilishi na viongozi wa serikali za mitaa.

Kutakuwa na Mkurugenzi wa Uchaguzi ambaye atateuliwa na Rais kutokana na majina yasiyopungua mawili yaliyopendekezwa na Tume ya Uchaguzi.
Mkurugenzi wa Uchaguzi atakuwa Katibu na Mtendaji Mkuu wa Tume.

Utagundua kuwa licha ya umuhimu wake mkubwa sana vyama vya upinzani haviwakilishwi katika uteuzi wake.
Kwa kila uchaguzi katika jimbo, Tume iteteua Msimamizi wa Uchaguzi na wasaidizi wake kusimamia chaguzi hizo.
Sifa za wasimamizi wa uchaguzi hazijawekwa bayana, zimeachwa mikononi mwa Tume.

Msimamizi wa Uchaguzi anaweza, kulingana na maelekezo ya Mkurugenzi wa Uchaguzi, kuteua watumishi kadiri anavyoona ni muhimu kwa utekelezaji wa uchaguzi katika jimbo.

Kenya ina Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka ambayo ina wajumbe wasiopungua watatu (3) na wasiozidi tisa (9). Utaratibu wa uteuzi wa Mwenyekiti, Makamu na wajumbe wake ni mrefu na shirikishi kwa aina yake kama ifuatavyo.

Mtu hawezi kuwa mjumbe wa Tume ya Uchaguzi ya Kenya endapo katika miaka mitano iliyopita alishika wadhifa au kugombea ubunge, uongozi wa chama cha siasa au utumishi wa seriMweny

Mwenyekiti na kila mjumbe wa Tume hiyo ataainishwa na kupendekezwa kwa uteuzi kwa namna itakayopendekezwa na sheria.
Rais wa Kenya atateua Jopo la Uteuzi la watu wanaostahili kuteuliwa kuwa Mwenyekiti au wajumbe wa Tume ya Uchaguzi. Jopo hilo ni la wafuatao: watu wanne, wawili wanaume na wawili wanawake, wateule wa Tume ya Huduma za Bunge (Parlimentary Service Commission); mtu mmoja mteule wa Muungano wa Mapadre Wakatoliki Kenya( Kenya Conference of Catholic Bishops) mtu mmoja mteule wa Baraza la Taifa la Makanisa ya Kenya (National Council of Churches of Kenya); mtu mmoja mteule wa Baraza Kuu la Waislamu wa Kenya (Supreme Council of Kenya Muslims), Umoja wa Kitaifa wa Viongozi wa Kiislamu (National Muslim Leaders Forum) na Baraza la Maimamu na Wahubiri Kenya (Council of Imams and Preachers of Kenya); mtu mmoja mteule wa Umoja wa Waevangelikali Kenya (Evangelical Alliance of Kenya); na mtu mmoja mteule wa Baraza la Wahindu Kenya (Hindu Council of Kenya).
Majina ya wateule wapendekezwa watano (5) kutoka asasi zilizotajwa hapo juu yatawasilishwa kwa Tume ya Huduma za Bunge (Parliamentary Service Commission) kwa minaajili ya uteuzi wa Rais kama Jopo la Uteuzi.
Tume ya Huduma za Bunge italipatia Jopo la Uteuzi Sekretariati kwa ajili ya shughuli zake

Ndani ya siku saba baada ya uteuzi wake Jopo la Uteuzi litaalika waombaji kutoka miongoni mwa watu wenye sifa na kuyachapa majina na sifa zao katika Gazeti la Serikali, magazeti mawili yenye mzunguko wa kitaifa na tovuti ya Tume ya Huduma za Bunge. Jopo hilo litafikiria orodha ya waombaji hao, litaipunguza na kuwahoji hadharani.

Baada ya kuwahoji na waombaji hao Jopo la Uteuzi litachagua watu wawili wenye sifa kuteuliwa kama Mwenyekiti na Makamu sita waliostahili kuteuliwa kama wajumbe wa Tume na kuyawasilisha kwa Rais kwa uteuzi wa mmoja kama Mwenyekiti na sita kama wajumbe wa Tume.

Ndani ya siku saba baada ya kupokea orodha ya majina ya waliopendekezwa atapeleka orodha ya wateule kwa ajili ya kuidhinishwa na Bunge.

Ndani ya siku saba baada ya kupokea majina yaliyoidhinishwa na Bunge, kwa taarifa ndani ya Gazeti la Serikali, Rais atawateua Mwenyekiti na wajumbe wengine wa Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka.

Mwenyekiti wa Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka sharti awe na sifa ya kuwa jaji wa Mahakama ya Juu. Na sio lazima awe ameshakuwa jaji kama ilivyo hapa Tanzania kama ilivyoelezwa hapo awali. Lakini wajumbe wa Tume wanatakiwa kuwa na shahada ya Chuo Kikuu kinachotambulika, wawe na ujuzi katika moja ya nyanja zifuatazo yaani masuala ya uchaguzi, utawala, fedha, uongozi, usimamizi wa umma au sheria. Sio lazima awe mtumishi wa serikali kama Tanzania.
Wajumbe wa Tume ya Uchaguzi watafanya kazi kwa muhula wa miaka sita tu na hawawezi kuteuliwa tena.

Tume itakuwa na Katibu wake ambaye atapatikana kutokana na njia ya wazi na ushindani. Nafasi hii inashabihiana na Mkurugenzi wa Uchaguzi Tanzania ambaye huteuliwa moja kwa moja na Rais bila uwazi wala ushindani, tena hutokana miongoni mwa watumishi wa serikali.

Katibu wa Tume anatakiwa kuwa na sifa zifuatazo: shahada ya Chuo Kikuu mashuhuri, awe na uzoefu wa utawala sio chini ya miaka mitano, na awe na uzoefu mwingine kama ule unaotakiwa kwa wajumbe wa Tume ulioelezwa punde tu hapo juu.

Kazi kubwa ya Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka, pamoja na mambo mengine ni kufanya na kusimamia kura za maoni na chaguzi za nafasi zozote zilizoainishwa na Katibu wa Bunge. Aidha itahakikisha usajili wa raia kama wapiga kura; mapitio ya kila mara ya daftari la wapinga kura na elimu ya wapiga kura.

Katibu atakuwa ndiye Mtendaji Mkuu wa Tume; mkuu wa Sekretariat na atatekeleza uamuzi wa Tume kadiri atakavyoelekezwa na Tume yenyewe. Katibu hatawajibika kwa yeyote bali Tume yenyewe. Anaweza kuondolewa madarakani na Tume yenyewe iwapo atashindwa kufanya kazi zake, kufilisika au tabia mbaya.

Tume inaweza kuajiri wafanyakazi wake kwa mujibu wa taratibu zake. Tunaamini wasimamizi wa chaguzi wanaweza kuajiriwa na Tume kwa utaratibu huu badala ya kutegemea watumishi wa serikali kama ilivyo Tanzania ambao dhahiri hupendelea serikali na chama tawala.

Uhuru wa Tume unalindwa na kifungu cha 26 cha Sheria ya Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka ambacho kinasema:

“Isipokuwa kama inavyoelezwa na Katiba, katika utekelezaji wa majukumu yake Tume haitapokea maelekezo au kudhibitiwa na mtu au mamlaka bali itatekeleza kanuni za ushirikishaji wa umma na matakwa ya kushauriana na wadau.”

Utaratibu wa kumuachisha au kumuondoa kazi mjumbe wa Tume ni mgumu sana.
Mtu anayetaka kumuondoa katika nafasi yake mjumbe wa Tume atawasilisha Hati ya Madai Bungeni akielezea sababu za kufanya hivyo. Bunge litajadili madai hayo na endapo itaona yanaonyesha sababu za msingi itapeleka Hati hiyo kwa Rais.

Baada ya kupokea malalamiko hayo Rais anaweza kumsimamisha kazi mjumbe huyo akisubiri matokeo ya malalamiko hayo kutoka Baraza Maalum ambalo litaongozwa na Mwenyekiti ambaye ni jaji au alipata kuwa jaji wa Mahakama Kuu, japo watu wawili ambao wanastahili kuteuliwa kuwa jaji wa Mahakama Kuu na mtu mmoja ambaye anaweza kuuchambua ushahidi wa kumuondoa mjumbe katika nafasi yake. Baraza hilo litachunguza malalamiko hayo haraka na kuwasilisha mapendekezo yasiyopingika (binding) kwa Rais ambaye atachukua hatua zilizopendekezwa ndani ya siku thelathini.

