CHADEMA ni mti wenye maembe, lazima utupiwe mawe - Mbowe | JamiiForums | The Home of Great Thinkers

Dismiss Notice
You are browsing this site as a guest. It takes 2 minutes to CREATE AN ACCOUNT and less than 1 minute to LOGIN

CHADEMA ni mti wenye maembe, lazima utupiwe mawe - Mbowe

Discussion in 'Jukwaa la Siasa' started by Halisi, Sep 18, 2009.

 1. Halisi

  Halisi JF-Expert Member

  #1
  Sep 18, 2009
  Joined: Jan 16, 2007
  Messages: 2,810
  Likes Received: 83
  Trophy Points: 145
  Godfrey Dilunga
  Septemba 16, 2009

  SEPTEMBA 7, mwaka huu, Mwandishi Wetu, GODFREY DILUNGA alifanya mahojiano na Mwenyekiti wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Freeman Mbowe, ikiwa ni takriban wiki mbili baada ya kuchaguliwa kuendelea na wadhifa huo kwa awamu ya pili. Yafuatayo ni mambo mbalimbali kuhusu mwenendo wa chama hicho yaliyoulizwa na kujibiwa wakati wa mahojiano hayo.

  Swali: Ni makosa gani ambayo umeyafanya pamoja na viongozi wenzako katika miaka mitano iliyopita ukiwa mwenyekiti wa CHADEMA?

  Mbowe: Kabla ya kuzungumzia makosa, niseme kwamba tumefanya mageuzi makubwa ndani ya chama. Tumefanya mabadiliko makubwa ya kimfumo, kisera na kimtazamo. Tumejenga chama kinacholenga kuimarisha vijana ambao kesho wanaweza kuwa viongozi waandamizi au hata wakuu wa nchi.

  Tulitoa umuhimu kipekee kwenye leadership development kwa vijana, tumewakuza vijana na kuwaweka mstari wa mbele kwenye masuala ya uongozi wa kisiasa. Na hili ni jambo ambalo nimelifanya kwa makusudi, kwa kipindi cha miaka mitano ya uongozi wangu.

  Tumefanya mabadiliko makubwa kisera na kimkakati. Mfano, tumebadilisha Katiba ya chama, kadi za uanachama, bendera na rangi zake na hata sera. Mabadiliko yaliyoipa CHADEMA sura mpya, kikaonekana chama kipya lakini ni kile kile cha miaka yote. Na ilikuwa muhimu kujenga sura mpya, tukazindua chama upya, kikiwa tumaini jipya.

  Lakini kwenye kila jambo kuna mazuri na mabaya. Sioni makosa au jambo lolote tunalolijutia kiuongozi kama ulivyouliza, ingawa makosa ya hapa na pale yanaweza kuwapo, lakini hakuna kubwa sana la kutisha.

  Swali: Ni yapi hayo makosa ya hapa na pale mliyowahi kufanya?

  Mbowe: Madogo madogo ambayo mnakosea mnaweza mkajikuta mnafanya uamuzi ambao si mzuri. Kwa mfano, uamuzi wa kushirikiana na vyama vingine vya upinzani tulikuja kugundua umetupotezea mwaka mmoja na nusu kwa sababu pengine dhamira za wenzetu (viongozi wa vyama vingine) hazikuwa sahihi.

  Wakati tukifikiria tunaweza kuunganisha vyama na kuvijenga kwa pamoja, tulikuwa na dhamira moja tu ya kuungana ili kupata madaraka, lakini hatukuunganisha fikra zetu na malengo yetu kwamba je, yanafanana?

  Swali: Kwa maelezo hayo, tuseme wakati mwingine viongozi mnakuwa dhaifu kupima na kuchambua mambo ili mfikie uamuzi sahihi, na mkajikuta mnashirikiana na watu ambao kumbe dhamira zinatofautiana?

  [​IMG]

  Mwenyekiti Freeman Mbowe

  Mbowe: Ni jambo la kawaida katika uongozi mahali popote, mnaweza kufanya uamuzi ambao unawagharimu. Uamuzi wa kushirikiana na vyama vingine tulikuwa tunajaribu kujibu kiu ya muda mrefu ya wananchi kutaka vyama viungane, vishirikiane.

  Lakini kitu ambacho mara nyingi wananchi hawajui ni kwamba je, hawa viongozi ni wakweli, wanadhamira moja, wana malengo yanayofanana? Sasa watu wanafikiria tu kuungana kwa ajili ya kuing’oa CCM, lakini kuungana kwa ajili ya kuing’oa CCM bila malengo ya baada ya kuing’oa CCM, inakuwa muungano au ushirikiano wenye misingi dhaifu.

  Swali: Kwenye uchaguzi mdogo wa ubunge Tarime, viongozi wa kitaifa wa vyama walielekeza wananchi waunge mkono mgombea asiye wa CHADEMA, lakini wenyeji wa kule wakasema tutamuunga mkono mgombea wa CHADEMA na akashinda. Huoni wakati mwingine ushirikiano huo unawanufaisha?

  Mbowe: Niboreshe kauli yangu. Ushirikiano mahali popote una matunda mema, lakini ni vizuri kutofautisha viongozi na wananchi. Wananchi na viongozi wa ngazi za chini wanataka tuungane, lakini viongozi wa kitaifa hawaioni hiyo dhana kwa dhati, wamekuwa na mtazamo au malengo tofauti.

  Sasa wananchi wa kawaida si wajinga. Kwa kadiri muda unavyokwenda wamejua chama gani kipo makini na ni kipi hakipo makini. Wakati tunakwenda kwenye chaguzi ndogo kilikuwa ni kielelezo tosha kwa wananchi kuonyesha hata kama vyama vitano vinashiriki uchaguzi wataunga mkono CHADEMA kwa sababu wanakiamini.

  Wanaunga mkono tunayosimamia kama chama, si sura ya Mbowe au kiongozi yeyote kwenye CHADEMA. Tunasimamia kwa vitendo mustakabali wa taifa letu, raslimali za taifa na vita dhidi ya ufisadi. Tumekuwa mstari wa mbele kupigania haya na wananchi wanaona CHADEMA ni tofauti na vyama vingine.

