CHADEMA sasa YATIKISHA NCHI..Idara zote serikali hapashikiki!!

eliesikia

JF-Expert Member
Oct 29, 2010
787
755
MAPAMBANO makali kati ya Polisi na wafuasi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) yaliyotokea juzi na jana mkoani Arusha yameleta mshtuko mkubwa kitaifa, hata kuilazimisha serikali kukubali mazungumzo ili kishughulikia mgogoro wa kisiasa uliosababisha machafuko ya kisiasa na kiusalama katika jiji la Arusha.

Kwa nyakati mbalimbali, CHADEMA, serikali, Chama Cha Mapinduzi, asasi za kiraia na kidini, Chama cha Wananchi (CUF), na wananchi katika makundi mbalimbali, walitoa matamko kuhusu mgogoro huo, huku wengi wakiishutumu serikali na polisi kwa kusababisha zogo na mauaji.

Waziri wa Mambo ya Ndani, Shamsi Vuai Nahodha, alizungumza na waandishi wa habari jana jijini Dar es Salaam, akasema serikali itaitisha mazungumzo ya amani ili kumaliza mgogoro wa kisiasa uliosababisha machafuko juzi jijini Arusha. Katika mkutano huo Nahodha aliambatana na Inspekta Jenerali wa Polisi nchini, Said Mwema.

Wakati serikali ikitoa tamko hilo, CHADEMA kiliwataka Nahodha na Mwema kujiuzulu kwa kushindwa kulinda amani na uhai wa wananchi wasio na hatia.

CCM nao, kupitia Umoja wa Vijana wa chama hicho, kilitoa tamko kushambulia CHADEMA kwa madai kuwa ndicho kilisababisha ghasia hizo.

Kauli ya serikali kukubali mazungumzo

Nahodha alisema meza ya mazungumzo ndiyo njia pekee itakayonusuru amani na uhai wa wakazi wa Jiji la Arusha; jambo ambalo siku chache zilizopita lilipendekezwa na Mbunge wa Monduli Edward Lowassa, likapuuzwa na Katibu Mkuu wa CCM Yusuph Makamba.

Mgogoro wa Arusha umetokana na uchaguzi wa Meya, baada ya CCM kuvunja sheria na kanuni za uchaguzi, wakachagua meya bila kuwashirikisha madiwani wa CHADEMA, njama zilizosimamiwa na serikali.

Nahodha alisema sasa kunahitajika busara ya viongozi wa pande mbili ili kurejesha amani mkoani Arusha.

“Mimi nasikitika kufa kwa watu hao, lakini lazima tufanye mazungumzo ya kutafuta amani Mkoani Arusha katika kuweka wananchi kuendelea na shughuli zao kwa kutawaliwa na amani,” alisema Nahodha.

Alipoulizwa iwapo serikali ingekuwa tayari kuwaachia viongozi wa CHADEMA bila kuwafungulia mashitaka yoyote ili kufanyike mazungumzo, alisema: “serikali bado inalitafakari suala hilo na ikijiridhisha kama kufanya hivyo kutamaliza mgogoro uliopo basi inaweza kuuzingatia ushauri huo.”

Kauli ya IGP Said Mwema

Mkuu wa Jeshi la Polisi Said Mwema alisema iwapo taarifa za kiintelijensia zitathibitisha kuwa polisi walisababisha vurugu hizo, atawajibika kwa mujibu wa sheria.

Alidai kuwa polisi walizuia maandamano hayo kutokana na taarifa za kiitelijensia kwamba yangesababisha uvunjifu wa amani; akasema kuwa kutokana na hali tete, jeshi hilo liliongeza nguvu kutokana mikoa jirani kukabiliana na ghasia ambazo zingeweze kutoka jana.

“Mimi nitawajibika kama kweli niliingilia utaratibu huo, lakini mahakama ... sio kwa sasa ...baada ya kutokea kwa vurugu hizo,” alisema Mwema
IGP Mwema alikiri kuwa jana jeshi la polisi liliagiza askari wengi zaidi kutoka maeneo mbalimbali ya nchi. Hata hivyo hakutaja maeneo hayo, huku akisisitiza kuwa hiyo ni sehemu ya mikakati ya siri ya jeshi hilo linapojipanga kuimarisha ulinzi kwenye operesheni kama hiyo.

Maswali ambayo yaliwashinda Mwema na Nahodha

Nahodha na Mwema walijibu baadhi ya maswali juu juu na kupuuza au kushindwa kujibu mengine, hasa yaliyohitaji majibu makini na ya kina.

