Elections 2010 CHADEMA: Matokeo yetu yamehujumiwa

nina90

Member
Oct 21, 2010
38
0
CHADEMA: Matokeo yetu yamehujumiwa


Na Alfred Lucas - Imechapwa 03 November 2010TUME ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) inatuhumiwa kuhujumu matokeo ya uchaguzi mkuu wa rais, wabunge na madiwani kwa lengo la kukinyima ushindi Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), MwanaHALISI imeelezwa.

Madai hayo yamo katika barua ambayo chama hicho kiliwasilisha jana NEC kulalamikia utaratibu mzima wa kutangaza matokeo.

Katika barua hiyo, mwanasheria wa CHADEMA, Mabere Marando anasema NEC inatumiwa na Chama Cha Mapinduzi (CCM) kuhujumu matokeo hayo ili chama tawala kionekane kimeshinda.

“Wamepanga kupora ushindi wetu. Ndiyo maana unaona kila ambapo CHADEMA imeshinda, CCM wamekataa kusaini karatasi za kura,” alisema Marando.

Akaongeza, “Lakini hata pale ambapo kura za madiwani na wabunge zimetangazwa, matokeo ya kura za rais hayatangazwi.”

Marando alisema NEC inafanya hivi kwa makusudi kwani maeneo ambako CHADEMA haikuwa imeweka mkazo, matokeo ya madiwani, wabunge na ya urais yametangazwa haraka.

Alisema maeneo hayo yametangazwa haraka kwa vile mgombea wa CCM, Jakaya Kikwete ameongoza, lakini katika mikoa ambayo CHADEMA imeshinda, kura za rais hazitangazwi.

“Hii ni hujuma,” anasema. “Kule ambako CHADEMA hatukuwa tumewekeza sana, kwa mfano, mikoa ya kusini hasa Lindi na Mtwara, matokeo yote yametangazwa kwa haraka yakiwamo ya rais.

“Bali, kule ambako chama chetu kimewekeza sana na tumekufanyia kazi vya kutosha, matokeo ya uchaguzi yametangazwa baada ya shinikizo kubwa,” anasisitiza.

Lakini hata katika mikoa ambayo CCM imeshinda, Marando anasema matokeo yanayotangazwa na NEC hayaendani nay ale yaliyokusanywa vituoni.

Anasema, “Huu ni uchakachuaji. CCM ilijiandaa mapema kuchakachua matokeo ya uchaguzi huu. Kitendo cha NEC kuamua kutangaza matokeo ya majimbo ya mikoa ya Lindi, Mtwara, Singida na Dodoma, hakukuwa kwa bahati mbaya. Kumelenga kutoa ujumbe kwa wananchi kuwa mgombea wenu ameshindwa.”

Mwanasheria huyo anasema, “Kwa nini wasitangaze matokeo ya majimbo ya mikoa ya Mwanza, Kagera na Mara, au Shinyanga, Arusha, Kilimanjaro na Manyara ambako mgombea wetu amepata kura nyingi?”

Wakati majimbo ambayo CCM imeshinda matokeo yake yalitangazwa mapema yale ambayo wagombea wa CHADEMA walikuwa wamepata ushindi kama vile Ilemela, Nyamagana yote ya Mwanza; Arusha Mjini; Mbeya Mjini, Biharamulo, Mbulu yalitangazwa baada ya wananchi kushinikiza kwa vurugu.

Hadi juzi usiku wa manane wasimamizi wa uchaguzi katika majimbo ya Ubungo, Kawe na Segerea yote ya Dar es Salaam walikuwa hawajatangaza matokeo ya ubunge na rais.

Msimamizi katika Jimbo la Ubungo, alikaririwa akidai kwamba mfumo wa kujumlisha matokeo kwa njia ya kompyuta ulikuwa umekwama.

Alipopelekewa kompyuta mpya alidai hajaizoea na alipoambiwa wajumlishe kwa mfumo wa kawaida, yeye alisisitiza kura zihesabiwe upya.

Marando alisema hivyo vyote ni visingizio vyenye lengo la kutaka kuchakachua matokeo hayo.

Marando alisema hadi juzi Jumatatu matokeo ambayo tayari walikuwa wamekusanya kutoka katika maeneo mbalimbali ya nchi, yanaonyesha mgombea urais kwa tiketi ya CHADEMA, Dk. Willibrod Slaa anaongoza kwa wastani wa asilimia 61.6.

Aidha, taarifa za ndani ya chama hicho zinasema kuwa Dk. Slaa mwenyewe amepanga kuwasilisha ushahidi mzito unaonyesha uchakachuaji mkubwa wa kura za urais ulivyofanyika.

Mtoa taarifa kwa gazeti hili amesema ushahidi ambao CHADEMA imepanga kuwasilisha NEC, ni pamoja na kile inachoita, “matokeo halisi ya uchaguzi” kutoka kituo hadi kituo.

Inaelezwa kwamba matokeo hayo yaliyokusanywa na CHADEMA kutoka vituoni yanapishana na matokeo ambayo NEC imekuwa ikiyatoa.

“Sijui kama hili linafanyika kwa bahati mbaya, kwamba kompyuta zinazotumika zinatoa taarifa tofauti, huu ni mpango uliosukwa kwa makusudi,” anasema afisa mmoja katika idara ya kompyuta ya CHADEMA.

Anasema, “Tunakwenda NEC kuanika kila kitu. Ni kwa sababu, matokeo ambayo tunayo yaliyotoka mikoani yanaonyesha namba tofauti.”

Alipoulizwa watachukau hatua gani kukabiliana na suala hilo, kwanza Marando amesema, “Kwa hatua ya sasa, tunakwenda NEC.

“Pili, tunakwenda kueleza nchi wahisani ambazo zimefadhili shughuli hii ya uchaguzi, lakini tatu na kubwa zaidi, tunakwenda kwa wananchi kuwaeleza kilichotokea, tena tukiwa na ushahidi kamili.”

Malalamiko haya ya CHADEMA yanakuja siku chache baada ya lori lililoingia nchini likitokea Zambia kukamatwa mjini Tunduma likiwa limesheheni karatasi za kupigia kura ambazo tayari ziliwekewa alama ya vema kwa Kikwete.

NEC ilikanusha kupitia kwa Mkurugenzi wake, Rajabu Kiravu, ikidai lori lile lilikuwa limesheheni vipodozi na si karatasi za kupigia kura.

Lakini katika kituo kimoja cha kupigia kura wilayani Musoma, lilikamatwa lori lililokuwa na karatasi za kupigia kura na tayari zilikuwa zimewekwa alama ya vema upande wa Kikwete. NEC haikutoa maelezo kuhusu tukio hilo.

NEC na serikali ndio wanaochochea wasiwasi huu kutokana na kutoa kauli tofauti. Wakati Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Bunge), Phillip Marmo alisema serikali imenunua mitambo ya kuchapia karatasi za kupigia kura, Tume ya Taifa ya Uchaguzi ilisema karatasi hizo zitachapishwa Uingereza.

Gazeti toleo na. 213
0
 

Toa taarifa ya maudhui yasiyofaa!

Kuna taarifa umeiona humu JamiiForums na haifai kubaki mtandaoni?
Fanya hivi...

Umesahau Password au akaunti yako?

Unapata ugumu kuikumbuka akaunti yako? Unakwama kuanzisha akaunti?
Contact us

Top Bottom