Mzee Mwanakijiji
Platinum Member
- Mar 10, 2006
- 33,391
- 39,484
Mtikila adai Chadema inafanya usanii
Stella Nyemenohi
HabariLeo; Monday,October 01, 2007 @00:03
Stella Nyemenohi
HabariLeo; Monday,October 01, 2007 @00:03
MWENYEKITI wa Democratic Party (DP), Christopher Mtikila ameibuka na kukishutumu Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kuwa kinafanya usanii wa kutumia majukwaa kujadili madai ya ufisadi dhidi ya viongozi wa Serikali kwa lengo la kufunika vyama vingine na kushika madaraka na siyo kuleta ukombozi kwa umma.
Mtikila, ambaye hata hivyo anaunga mkono madai hayo ya Chadema, alisema kitendo cha viongozi wa chama hicho kuacha kwenda mahakamani kinadhihirisha hawana nia thabiti ya kukabili tatizo, bali wanapoteza muda katika majukwaa kujipatia umaarufu.
Hawa watu (Chadema) ni wasanii. Wanataka washangiliwe kwa gharama ya taifa. Mikataba ni suala la kisheria, haki ya kisheria haipatikani katika majukwaa. Wao hawataki mahakamani ambako ndiko wangepata haki? Mtikila aliiambia HabariLeo jana.
Alisema kitendo cha baadhi ya viongozi waliotuhumiwa kuwa mafisadi kwenda mahakamani, ni mwelekeo wa kuzimaliza hoja hizo ambazo kama zingeshughulikiwa katika mkondo unaostahili, umma wa Watanzania ungeshuhudia mabadiliko.
Viongozi waliotangaza uamuzi wa kwenda mahakamani kumfungulia mashitaka Mbunge wa Karatu, Wilbrod Slaa, kwa madai ya kuitwa mafisadi ni Waziri wa Nishati na Madini, Nazir Karamagi, Katibu Mkuu Wizara ya Fedha, Grey Mgonja na Katibu Mkuu, Wizara ya Maji, Patrick Rutabanzibwa.
Kitendo cha walioshutumiwa kwenda mahakamani, hapo ndipo wamewabana. Lazima waanguke. Hapa suala la kujiuliza ni kwa nini Chadema hawakwenda wakati walikuwa na haki na hoja ni za kweli? alihoji.
Kwa mujibu wa Mtikila, aliwashauri viongozi hao wa Chadema kufungua kesi kupitia mawakili watatu ambao kwa mujibu wake, walitaka walipwe Sh milioni 10 kwa kazi hiyo, lakini viongozi hao wakakataa.
Katika kile anachosisitiza kuwa ni usanii wa kutaka kutumia hoja hizo kwa ajili ya maandalizi ya uchaguzi mkuu ujao, Mtikila alisema ushauri wake ulilenga kufungua kesi itakayotoa suluhu la ufisadi kwa upana, ikiwa ni pamoja na kuondoa kipengele cha usiri katika mikataba.
Mtikila aliendelea kukishutumu chama hicho cha upinzani kuwa kinafanya hivyo kujizoelea sifa kwa kutumia hoja ambazo siyo ngeni ili kukidhi matakwa ya wafadhili wao wanaowataka wahakikishe kinaingia madarakani katika uchaguzi ujao, na wala si kwa masilahi ya umma.
Wanaposema Karamagi kasaini mkataba Uingereza, Chadema nao hawana tofauti naye. Hawa wana Barrick, wao wana Conservative, wamewaambia lazima waingie madarakani, alidai Mtikila.
Akisisitiza kuwa shutuma hizo dhidi ya Chadema hazitokani na wivu wa siasa, Mtikila alisema, vyama vya usanii vitanyauka. Ni mara ngapi tumekuwa tukitupwa gerezani, hata siku moja hawajawahi kuandamana kutetea haki zetu?
Akizungumza kuhusu shutuma hizo za Mtikila, Mbunge wa Karatu, Dk. Slaa alisema, anazungumza asichokijua. Suala siyo mahakama, kama ni taratibu, zote tulizifuata. Nikipeleka suala hili mahakamani, ujue majibu yake ni katika miaka 20. Sisi tumeamua tulipeleke kwa wananchi wenyewe ndiyo waamue.
Katika kuzungumzia madai ya Mtikila kuhusu kuwatafutia mawakili, Dk. Slaa alidai kwamba Mwenyekiti huyo wa DP aliwaomba wamchangie Sh milioni 10 kwa ajili ya mawakili aliowaandaa. Hata hivyo, alisema hawakukubaliana naye kwa kuwa Dk. Slaa ana mawakili wanaomtetea bila gharama yoyote.
Kuhusu Chadema kubinafsisha hoja, Dk. Slaa alisema hoja hizo za ufisadi wa viongozi ni za vyama vyote. Yeye (Mtikila) anataka aingie kwa nguvu, alisema. Alikanusha madai ya kutumiwa na Conservative kwa kumtaka Mtikila aonyeshe ushahidi.
Wakati huo huo, Dk. Slaa amesema bomu alilokuwa ameahidi kulilipua wiki iliyopita, limeathiriwa na majibu ya serikali yaliyotolewa ambayo hata hivyo ameelezea kutoridhika nayo.
Ameitaka Serikali kutoa majibu ya hoja zake kwa kile alichodai majibu yaliyotolewa ni propaganda za siasa zisizowasaidia wananchi.