Chadema nusura wazichape msibani ifakara, mbowe aipiga serikali kijembe, makani aanguka akiaga mwili

Relief

JF-Expert Member
Aug 6, 2010
254
47
Kufuatia Msiba wa Marehemu Regia.........................

MAKUNDI mawili yanayopinga ya wanachama wa Chadema jana nusura yazichape kavukavu yalipokuwa katika msiba wa aliyekuwa Mbunge wa Viti Maalumu kwa tiketi ya chama hicho, Regia Mtema huko Ifakara, kutokana na chuki na makovu ya uchaguzi wa wa ndani wa chama hicho wa mwaka 2010.

Wakati hayo yakitokea huko Ifakara, jijini Dar es Salaam, Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe alitumia fursa aliyopewa wakati wa kuaga mwili wa mbunge huyo kuipiga vijembe Serikali huku Mwenyekiti Mstaafu wa chama hicho, Bob Makani akianguka ghafla.

Marehemu Regia ambaye alifariki dunia Jumamosi iliyopita kwa ajali ya gari iliyotokea Ruvu, Pwani, unatarajiwa kuzikwa leo Ifakara.

Katika tukio la Ifakara, mgogoro baina ya kambi mbili zilizotokana na makovu ya uchaguzi huo wa ndani kati ya wafuasi wa marehemu na ya Mbunge wa Viti Maalumu, Susan Kiwanga ulisababisha kutimuliwa msibani hapo kwa Mwenyekiti wa Chadema Wilaya ya Kilombero, Salum Ngozi.

Ilielezwa kwamba baada ya Ngozi kufika msibani hapo juzi majira ya saa moja usiku na kusalimiana na viongozi wa Serikali, alifuatwa na baadhi ya makada wa chama hicho wakimtaka aondoke eneo hilo jambo ambalo aliligomea. Wafuasi hao wa Chadema waliamua kutumia nguvu kumwondoa hali iliyowalazimu polisi waliokuwa eneo hilo kuingilia kati. Askari walimtoa mwenyekiti huyo na kumpeleka katika Kituo cha Polisi Wilaya.

Hiyo ilikuwa mara ya pili kwa Ngozi kutimuliwa katika msiba huo. Mara ya kwanza ilikuwa juzi na kumlazimu Kaimu Mkuu wa Wilaya ya Kilombero, Francis Miti kuingilia kati.

Alipoulizwa kuhusu tukio hilo, Ngozi alikiri kutokea vurugu hizo msibani na kudai kwamba, alifanyiwa fujo na kikundi cha watu aliowaita wahuni na kwamba amefungua kesi ya kufanyiwa vurugu katika Kituo cha Polisi Wilaya ya Kilombero na kwamba baada ya kumalizika kwa mazishi atasimamia suala hilo ili haki itendeke.


Naibu Katibu Mkuu wa Chadema, Zitto Kabwe mbali na kukiri kuufahamu mgogoro huo, alisema asingependa kuzungumzia suala hilo sasa wakati watu bado wanaendelea na msiba.

Mbowe aipiga vijembe Serikali

Jijini Dar es Salaam, tukio la kuaga mwili wa marehemu Regia liligeuka jukwaa la siasa baada ya Mbowe na Makinda kupiga siasa.Mbowe alitumia msiba huo kutoa dukuduku lake juu ya shughuli za chama chake kisiasa na kiutendaji wakati akitoa salaam za rambirambi kwa marehemu.Mbowe aliirushia kombora Serikali na vyama vingine vya upinzani kuhusu mwenendo wa Chadema kuendesha siasa katika vyuo vya elimu ya juu akisema ni mpango maalumu kuwanoa wanasiasa mahiri.

Aliishauri Serikali na vyama vingine vya siasa kuiga utaratibu huo wa Chadema akisema unasaidia kukuza vipaji na kuwaandaa viongozi makini kwa kuwapa nafasi vijana kushiriki katika uongozi.

“Kuna jambo moja ambalo ningependa Serikali, Chama Cha Mapinduzi (CCM) na vyama vingine walitafakari na wasilibeze hili. Viongozi huandaliwa na viongozi makini hawazuki tu,” alisema na kuongeza;

“Naeleza hivyo maana mara nyingi tumekuwa hatueleweki na tumekuwa tukibezwa. Sisi tunatambua viongozi wa baadaye kisha tunakuza vipaji na kutoa fursa za nafasi za uongozi kwa vijana.”