4.0 TUME YA UCHAGUZI YA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA

Kwa kuzingatia ibara ya 74(1) na (2) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977, ikisomwa pamoja na kifungu cha 4(1) cha Sheria ya Taifa ya Uchaguzi, Sura ya 343, Tume inaundwa na Wajumbe saba. Wajumbe hao ni Mwenyekiti na Makamu Mwenyekiti ambao wanapaswa kuwa na sifa ya Jaji wa Mahakama Kuu au Mahakama ya Rufani au mtu mwenye sifa ya kuwa Wakili na amekuwa na sifa hizo kwa muda usiopungua miaka 15. Katika uteuzi wao, Rais atazingatia kuwa endapo Mwenyekiti ni mtu anayetoka sehemu moja ya Muungano, Makamu Mwenyekiti na wajumbe wengine wanaotajwa na Sheria iliyotungwa na Bunge.

Mjumbe mwingine atateuliwa kutoka miongoni mwa wanachama wa Chama cha Wanasheria Tanganyika (Tanganyika Law Society - TLS). Wajumbe wanne watatakiwa wawe na uzoefu wa kutosha wa kuendesha au kusimamia uchaguzi wa Wabunge au sifa nyingine kama ambavyo Rais wa Jamhuri ya Muungano atakavyoona inafaa kwa utekelezaji wa majukumu ya Tume. Kiutendaji wakati wa uchaguzi, mamlaka ya Tume hutekelezwa na Wakurugenzi wa Majiji, Manispaa, Miji na Halmashauri za Wilaya na watendaji mbali mbali walio chini yao. Hii ni kwa mujibu wa Sheria ya Uchaguzi wa Taifa.

Mkuu wa Tume ya Uchaguzi ndiye Mkurugenzi wa Uchaguzi ambaye huteuliwa na kufanya kazi kwa mujibu wa masharti ya Sheria iliyotungwa na Bunge. Sheria yenyewe ni Sheria ya Taifa ya Uchaguzi.

Ikumbukwe kuwa Sheria hii imetokana na Sheria ya Uchaguzi ya mwaka 1970, ambayo ilifanyiwa marekebisho mwaka 1985 na hatimaye Juni 30, 2010. Ndiyo kusema kuwa kimsingi sheria hii ilikuwa kwa ajili ya chaguzi za chama kimoja ingawa inadaiwa kufanyiwa mabadiliko kukidhi haja ya chaguzi za vyama vingi vya siasa.

Mkurugenzi wa Uchaguzi ambaye ndiye Mtendaji Mkuu wa Tume ya Uchaguzi, huteuliwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Wasimamizi wa Uchaguzi ni Wakurugenzi wa Jiji, Wakurugenzi wa Manispaa, Wakurugenzi wa Miji na Wakurugenzi Watendaji wa Wilaya. Na Tume yenyewe pia inaweza kuteua idadi ya maafisa wengine kuwa wasimamizi wa uchaguzi au wasaidizi wa wasimamizi wa uchaguzi. Izingatiwe hapa kuwa maafisa hao wanaweza kuchaguliwa na Tume kama ni waajiriwa wa umma, yaani serikali.

Aidha kila Mkurugenzi wa Jiji, Mkurugenzi wa Manispaa, Mkurugenzi wa Mji na Mkurugenzi Mtendaji wa Wilaya watakuwa Maafisa Waandikishaji wa chaguzi nchini. Na Tume yenyewe pia imepewa mamlaka ya kuteua idadi yoyote ya maafisa wa serikali kuwa wandikishaji wasaidizi wa uchaguzi.

Na mwisho, Tume yenyewe inaweza wakati wowote wa uchaguzi kumteua afisa yeyote wa serikali kuwa Mratibu wa Uchaguzi wa Mkoa.

Kwa hiyo basi wajumbe wote wa Tume ya Uchaguzi ya Taifa, yaani Mwenyekiti, Mkurugenzi wa Uchaguzi, makamishna na maafisa wote muhimu wa Tume huteuliwa na Rais wa nchi. Muhimu kupita yote ni kuwa watumishi wote sharti wawe wanatoka serikalini.

Kifungu cha 7(1)(5) cha Sheria ya Taifa ya Uchaguzi mintaarafu Wasimamizi wa Uchaguzi, wasaidizi wao na wafanyakazi wengine chini yao ni sawa kabisa na kifungu cha 9 (1)-(5) Sheria ya Uchaguzi wa Serikali za Mitaa.

Isipokuwa kifungu cha 9(6) cha Sheria ya Uchaguzi wa Serikali za Mitaa kinasema kuwa:

“Bila kujali masharti ya kifungu kidogo (1), Tume inaweza, iwapo inahitajika, kwa Tangazo lililochapishwa katika Gazeti la Serikali, kumteua mtu yeyote kwa jina au ofisi kuwa Msimamizi wa Uchaguzi kwa ajili ya serikali ya mtaa yoyote badala ya yule aliyetajwa katika kifungu cha (1) na iwapo mtu huyo atateuliwa Mkurugenzi wa Jiji, Mkurugenzi wa Manispaa, Mkurugenzi wa Mji au Mkurugenzi Mtendaji wa Mji au Mkurugenzi Mtendaji Wilaya, ataacha kuwa Msimamizi wa Uchaguzi wa serikali ya mtaa inayohusika.”

Neno ‘any person’ lililotumika katika kifungu hiki ina maana kuwa Msimamizi wa Uchaguzi anaweza asiwe mtumishi wa serikali. Lakini ukweli ni kuwa jambo hili haliwezekani kwa mujibu wa Kanuni za Uchaguzi wa Rais na Wabunge, 2010 na kanuni ya 9 ya Kanuni za Uchaguzi za Serikali za Mitaa, 2010 ambazo zinawataka kuwa watumishi wa serikali.

Rais wa Jamhuri ya Muungano Tanzania anaweza kumuondoa katika madaraka mjumbe yeyote wa Tume ya Uchaguzi akipenda kufanya hivyo. Kwa hiyo basi Rais wa Chama Tawala ndiye mteuzi mkuu, mdhibiti na mnadhimu wa wajumbe, watendaji wakuu na hata wafanyakazi wote wa Tume ya Uchaguzi.

Ripoti ya Tume ya Jaji Nyalali ya mwaka 1991 ndiyo ilipendekeza kurejesha demokrasia ya vyama vingi nchini Tanzania. Lakini ilisisitiza haja ya kuwa na demokrasia ya kweli ya vyama vingi. Vinginevyo ni uwezekano wa kuanzishwa kwa utitiri wa vyama pandikizi vya kisiasa kuzuga watu wa Tanzania kwamba kuna demokrasia ya vyama vingi wakati sio kweli.

Tume hiyo ilitoa mfano wa nchi nyingi za aina hiyo kama vile Senegal. Hatari yake ni mauaji, machafuko na kudidimia kwa ustawi wa nchi. Watu wakijua kuwa chaguzi zinazo fanywa na nchi zao ni feki basi lazima kutazuka fujo ambayo haijulikani itaishia wapi. Mfano mzuri ni mauaji ya Pemba katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2000 nchini Tanzania, Kenya na Zimbabwe mwaka 2008. Hivyo basi Tume ya Jaji Nyalali ilisisitiza kuwa muundo wa Tume ya Uchaguzi ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ubadilike ili kukidhi haja ya demokrasia ya vyama vingi. Ili kuhakikisha kuwa Tume hiyo inakuwa huru Ripoti hiyo ilipendekeza:

“Mwenyekiti na wajumbe wa Tume ya Uchaguzi sharti wachaguliwe na Bunge au Baraza la Wawakilishi... wakurugenzi wa uchaguzi ambao watakuwa ni makatibu wa Tume ya Uchaguzi nao sharti wachaguliwe na Baraza la Wawakilishi baada ya kupendekezwa na Tume Ajiri zinazohusika.”