Kwa mfano, Nahodha alipoulizwa kwanini serikali inataka mazungumzo baada ya watu kufa wakati ilipuuza ushauri huo huko nyuma, alisema: ”muda wa kufanya mazungumzo ya kina usingeweza kutosha.”
IGP Mwema alipoulizwa kwa nini polisi wanapeleka wananchi na viongozi wa CHADEMA mahakamani, huku wakikataa kuwakamata na kuwafikisha mahakamani polisi walioua raia jijini Arusha, hakuweza kutoa jibu lolote. Badala yake, alirukia maswali mengine. Hata alipoulizwa swali hilo mara kadhaa, aliipuuza.

Alipoulizwa kwanini wafuasi wa CHADEMA na viongozi wao walipoandamana kwa takribani kilomita mbili hakuna fujo zilizotokea hadi polisi walipoanza kuwapiga, IGP Mwema alikwepa kabisa kujibu swali hilo. Badala yake aliendelea kusisitiza kwamba taarifa za kiitelijensia walizokuwa nazo zilionyesha kwamba kungekuwa na tishio la amani.

Mwema alidai kuwa matokeo ya kuchomwa moto kwa baadhi ya vibanda na nyumba mjini Arusha, ni ushahidi kuwa taarifa za kiitelijensi walizokuwa nazo zilikuwa sahihi. Lakini alipobanwa kwa maswali kwamba kwa nini uchomaji huo haukujitokeza mchana kabla ya polisi kukamata, kupiga na kuua watu, hakuweza kutoa majibu.

Maafa yaliyotokea Arusha

Taarifa za polisi mkoani Arusha zilisema watu watatu walifariki dunia na wengine sita walilazwa katika Hospitali ya Mkoa wa Arusha, Mt.Meru. Miongoni mwa waliokuwa wamelazwa hospitalini hapo ni Josephine Mushumbusi, ambaye ni mchumba wa Katibu Mkuu wa CHADEMA, Dk. Willibrod Slaa.

Mganga mkuu wa hospitali hiyo, Salash Toure, alisema miongoni mwa waliokuwa hospitalini hapo ni majeruhi 16. Wengi wao walijeruhiwa vibaya kwa risasi za moto.

Kamanda wa Polisi Mkoani Arusha, Thobias Andengenye, wengi wao walijeruhiwa walipokuwa wanatoka kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika katika viwanja vya NMC Unga Limited wakielekea kituo kikuu cha polisi kuwanusuru viongozi wao waliowekwa chini ya ulinzi juzi.

Waliofariki dunia Ismail Omari, Denis Michael na Geogre Mwita. Hadi jana hawakujulikana walikokuwa wanaishi.

Hata hivyo, inadaiwa kuwa askari mmoja naye alipoteza maisha lakini kamanda Andengenye hakutaka kuthibitisha hilo.

Nyumba ya mkazi mmoja, Salimu Ally, iliteketea yote kwa moto; na kibanda cha kuuzia vocha za simu cha Arusha by Night, kiliungua halafu polisi waliwahi kuzima moto huo.

Baadhi ya mashahidi wa tukio hilo walidai moto huo ulisababishwa na polisi; huku polisi wakidai ulisababishwa na raia.

“Kituo kidogo cha polisi cha kaloleni wananchi tayari walikuwa wameshakimwagia mafuta aina ya Petroli kwa lengo la kukiteketeza ndipo polisi walitokea na kuwasambaratisha na mabomu ya machozi huku wananchi hao wakiwa hawakubali na kunawa nyuso zao kwa maji na kutaka kuendelea na zoezi hilo,” alisema andengenye.

Kamanda Andengenye alisema kuwa miili ya marehemu wote imehifadhiwa katika hospitali ya mkoa kwa uchunguzi zaidi na huku taratibu za mazishi zikiendelea kwa ndugu wa marehemu hao.

Viongozi na wafuasi 31 wa CHADEMA waliokamatwa juzi na kulazwa rumande jana walipandishwa kizimbani, wakasomewa shitaka la kuandamana bila kibali.

Miogoni mwa waliofikishwa mbele ya Hakimu Mfawidhi Charles Magese wa Mahakama ya Mkoa ni Mbunge wa Hai Freeman Mbowe, mbunge wa Moshi mjini Filemon Ndesamburo, Mbunge wa Rombo Joseph Selasini, Mbunge wa Arusha Mjini Godbless Lemana na Dk Willibrod Slaa.

