Chadema na Kisa Cha Mjukuu Mchawi

Abdull Kazi

JF-Expert Member
Dec 29, 2012
322
255
08/12/2013 | Posted by Abdallah Khamis | Makala | 0 comments | 48 views |
KATIKA makuzi yangu, marehemu babu yangu Abdallah Idd, alinisimulia kisa cha bibi aliyemfundisha mjukuu wake masuala ya uchawi.
Bibi alianza kumpa mafunzo mjukuu wake katika umri mdogo ili ashike kikamilifu kwa muktadha wa kumrithisha kile alichokuwa akikifanya.
Mjukuu alikua na akafikia umri wa kwenda shuleni kusoma, ambako alichanganyika na vijana wenzake wengi. Katika mchanganyiko huo wapo waliokuwa manunda, wanyonge na waoga.
Miongoni mwa makundi hayo, mjukuu aliyefuzu uchawi kwa kiwango cha juu alikuwa katika kundi la wanyonge hali iliyomfanya aonewe kila mara, na aliyekuwa akimuonea alikuwa ni kijana anayeongozana nae mara kwa mara.
Katika kuonewa huko, mjukuu alienda kushitaki kwa bibi yake ili apate ridhaa ya kumdhuru mtemi wake kishirikina.
Bibi alimsikiliza mjukuu wake, akampa ushauri namna ya kutimiza malengo yake bila kuathiri taswira yake mbele ya jamii.
Alimpangia mikakati na muda wa kutekeleza malengo yake, na sharti alilopewa ni kuwa asubiri kipindi cha masika mvua itakaponyesha ili kumdhuru kijana aliyekuwa akimuonea.
Masika ilifika, mjukuu akamrudia bibi yake na kumueleza kuwa ni wakati wa kutekeleza mpango wake wa kulipa kisasi. Bibi kwa busara zake akamwambia avute subira na atekeleze malengo yake katika kipindi cha kiangazi.
Mjukuu akaukubali ushauri huo. Aliendelea kuvumilia mateso na ubabe wa mtemi wake, lakini akiwa na tumaini la kumshughulikia kitakapofika kiangazi.
Kiangazi kilipofika, mjukuu alimfuata bibi yake akitaka jambo lake lifanyike, lakini akastaajabu alipoambiwa asubiri tena hadi masika. Jibu hili lilimnyong’onyeza, akaanza kukata tamaa ya kutimiza azima yake.
Siku moja wakati mjukuu aliyefundishwa uchawi akiwa amekataa tamaa ya kutekeleza nia yake, yule mtemi akakorofishana na kijana maarufu mtaani kwao. Ugomvi wao ulikuwa mkubwa na ukawavuta watu wengi kushuhudia.
Kijana mtemi kwa kuwa alikuwa ni mpiganaji mzoefu, alimuadabisha mgomvi wake kwa kiwango kikubwa kiasi cha kuwaogofya wengine.
Hata hivyo, katika ugomvi huo walijitokeza waungwana wakauamua, lakini yule kijana mtemi hakuisha kujinasibu kwa kumshikisha adabu mpinzani wake aliyekuwa akigaagaa chini kwa maumivu ya kipigo alichokipata.
Yule aliyeachwa akigaagaa chini, kwa sababu ya umaarufu aliokuwa nao hakutaka kuonyesha kuwa ameshindwa katika ugomvi ule, alianza kujitapa kuwa wasingekuwa waungwana waliowaamua angemuonyesha kazi mpinzani wake.
Huku akijipangusa vumbi iliyochanganyikana na damu katika uso wake aliinuka kutoka alipokuwa na kuanza kutoa maneno ya kujiapiza kuwa “utaniona, nitakuonyesha, ipo siku utajuta.”
Taarifa za ugomvi huo na vitisho vya kijana maarufu vikamfikia bibi aliyekuwa na mjukuu mchawi, naye akaona huo ndio muafaka wa kumshauri mjukuu wake kutimiza malengo ya kulipa kisasi pasipo kujulikana.
Mjukuu akapewa rungu na matunguri ya uchawi na kwenda kumdhuru mbaya wake ambaye alishasahau ugomvi wao.
Alitimiza lengo lake la kumdhuru mbaya wake, na huo ukawa mwisho wa maisha ya kijana yule kwakuwa alikufa katika mazingira ya kutatanisha.
Wananchi waliposikia kifo cha kijana mtemi, wakamgeukia aliyetoa kauli za vitisho hadharani na kumhusisha na kifo kile bila kujua hakuhusika kwa namna yoyote ile.
Kwa hasira walizokuwa nazo walianza kumpiga kwa fimbo hadi kusababisha kifo cha kijana yule ambaye hata hivyo hakupata muda wa kueleza kutohusika na kifo cha mgomvi wake.
Maziko ya vijana hao wawili yalihudhuriwa na watu mbalimbali, akiwemo mjukuu mchawi aliyekuwa akijisifu moyoni alivyotimiza azima yake kwa ustadi mkubwa bila kushukiwa.
Mjukuu yule alijiona ni mshindi, huku jamii ikiendelea kumuona kuwa ni kijana mvumilivu na mnyenyekevu asiyependa ugomvi.
Nimeikumbuka hadithi hii niliyosimuliwa zaidi ya miaka 20 iliyopita kutokana na hali inayoendelea sasa ndani ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA).
Kabla na baada ya kuvuliwa nafasi ya uongozi kwa Naibu Katibu Mkuu wa chama hicho, Zitto Kabwe, mjumbe wa Kamati Kuu, Dk. Kitilla Mkumbo na Samson Mwigamba aliyekuwa Mwenyekiti wa CHADEMA Mkoa wa Arusha, kulikuwa na majibizano yasiyoridhisha katika mitandao ya kijamii.