  Kwa hiyo, tunaona badala ya kupoteza muda zaidi kushauriana na viongozi wa kitaifa ambao pengine malengo yetu yanatofautiana, ni bora tulenge moja kwa moja matakwa ya wananchi wa kawaida.

  Swali: Hii maana yake nini, hasa kwenye uchaguzi mkuu wa mwakani. Je, CHADEMA itasimamisha mgombea kila jimbo la uchaguzi, hata kwenye majimbo ambayo wagombea wa chama kingine cha upinzani wataonekana kukubalika?

  Mbowe: Si lazima. Kwenye siasa kuna kitu kinaitwa Strategic Alliance (umoja mkakati) ambayo inaweza kuwa na mazingira tofauti kutoka jimbo moja hadi jingine. Nakiri siku zote tunaamini katika ushirikiano na chama madhubuti na makini, chama kinachofanya siasa ni utumishi wa umma, na si ajira au mchezo.

  Bado tunayo nia ya kushirikiana lakini lazima kiwe chama serious. Kwenye strategic alliance ninayozungumza ni kwamba tuko tayari kushirikiana na vyama vingine lakini kubwa zaidi ni je, ushirikiano huo unalenga nini?

  Swali: Mtatumia kipimo au vigezo gani kuamini kuwa chama fulani mnachotaka kushirikiana nacho kipo serious?

  Mbowe: Hayo ni mambo ya ndani, sitaweza kuyazungumza hapa.

  Swali: Kuna kosa jingine mmewahi kufanya ukiwa mwenyekiti, na hasa katika kampeni za uchaguzi mkuu 2005?

  Mbowe: Uchaguzi wowote unahitaji sana raslimali watu, fedha na vifaa mbalimbali. Tulivyoingia uchaguzi 2005, CHADEMA tulikuwa na upungufu mkubwa wa raslimali watu, fedha na wagombea (ubunge).

  Tulikuwa na wagombea 166 kati ya hao 10 kutoka visiwani, baadhi yao hawakuwa na nyezo walikuwa wanategemea makao makuu ambako sisi viongozi pia tulikuwa wagombea. Tulifanya kampeni katika mazingira magumu, ilibidi wengine tutoe fedha zetu tukisaidie chama angalau tuendeshe kampeni katika baadhi ya majimbo tu.

  Wapo waliolalamika kuwa tumetumia helkopta; eti ni gharama kubwa. Haikuwa gharama, hatujutii na hata kwenye vikao rasmi vya chama tumekubaliana tuendelee kuitumia.

  Ulikuwa ubunifu uliotuwezesha kukuza chama kwa haraka sana.

  Kwenye kampeni kuna mambo mawili. Kushinda uchaguzi na kufikisha ujumbe. Nina hakika tulifikisha ujumbe vizuri sana na ndiyo kati ya mambo yaliyoipa CHADEMA misingi mizuri ya kukua.

  Swali: Kwa hiyo wabunge walioshinda 2005, walitumia zaidi nguvu na uwezo binafsi?

  Mbowe: Kweli, kuna maeneo yaliyokuwa na mtandao wa chama kama Karatu na Kigoma. Lakini, bado ni kweli wabunge walitumia zaidi raslimali zao, ingawa walisaidiwa kidogo na chama.

  Swali: Mara baada ya uchaguzi mkuu 2005 mlianzisha kampeni maalumu kujenga mtandao wa chama chenu iliyoitwa “CHADEMA ni msingi.” Je, ilifanikiwa na sasa imefia wapi hadi inaibuka Operesheni Sangara?

  Mbowe: Kujenga chama ni mchakato wa kudumu. Kila siku mnakuwa na mkakati ambao mnaweza kuutathmini na ikibidi kubadilisha mbinu za kiutekelezaji. Ni uwendawazimu kuwa na mkakati wa milele usiofanyiwa tathmini au kubadilishwa ili kuufanikisha.

  Ni kweli baada ya uchaguzi ilibidi kupeleka mawazo mapya kwa wananchi, tukiwa na operesheni ya tumaini jipya tukijua tunahitaji kujenga chama kwa wananchi wa kawaida. Tukawa na programu iliyoitwa "CHADEMA ni msingi" ikilenga kujenga chama kwenye kaya au familia ya kila Mtanzania.

  Swali: Kabla ya kifo chake, huo mkakati wa CHADEMA ni Msingi ulifanikiwa kwa asilimia gani?

  Mbowe: Ulifanikiwa, tulifanya majaribio na ulifanikiwa kwa baadhi ya maeneo kama Karagwe lakini kwingine ulifeli. Ilionekana unatumia raslimali nyingi na matokeo yasiyoridhisha. Tukabadilisha mbinu licha ya kwamba dhana ya CHADEMA ni Msingi ilibaki.

  Tukabadili na kuwa Operesheni Sangara tuliyozindua Mwanza, Septemba 15, 2007, tukafika ngazi ya kata, vijijini tunaweka uongozi wa chama na kufungua matawi.

  Swali: Kuna malalamiko kwamba, Operesheni Sangara ilitumika kufanya kampeni kabla ya muda rasmi kutangazwa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) kwenye chaguzi ndogo za ubunge, unasemaje kuhusu hili?

  Mbowe: Si kweli. Hii dhana ya muda rasmi wa kampeni imepitwa na wakati. Kampeni inaweza kufanyika wakati wowote, kazi ya chama cha siasa ni ya wakati wote, huwezi kusema ni kipindi fulani tu.

  Kipindi chote tunafanya siasa, hiyo ni dhana tu ya mtazamo wa kizamani, ingawa pia tulijua majimbo fulani kuna uchaguzi ilikuwa jukumu letu kuweka mtandao huko ili kujiandaa. Huo ni wajibu wetu kisiasa, sio kusema tumekiuka sheria za uchaguzi kwa sababu bado hatukuwa tumeweka mgombea.

  Swali: Hatujui Operesheni Sangara itakwisha lini, nadhani utatuambia leo, lakini tueleze imefanikiwa kwa kiasi gani hadi sasa?