“Vijana lazima waandaliwe kimaadili na ndiyo maana tuliingia vyuo vikuu lakini tukatafsiriwa kuwa ni wakorofi na wachochezi wa vurugu. Lakini leo tumepata viongozi wazuri vijana kwa njia hiyo kutoka vyuoni kama vile Mheshimiwa Zitto (Zuberi Kabwe, Mbunge wa Kigoma Kaskazini), Mnyika (John Mbunge wa Ubungo, Mdee (Halima-Mbunge wa Kawe), Silinde (David Mbunge wa Mbozi) na Mtema (Regia Marehemu).

“Hawa tuliwaandaa, hawakuzuka. Rai yangu kwa Serikali na kwa wazazi ni kwamba vijana hawa wakifanya siasa tusiwakwaze na kuwafukuza, bali tuwalee.”

Spika Makinda katika kile kilichoonekana kama ni kumjibu Mbowe, alitumia fursa hiyo kufafanua uendeshaji wa shughuli za Bunge akisisitiza kwamba linaendeshwa kwa kanuni na wala si kufurahisha watu.
Alimsifia marehemu Mtema kwamba alikuwa akizijua vyema kanuni za Bunge: “Bunge huendeshwa kwa kanuni na si kwa matakwa tu ya kufurahisha watu. Yeye marehemu alizijua kanuni ndiyo maana hata wakati alipokuwa akikosea alikuwa tayari kuomba radhi.”

Mzee Makani aanguka
Hata hivyo hafla hiyo iliingia dosari baada ya Makani kuanguka muda mfupi baada ya kuuaga mwili wa marehemu. Baada ya tukio hilo, alibebwa na kupelekwa pembeni ambako alipepewa kwa takriban dakika tano kisha kurejea katika hali yake ya kawaida na kurudi kwenye kiti chake.

Baadaye Mwenyekiti wa NCCR Mageuzi, James Mbatia ambaye alikuwa mmoja wa watu waliokuwa wakimpatia Mzee Makani huduma ya kwanza aliwaambia waandishi wa habari kuwa alianguka baada ya kuishiwa nguvu ghafla.

“Sasa anaendelea vizuri na amerudi kushiriki kumuaga mpendwa wetu katika safari yake hii ya mwisho,” alisema Mbatia.

Kafulila ashangiliwa

Mbunge wa Kigoma Kusini (NCCR-Mageuzi), David Kafulila jana alishangiliwa kwa makofi baada ya kutangazwa kuwa mmoja wa wabunge walioteuliwa na Ofisi ya Bunge kuwamo katika msafara kusindikiza msiba huo akiwakilisha chama chake.

Baada ya kiongozi wa shughuli hiyo, Ofisa Mwandamizi wa Ofisi ya Bunge, Saidi Yakub kumtaja Kafulila baadhi ya waombolezaji walishangilia kwa makofi, vicheko vya chini kwa chini na minong’ono ya hapa na pale.

Hatua hiyo ya waombolezaji inatokana na hali ya kisiasa ilivyo kati ya Kafulila na chama chake hicho ambacho mwishoni mwa mwaka jana kilitangaza kumvua uanachama hatua ambayo ameipinga mahakamani. Kama ikitekelezwa, itamvua ubunge.

SOURCE: Mwananchi

Sasa hapa Jiulize mwenyewe!:A S 465:
 
mbowe kaongea point ambayo najua wana ccm ni vigumu kuikubali

ukombozi wa nchi hii utatoka kwa vijana makini na wasomi, mpendwa wetu hajaama kutoka ccm kwenda chadema na hao ndio watakao kijenga chama na kuleta mabadiliko na sio watu kuhama ccm kuhamia chadema

vijana wengi tu hum jf wapo wazuri sana tena sana jiungeni na chadema na mgombee uongozi hiyo ndio njia pekee ya kulikomboa hili taifa sio kukosoa tu humu, na twende tukapige kura zikiwa nyingi mno watachakachuaje?
 
mbowe kaongea point ambayo najua wana ccm ni vigumu kuikubali

ukombozi wa nchi hii utatoka kwa vijana makini na wasomi, mpendwa wetu hajaama kutoka ccm kwenda chadema na hao ndio watakao kijenga chama na kuleta mabadiliko na sio watu kuhama ccm kuhamia chadema

vijana wengi tu hum jf wapo wazuri sana tena sana jiungeni na chadema na mgombee uongozi hiyo ndio njia pekee ya kulikomboa hili taifa sio kukosoa tu humu, na twende tukapige kura zikiwa nyingi mno watachakachuaje?

Mwamikili una udugu wowote na Mwanakili90 au ni sawa na house na nyumba?
 