Kwa baadhi yao, wapo waliotuhumiwa kusambaza waraka unaodaiwa kuwa ni wa uongo kwa lengo la kuuchafua uongozi ulio madarakani. Pia kuwapo kwa nyaraka zinazoonyesha namna Zitto anavyotumiwa na baadhi ya taasisi za serikali kuidhoofisha CHADEMA.
Katika muktadha huu, iwe kweli au si kweli juu ya nyaraka zilizowekwa katika mitandao ya kijamii, ukweli utabaki kuwa wapo wabaya wa CHADEMA waliojitokeza wakiwa na malengo maalumu.
Wapo walioamua kuwa upande wa Zitto kwa makusudi huku wakijulikana waziwazi kuwa ni wapinzani wa CHADEMA kiitikadi, lengo likiwa ni kuzidisha mpango mkakati wa wanachadema kutokuwaamini viongozi wao.
Wapo waliokuwa upande wa nyaraka waliojitambulisha kuwa wafuasi wa CHADEMA na kumuonyesha Zitto kuwa ni msaliti.
Mpambano wa hatua hii ulihitimishwa na majibizano ya moja kwa moja baina ya Mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema na Zitto, hata hivyo CHADEMA makao makuu iliingilia kati na kuwataka kumaliza tofauti zao katika vikao vya chama.
Katika mlolongo wote huu wa kwenye mitandao ya kijamii, kila upande ulipata watu wa kuwaunga mkono na dhamira ya uungwaji huo ikiwa imesimama katika hali ya kuwagawa na si ya kuwaunganisha.
Dhamira ya watu hawa wa kati waliojichagulia upande ukichunguza kwa umakini si kusaidia upande wowote katika mzozo huu wa Zitto, Dk. Mkumbo, Mwigamba na chama chao zaidi ya kuwabomoa na kuwa manufaa ya chama kilicho madarakani.
Wakati mtafaruku huo ukiwa katika mapumziko ya muda Kamati Kuu ya CHADEMA ikaitisha kikao cha kawaida ambacho Zitto hakuhudhuria siku ya kwanza, lakini siku ya pili alihudhuria na kusomewa mashitaka yake.
Mashitaka yaliendeshwa na hukumu ikatolewa. Waliohukumiwa wamepokea katika mitazamo yao.
Baada ya kuvuliwa nyadhifa viongozi hao wa CHADEMA, pia mijadala mbalimbali imekuwa ikiendelea katika jamii kupitia mitandao, na bado wengi wamesimama katika kuwagawa badala ya kutafuta muafaka.
Katika hali rahisi kutambulika, sasa CHADEMA si moja tena, kuna kundi la uongozi ulio madarakani na kundi linalomuunga mkono Zitto, na huu ni mkakati wa hali ya juu umetengenezwa kwa dhamira ya kukimaliza chama hicho.
Namna wanamkakati wa mipango hii wanavyojipenyeza katika kuhakikisha mtafaruku hautulii ndani ya CHADEMA, inadhihirishwa na matamko yanayotolewa na viongozi mbalimbali wa CCM, huku wale wanaosadikiwa kuwa katika kundi la Zitto, ambao awali walikuwa CHADEMA, wameamua kushiriki katika mchezo huu.
Hili linadhihirishwa na namna Habibu Mchange na Mtela Mwampamba walivyokuwa wakijishughulisha katika mkutano wa Dk. Mkumbo na Zitto uliofanyika katika hoteli ya Serena wiki chache zilizopita.
Hawa wakiwa wanajulikana kuwa ni watu waliofukuzwa ndani ya CHADEMA na miongoni mwao kujiunga na CCM, walihakikisha wanafanya kila mbinu waonekane wapo karibu na Zitto wakati wa kutoa tamko lake ili kuhitimisha mpango mkakati wa kuthibitisha makada hao ni wasaliti.
Tayari wana mkakati wa mpango huu (mjukuu mchawi) wamefanikiwa. Matamko na kurudisha kadi za CHADEMA mikoani ni kiashirio tosha cha ushindi wao na hakika watu hawa hawatakaa chini kutaka kuona chama hicho kinasimama.
Watamuonyesha mwingine ndani ya CHADEMA kuwa ni tatizo na watapigania hili kuhakikisha chama hiki hakipati kutulia, watakuwa wametimiza dhamira ya kukivuruga pasipo kujulikana.
Mwigulu, Wassira na Lukuvi hawatakaa kimya wakati huu, watalia machozi ya mithili ya mamba kwa kujitengeneza kuwa upande wa Zitto, na kwa kulifanya hilo hakuna atakayefikiria kuwa na suluhu ndani ya chama katika kipindi hiki cha mpito.
Mchange Mtela na Juliana Shonza walioondolewa CHADEMA kwa kushiriki mipango haramu, watatembezwa kila mahali patakapohisiwa watu hawakubaliani na uamuzi wa Kamati Kuu ya CHADEMA, watajipenyeza katika uamuzi wa watu, watapiga picha kwa makusudi ilimradi jamii ijue uwepo wao nyuma ya matamko hayo.
CHADEMA watakaposhituka kuwa ni michezo ya kisiasa, muda utakuwa umeshawatupa mkono. Matumaini ya Watanzania katika kupata mabadiliko yatakuwa yamepotezwa, na watabaki kujiandaa na uchaguzi wa 2020 na si wa 2015.
Source Tanzania Daima Disemba 8

 
Back
Top Bottom