Mwendesha Mashitaka wa Serikali Zakaria Isaria alisema wote kwa pamoja wanadiwa kufanya mkusanyiko bila kibali.

Wengine ni Dadi Igogo, mwenyekiti wa chama hicho wilaya ya Arusha Deliki Magoma, na wanachama wengine 20. Josephine Mushumbusi na wenzake watano walisomewa mashitaka wakiwa katika Hospitali ya Mount Meru walikokuwa wamelazwa.

Washitakiwa wote walikana kosa, wakaruhusiwa kwa dhamana ya Sh 2m kila mmoja. Kesi yao itatajwa tena Januari 21 mwaka.

Tamko la CHADEMA

Jijini Dar es Salaam, CHADEMA kilitoa tamko kulaani vurugu hizo, kikiwatuhumu Jeshi la Polisi, CCM na Rais Jakaya Kikwete ambaye kinadai mwishoni mwa mwaka alitoa hotuba yenye maelekezo kwa polisi kuwadhibiti wapinzani kwa nguvu wasifanye siasa.

Tamko hilo liliandaliwa na Naibu Katibu Mkuu Hamad Yusuf na kusomwa na Mjumbe wa Kamati Kuu Mabere Marando. CHADEMA iliwataka Nahodha na Mwema wajiuzulu mara moja.

“CHADEMA inasisitiza kuwa yote haya yamefanyika kutokana na maelekezo ya hotuba ya Rais Kikwete ya kufunga mwaka …hivyo kwa mila na desturi, kistaarabu kama walivyofanya viongozi wengine kama Mzee Ali Hassan Mwinyi akiwa waziri wa mambo ya ndani alipotakiwa kujiuzulu kufuatia sakata la mahabusu …tunataka na Nahodha na IGP Mwema kufanya hivyo,” alisema Marando
Marando alisema uongozi wa CHADEMA Arusha ulitoa taarifa ya nia ya kufanya maandamano na baadaye Jeshi la Polisi likawaandikia CHADEMA kukubali nia yao.

Alisema mara baada ya Jeshi la Polisi kukubali maandamano hayo uongozi wa taifa wa chama hicho, ulisafiri kwa ajili ya kushiriki tukio hilo lakini baadaye walipata taarifa kupitia vyombo vya habari kwamba IGP Mwema amezuia maandamano hayo.

Alisema kilichotokea baada ya hapo ni viongozi na wafuasi wa chama wa CHADEMA kutembea kwa miguu kuelekea sehemu ya mkutano kabla ya kuzuiwa, kupigwa, kukamatwa na hata wengine kuuawa na polisi.

Marando alisema kinachotokea Arusha ni ashirio kuwa CCM wanajiandaa kung’ang’ania madaraka mwaka 2015 watakaposhindwa; kama alivyofanya Rais Laurent Gbagbo wa ivory Coast.

Alisema vurugu za Arusha ni ushahidi wa wazi zaidi juu ya umuhimu wa kuandikwa kwa katiba mpya ya nchi ambayo itathibiti madaraka ya rais na chama tawala na kuanzisha uwazi zaidi kuwa madaraka ya rais kama amiri jeshi mkuu si kuamrisha majeshi dhidi ya wananchi, bali kulinda haki za wananchi na mipaka ya nchi.

Aiongeza: “Pamoja na yaliyojiri mkoani Arusha, bado azima ya CHADEMA kuandamana, kufanya mikutano ya hadhara, operesheni Sangara na mingine kwa ajili ya kuwaunganisha Watanzania n akutetea haki zao iko pale pale.”
Akijibu hoja ya UVCCM waliodai kuwa watajibu mapigo, Marando alisema kama UVCCM watafanya hivyo, hawatakuwa wanapambana na CHADEMA bali wananchi. Alisema: “Twende kwa wananchi kushindana, tusiende kwa wananchi kupigana.”
Klabu ya waandishi Arusha yalaani polisi

Klabu ya waandishi wa habari mikoa wa Arusha [APC] jana ilitoa tamko kulaani kitendo cha askari polisi kuwashambulia, kuwajeruhi na kuharibu mali za waandishi wa habari wakiwa kazini katika tukio la juzi wakati wakivunja maandamano ya CHADEMA.

Katibu wa Arusha Press Club Eliya Mbonea alisema kuwa kitendo kilichofaywa na jeshi la polisi hakivumiliki. Aliwapa polisi siku tano kuomba radhi kabla ya kuhatarisha uhusiano wao na vyombo vya habari mkoani Arusha.