  Mbowe: Operesheni Sangara imefanikiwa sana. Tumefanya mkoa wa Mwanza, Kagera, Mara, Kilimanjaro, Dar es Salaam, Mbeya lakini bado tutaendelea, dhamira yetu ni kupita mikoa yote kabla ya Uchaguzi Mkuu wa 2010.

  Hatuna muda maalumu wa kuhitimisha operesheni hiyo mpaka Uchaguzi Mkuu 2010 kwa sababu mambo mengi yamekuwa yakiingilia kama ratiba za wabunge wetu wanapokuwa bungeni, kampeni za chaguzi ndogo zilivuruga sana mwenendo wa operesheni hiyo.

  Tungetakiwa tuwe tumepita asilimia 60 ya mikoa yote, tunataraji kuendelea baada ya huu uchaguzi wa ndani ya chama.

  Swali: Uendeshaji Operesheni Sangara unahitaji raslimali kama kampeni. Kwa mujibu wa maelezo yako, mwaka 2005 hamkuwa na fedha za kutosha. Mnamudu vipi kuendesha operesheni, fedha zinatoka wapi?

  Mbowe: Operesheni Sangara inachangiwa na vyanzo viwili vya mapato. Kwanza ni ruzuku ya chama iliyoongezeka kutoka milioni 5 kabla ya 2005 hadi milioni 65, baada ya 2005. Lakini kinachofanikisha zaidi Operesheni Sangara ni michango ya viongozi, wakiwamo wabunge.

  Operesheni Sangara inahitaji vifaa vingi. Kwa mfano, msafara mmoja una magari hadi 15 na vifaa vyake kupeleka viongozi kwenye kata na maeneo mengine, unaweza kukuta kwenye hayo magari 15, matatu tu ndiyo ya chama mengine 12 ya viongozi wanajitolea bure. Kama utapiga hesabu za fedha kukodi ni hesabu za kutisha.

  Viongozi wetu wanachangia fedha taslimu na tunapokwenda kwenye operesheni, viongozi kuanzia mwenyekiti na wabunge tunatoa fedha, hatulipwi. Tunajitahidi kuwalipa wenzetu tunaoambatana kwenye misafara.

  Kwa hiyo CHADEMA imejengwa zaidi kwenye misingi ya kujitolea kuliko kujilipa.

  Swali: Tathmini yenu ikoje kwa kulinganisha juhudi hizo na matarajio kwenye uchaguzi mkuu ujao?

  Mbowe: Nisingependa kupiga ramli kwenye suala hilo, isipokuwa niseme Operesheni Sangara imefanikiwa sana, maeneo tofauti na Tarime ambako ni kwetu, kama Busanda eneo jipya, Mbeya Vijijini na Biharamulo tumetoa changamoto kubwa kwa CCM. Kwa hiyo tukisema tuna matarajio gani uchaguzi ujao hatusindikizi mtu wala chama, tunakwenda na dhamira ya kuja kuunda serikali.

  Swali: CHADEMA imekuwa na uhusiano na vyama vya nje ya nchi. Uhusiano wenu na Chama Cha Conservative cha Uingereza umejikita maeneo gani...ni uhusiano wa kupewa fedha, mafunzo, vifaa…ni nini hasa?

  Mbowe: Uhusiano wetu na Conservative unapitia WFD ambayo ni Westminster Foundation For Democracy. WFD ni taasisi iliyoko chini ya Wizara ya Mambo ya Nje ya Bunge la Uingereza, ni idara inayojenga demokrasia duniani. Vyama vyote vitatu vikuu vya Uingereza, ambavyo ni Labour, Conservative na Liberal Democrat, vyote vinaingiza fungu fulani la fedha WFD kusaidia kujenga demokrasia na uhusiano wa kimataifa na vyama mbalimbali duniani. Kwa hiyo, utaona Conservative haiwasiliani tu na CHADEMA bali na vyama mbalimbali duniani kupitia WFD.

  Swali: Nini maslahi ya huo mtandao kwenu, mnaunganishwa na ajenda gani au kwa sababu sera zenu zinafanana?

  Mbowe: Si rahisi kuwa na sera zinazofanana, sera za chama Uingereza au Marekani haziwezi kufanya kazi Tanzania kutokana na utofauti wa mazingira. Hatuunganishwi kwa sera bali ni masuala tunayoamini yana maslahi kwa umma.

  Mfano, wote tunaamini kuwa na serikali ndogo katika nchi, lakini yenye ufanisi mkubwa. Tunakubaliana kuwa na soko huru wenzetu wanataka soko huru ambalo haliingiliwi na serikali, sisi tunataka soko huru linaloweza kuingiliwa na serikali inapobainika maslahi ya taifa yanapotea.

  Tunakubaliana katika mfumo wa vyama vingi vya kisiasa na mengine. Uhusiano wetu unajengwa kwenye mazingira hayo, tuna uhusiano na vyama vingine sio Conservative pekee, mfano; Republican na Democrat vyote vya Marekani, UNDP cha Ghana, Chama cha Ujerumani anachotoka Kansela Angela Markel na vyama vingine vingi.

  Huko kwa wenzetu tunatumia fursa hiyo kujifunza masuala kama ya chaguzi na hata kampeni zao, wanatuletea watalaamu wakati mwingine kutufundisha.

  Na suala la kifedha, Conservative hawatujengi kifedha kama wengi wanavyofikiri kwamba tunapata mabilioni. Ukweli ni kwamba hatupewi fedha kwa mtazamo huo, ingawa pia wameweza kufadhili miradi midogo ya mafunzo na kuchapisha vitabu.

  Swali: Hivi karibuni mmezindua utaratibu mpya wa kuingiza wanachama kwa simu za mkononi. Hili wazo limetokea wapi na limeingiaje CHADEMA?

  Mbowe: Ni wajibu kwa kila kiongozi au mwanachama kutafuta mbinu ya kukijenga chama. Kila siku shida inafundisha watu na sisi tuna shida kubwa ya nyezo. Kwa hiyo kila siku tunalazimika kubuni mbinu ya kukabili shida hiyo kwa kupata fedha za halali na si za kifisadi. Nasisitiza…fedha safi za halali zisizo za kifisadi.

  Swali: Ukisema fedha safi na halali maana yake nini…zipi fedha chafu na haramu?