Ni dhahiri mapendekezo hayo ya Tume ya Jaji Nyalali yalizingatia kuwa uchaguzi wa vyama vingi sharti uendeshwe kwa viwango vinavyokubalika kisheria na kimataifa duniani kote. Mathalani Tamko la Dunia kuhusu Haki za Binadamu la mwaka 1948 linasisitiza kufanyika kwa uchaguzi wa kweli ulio huru na haki. Na msemo maarufu labda kupita yote mintaarafu haki za binadamu duniani kote ni kuwa, “Haitoshi kwamba haki inatendeka, sharti ionekane kuwa inatendeka.”

Mwaka 1999 iliundwa Kamati ya Kuratibu Maoni kuhusu Katiba iliyoongozwa na Jaji Rufani (marehemu) Robert Kissanga. Hoja ya kumi na moja iliyowasilishwa mbele ya Kamati hiyo ilidai:

“Kwamba muundo wa Tume ya Uchaguzi hauzingatii uwakilishi wa vyama vya siasa na kwamba wajumbe wa Tume huteuliwa na Rais ambae pia anaweza kuwa ni kiongozi wa chama cha siasa kinachotawala. Kwa sababu hiyo, wajumbe wa Tume katika utendaji wa kazi zao, ama watakuwa na upendeleo kwa chama husika au watakuwa wanalipa fadhila kwake. Wanaotoa hoja hii wanapendelea kwamba kuwe na ama uwakilishi wa vyama vya siasa, ama kuwe na chombo kitakachochuja majina ya wajumbe wa Tume kabla Rais hajawateua.”

Ikumbukwe kwamba hoja hii inakaribiana na mapendekezo ya Tume ya Jaji Nyalali ambayo tumeyajadili kabla. Maoni ya serikali mintarafu hoja hiyo ya kumi na moja yalikuwa kama ifuatavyo:

“ ... kwamba ili Tume ya Uchaguzi iweze kutekeleza majukumu yake bila woga wala upendeleo, inapaswa kuwa ya kitaalamu au yenye wajumbe wenye hadhi, wanaokubalika na ambao uteuzi wao hautazingatia mwelekeo wa siasa wa chama chochote. Muundo wa sasa wa Tume unazingatia sifa hizo na serikali inaona muundo huo uendelee.”

Kisha serikali ilihitimisha maoni yake kuhusu hoja hiyo kwa kudai kwamba:

“Kwa upande wa uteuzi wa Tume (ya uchaguzi) serikali inaona kwamba Rais ambaye ana dhamana kubwa kikatiba ya kuwateua hata majaji, aendelee kuwateua wajumbe wa Tume.”

Hakika majibu ya serikali kupinga hoja iliyotolewa ni chapwa na hayana mashiko kwa sababu kuu mbili. Kwanza sio kweli kuwa uteuzi wa wajumbe wa Tume kwa mazingira yaliyopo hauzingatii mwelekeo wao wa kisiasa. Ukweli ni kuwa wateule hao watakuwa na shauku ya wazi au siri kulinda maslahi yao hususan ya yule aliyewateua. Ni fadhila kati ya vidole na kinywa! Kinywa kamwe hakiwezi kuving’ata vidole vinavyokula chakula! Abadani. Hakika dhama hii inatambulika kisheria. Pili, kuwa na dhamana ya kuwateua majaji hakumfanyi Rais wa Tanzania kukaribiana na malaika asiyetaka kulinda maslahi yake!

Baada ya kukusanya maoni ya watu waliohojiwa na Kamati hiyo na kuyatafakari hatimaye Kamati ilitoa mapendekezo yafuatayo kwa serikali:
“Rais ateue wajumbe wa Tume kwa kushauriana na Bunge kwa utaratibu ufuatao:

(i)Rais aandae orodha ya majina ya watu anaotarajia kuwateua na kuiwasilisha Bungeni.
(ii)Orodha hiyo itajadiliwa na Bunge.
(iii)Baada ya hapo majina hayo yatarudishwa kwa ajili ya uteuzi wa wajumbe.”

Sisi hatuamini kuwa hata mapendekezo haya ya Kamati ya Jaji Kisanga yangehakikisha uhuru wa Tume ya Uchaguzi ya Taifa kwa sababu hayajakidhi maslahi na utashi wa vyama vya upinzani katika bunge ambalo limejaa wabunge wa chama tawala. Lakini afadhali yalikubali kuwepo kwa uwezekano wa upendeleo na kutaka kuhusishwa kwa Bunge katika uteuzi wa majina ya wajumbe wa Tume. Itakumbukwa pamoja na ukweli huo, jazaa na mapendekezo yale ya Jaji Kissanga na wajumbe wenzake ni kudhalilishwa kwao hadharani na Rais Mkapa wakati akipokea na kuzungumzia taarifa hiyo.

5.0 TUME YA UCHAGUZI KATIKA RASIMU YA KATIBA YA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA

Tume ya Mabadiliko ya Katiba, maarufu kama Tume ya Warioba ilipendekeza kuwe na Tume Huru ya Uchaguzi.
Tume hiyo itakuwa na Mwenyekiti, Makamu Mwenyekiti na wajumbe wengine saba watakaoteuliwa na Rais baada ya kupendekezwa na Kamati ya Uteuzi.Na watashika madaraka baada ya kuthibitishwa na Bunge.

Mwenyekiti na Makamu Mwenyekiti wa Tume hiyo watakua na sifa zifuatazo: awe mtu aliyewahi kushika madaraka ya Jaji wa Mahakama ya Juu, Mahakama ya Rufani na Mahakama Kuu kwa kipindi kisichopungua miaka mitano. Awe muaminifu, muadilifu na mwenye mwenendo usiotiliwa shaka na jamii. Na awe hajawahi kushika madaraka ya chama cha siasa.

Mjumbe wa Tume hiyo anatakiwa awe muadilifu, muaminifu na mwenendo usiotiliwa shaka na jamii. Awe hajashika nafasi yoyote katika chama cha siasa. Na awe na shahada.

Wajumbe wa Baraza la wa Wakilishi, madiwani na watumishi wa umma hawawezi kuwa wajumbe wa Tume.

Kutakuwa na Kamati ya Uteuzi wa Mwenyekiti, Makamu Mwenyekiti na wajumbe wa Tume itakayokuwa na wajumbe wafuatao: Jaji Mkuu wa Jamhuri ya Muungano ambaye atakuwa Mwenyekiti; Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano ambaye atakuwa Makamu Mwenyekiti; Spika wa Baraza la Wawakilishi la Zanzibar; Spika wa Bunge la Tanganyika; Jaji Mkuu wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Tume ya Maadili ya Uongozi na Uwajibikaji.

Kamati ya Uteuzi itakuwa na jukumu la kupokea na kuchambua majina ya watu walioomba na kupendekezwa kuwa wajumbe wa Tume.

Kwa kuzingatia masharati ya ibara ndogo ya (3)b Kamati ya Uteuzi mara baada ya kuchambua majina ya watu walioomba na waliopendekezwa kuwa wajumbe wa Tume itapeleka kwa Rais majina ya watu wanaofaa kuteuliwa kuwa wajumbe.
Rais atateua Mwenyekiti, Makamu Mwenyekiti wa wajumbe wa Tume kutoka miongoni mwa majina yaliyowasilishwa na Kamati ya Uteuzi na atawasilisha majina hayo Bungeni kwa ajili ya kuthibitishwa na Bunge.

Asasi za kiraia na zisizo za kiserikali zinaweza kupendekeza majina ya watu wanaoweza kuteuliwa kuwa Mwenyekiti, Makamu Mwenyekiti na wajumbe wa Tume. Kwa hiyo jukumu kubwa la wanaofaa kuwa Mwenyekiti, Makamu Mwenyekiti na wajumbe wa Tume ya Uchaguzi liko mikononi mwa Kamati ya Uteuzi ambayo kwa hali ya kisiasa ilivyo sasa wote ni wateule wa Rais au wanatoka Chama tawala kama vile Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano na Baraza la Wawakilishi la Zanzibar. Bila shaka yeyote watapenyeza majina ya watu watakaopendelea serikali na Chama Tawala. Nyadhifa zao hazitoshi kuwatakasa kuwa watakatifu. Tunarejea palepale, kuwa haitoshi haki kutendeka, sharti ionekane inatendeka. Hakuna atakayewaamini wajumbe hawa wa Kamati ya Uteuzi kutopendelea katika uteuzi wao.