“Tunatoa siku tano kwa Jeshi la polisi kuomba radhi kwa vitendo hivyo ya kinyama ambavyo vinazidi kushika kasi kwa askari kila mara kuwadhalilisha wanahabari hapa nchini wanapokuwa kazini; baada ya siku hizo tano tutasitisha ushirikiano na jeshi hilo rasmi,’’ alisema Mbonea.

Polisi walimjeruhi vibaya mwandishi wa gazeti la Mwananchi Moses Mashala na kuwakamata wengine wawili Musa Juma na Moses Kilinga walipokuwa wanafanya mahojiano na Dk. Slaa katika Hoteli ya Mount Meru.

CHADEMA yashinda umeya Mwanza

Wakati CHADEMA kikiwa katikati ya vurugu za Arusha, mkoani Mwanza kilikibwaga CCM katika uchaguzi wa Meya, katika uchaguzi uliofanyika chini ya ulinzi mkali wa polisi.

Mkurugenzi wa jiji la Mwanza Wilson Kabwe alimtangaza Josephat Manyerere wa CHADEMA amechaguliwa kuwa Meya wa jiji la Mwanza, aliyepata kura 17 na kumshinda Stanslaus Mabula wa CCM aliyepata kura 15.

Kiti cha Naibu Meya wa jiji la Mwanza kimekwenda kwa Charles Chinchibela (CHADEMA) aliyepata kura 17 na kumshinda wa CUF Daud Mkama aliyepata kura 15.

Katika uchaguzi huo, CHADEMA walikuwa na madiwani 17, CCM 13 na CUF wawili. Madiwani wote wa CUF waliwapigiakura wagombea wa CCM walioshindwa.

Hii ni mara ya kwanza mwa Jiji la Mwanza kuwa na Meya asiye wa CCM; na ni mara ya kwanza kwa CHADEMA kuongoza jiji hilo.

CUF yatoa tamko kulaani polisi

Mwenyekiti wa CUF Prof Ibrahimu Lipumba aliungana na Cahdema kumtaka Inspekta Jenerali wa Polisi (IGP) Said Mwema kutofanya kazi kisiasa.

Alitoa tamko hilo mbele ya waandishi wa habari jijini Dar es Salaam, akisema kitendo cha IGP kuzuia maandamano na kusababisha vifo vya watu ni uzembe uliokithiri na ni dhahiri kwamba anafanya siasa badala ya kutekeleza majukumu yake.

“Mimi binafsi nilikuwa namuheshimu sana IGP, lakini kwa hili la kuumizwa kwa watu kutokana na yeye kutoa kauli ya kuwakataza CHADEMA, huku kikiwa ni chama cha siasa kilichosajiliwa, amenikosesha imani kabisa...” alisema Profesa Lipumba.

Prof. Lipumba alisema CUF inalaani ushirikiano mchafu kati ya polisi na CCM dhidi ya CHADEMA na wapenda haki na demokrasia ndani na nje ya nchi.

“CUF Inaamini kuwa Polisi na Serikali ya CCM wanataka kutumia kitisho cha ugaidi kilichozikumba Kenya na Uganda kama sababu za kupinga mikusanyo mikubwa ya kisiasa kwa lengo la kuitetea serikali hii. Kuna haja ya kujiuliza, hivi magaidi wakitaka kulipua Tanzania mbona kuna sehemu nyingi sana ambazo wanaweza kufanya hivyo bila kusubiri maandamano ya CHADEMA au CUF au vyama vingine?” alihoji Lipumba.

Alisema CUF Inamtaka Rais Kikwete kutumia busara badala ya mabavu katika kuendesha nchi, vinginevyo itamshinda.

Viongozi wa dini, wananchi nao walaani

Baadhi ya viongozi wa dini nao wamemtaka Waziri Nahodha kujiuzulu kwa kashfa hii.

Kauli hiyo imetolewa jana na askofu Dornald Mhango ambaye ni <akamu Askofu Mkuu wa Kanisa la Christian Mission Fellowship mkoani Dodoma.

Askofu Mhango alidai kuwa kwa sasa Jeshi la Polisi limeisha onyesha udhaifu mkubwa na kuifanya jamii kutokuwa na imani nalo, kwani wamekuwa wakifanya kazi zao kwa shinikizo la viongozi wa kisiasa walio madarakani, kinyume cha kiapo walichokula kulinda amani ya wananchi.