  Mbowe: Fedha chafu na haramu ni fedha za kifisadi. Zilizoibwa Benki Kuu ya Tanzania kwenye EPA, zikatumiwa na CCM kwenye uchaguzi 2005. Fedha chafu pia ni fedha za watu wasiolipa kodi katika taifa hili. Fedha za wanaoifadhili CCM ili kuficha madhambi yao…hizo zote ni fedha chafu na haramu zilizopatikana kwa kuuza mashirika ya umma kiharamu, watu wamenunua mali za umma kiharamu halafu wanapeleka mafungu ya fedha CCM, hizo ndizo fedha chafu.

  Wapo Watanzania wengi wenye uwezo mkubwa wa kiuongozi lakini wanashindwa kupata uongozi kwa sababu hawana fedha za kuwawezesha kwenye kampeni, kampeni siku hizi zimegeuzwa kama biashara ya fedha, ni mnada mwenye fedha nyingi ndiye anayeshinda. Kwa hiyo tunajaribu kukiweka chama katika nafasi ya kupata fedha halali kutoka kwa wananchi wake.

  Pesa ndogo ambazo hazitamuumiza mwananchi wa kawaida ili hatimaye wapate viongozi bora watakaowezesha taifa kupata viongozi waadilifu, wasiochaguliwa kwa fedha zao bali kwa uwezo wao wa kuongoza.

  Tukipata wagombea safi wenye fedha kama akina Mzee Ndesamburo well and good lakini kama hawana, tutatumia hizo fedha za wananchi kuwawezesha kupata uongozi.

  Nilivyokwenda Marekani kwenye mkutano mkuu wa Chama cha Democrat cha Obama, tulikuwa na kitu kinaitwa ILF - International Leaders Forum. Kwa wiki nzima tuliangalia mikakati ya wenzetu walivyojipanga kwenye kampeni na walifanya vipi kuchangisha fedha.

  Nikajifunza umuhimu wa kuunganisha michango ya fedha na wapiga kura. Wenzetu walitumia zaidi internet na wanazo kadi za benki zinazotumika kununua bidhaa, asilimia 99 ya Wamerekani wana akaunti, na hivyo wanaweza kulipa chochote kupitia credit card na internet - ilikuwa rahisi kwao, walimwezesha Obama na timu yake kukusanya fedha nyingi sana.

  Kwa hiyo, utaona Obama hakujifunga kwa matajiri wakubwa. Shida tunayoona kwenye taifa letu leo, Rais Jakaya Kikwete amefungwa na matajiri wakubwa na mafisadi kwa sababu hao ndiyo wafadhili wakubwa wa kampeni zake.

  Sasa uhuru wa taifa unapotea pale uongozi wa nchi unapokuwa umesimikwa na fedha za watu wachache wachafu, lakini inapokuwa wananchi wote kwa ujumla wamechangia kuwaweka viongozi na hasa wananchi wadogo kiuchumi kwa kutoa shilingi 200 au 300, kunakuwa na uchungu wa wananchi wote. Kwa hiyo, mambo haya tumejifunza huko.

  Tukatafakari mazingira hayo ya kuchangisha fedha kwa akaunti na internet na tukaona ni tofauti na ya hapa Tanzania. Kwa hiyo tukaona tukitumia mtindo wa sms tutawafikia wananchi wengi na kwa haraka. Watanzania wengi hawana akaunti wala credit card lakini wengi wana simu, kwa hiyo kupitia simu tunaweza kupata fedha safi na halali ambazo haziwezi kumfanya mtu yoyote ajione amekinunua chama au utawala wa taifa kwa sababu shilingi 300 ni kidogo.

  Swali: Kwenye taasisi za serikali zinazopaswa kuhalalisha mpango huo wa simu za mkononi, mapokeo yalikuwaje?

  Mbowe: Hofu zipo kwenye taasisi za umma, jambo lolote linalofanywa na upinzani kwenye taasisi za serikali hupokelewa kwa hofu sana, na hiki ni kithibitisho kwamba serikali imekuwa ikitumia taasisi zake kukandamiza upinzani.

  Baadhi ya watendaji hawafanyi kazi zao kwa uhuru kwa kuzingatia kanuni za sheria wakihofia kukikwaza Chama Cha Mapinduzi, lakini kwa kuwa ni mambo ya kisheria na hayana utata tulifanikisha.

  Swali: Kwenye uchaguzi wa mwenyekiti mshindani wako, Kabwe Zitto, kwa kushauriwa na wazee alijitoa, unazungumziaje hatua hiyo?

  Mbowe: Kwenye suala hili kuna mambo mawili ya kuzungumza. Kwanza haki ya kila mwanachama kuwa kiongozi, hiyo tunaisimamia bila kujali wagombea walikuwa katika kundi moja la uongozi unaomaliza muda wake. Pili; kama viongozi au wanachama, tuna wajibu zaidi kwa chama wakati mwingine haki zetu zikiwa nyuma.

  Kwa hiyo, tuna wajibu ndani ya chama kuangalia tunachokipigania kama taasisi, nini wajibu wetu kitaifa. Hivyo, tunapozungumzia wajibu wetu kitaifa moja kwa moja tunaangalia jambo lenye manufaa zaidi kwa chama.

  Kukijenga chama imara cha upinzani si kazi nyepesi, lakini kukibomoa chama cha upinzani ni kazi ya siku moja na chama kikiporomoka kukifufua ni kazi ngumu mno.

  CHADEMA ni chama cha watu, siyo cha Mbowe, Zitto au mtu mwingine yoyote. Kwa hiyo maamuzi yetu binafsi siku zote ni lazima yaangalie yana maslahi gani kwa chama, tunaweza kutenda demokrasia, lakini kwa gharama ya kuua upinzani Tanzania.

  Tutakuwa tumelisaliti taifa. Kwa hiyo ni lazima sisi viongozi na wazee wa chama tushauriane na kushaurika kwamba, jamani sawa tuna demokrasia; lakini kwa demokrasia hii tuna hatari yaani tunafanya experiment (majaribio) ambayo inaweza kuligharimu taifa.