Mjumbe wa Tume ya Uchaguzi atashika nafasi yake kwa kipindi cha miaka mitano na anaweza kuteuliwa tena kwa kipindi kingine kimoja cha miaka mitano.
Wajibu wa Tume Huru ya Uchaguzi ni kusimamia na kuendesha shughuli zote za uchaguzi wa wabunge na Rais; kusimamia na kuendesha kura ya maoni; kusimamia na kuratibu uandikishaji wa wapiga kura; na kugawa na kutangaza majimbo ya uchaguzi wa wabunge.

Katika kutekeleza madaraka yake Tume haitalazimika kufuata amri, maagizo au maoni ya mtu yeyote, mamlaka yoyote ya serikali, chama cha siasa, taasisi au asasi yoyote. Ukweli hii ni dhana tupu kwa sababu Tume ya Uteuzi na Rais ambaye hatimaye huteua Mwenyekiti na Makamu wake na wajumbe wa Tume ya Uchaguzi ni watendaji wakuu wa serikali au wa CCM ambao sharti watakuwa na haja ya kulinda na kutetea maslahi ya Chama Tawala. Kinywa haking’ati vidole vinavyokilisha, aslani!

Watu wanaohusika na uchaguzi hawaruhusiwi kujiunga na chama chochote cha siasa isipokuwa watakuwa na haki ya kupiga kura. Kiuhalisia kwa hali ya sasa wote wanaohusika na mfumo wa uchaguzi ni watumishi wa serikali au wana mwelekeo wa kukipendelea chama tawala.

Tume itakuwa na Mkurugenzi wa Uchaguzi atakayeteuliwa na Rais baada kupendekezwa na Tume ya Utumishi wa Umma na kuthibitishwa na Bunge.
Sifa za Mkurugenzi wa Uchaguzi ni mtu muaminifu, muadilifu, na mwenendo usiotiliwa shaka na jamii; awe hajawahi kushika nafasi ya madaraka yoyote katika chama cha siasa na awe na shahada. Mkurugenzi wa Uchaguzi atakua ndiye Msimamizi na Mtendaji Mkuu wa shughuli ya kila siku za Tume ya Uchaguzi kuhusiana na masuala ya uchaguzi, uandikishaji wa wapiga kura na uendeshaji wa kura za maoni. Atatekeleza majukumu yake kwa kusaidiwa na watendaji ambao ni watumishi wa umma kwa kadiri ya idadi inayowajibika.

Hatari iliyopo hapa ni kuwa watumishi wote wa Tume hasa wasimamizi na waandikishaji wa uchaguzi ni watendaji muhimu serikalini ambao huwajibika moja kwa moja kwa Rais aliyewateua na Chama Tawala.

Inadaiwa kuwa katika kutekeleza majukumu yake Mkurugenzi huyo atawajibika kwa Tume ya Uchaguzi. Inawezekana ikawa hivyo kimuundo, kiuhalisia atawajibika zaidi kwa Rais aliyemteua.

Isemwe hapa kwa muhtasari tu kwamba mapendekezo ya Tume ya Warioba kuhusiana na uteuzi wa watendaji wa Tume ya Uchaguzi yanashabihiana na yale ya Tume ya Jaji Nyalali na baadaye Jaji Kissanga kwa kutaka kulihusisha Bunge na Baraza la Wawakilishi. Kama itavyoelezwa hapo baadaye,Bunge la Jamhuri ya Muungano lilikataa mapendekezo hayo.

6.0 TUME YA UCHAGUZI KATIKA KATIBA INAYOPENDEKEZWA

Itakumbukwa kuwa Katiba Inayopendekezwa ilipitishwa na Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambalo lilibaki na idadi kubwa ya wabunge baada ya wale wa Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA) kususia vikao vya Bunge hilo.

Ibara nyingi zilizopendekezwa na Rasimu ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano zilibakia kama zilivyo isipokuwa chache muhimu zilibadilishwa kama ifuatavyo.

Kwanza ibara ya 190 (3) ya Rasimu ya Katiba ilisomeka kama hivi:
“Mwenyekiti, Makamu Mwenyekiti na wajumbe wa Tume Huru ya Uchaguzi watashika madaraka mara baada ya kuthibitishwa na Bunge.”

Lakini ibara ya 217 (3) ya Katiba Inayopendekezwa inasomeka kama ifuatavyo:

“Mwenyekiti, Makamu Mwenyekiti na wajumbe wa Tume Huru ya Uchaguzi watashika madaraka mara baada ya kuapishwa na Rais.”

Kwa hiyo ni dhahiri sharti la kuthibitishwa na Bunge kwa wajumbe hao kabla ya kuapishwa na Rais limeondolewa kabisa.

Ibara ya 190 (5)(e) ya Rasimu inasomeka:

“Mwenyekiti na Makamu Mwenyekiti wa Tume Huru watakuwa na sifa zifuatazo:

(e) awe ni mtu ambaye hajawahi kutiwa hatiani kwa kosa lolote la jinai linalohusiana na udanganyifu.”

Lakini ibara ya 217(5)(e) ya Katiba Inayopendekezwa inataka:

“awe ni mtu ambaye hajawahi kutiwa hatiani kwa kosa lolote la jinai.”

Ina maana hata mtu ambaye kwa bahati mbaya anatiwa hatiani kwa kumtukana mwingine hawezi kugombea nafasi hizo. Huku ni kutafuta malaika, sio viongozi wanadamu!

Sifa hii pia inarejewa kwa wajumbe wa Tume.

Pia kuna mabadiliko makubwa katika ibara ya 191(1) ya Rasimu inayosema kuwa:

“Kutakuwa na Kamati ya Uteuzi wa Mwenyekiti, Makamu Mwenyekiti na wajumbe wa Tume Huru ya Uchaguzi itakayokuwa na wajumbe wafuatao:

(a) Jaji Mkuu wa Jamhuri ya Muungano ambaye atakuwa ni Mwenyekiti
(b) Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano ambaye atakuwa Makamu Mwenyekiti
(c) Spika wa Baraza la Wawakilishi la Zanzibar
(d) Spika wa Bunge la Tanganyika
(e) Jaji Mkuu wa Tanganyika
(f) Jaji Mkuu wa Zanzibar; na
(g) Mwenyekiti wa Tume ya Maadili ya Uongozi na Uwajibishaji.

Lakini ibara ya 218(1) ya Katiba Inayopendekezwa inasema kuwa Kamati ya Uteuzi itakuwa na wajumbe wafuatao:

(a)Jaji Mkuu wa Jamhuri ya Muungano ambaye atakuwa ni Mwenyekiti
(b)Jaji Mkuu wa Zanzibar ambaye atakuwa Makamu Mwenyekiti
(c)Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano
(d)Spika wa Baraza la Wawakilishi la Zanzibar
(e)Jaji Kiongozi; na
(f)Mwenyekiti wa Tume ya Maadili ya Viongozi wa Umama

Aidha ibara ya 191(5) ya Rasimu imefanyiwa mabadiliko na ibara ya 218(5) ya Katiba Inayopendekezwa. Rasimu ilipendekeza majina ya wajumbe wa Kamati ya Uteuzi yaidhinishwe na Bunge kabla ya kuteuliwa na Rais. Lakini Katiba Inayopendekezwa inaondoa sharti hilo.

Ibara ya 195(1) ya Rasimu pia imefanyiwa mabadiliko na ibara ya 222(1) ya Katiba Inayopendekezwa ambayo Mkurugenzi wa Uchaguzi atateuliwa moja kwa moja na Rais bila kupendekezwa na Tume ya Utumishi wa Umma na kuthibitishwa na Bunge.

Aidha Mkurugenzi anatakiwa awe ni mtu ambaye hajawahi kutiwa hatiani kwa kosa lolote la jinai badala ya lile ambalo linahusiana na uaminifu kama ilivyopendekezwa.