“Jeshi la Polisi limeshindwa kazi, na waziri mwenye dhamana anatakiwa kujiuzulu mara moja, kwani jeshi hili limekuwa likiendeshwa kisiasa,“ alisema.

Nayo asasi ya kiraia ya ForDIA, ambayo ni sekretarieti ya Mtandao wa Usalama na Amani katika eneo la Maziwa Makuu (PeSeNet) na Jukwaa la Uwazi Tanzania (TRAFO) imesikitishwa na tukio la jana, Januari 05, 2011, la vitendo vya Jeshi la Polisi mkoani Arusha kupiga, kuumiza, kukamata, kutia ndani na kuvuruga amani ya wakazi wa Arusha mjini
walioshiriki maandamano ya amani kupinga vitendo vilivyokiuka maadili na misingi ya utawala bora.

Taraifa iliyosainiwa na Mkurugenzi Mtendaji wa Fordia, Bubelwa Kaiza, ililaani vikali kitendo cha Polisi kukiuka maadili ya kazi yake, kuumiza watu, kufanya vurugu na kukiuka haki za binadamu za wakazi wa Arusha na pengine Watanzania wote kwa ujumla.

Ilisema: “polisi ni chombo cha dola kinachoaminiwa na raia, kwa ajili ya kulinda usalama wao, na hivyo kukabidhiwa silaha na zana za ulinzi; marungu, maji ya pilipili (washawasha), pingu, risasi za mpira, mabomu ya machozi, bastola, bunduki na pengine risasi za moto. Vifaa hivi vyote ni mali ya dola la Watanzania vinavyokusudiwa kulinda, sio kudhuru usalama wa raia.”
Naye Luteni UTENI Msataafu Letilall Ole-Molloimet ameungana na Watanzania wengine kulilaani Jeshi la Polisi kwa nguvu kubwa iliyotumika kuwadhibiti wafuasi wa CHADEMA.

Akizungumza na Tanzania Daima kwa simu kutoka kijijini kwake Isinya mpakani mwa Kenya na Tanzania, alisema nguvu hiyo ya polisi ingetumika kuwalinda wafuasi hao badala ya kumwaga damu ya watanzania wenye kiu ya mabadiliko.

Alisema kitendo cha kuzuia wanasiasa kuandamana ni kinyume cha Katiba iliyotumika kuruhusu uwepo wa vyama vingi vya saiasa huku akisisitiza kuwa amri ya polisi kuwadhuru waandamanaji wa CHADEMA, ni ulevi wa kisiasa walionao baadhi ya watalawa wa serikali ya Chama Cha Mapinduzi (CCM).

“Nawalaumu viongozi wa CCM kuwa chanzo cha mauvo yaliyofanyika jana (juzi ) pale Arusha… naamini polisi imepokea maelekezo kutoka kwa viongozi hao kitendo ninachokitafsiri kuwa ni hujuma ya kisiasa.

“Kilichofanyika pale kinastahili kulaaniwa ndani na nje ya nchi kwa sababu kimeathiri hadi sekta ya utalii, wameharibu kitovu cha utalii wetu ni walevi wa siasa hao ambao hawataki kukosolewa.

“…Lazima tujiulize kwa nini askari walikuwa na mawazo potofu ya kuwepo kwa fujo? Kwa nini wasingejipanga kuzuia fujo hizo kuliko kilichotokea? Si kazi ya polisi kuzuia maandamano popote pale jukumu lao ni kuwalinda wanaoandamana.

“Lazima CCM ikubali kuwasikiliza wapinzani ili nao wapate cha kusema kwenye meza zao… serikali iliyopo madarakani iwavumilie wanasiasa wengine na kurekebisha makosa yao kwa kukubali kukosolewa. Nadiriki kusema viongozi wengi wa CCM ni sawa na umande wa asubuhi wanatumia nguvu badala ya busara kujirekebisha,” alisema.

Wakati huo huo, taraifa zinasema Diwani wa Kata ya Sombetini (CCM), Alphonce Mawazo, amehamia CHADEMA akisema amechukizwa na ukatili wa CCM dhidi ya wananchi.


source: Tanzania
 
Thanks for the information, well detailed and articulated, Nadhani Jeshi la polisi will never get away with this, not now, police and the government should protect us not harm us, i gueess we have a lot of sick politician in ccm who dont real gets it that we wont toloret to be given orders while our constitutional rights are surpressed, this cant be happening in my own country
 
Afande Mwema tulidhani kuwa amejitofautisha na maafande wengine kwa kutumia busara zaidi, kumbe ni walewale. Mwema lazima awajibike kwa ujinga aliyofanya, ndo maana anawatetea askari wake. Kisheria mtu akiua lazima afikishwe mahakamani lakini amashindwa kuwakamata askari wake ili wahojiwe kuona usahihi wa kitendo chao cha kuwaua raia wasiyo na silaha.
Ni jambo la kusikitisha sana kuona watu wanaandamana wameshikana mikono wakiwa na vitambaa vyeupe alafu wanafyatuliwa risasi za mote kwa sababi za shinikizo za viongozi wa CCM. Mungu atujalie amani Tanzania.
 