  Tunaweza kusema kweli ni demokrasia lakini tukatengeneza kambi mbili ndani ya chama na unapotengeneza kambi mbili ndani ya chama, chama hakiwezi kuwa kimoja tena. Mtaanza kuwindana badala ya kukijenga chama chenu na tunajifunza, kwenye chama cha siasa uhuru na demokrasia yoyote ina mipaka.

  Swali: Maana yake nini, je, mnaweza kubadili utaratibu wa kupata mwenyekiti au viongozi wengine?

  Mbowe: Tunaweza kutazama na kuamua kwa busara na manufaa ya chama chetu na taifa kwa siku za usoni kuwa na utaratibu au mfumo mzuri zaidi wa namna ya kuepusha mgawanyiko kama huu.

  Wengine wamehukumu kwamba CHADEMA wameminya demokrasia, sisi tunawauliza wenzetu CCM wanaopiga hiyo kelele mbona majina ya wagombea urais wao hawapeleki yote kwenye mkutano mkuu na anapokuwa rais anayepaswa kumaliza awamu ya pili, wanapitisha jina moja?

  Kwa hiyo, wakati mwingine tunajifunza. CCM wapo kwa miaka mingi, kuna vitu tunaweza kujifunza. Kwa sura ya haraka haraka mnaweza kuona ni kuua demokrasia lakini kwa mtazamo mpana pengine ni njia ya kukiimarisha zaidi chama chetu.

  Swali: Kuna shutuma dhidi yako kuhusu matumizi mabaya ya ruzuku, una majibu gani kuhusu suala hili?

  Mbowe: Niseme tu kwamba, ruzuku ni asilimia 50 tu ya fedha za kuendesha chama, zilizobaki tunachangia sisi viongozi. Watanzania waelewe viongozi wa CHADEMA tunajitolea hatulipwi mshahara, tunajitolea raslimali zetu na muda wetu.

  Pili, chama kinapata ruzuku ya Sh. milioni 65 lakini CCM wanaozusha hayo, wanapata ruzuku ya Sh. bilioni mbili, hawazungumzii hizi. Lakini jambo jingine ni kwamba, mimi kama mwenyekiti wa chama ningestahili kupata malipo - mshahara, nyumba, mafuta ya gari, simu, walinzi; lakini hizo zote chama hakinilipii na ukienda CHADEMA hutakuta vocha yoyote kuhusu mwenyekiti kuchukua pesa.

  Swali: Chama hakikulipi kwa sababu hakuna huo utaratibu au kwa wewe binafsi hutaki?

  Mbowe: Tumeamua kama viongozi wakuu tusijilipe, na hata Kamati Kuu ya CHADEMA ilitoa agizo kwa sekretariati ya chama (taifa) itoe shilingi milioni tano kila mwezi kwa ajili ya shughuli mbalimbali za ofisi za mwenyekiti.

  Kama mwenyekiti, nina shughuli mbalimbali za kusafiri, kuhudhuria hafla za kikazi au mikutano, shughuli hizi zinazohitaji fedha.

  Kwa hiyo, chama kiliona mzigo ambao mwenyekiti naubeba kugharimia mambo hayo, wakapitisha utaratibu nipewe shilingi milioni tano kila mwezi isaidie kuniwezesha, lakini tangu kamati kuu itoe maagizo hayo, sijawahi kuchukua hata senti tano.

  Sikuwahi kuchukua fedha yoyote kwa sababu najua chama hiki kikiishiwa kinakuja kwa Mbowe, kwa Ndesamburo, kwa Dk. Slaa, kwa Zitto na wabunge wengine kuomba misaada.

  Sasa kama tunapeleka misaada kwenye chama halafu tunakuja kuchukua fedha hizo, tunafanya nini? Shutuma za kula ruzuku naamini ni uwendawazimu.

  Kwenye vikao vyetu vya chama bajeti inapelekwa kwenye Kamati Kuu ya watu 34 makini. Wapo Bob Makani, Balozi Ngaiza, Edwin Mtei, Profesa Mwesiga Baregu, wapo mawakili, wenyeviti wa mikoa, wabunge kama akina mzee Arfi na Ndesamburo, wote hawa watakuwa wanaangalia tu hela za chama zinaliwa?!

  Na Mwenyekiti hahusiki na masuala ya fedha, anayesimamia ni Katibu Mkuu, lakini kwa sababu wanaamini katika falsafa ya mpige mchungaji na kondoo watatawanyika, basi lawama zote zinatupiwa kwa Mbowe.

  Hakuna suala ninaloamua binafsi, kwa hiyo ni propaganda za kupakana matope.

  Swali: Kwa mujibu wa hotuba yako ya kufungua mkutano mkuu, mipango yenu mipya ni pamoja na kuanzisha kamati ya maadili kwenye CHADEMA. Bado mnakusudia kubadili muundo wa chama chenu?

  Mbowe: Cha msingi kama chama tunajiweka katika mfumo wa kwenda kwenye kampeni za uchaguzi mkuu, kwa hiyo tunakwenda kuimarisha kanda mbalimbali za chama, tunakwenda kuwatafuta na kuwafunza wagombea mapema, na kutengeneza ilani katika ngazi mbalimbali za chama.

  Swali: Kabla hujaendelea, kuwa na wagombea mapema, maana yake nini...je, mtakuwa na wagombea mtakaowatangaza kabla ya muda rasmi wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi?

  Mbowe: Sahihi kabisa, tunakusudia kwamba tuandae wagombea ubunge kwenye majimbo mapema sana. Hatutaki wale wagombea wa kukurupuka dakika za mwisho, tunataka wagombea ambao wanapokwenda kugombea tayari wanakuwa wamepimwa kwa vigezo, kwa sababu tunataka wabunge imara wanaoweza kupeleka taswira na dhamira yetu kama CHADEMA, mbele ya umma.

  Swali: Huoni kwamba mkitangaza wagombea wenu mapema mtakuwa mnaingilia misingi ya demokrasia, ambayo inaruhusu wanachama wengi kuchukua fomu na kupitishwa kwenye mchakato rasmi kuliko kuteua tu?

  Mbowe: Hapana, viongozi wa kuibukia mwishoni si viongozi imara. Kila chama kina mkakati wa kupata wagombea hata kama fomu zinatolewa kupata wagombea wazuri tunapima historia ya mtu katika chama, uwezo wake, uwajibikaji wake na kujituma kwake.