7.0 PENDEKEZO KUTOKA KWENYE TAASISI NA WATU WENGINE

7.1. Taasisi ya uangalizi wa uchaguzi mkuu mwaka 2020- tanzania election watch-tew
Miongoni mwa mapendekezo yaliyotolewa na waangalizi wa uchaguzi mkuu wa mwaka 2020 ni pendekezo la kwamba vyombo vinavyosimamia uchaguzi kupewa uhakika wa kazi zake kikatiba, upatikanaji wa makamishna wa tume kuwa shirikishi na wao kutokuwa na upande wanaohegemea, aidha makamishina kuwa huru kuchagua secretariat yake sambamba na kuchagua watendaji wao kwa vigezo vyao vilivyo huru na hivyo kuwa na uwezo wa kuwawajibisha kulingana na taratibu zao za uajili.

7.2. Jaji Mstaafu Damiani Lubuva
Kwa mujibu wa tovuti ya Tume ya Uchagu, taarifa iliyowekwa August 28, 2017- inasomeka kuwa;

“Jaji Lubuva amesema kuwa uhuru wa Tume ambao Wananchi wengi wamekuwa wakiuzungumzia ni fikra tu za mtu anavyodhani juu ya namna Tume iundwe na si utendaji halisi wa Tume namna inavyotekeleza majukumu yake.
Ili kuondoa dhana hiyo, Tume ya Taifa ya Uchaguzi imependekeza katika katiba inayopendekezwa kuwa mfumo wa kuwapata Wajumbe wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi ufanyiwe marekebisho ili kuwapata wajumbe kwa njia tofauti na ilivyo sasa.

Hata hivyo Jaji Lubuva ameshauri kuwa, Wajumbe wanaounda Tume ya Taifa ya Uchaguzi wasitokane na itikadi za vyama vya siasa ili kuepusha mgongano wa kimaslahi ambao unaweza kujitokeza katika utekelezaji wa majukumu hasa wakati wa kufanya maamuzi.”

Hayo ni maoni ya aliyekuwa Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi, na ni dhahiri kuwa wajumbe wa Tume wamekuwa wakifanyakazi kwa kusukumwa na Itikadi za vyama vyao na hivyo kuinyima Tume uhalali wa kutenda kazi zao kwa uhuru na badala yake kugubikwa na mgongano wa maslahi miongoni mwa wajumbe na watendaji.

7.3. Mapendekezo toka Tume ya Taifa ya Uchaguzi
Ili kuboresha uendeshaji wa uchaguzi, Tume inapendekeza yafuatayo: -
i. itungwe sheria ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi ambayo itaiwezesha Tume kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi zaidi;
ii. Kuwe na watendaji wa Tume hadi ngazi ya halmashauri;
iii. mamlaka husika ziangalie uwezekano wa kuunganisha Sheria ya Taifa ya Uchaguzi, Sura ya 343 na Sheria ya Uchaguzi ya Serikali za Mitaa, Sura ya 292 ili kurahisisha utekelezaji wa sheria hizo;
iv. Sheria za uchaguzi zitafsiriwe kwa lugha ya Kiswahili; na
v. Serikali iangalie uwezekano wa kuziwezesha kifedha asasi na taasisi zinazotoa elimu ya mpiga kura katika hatua mbalimbali za mchakato wa uchaguzi.

8.0. MTAZAMO NA MAPENDEKEZO YA CHADEMA KUHUSU TUME HURU NA UCHAGUZI WA HAKI
Utafiti huu umedhihirisha kuwa kuna mifumo miwili mikuu kusimamia chaguzi za kidemokrasia duniani. Mfumo katika muktadha huu ni Katiba, sheria na kanuni zinazosimamia chaguzi hizo. Chombo kikuu katika mifumo hiyo ni Tume za Uchaguzi.

Tume za Uchaguzi za aina ya kwanza ni zile ambazo watendaji wake wote wakuu huteuliwa na kiongozi wa nchi ambaye aghalabu ni Mwenyekiti wa chama tawala kama ilivyo Tume ya Uchaguzi ya Taifa Tanzania. Tume hizi hazina sifa ya kusimamia chaguzi huru na haki kama ilivyoainisha Ripoti ya Jaji Francis Nyalali na baadaye Jaji Robert Kissanga.
Aina ya pili ni zile Tume za Uchaguzi shirikishi kwa maana ya kuwa uteuzi wa watendaji wake wakuu unahusisha kwa kiasi kikubwa au kidogo cha ushirikishaji wa wadau wakuu wa chaguzi. Ikumbukwe kuwa wadau wakuu wa kwanza wa chaguzi ni wapiga kura wenyewe ambao wanataka kuona kuwa hakuna ghiliba katika kura wanazopiga. Hawatangaziwi matokeo ya uongo! Wa pili ni wawakilishi wa wapiga kura yaani vyama vya siasa. Wapiga kura ni wanachama wa vyama hivyo au raia tu wanaopiga kura katika mchakato wa demokrasia kupata viongozi wanaowafaa.
Watendaji wakuu wa aina hii ya pili ya Tume huteuliwa na kiongozi mkuu wa nchi lakini sharti wapate ridhaa ya Bunge.

Dhana kuu hapa ni kuwa Bunge huwakilisha maslahi mapana ya wapiga kura na raia wote wa nchi husika. Tatizo ni kuwa aghalabu dhana hii ni potofu kwa vile mabunge mengi katika dunia ya tatu na demokrasia changa hutoka chama tawala tu. Hawa daima hulinda maslahi finyu ya vyama vyao. Dhana hii inafanya kazi nzuri katika demokrasia pevu mathalan Canada kama ilivyoainishwa katika utafiti huu.

Wakati mwingine kunafanyika jitihada dhahiri kuhakikisha uteuzi wa viongozi hao hupitia katika mchakato shirikishi na wazi. Hapa huwa kuna Kamati Teule ambazo husimamia uteuzi na mapendekezo ya viongozi wakuu na wajumbe wa Tume za Uchaguzi. Mfano mzuri ni Kenya.
Utaratibu wa ushirikishi mwingine ni ule unaovihusisha vyama vya upinzani katika uteuzi wa viongozi wa Tume za Uchaguzi. Mathalan Tume ya Uchaguzi ya India imetoa mapendekezo kumtaka Kiongozi wa nchi ateue watendaji wakuu wa Tume baada ya kupata ridhaa ya kiongozi wa chama kikuu cha upinzani nchini. Mapendekezo haya bado hayajafanyiwa kazi na serikali ya India.

Utaratibu mwingine ni ule unaoruhusu vyama vikuu vya siasa kuwa na watendaji wakuu katika Tume za Uchaguzi. Hii hukata mzizi wa fitina wa kupinga matokeo ya chaguzi kwa vile wote watakuwa wanashiriki katika hatua zote muhimu za uchaguzi kama vile aina ya karatasi na maboksi ya kupiga kura, usajili wa wapiga kura, mgao wa ruzuku na ulinzi katika mchakato wa upigaji kura. Utaratibu huu umetumika kwa mafanikio makubwa Marekani.

Watendaji wakuu wa Tume hufanya kazi kwa muhula mmoja tu kuepuka mazoea na uwezekano wa upendeleo.Na hawawezi kuachishwa kazi kwa utashi wa kiongozi wa nchi tu ila kwa utaratibu madhubuti utakaotenda haki.

Sheria na kanuni za uchaguzi zinatakiwa kuzipa Tume mamlaka ya wazi kuajiri watumishi wake kusimamia mfumo wote wa uchaguzi ambao sio watumishi wa serikali kuepuka upendeleo.
Kwa utaratibu huu Tume itakuwa daima na watumishi wake nchi nzima bila kutegemea watendaji wachache wakuu Makao Makuu ya Tume Dar es Salaam.
Tume inahakikishiwa fedha za kutosha (aghalabu kutoka (consolidated Fund) kutekeleza majukumu yake bila ya kutegemea huruma ya Serikali Kuu.
Kwa kulingana na utafiti huu Chadema tunapendekeza Tanzania iwe na Tume Huru ya Uchaguzi ya Taifa itakayofuata mfumo shirikishi wa pili, kwani mazingira ya digitali yalivyo sasa na Dunia inakoelekea itakuwa ni rahisi sana wananchi kushiriki katika kila jambo kama fursa itatolewa ya wao kushiriki.