Haya sasa Daktari anasema hospitali imepokea majeruhi 16 wengine wakiwa wameumizwa kwa risasi za moto.Jamani kwa nini risasi za moto zitumike? Hiyo ni nia dhahiri ya kuua raia.. This is really insane!
 
Mapambano ndio yanaanza sasa , Watanzania si wale wa miaka ya 1990. Viongozi wajue kuwa Binadamu anahitaji mabadiliko na si kuwa katika sehemu Moja.

hata Mimi nalaani Mauaji ya watanzania wasiokuwa na hatia JIJINI ARUSHA.

Mungu Zilaze Roho Za MAREHEMU MAHALI PEMA PEPONI AMEN!
 
JK akiambiwa asome alama za nyakati naona anaenda kuangalia nyota za Gemini, Leo, Aries nk. This country is ours as a whole sio ya wanasisiem and as a president he should have had spoken by now against the killings of those innocent people, au anasikilizia upepo unavumia wapi ajue atoke vp?
 
hii taarifa imekaa vizuri sana.........kwa kweli mwema na nahodha ni wapuuzi na punguani wakubwa

wao ndo wamesababaisha maafa na machafuko yote haya..........
 
Maskini CCM wanamtafuta mchawi, risasi haziwezi kamwe kuleta amani! huyu RPC mpuuzi alidhani ndo atapata sifa? amuulize TIDO MHANDO! Aaangalie historia, asiwe mjinga!
 
:angry: nadhani kama vile kuna haja ya kuanzisha majeshi mengine ya wananchi ........... haya yaliyopo naona kama sio ya wananchi:angry:
Mungu awalaze pema marehemu na awatie nguvu jamaa zao
 
:angry: nadhani kama vile kuna haja ya kuanzisha majeshi mengine ya wananchi ........... haya yaliyopo naona kama sio ya wananchi:angry:
Mungu awalaze pema marehemu na awatie nguvu jamaa zao

Siku hizi naskia wanauza matrekta ya wahindi...Jeshi la Wahindi wa Tanzania(JWTZ)
 
Hii ni Master-Piece katika taarifa za Mauaji ya Arusha!..(japokuwa nina shaka kwenye idadi ya waliofariki...hii inaonyesha ni wa3, wakati taarifa zingine zimesoma kuwa ni wa2!)
 
Hii ya Arusha ni mbaya sana kwa nchi yetu. Kwa ufupi haikubaliki. Haiwezekani ulevi wa madaraka na kujipendelea kutukuzwa kwa wanasiasa ituletee kuuwawa kwa watu wasio na hatia! This should not go unpunished. Ni lazima na ni muhimu Nahodha, Mwema na Andengenye wawajibike. Again watu wamepoteza maisha kwa sababu za kijinga kabisa ni lazima mkulu mkuu tumsikie anasemaje wkt dhamana na silaha walizopewa askari ni kulinda raia na siyo kuwadhuru! I Really hate this
 
Wapenda amani wote tunasikitishwa na mauaji ya Arusha, RIP wote na pole kwa familia zao. CDM tunatakiwa kuweka majina hayo ya mashujaa wa ukombozi wa Tanzania toka kwa madhalimu CCM katika vitabu vyetu vya kumbukumbu. Safari ya ukombozi ndio imeanza. Personally nitatunza hayo majina for future ili kuonyesha ukatili wa serikali ya JK
 
Yaani hawa jamaa ipo tu siku yao! Hao polisi ndio walioanzisha hizo vurugu.............lengo lao lilikuwa ni kuua watu na si kingine.
 
Jamani naomba mtu achukue mada inayosema 'CHADEMA YATIKISA NCHI' kutoka Gazeti la Tanzania daima tuijadili kwa sababu ina maswali mazuri yaliyomshinda Nadhoha na IGP Mwema kujibu jana walivyokuwa na vyombo vya habari.
 
Back
Top Bottom