  Hatutaki wabunge wa kuibukia mwishoni. Sasa hivi wanachama wetu wajue mapema na hili tumelitangaza mara nyingi.

  Kwamba mtu yoyote anayetaka kugombea udiwani, ubunge aje kwenye chama, ajitambulishe, afanye kazi, aelewe sera na falsafa ya chama.

  Tunapopeleka makada wetu kuwa viongozi ndani ya serikali au bungeni wanakuwa wanakijua chama. Hawa watu wa kukurupuka dakika za mwisho kwa sababu wamekosa fursa CCM wakakimbilia CHADEMA, ni watu wanaowinda tu fursa, lakini si kweli wana nia ya kukitumikia chama.

  Swali: Kuna shutuma kwamba CHADEMA ni chama cha ukoo na wanakutazama wewe na Mzee Edwin Mtei ambaye ni mkwe wako, wanaona muunganiko wa kifamilia, unazungumziaje hilo?

  Mbowe: Jambo lolote lina chimbuko lake, Mtei alikuwa muasisi wa chama hiki wakati tayari mimi nimemuoa binti yake. Kwa hiyo, masuala ya uhusiano na familia ya Mtei yalianza kabla ya mfumo wa vyama vingi kuanza - hilo la kwanza.

  Pili; kila Mtanzania ana haki zake binafsi za kikatiba, kwa hiyo kuoa mtoto wa Mtei hakunifungi mimi kuwa kiongozi wa chama cha siasa kama nachaguliwa na watu. Nimechaguliwa na mkutano mkuu, sikuchaguliwa na familia ya Mtei.

  Na wote mlikuwa mashuhuda, kwamba mkutano mkuu ulikuwa na wajumbe kutoka wilaya zote za Tanzania hadi Pemba. Wote hao si ukoo wa Mtei, hiyo ni shutuma dhaifu.

  Ingekuwa vyeo vyetu tunapeana, hilo ni suala tofauti. Mimi nimechaguliwa kutokana na mchango na uwezo wangu kisiasa ndani ya chama.

  Ninaweza nikasema nimekuwa na msimamo usioyumba ndani ya chama na ndiyo sababu wakanipa awamu nyingine ya uongozi.

  Lakini pia, kumekuwa na hizi hofu za ukabila ambazo ni propaganda. Wakisema kina Ndesamburo mbunge, mkwewe mbunge, mtoto wake naye mbunge; lakini tunarudi pale pale, kila mtu ana haki ya kuwa mgombea; lakini watu hawa wanapozungumza hivi ni watu wa CCM.

  Hawazungumzi ndani ya chama chao CCM kuna nini. Malecela na mkewe ni wabunge, kwa hiyo tuite CCM ni chama cha Malecela? Sitta na mkewe ni wabunge na mmoja ni Spika, mwingine ni waziri, Msekwa alikuwa Spika na mkewe waziri, Kigoda ni mbunge na dada yake ni mbunge, Shelukindo na mkewe ni wabunge, Baba wa Taifa Mwalimu Nyerere, mwanawe Makongoro Nyerere ni Mwenyekiti wa mkoa anakotoka Nyerere.

  Vita Kawawa yuko bungeni, Ridhiwani, mama yake (Salma Kikwete) na Kikwete mwenyewe wapo CCM; sasa huwezi kuwanyima watu hawa uhuru wao wa kisiasa kwa sababu eti ni wanafamilia au wanandoa. Kila mmoja ana haki ya kugombea, hata wana-CCM mimi siwalalamikii.

  Unajua kuwa mwanasiasa wa upinzani ni maumivu, kuwa CHADEMA ni maumivu. Kama Wachaga walisukumwa kuiunga mkono CHADEMA wasihukumiwe, wapongezwe kama watu jasiri kukomboa taifa hili.

  Hakuna kabila lolote wala mtu yeyote aliyetaka kuingia CHADEMA akanyimwa nafasi.

  Hata ukiangalia kwenye kamati kuu iliyopita kulikuwa na Wachaga wanne tu kati ya watu 34 ambao ni mimi Mbowe, Mzee Mtei anayeingia kama mwanzilishi na mwenyekiti mstaafu, Ndesamburo aliyeingia na kofia yake kama Mwenyekiti wa Mkoa wa Kilimanjaro kwa upande wa chama, Grace Kiwelu akiwakilisha wabunge kwa sababu wabunge wetu wanawakilishwa kwenye kamati kuu.

  Lakini wengine 30 ni wa makabila mengine nchini. Huwezi kuniambia kina Baregu, Ngaiza, Mbogoro, Akunai, Slaa, Zitto, Arfi, Mhonga Saidi na wengine; hao wote ni Wachaga. Na kundi hili ndilo linafanya uamuzi ndani ya chama.

  Sasa habari ya kuwanyanyapaa Wachaga mimi inanisikitisha sana, na hatuwatendei haki kwa sababu kama wote wangekwenda CCM wakashiriki kwenye ufisadi, sijui Watanzania wangesema nini? Lakini wanatoa fedha zao, raslimali na muda wao kukomboa taifa hili, na si kukomboa Kilimanjaro.

  Hawa wanakwenda kupiga kampeni Biharamulo, Rufiji, Mpanda Rukwa. Ni kulikomboa Taifa, sio kukomboa Kilimanjaro. Kwa hiyo, badala ya kuhukumiwa Watanzania wangewaenzi kwa sababu hakuna kabila lolote kwenye nchi hii limezuiwa kuingia kwenye harakati za mageuzi.

  Lakini ni ukweli kuwa Mkoa wa Kilimanjaro umetoa wanamageuzi wengi wa vyama vingi, sasa kama kigezo ni uchaga, kuna vyama vingine vina Wachaga mbona vinakufa?

  CHADEMA leo kinashamiri. Shutuma zote hizi mimi nasema mti wenye maembe ndiyo unaotupiwa mawe. CHADEMA leo kinakubalika nchi nzima, na ndiyo sababu CCM kinaibua propanda hizi ili kukichafua na kuwajaza hofu wananchi.