Tukumbuke kuwa uchaguzi ni mali ya wananchi na hivyo ushiriki wao katika kila hatua ni muhimu sana katika upatikanaji wa maendeleo endelevu.

9.0. MAENEO YA KATIBA NA SHERIA YA UCHAGUZI YANAYOHITAJI MAREKEBISHO KUHUSU TUME

a) Ibara ya 74(1) inayompa Rais wa Jamhuri ya Muungano mamlaka ya kuteua Mwenyekiti, Makamu Mwenyekiti na Wajumbe wa Tume.

b) Ibara ya 74(5) inayompa Rais mamlaka ya kumwondoa madarakani mjumbe yeyote wa Tume kwa sababu ya kushindwa kutekeleza kazi zake, ama kutokana na maradhi au kwa sababu yoyote au kwa tabia mbaya au kwa kupoteza sifa za kuwa mjumbe.

c) Ibara ya 74(12) inayonyang'anya Mahakama mamlaka ya kuchunguza jambo lolote lililofanywa na Tume katika kutekeleza madaraka yake.

d) Ibara ya 75 (1) na (2) inayoizuia Tume kugawa majimbo ya uchaguzi na kuweka mipaka yake bila kupata kibali cha Rais.
e) Ibara ya 75 (6) inayokataza Mahakama kuchunguza jambo lolote lililofanywa na Tume katika kutekeleza madaraka yake ya kugawa majimbo ya uchaguzi na kuweka mipaka yake.

f) Ibara ya 74(7) ikisomwa pamoja na kifungu cha 6 (1) cha Sheria ya Uchaguzi inayompa Rais mamlaka ya kuteua Mkurugenzi wa Uchaguzi, ambaye ni mtendaji mkuu wa Tume, kutoka miongoni mwa watumishi waandamizi wa serikali watakaopendekezwa na Tume.

g) Kifungu cha 7(1) cha Sheria ya Uchaguzi kinachowapa Wakurugenzi wa Majiji, Manispaa, Miji na Halmashauri za Wilaya mamlaka ya kuwa wasimamizi wa uchaguzi unaofanyika katika majimbo ya uchaguzi.
h) Kifungu cha 7 (2) na (3) cha Sheria ya Uchaguzi kinachoilazimisha Tume kuteua mtumishi mwingine yeyote wa serikali kuwa msimamizi wa uchaguzi.

9.1. Mfumo Huu wa Usimamizi wa Uchaguzi Sio Huru na
Hauwezi Kuendesha Uchaguzi Huru, Wa Haki na Halali.
(a) Kwa mujibu wa Sheria ya Utumishi wa Umma, Wakurugenzi wa Halmashauri za Serikali za Mitaa ni wateule wa Rais (Wakurugenzi wa Majiji); au wa Tume ya Utumishi wa Umma (Wakurugenzi wa Manispaa, Miji na Halmashauri za Wilaya). Mwenyekiti, Makamu Mwenyekiti na Wajumbe wa Tume ya Utumishi wa Umma, kama ilivyo kwa Tume nyingine zote, ni wateule wa Rais kwa mujibu wa ibara ya 36 (3) ya Katiba. A

(b) Wakurugenzi wote wa Halmashauri za Serikali za Mitaa waliopo madarakani kwa sasa wameteuliwa na Rais na hivyo kuwajibika kwake.

(c) Mkurugenzi wa Uchaguzi na wasimamizi wa uchaguzi wote wanaweza kuondolewa madarakani wakati wowote na Rais mwenyewe chini ya ibara ya 36 (4) ya Katiba; au na Tume ya Utumishi wa Umma ambayo imeteuliwa na Rais.

(d) Wasimamizi wa uchaguzi wa ngazi zote sio watumishi wa Tume kwa maana ya uteuzi na uwajibikaji wao kiutendaji na kinidhamu. Ni 'watumishi wa Tume' kwa matakwa ya Sheria ya Uchaguzi na kwa wakati wa uchaguzi tu.

(e) Mwenyekiti, Makamu Mwenyekiti na Wajumbe wa Tume hawana ulinzi wowote wa kikatiba wa ajira zao. Hii ni tofauti kabisa na ulinzi wa kikatiba wa ajira walionao Majaji wote wa Mahakama Kuu na Mahakama ya Rufaa ya Tanzania; Mwenyekiti, Makamu Mwenyekiti na Wajumbe wa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora, na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali.

9.2. Maeneo ya Katiba na Sheria ya Uchaguzi yanayohitaji
Marekebisho
(a) Matokeo ya Rais yapingwe Mahakamani na Rais asiapishwe mpaka shauri lililofunguliwa kwa hati ya dharura liamuliwe. Tunapendekeza ibara ya 41(7) ya Katiba ifanyiwe marekebisho.

(b) Ibara ya 74 (1) ya Katiba irekebishwe ili kuviwezesha vyama vya siasa na asasi na taasisi za kiraia, ambao ni wadau wakuu wa uchaguzi, kupendekeza majina ya Wajumbe wa Tume ya Uchaguzi kwa ajili ya uteuzi wa Rais, baada ya kukidhi masharti ya kitaaluma na kiutendaji yaliyowekwa na Katiba.

(c) Ibara ya 74 (5) ifanyiwe marekebisho ili kuwapatia Wajumbe wa Tume ulinzi wa kikatiba wa ajira zao, sawa na Majaji, Wajumbe wa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali.

(d) Ibara ya 74 (7) na kifungu cha 6(1) cha Sheria ya Uchaguzi virekebishwe ili kuwezesha Mkurugenzi wa Uchaguzi kuteuliwa na Tume, bila kujali ni mtumishi mwandamizi wa serikali au la, ili mradi ametimiza masharti ya kitaaluma na kiutendaji yaliyowekwa na Katiba au Sheria ya Uchaguzi.

(e) Ibara za 74 (12) na 75 (6) irekebishwe ili kuondoa kinga dhidi ya mashtaka kwa Tume kutokana na utekelezaji wa madaraka yake na ugawaji wa majimbo ya uchaguzi kwa mujibu wa Katiba na Sheria ya Uchaguzi.

(f) Kifungu cha 7 cha Sheria ya Uchaguzi kirekebishwe ili kuipa Tume mamlaka ya kuteua wasimamizi wote wa uchaguzi wenye sifa za kitaaluma na kiutendaji bila kujali ni watumishi wa serikali au la. Tume iwe na mamlaka pekee ya uteuzi wa watumishi wake wote.

9.3. Mchakato wa Kutoa na Kurudisha Fomu za Uteuzi wa Wagombea
(a) Kifungu cha 38 (6) cha Sheria ya Uchaguzi kinawaelekeza wasimamizi wa uchaguzi kutoa na kumpatia mgombea au mpiga kura yeyote idadi ya fomu za uteuzi wa wagombea atakazohitaji.

(b) Kifungu cha 38 (7) kinamtaka kila mgombea au mdhamini wa mgombea kuwasilisha fomu za uteuzi kwenye ofisi ya msimamizi wa uchaguzi kabla ya saa 10 jioni ya siku ya uteuzi wa wagombea.

(c) Hakuna masharti yoyote ya kisheria yanayomlazimu msimamizi wa uchaguzi kuwepo ofisini kwake wakati wote wa kutoa na kurudisha fomu za uteuzi. Aidha, hakuna masharti yoyote ya kisheria ya kumlazimisha msimamizi wa uchaguzi kutoa au kupokea fomu za uteuzi za wagombea wa vyama vyote vya siasa vinavyoshiriki kwenye uchaguzi.

(d) Kumekuwa na matukio mengi ya wasimamizi wa uchaguzi kutoa au kupokea fomu za uteuzi kwa wagombea wa CCM na kisha kukimbia ofisi zao ili wasitoe au kupokea fomu za uteuzi kwa wagombea wa vyama vya upinzani.

(e) Kumekuwa na matukio mengi yaliyoshuhudiwa wakati wa uchaguzi wa serikali za mitaa, 2019 ya wasimamizi wa uchaguzi kuongeza herufi au namba kwenye fomu za wagombea wa upinzani kwa lengo la kuziharibu na hivyo kuwafanya wakose sifa za kugombea .