Angalia picha za maelfu ya wakazi wa Ifakara waliojitokeza kumpokea Regia jana usiku...

Anaripoti mdau wa Mjengwablog.com aliye Ifakara
Maelfu ya wananchi wa mji wa Ifakara wakiwa barabarani ambako walizuia ambulance iliyobeba mwili wa marehemu.Kwa mujibu wa wenyeji, haijawahi kushuhudiwa mapokezi kama haya katika msiba wowote ule katika historia ya mji huu.Mwenyekiti wa CHADEMA taifa alilazimika kuwaomba vijana kutulia kwani walikuwa wamejawa na jazba na taharuki.Baada ya mwili kuingizwa katika nyumba ya familia kwa muda, ulihamishiwa hospitali hadi baadaye utakapotolewa kwa ratiba nyingine.Msafara kutokea Dar es salaam uliwasili Ifakara saa 4 usiku na maandamano yaliuchelewesha kufika nyumbani kwa marehemu.wageni kutoka dar es salaam walifika ndani saa 5 usiku.Msafar kutoka Dar es salaam ulikuwa na magari yapatayo 60,ambayo mwandishi wa habari hii aliweza mwenyewe kuhesabu.Tutaendelea kuwahabarisha kutokea Ifakara. Angalia picha: Mjengwa Blog::Habari,Picha,Matangazo
 
Mhariri wa mwananchi na Zitto ambao ni marafiki at work. Natafakari kuachana na gazeti hili binafsi na nitaanza kushawishi ktk ofisi yetu wasiinunue hadi wajirekebishe. Heri Sauti huru kuliko haya.
 
Kwa maelezo haya,sioni kama Mbowe alitumia nafasi hiyo kupiga siasa,alikuwa anaonyesha umuhimu wa kuandaa watu kwa umakini toka chini...kama viongozi wa michezo wanaimizwa kuandaa watoto toka shule za msingi,kwanini isiwe kwa wanasiasa na vyama vya siasa? Na kwa hili la Makinda,tuache kutafsiri mambo kihuni,yeye amesema Regia alikuwa anazifahamu kanuni,na hajasema kuwa wabunge wengine wa CDM hawajui kanuni...tatizo la kuwa na waandishi wa habari makanjanja ndio hii.
 
Kivipi mkuu? hawafichi matukio yanayoweza kuwakera watu ama?


Sio suala la kukera ama kufurahisha watu, bali ni ukweli wa mambo ndio unaotakiwa.

Watu tuliokuwepo viwanja vya karimjee jana tunafahamu kwa uhakika kwamba kafulila hakushangiliwa ama kupigiwa makofi wakati anatajwa kuhudhuria mazishi ifakara kama mbunge toka nccr mageuzi. Kilichotokea ni kwamba watu waliguna na kuanza kunong'ona. Sasa kama miguno na minong'ono nayo ni kushangilia, let it be so!!

Baadaye wakati msafara wa kwenda ifakara unaondoka, Kafulila aliwapungia mkono watu ndipo nao wakampungia huku wakimtania kwa kumuita mbunge wa mahakama. Sasa inapotokea mwandishi anaandika habari yake mwenyewe ama anatia vikorombwezo katika habari ambayo ilishuhudiwa na watu wengi inakuwa ni aibu kwake na kwa chombo chake, na chombo chenyewe ni mwananchi!
 
Mhariri wa mwananchi na Zitto ambao ni marafiki at work. Natafakari kuachana na gazeti hili binafsi na nitaanza kushawishi ktk ofisi yetu wasiinunue hadi wajirekebishe. Heri Sauti huru kuliko haya.

kwani wewe kimekukwaza nini hapo mbona sikuelewi?
 
mbowe kaongea point ambayo najua wana ccm ni vigumu kuikubali

ukombozi wa nchi hii utatoka kwa vijana makini na wasomi, mpendwa wetu hajaama kutoka ccm kwenda chadema na hao ndio watakao kijenga chama na kuleta mabadiliko na sio watu kuhama ccm kuhamia chadema

vijana wengi tu hum jf wapo wazuri sana tena sana jiungeni na chadema na mgombee uongozi hiyo ndio njia pekee ya kulikomboa hili taifa sio kukosoa tu humu, na twende tukapige kura zikiwa nyingi mno watachakachuaje?

umenena vyema,ni wakati wa vijana kujiunga kwa wingi CHADEMA ili kuleta uongozi ulo bora kwa TZ yetu.
 
Back
Top Bottom