  Swali: Kuna madai umechukua mkopo NSSF na kugoma kumalizia malipo, unazungumziaje suala hili?

  Mbowe: Mkopo ni msingi wa kufanya biashara halali, ningesikitika kama mtu angedai nimeiba pesa mahali lakini nimekopa hela halali kwa taasisi halali kwa miradi halali, tukashindana katika utaratibu wa malipo. Hili si kosa, wala sio ufisadi.

  Swali: Imekuwaje mshindwane wakati mikopo ni lazima iwe na makubaliano ya kisheria?

  Mbowe: Kwanza mkopo wenyewe umepotoshwa. Wanasema Mbowe anadaiwa bilioni mbili, pesa niliyokopa mimi ni milioni 15, na katika milioni 15 nimeshalipa milioni 75. Sasa tulishindana katika kitu kinaitwa riba, na ndiyo maana kesi ipo Mahakama Kuu.

  Hata Mahakama Kuu wameona kuna msingi wa kisheria. Hapa tulishindwana katika riba kwamba wakati kesi ipo Mahakama Kuu ni halali kuendelea kutoza riba ya asilimia 31 iliyokuwa kwenye mkataba, sheria za madai zinasema tangu kesi inapopelekwa Mahakama Kuu riba ya kibenki inakoma, inaanza riba ya ki-mahakama ambayo ni kati ya asilimia saba na 12.

  Hapo ndipo kwenye ubishi wetu na inakuwa ni simple interest na si compound interest. Sasa kesi ile imekaa mahakamani miaka 10. Siyo kosa langu, na kukaa mahakamani miaka 10 wao wanadai riba ya asilimia 31 ambayo ni tofauti na utaratibu wa kisheria.

  Kwa hiyo ni masuala ya kawaida ya kibiashara kwamba watu wanadaiana. Mimi nimekopa mabenki mengi…nimekopa CRDB nimelipa, nimekopa Barclays nimelipa, nimekopa Stanbic nimelipa, nimekopa NBC nimelipa, naendelea kukopa nitalipa.

  Hata mwaka huu nimekopa nitalipa, kwa sababu nawekeza. Mimi ni mwekezaji wa hapa nchini na nje ya nchi.

  Kwa hiyo ninapowekeza, najiamini kabisa nawekeza kwa mikopo halali. Sasa hawa wanaosema Mbowe amekopa NSSF hajalipa, ni propaganda za kisiasa, na baada ya kuwahi kuwajibu sikusikia wakisema tena.

  Lakini kudai na kudaiwa kwenye taratibu za kibiashara ni jambo la kawaida kabisa, na mara nyingi unapokuta biashara kubwa haidaiwi, kuna uwezekano mkubwa hiyo ni biashara inayoendeshwa kifisadi.


  Chanzo: http://www.raiamwema.co.tz/news.php?d=1702
   
 2. Josh Michael

  Josh Michael JF-Expert Member

  #2
  Sep 18, 2009
  Joined: Jun 12, 2009
  Messages: 2,525
  Likes Received: 5
  Trophy Points: 135
  Chadema Siku zote itakuwa Imara, Na Kama kweli CCM wanataka kuwa Makini basi wanapaswa watambue kuwa Chama ambacho Kitatoa pressure kubwa kwa serikali na watu wote na kuona Taifa letu linelekea kule ambapo watu wengi tunaota kuwa sehemu nzuri basi wanapaswa kuruhusu watu huru na makini na kuacha Chama Makini kama CHADEMA
   
 3. M

  Mfwatiliaji JF-Expert Member

  #3
  Sep 18, 2009
  Joined: Oct 5, 2007
  Messages: 1,325
  Likes Received: 5
  Trophy Points: 0
  Safi sana M/kiti Mbowe. Maelezo yako yametulia
   
 4. Ngalikihinja

  Ngalikihinja JF-Expert Member

  #4
  Sep 18, 2009
  Joined: Sep 1, 2009
  Messages: 16,428
  Likes Received: 3,790
  Trophy Points: 280
  Isije ikawa nguvu ya soda kama ilivyokuwa NCCR Mageuzi..............
   
 5. J

  Jasusi JF-Expert Member

  #5
  Sep 18, 2009
  Joined: May 5, 2006
  Messages: 11,484
  Likes Received: 165
  Trophy Points: 160
  Hii ni wishful thinking ya wale wanaofaidika na status quo.
   
 6. A

  AmaniGK JF-Expert Member

  #6
  Sep 18, 2009
  Joined: Jan 10, 2008
  Messages: 1,101
  Likes Received: 28
  Trophy Points: 145
  Huyu jamaa ana nguvu sana katika kujenga hoja na tumani pia katika utekelezaji anaweka nguvu kama hizi pia
   
 7. Semilong

  Semilong JF-Expert Member

  #7
  Sep 18, 2009
  Joined: Mar 5, 2009
  Messages: 1,711
  Likes Received: 41
  Trophy Points: 145
  amejibu maswali yake vizuri sana, mambo karibuni yote wananchi wanayotaka kuyajua ameyatolea ufafanuzi
  hajakimbia hoja kama JK alinavyokimbia hoja, "unaweza kuirudia kuisoma"
  kaza buti mbowe usisikilize fitina za wana ccm
   
 8. M

  Magezi JF-Expert Member

  #8
  Sep 18, 2009
  Joined: Oct 26, 2008
  Messages: 2,827
  Likes Received: 87
  Trophy Points: 145
  maelezo mazuri, kaza buti kiongozi
   
 9. Kilasara

  Kilasara JF-Expert Member

  #9
  Sep 18, 2009
  Joined: Dec 21, 2008
  Messages: 578
  Likes Received: 5
  Trophy Points: 0
  Hongera Freeman Mbowe. Uzi ni huo huo!

  WanaJF wanaotakia Tz mema walinganishe majibu haya ya Mbowe na yale ya JK aliyotoa kwa Tido Mhando wa TBC juma lililopita.
   
 10. IronBroom

  IronBroom JF-Expert Member

  #10
  Sep 18, 2009
  Joined: Jun 12, 2008
  Messages: 524
  Likes Received: 2
  Trophy Points: 35
  Big up Mbowe kwa majibu mazuri.Hongera zaidi mkuu Godfrey Dilunga kwa kuuliza maswali haswa.
   