9.4. Maeneo ya Sheria ya Uchaguzi yanayohitaji Marekebisho Kuhusu Mchakato wa Kutoa na Kupokea Fomu za Uteuzi wa Wagombea.
(a) Kifungu cha 38 (6) cha Sheria ya Uchaguzi kirekebishwe ili pale ambapo msimamizi wa uchaguzi anapokuwa hayupo ofisini kwake wakati wote wa zoezi la kutoa fomu za uteuzi; au anapotoa fomu za uteuzi kwa mmoja au baadhi tu ya wagombea, basi zoezi zima la kutoa na kurudisha fomu za uteuzi litasimama hadi hapo msimamizi wa uchaguzi atakapotoa fomu kwa wagombea wote wanaohitaji fomu za uteuzi. Hii itaondoa tabia mbaya ya wasimamizi wa uchaguzi kukimbia ofisi zao ili kukwepa kutoa fomu za uteuzi kwa wagombea wa vyama vya upinzani.

(b) Kifungu cha 38 (7) kirekebishwe ili pale ambapo msimamizi wa uchaguzi hayupo ofisini kwake wakati wote wa zoezi la kurudisha fomu za uteuzi kwa sababu yoyote ile; au anapoondoka ofisini baada ya kupokea fomu za uteuzi za mgombea mmoja au baadhi tu ya wagombea, basi zoezi zima la kurudisha fomu za uteuzi na hatua nyingine zinazofuata litasimama hadi hapo msimamizi wa uchaguzi atakapopokea fomu za uteuzi za wagombea wote waliochukua fomu hizo.
Hii itaondoa tabia ya wasimamizi wa uchaguzi kukimbia ofisi zao ili kukwepa kupokea fomu za uteuzi za wagombea wa vyama vya upinzani.

(c) Kifungu cha 38 kirekebishwe kwa kuongeza kifungu kidogo kitakachowalazimisha wasimamizi wa uchaguzi kutoa au kupokea fomu za uteuzi za wagombea wa vyama vyote vya siasa vinavyoshiriki kwenye uchaguzi kwa pamoja au kwa wakati mmoja. Hii pia itaondoa tabia ya wasimamizi wa uchaguzi kutoa au kupokea fomu za uteuzi kwa wagombea wa CCM tu na kisha kukimbia ofisi zao ili kukwepa kutoa au kupokea fomu za uteuzi za wagombea wa vyama vya upinzani.

(d) Kifungu cha 38 kirekebishwe kwa kuongeza kifungu kidogo ili kuwezesha wagombea waliopoteza au kunyang'anywa fomu za uteuzi kupatiwa fomu nyingine za uteuzi ili waweze kushiriki kwenye zoezi la uchaguzi.
Hii itaondoa tabia inayojitokeza kwa kasi ya wagombea wa vyama vya upinzani kutekwa nyara na kisha kunyang'anywa fomu zao za uteuzi na hivyo kushindwa kuzirudisha kabisa, au kuzirudisha nje ya muda uliopangwa kwa ajili hiyo.

(e) Tunapendekeza kuwepo kwa marekebisho ya sheria ili kuiwezesha Tume kuweka kwenye mtandao fomu zote za uteuzi wa wagombea na hivyo kila mgombea kuwa na fursa ya kupakua fomu hizo kuzijaza na kuzirejesha. Fomu irejeshwe kwa msimamizi wa uchaguzi ikiwa na uthibitisho wa Chama cha Siasa kilichomteua na nakala ya fomu hiyo itumwe Tume Makao makuu kwa njia ya mtandao kama uthibitisho wa fomu kurejeshwa na Mgombea. Hatua hii itaondoa tabia ya wasimamizi wa uchaguzi kukimbia ofisi zao siku ya kutoa na kurejesha fomu za uteuzi.

9.5. Sifa na Masharti ya Kugombea Uchaguzi
(a) Kifungu cha 36 cha Sheria ya Uchaguzi kinakataza mtu yeyote kuteuliwa kuwa mgombea wa uchaguzi wa Ubunge mpaka awe na sifa za kuchaguliwa hivyo kwa mujibu wa ibara ya 67 ya Katiba.

(b) Sifa zilizowekwa na ibara ya 67 (1) na (2) ya Katiba ni uraia wa Tanzania; umri wa miaka 21 au zaidi; kujua kusoma na kuandika Kiswahili au Kiingereza; kuwa mwanachama na kupendekezwa na chama cha siasa; kutokuwa na hatia ya kosa la kukwepa kodi; kutokuhukumiwa adhabu ya kifo, au kufungwa kwa zaidi ya miezi 6 kwa kukutwa na hatia ya kosa lolote la utovu wa uaminifu; kutokuhukumiwa na Mahakama kwa kukutwa na hatia ya kosa la utovu wa uaminifu au kwa kuvunja Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma; kutokuwa na maslahi na mkataba wa aina yoyote uliowekewa miiko na kukiuka miiko hiyo; kutokuwa afisa mwandamizi wa serikali; na kutokuzuiliwa kujiandikisha kama mpiga kura katika uchaguzi wa Wabunge.

(c) Nje ya masharti haya ya Katiba, kifungu cha 38 cha Sheria ya Uchaguzi kimeweka masharti mengine ya ziada yafuatayo:
(i) Kupata udhamini wa wapiga kura 25 waliojiandikisha kupiga kura kwenye jimbo husika. (Kifungu cha 38(1).
(ii) Kutokukatazwa na Tume ya Uchaguzi kuwa mgombea kwa mujibu wa Sheria ya Gharama za Uchaguzi. (Kifungu cha 38(2).
(iii) Jina, anwani na kazi ya mgombea; majina, anwani za wadhamini na namba za kadi zao za wapiga kura, na hati ya kiapo ya mgombea kuwa yuko tayari na ana sifa za kugombea uchaguzi. (Kifungu cha 38(3).
(iv) Hati ya kiapo iliyosainiwa na mgombea mbele ya hakimu kwamba ana sifa na kwamba hajazuiliwa kugombea uchaguzi; picha za mgombea zilizopigwa ndani ya miezi mitatu kabla ya uteuzi, na maelezo binafsi ya mgombea. (Kifungu cha 38(4).

(d) Kifungu cha 38 (5) kinatamka wazi kwamba pale ambapo fomu za uteuzi hazijaambatanishwa na nyaraka zilizotajwa na kifungu cha 38 (4), basi uteuzi wa mgombea husika utakuwa batili.
Hata hivyo, Tume inaweza, endapo itaona inafaa, kuelekeza kwamba fomu za uteuzi za mgombea huyo zikubaliwe kuwa ni halali endapo nyaraka zikizokosekana zitawasilishwa kwa msimamizi wa uchaguzi ndani ya muda wa nyongeza uliowekwa na Tume. (Proviso ya kifungu cha 38 (5).

9.6. Maeneo yanayohitaji Kufanyiwa Marekebisho Kuhusu Sifa na Masharti ya Kugombea.
(a) Kifungu cha 38 (5) cha Sheria ya Uchaguzi kirekebishwe ili fomu za uteuzi zenye mapungufu ya nyaraka zilizotajwa na kifungu cha 38 (4) zisiwe batili. Badala yake, kifungu kipya kielekeze kwamba mgombea husika atapatiwa muda wa kurekebisha mapungufu ya nyaraka yaliyoonekana.
Faida ya pendekezo hili ni kwamba sababu pekee ya kubatilisha fomu za uteuzi wa wagombea itakuwa ni kukosa sifa za kugombea au kuchaguliwa zilizotajwa na ibara ya 67 ya Katiba.

Mapungufu mengine yote yasiyohusu kukosa sifa za kikatiba yataweza kurekebishwa na hivyo kuwezesha wagombea wote wenye sifa za kikatiba kushiriki kwenye uchaguzi.

9.7. Mchakato wa Kuweka na Kuamua Mapingamizi Dhidi ya Uteuzi wa Wagombea.
(a) Kifungu cha 40 cha Sheria ya Uchaguzi kimeweka sababu za fomu za uteuzi wa wagombea kuwekewa mapingamizi, na utaratibu wa kusikiliza na kuamua mapingamizi hayo.

(b) Kifungu cha 50A kimeweka utaratibu wa ziada kuweka mapingamizi wakati wa kampeni za uchaguzi.

(c) Kifungu cha 40 (3) kinawataja watu wenye haki ya kuweka mapingamizi dhidi ya uteuzi wa wagombea kuwa ni wagombea, msimamizi wa uchaguzi, Mkurugenzi wa Uchaguzi, Mwanasheria Mkuu wa Serikali na Msajili wa Vyama vya Siasa.

(d) Mapingamizi yote katika hatua hii yanapaswa kuwasilishwa kwa msimamizi wa uchaguzi sio zaidi ya saa 10 ya siku inayofuatia uteuzi wa wagombea. (Kifungu cha 40(2).

(e) Baada ya uteuzi wa wagombea kufanyika na mapingamizi yoyote kuamuliwa, kifungu cha 50A (1) kinamruhusu Msajili wa Vyama vya Siasa kumwekea pingamizi kwenye Tume mgombea yeyote anayekiuka masharti ya Sheria ya Gharama za Uchaguzi, wakati kampeni za uchaguzi zikiwa zinaendelea.

(f) Baada ya kusikiliza pingamizi hilo, Tume inaweza kumfuta mgombea husika kwenye orodha ya wagombea na kumzuia kuendelea na mchakato wa uchaguzi. (Kifungu cha 50A (2).

(g) Tofauti na utaratibu wa mapingamizi ya awali chini ya kifungu cha 40, hakuna utaratibu wowote wa rufaa kwa mapingamizi yanayowekwa au kuamuliwa chini ya kifungu cha 50A.

(h) Tofauti na utaratibu wa mapingamizi ya awali chini ya kifungu cha 40, utaratibu wa mapingamizi chini ya kifungu cha 50A umeondolewa kwenye mikono ya wasimamizi wa uchaguzi na kupelekwa kwenye mikono ya Tume moja kwa moja. Kwa maneno mengine, mapingamizi chini ya utaratibu huu yatawasilishwa, kusikilizwa na kuamuliwa kwenye ofisi za Tume; badala ya kuwasilishwa, kusikilizwa na kuamuliwa kwenye ofisi za wasimamizi wa uchaguzi walioko majimboni.

9.8. Maeneo yanayohitaji Marekebisho Kuhusu Mchakato wa Kuweka, Kusikiliza na Kuamua Mapingamizi.

(a) Kifungu cha 40 (3) kinachohusu watu wenye haki ya kuweka mapingamizi kirekebishwe ili pale ambapo mweka pingamizi ni msimamizi wa uchaguzi, au Mkurugenzi wa Uchaguzi au Msajili wa Vyama vya Siasa au Mwanasheria Mkuu wa Serikali, basi pingamizi hilo lisikilizwe na kuamuliwa na Hakimu Mkazi wa Mahakama ya Wilaya au Mahakama ya Hakimu Mkazi ya eneo la jimbo husika la uchaguzi.

Hii itaondoa hatari ya watu wanaohusika na uchaguzi kuwa waweka mapingamizi na waamuzi wa mapingamizi hayo.

Itaondoa pia uwezekano wa Mkurugenzi wa Uchaguzi anayeweka pingamizi kumshinikiza msimamizi wa uchaguzi ambaye yuko chini yake kimamlaka kuamua pingamizi hilo kwa upendeleo.

Aidha, pendekezo hili litaondoa uwezekano wa wateule hawa kula njama za kuwaengua wagombea wa vyama vya upinzani.

(b) Kifungu cha 40 kirekebishwe kwa kuongeza kifungu kingine kidogo kitakachoweka wazi kwamba sababu pekee ya kubatilisha uteuzi wa mgombea aliyewekewa pingamizi ni kama fomu zake za uteuzi zinaonyesha kwamba hana sifa za kugombea au kuchaguliwa zilizotajwa na ibara ya 67 ya Katiba.

(c) Kifungu cha 40 (6) kirekebishwe ili kuondoa kinga dhidi ya mashtaka kwa Tume kutokana na uamuzi wake juu ya rufaa za mapingamizi ya uteuzi wa wagombea mara baada ya kutolewa uamuzi huo, badala ya kusubiri uchaguzi husika kukamilika kwanza.

Pendekezo hili litawezesha uamuzi wa Tume kuengua wagombea wa vyama vya upinzani kubatilishwa kabla ya uchaguzi kufanyika na hivyo kuwaruhusu kuendelea na kampeni na kushiriki kwenye uchaguzi.
Kwa uzoefu wa mashauri ya mapingamizi kabla ya uchaguzi na mashauri ya kesi za uchaguzi baada ya uchaguzi; ni rahisi zaidi kwa mashauri ya mapingamizi kusikilizwa na kuamuliwa kabla ya uchaguzi kuliko kesi za uchaguzi zinazofunguliwa baada ya uchaguzi kufanyika na washindi kutangazwa.

(d) Kifungu cha 50A kifutwe kabisa kwa sababu kinaweza kutumiwa vibaya kwa kuwaonea wagombea, hasa wa vyama vya upinzani, kwa kuwaengua kabisa kwenye mchakato wa uchaguzi, au kwa kuvuruga kampeni zao za uchaguzi.

9.9. Sheria ya Gharama za Uchaguzi
Sharti na katazo la kisheria kwa mujibu wa kifungu cha 12 (1), (2), (3) na (4) kinachotaka vifaa vya uchaguzi kuingizwa siku 90 kabla ya uchaguzi lifutwe. Hii ni kutokana na ukweli kwamba katazo hilo halijazingatia uteuzi unaofanywa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi kwani Tume inateua wagombea ikiwa imesalia siku moja kabla ya kampeni kuanza, inawezekana vipi kwa chama cha siasa kuagiza vifaa bila kuwa na mgombea aliyeteuliwa na Tume. Aidha katazo hili la kisheria halijazingatia ugumu wa kuagiza, kuzalisha na kusafirisha vifaa hivyo kutoka nje ya nchi.
Mapendekezo haya ya marekebisho ya sheria yaende sambasamba na kuboresha Sheria ya uchaguzi wa Madiwani “The Local Government (Elections) Act Ca. 292” kwa sababu uchaguzi huo pia ni muhimu na unafanyika sambasamba na uchaguzi wa Rais na Wabunge.

10.0. HITIMISHO
Ili kuwa na Tume Huru ya Uchaguzi mabadiliko ya kikatiba na kisheria yanapaswa kuzingatia misingi ifuatayo:

Mosi, watu kuomba au kupendekezwa na makundi yanayotambulika na yenye uhalali (legitimacy)katika jamii.

Pili, mchujo wenye kuhusisha umma (public scrutiny) kufanyika.

Tatu, uteuzi kufanywa na chombo huru (badala ya kufanywa na mtu mmoja Rais).

Nne, uthibitishwaji (Confirmation Hearing) ufanywe na Bunge.

Tano, uapishwaji wa wateule ufanywe na Jaji Mkuu (badala ya Rais)
Maoni na mapendekezo yatolewe kwa kuzingatia misingi hii ili upatikane muundo utakaowezesha kuwa na Tume Huru Ya Uchaguzi.
Lakini kuwa na Tume Huru tu ngazi ya Taifa hakuwezi kujitosheleza kuwa na uchaguzi wa haki. Baada ya kuwa na Tume Huru katika ngazi ya Taifa tume hiyo ndio inapaswa kupewa mamlaka na katiba na sheria kuteua au kuajiri watendaji wake mf. Mkurugenzi wa Uchaguzi, wakurugenzi wasaidizi wa Tume ngazi ya Taifa, wasimamizi wa Uchaguzi kwenye majimbo, kata nk.
"Imetolewa 28 Oktoba 2021 na:

John Mnyika
Katibu Mkuu-Chadema
Katika kumbukizi ya #UchafuziMkuu2020"

219892614.jpg
 
Mnyika safi sana, hii ndo siasa tunayotaka uchambuzi na kutoa muelekeo sio matusi na misimamo isiyo na msingi.
 
View attachment 2062398
Nondo za Kufa Mtu. Vijana kama vijana mnajitambua.

Kazi kama hizi zinatuheshimisha sana kama Bavicha.
 
Tume huru ni jambo muhimu ili kuwa na uchaguzi badala ya uchafuzi
 
9 Reactions
Reply
Back
Top Bottom