 11. Lunyungu

  Lunyungu JF-Expert Member

  #11
  Sep 18, 2009
  Joined: Aug 7, 2006
  Messages: 8,836
  Likes Received: 75
  Trophy Points: 145
  Ndiyo inavyo takiwa mtu kujijua kwa nini ni kiongozi na ameomba uongozi ili iwe nini . Thanks so much Mwenyekiti
   
 12. Field Marshall ES

  Field Marshall ES JF-Expert Member

  #12
  Sep 18, 2009
  Joined: Apr 27, 2006
  Messages: 12,659
  Likes Received: 69
  Trophy Points: 0
   
 13. Field Marshall ES

  Field Marshall ES JF-Expert Member

  #13
  Sep 18, 2009
  Joined: Apr 27, 2006
  Messages: 12,659
  Likes Received: 69
  Trophy Points: 0


  - Again do we have demokrasia au hatuna? I mean tunawezaje kutenda demokrasia kama kweli tunayo si inajitenda yenyewe kikatiba, sasa demokrasia tunayoweza kuitenda when we feel like ni demokrasia ya kweli au ni ya kutenda tu tukitaka?

  - Eti wakuu ni kweli haya maneno yamesemwa na Mwenyekiti wa chama cha demokrasia makini?, is this a demokrasia makini inayoweza kutendwa na kutokutendwa depending on the situation?

  - Eti is this kind of demokrasia Chadema, envision for our nation wakipewa utawala wa taifa, yaani demokrasia ya kuvizia, between viongozi na wazee wa chama?

  Respect

  Kamanda Es!
   
 14. J

  Jasusi JF-Expert Member

  #14
  Sep 18, 2009
  Joined: May 5, 2006
  Messages: 11,484
  Likes Received: 165
  Trophy Points: 160
   
 15. Field Marshall ES

  Field Marshall ES JF-Expert Member

  #15
  Sep 18, 2009
  Joined: Apr 27, 2006
  Messages: 12,659
  Likes Received: 69
  Trophy Points: 0


  - Demokrasia makini ya experiment, is that so? Somebody help me haya maneno yamesemwa na Mwenyekiti aliyegombea urais wa jamhuri, kwamba ndani ya chama chake kuna demokrasia ya exeperiment and not a real demokrasia?  - wow! wow! anasema kwamba ana wasi wasi kwamba should Chadema practice a true demokrasia then kutakuwa na makundi na kuwindana, why is that?

  - Ina maana either wanachama wa Chadema, au viongozi wa chama, bado kuelewa na kuikubali demokrasia ya kweli kwamba ndio the way to go, maana ikifanyika kweli basi itakuwa ni kuwindana that is incredible jamani kama kweli I am reading right na betweeen the lines, au?

  - Halafu toka lini demokrasia ikawa na mipaka ya kuamuliwa na busara tu za wazee wa chama, badala ya mipaka ya katiba ya chama?

  - This is incredible, mbona CCM wanafanya kuminya katiba na demokrasia why not us Chadema?


  - Anasema Chadema kuiminya demokrasia leo, it is okay, ili kuimarisha chama chao cha kesho, this is sad very sad indeed! Wakuu nimesikitishwa sana na hizi quotes, infact siamini kwamba haya maswali yaliulizwa kwa papo kwa papo, nina wasi wasi kwamba kuna faulo ilifanyika, na besides ya kutojali demokrasia kwa sababu ya kuimarisha chama, yanasikitisha sana, ingawa ameongea mengine mengi mazuri, lakini kwenye the heart of the matter, mapungufu ni makubwa mno kwa maoni yangu.

  Mungu Aibariki Tanzania!

  Respect.

  Kamanda FMEs!
   
 16. J

  Jasusi JF-Expert Member

  #16
  Sep 18, 2009
  Joined: May 5, 2006
  Messages: 11,484
  Likes Received: 165
  Trophy Points: 160
  Kamanda,
  Soma tena kwa utulivu. You may come to a different conclusion.
   
 17. Field Marshall ES

  Field Marshall ES JF-Expert Member

  #17
  Sep 18, 2009
  Joined: Apr 27, 2006
  Messages: 12,659
  Likes Received: 69
  Trophy Points: 0
   
 18. J

  Jasusi JF-Expert Member

  #18
  Sep 18, 2009
  Joined: May 5, 2006
  Messages: 11,484
  Likes Received: 165
  Trophy Points: 160
   
 19. Field Marshall ES

  Field Marshall ES JF-Expert Member

  #19
  Sep 18, 2009
  Joined: Apr 27, 2006
  Messages: 12,659
  Likes Received: 69
  Trophy Points: 0
  - Jasusi is it with your clear conscience, unaposema kwamba nikirudia tena this quotes nitakuja to a defferent conclusion? kwamba it is a good thing kuiminya demokrasia na katiba ya chama kwa manufaa ya chama, na kuepusha kuwindana should a full demokrasia be allowed to be practiced ndani ya chama, na kwamba this is good kwa masilahi ya taifa in the future, infact even TANU did it na hata CCM are still doing it, sasa why not us Chadema?

  - Jasusi, kweli are you supporting this very backwards ideas mkuu na kwamba eti nikisoma tena I might come to a different conclusion, like what mkuu?

  Respect.

  FMEs!
   
 20. J

  Jasusi JF-Expert Member

  #20
  Sep 18, 2009
  Joined: May 5, 2006
  Messages: 11,484
  Likes Received: 165
  Trophy Points: 160
  Kamanda,
  Ningependa kuendelea huu mjadala lakini nina kasafari kadogo kwenda kumwona rafiki yangu Ganesh pale NY. Labda nikirudi na topic bado ni ya moto nitaendelea nayo. Meanwhile soma tena kwa utulivu usirukie snipets za quotes here and there. Ni demokrasia iliyotumika katika chama kichanga kama Chadema na hata ushauri wa wazee ulikuwa ni katika context hiyo hiyo ya demokrasia. Nina hakika CCM wangefurahi kuona Chadema wanakatana mapanga lakini haikutokea.
   
Loading...