Chief Isike
JF-Expert Member
- Jan 17, 2010
- 445
- 462
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
KAULI YA RAIS JAKAYA KIKWETE NI KILELE CHA USHAHIDI WA CCM KUHUSIKA NA MATUKIO YA MAUAJI YANAYOFANYWA NA POLISI
Kwa kuangalia muktadha wa mtiririko wa matukio ya kudhibiti upinzani kwa kuvuruga kazi za kisiasa za vyama vya upinzani na utoaji wa mawazo mbadala nchini yanayofanywa na vyombo vya dola, hususan Jeshi la Polisi, kwa kuua Watanzania wasiokuwa na hatia…
Halikadhalika kwa kuangalia mtiririko wa mantiki ya hoja mbalimbali za wajumbe wakiwemo viongozi waandamizi kama Rais Kikwete katika mkutano mkuu wa CCM uliomalizika karibuni, hitimisho la kimantiki katika kauli ya Rais Kikwete ni kwamba wapinzani anaomaanisha Rais Kikwete na kuwaambia wenzake kuwa wasitegemee polisi kupambana nao ni; CHADEMA, mtu, watu au makundi mengine ya kijamii ambayo kila yanapodai haki na uwajibikaji nchini, yamekuwa yakihusishwa na CHADEMA.
Kutokana na ukweli huo, Kurugenzi ya Ulinzi na Usalama ya CHADEMA imeona kwa sababu kauli hii sasa imesaidia kumaliza fumbo lililokuwepo juu ya madai ya muda mrefu kuwa Jeshi la Polisi linatumika kisiasa na viongozi wa CCM na watendaji wa serikali, ni muhimu kuweka kumbukumbu sawa.
Kauli hiyo ya Kikwete imetufikisha kwenye kilele cha ushahidi kuwa Jeshi la Polisi linatumika kisiasa kukabiliana na hoja na shughuli halali za kisiasa zinazofanywa na CHADEMA, chama mbadala kwa sasa kinacholenga kuiondoa CCM madarakani, kwa mantiki ifuatayo;
Kikwete amethibitisha pasi na shaka kuwa CCM waliwatumia polisi katika kumuua kijana Ally Singano Zona wakati wanachama na wapenzi wa CHADEMA walipofanya mapokezi ya viongozi wao wa kitaifa siku ya Agosti 27, 2012, mjini Morogoro. Itakumbukwa kuwa tukio hilo lilitokea baada ya mafanikio mazuri ya mikutano ya M4C iliyofanyika katika 95% ya kata na 83% ya vijiji katika majimbo yote mkoani Morogoro, ambako maelfu ya wananchi wasiokuwa na vyama na wengine walioiasi CCM na vyama vingine walijiunga na CHADEMA.
Kauli hii pia imesaidia kufumbua fumbo la kwa nini Jeshi la Polisi Mkoani Iringa, chini ya usimamizi wa RPC Michael Kamuhanda waliamua kutumia nguvu kubwa kuingilia shughuli halali ya CHADEMA kufanya mikutano ya ndani, ikiwemo ufunguzi wa matawi katika Kijiji cha Nyololo, mkoani Iringa, na hatimaye wakamuua Mwandishi wa Habari, Daudi Mwangosi, Septemba 2, 2012.
Kwa kuangalia mtiririko wa matukio ya huko nyuma kama ambavyo tumewahi kuyatolea kauli na taarifa huko nyuma na kuangalia ripoti za uchunguzi wa tukio la Nyololo hasa uchunguzi uliofanywa na Baraza la Habari Tanzania na Tume ya Utawala Bora na Haki za Binadamu (TUBHB), sasa ni wazi kila mmoja anaweza kuona kulikuwa na kila aina ya dalili ya maelekezo ya kisiasa kutumia polisi kuidhibiti CHADEMA.
Kikwete pia amewasaidia Watanzania kuanza kutafuta majawabu kwa nini watuhumiwa wa kesi ya mauaji ya aliyekuwa Kiongozi wa CHADEMA Kata ya Usa River, Msafiri Mbwambo, ambao katika tuhuma zao walishirikiana na viongozi wa CCM kuua, waliweza kutoroka mahakamani mikononi mwa polisi na hadi sasa hakuna hatua yoyote iliyochukuliwa.
itakumbukwa pia namna ambavyo mmoja wa viongozi waandamizi wa CCM ngazi ya taifa ambaye pia ni mbunge wa chama hicho, amekuwa katikati ya tuhuma za kuandaa kikundi cha vijana ili wavuruge mkutano wa CHADEMA katika Kijiji cha Ndago, wilayani Iramba, huku polisi wakiangalia vijana hao wakirusha mawe bila kuchukua hatua yoyote.
Mbali ya kwamba vurugu hizo zilifumbiwa macho na polisi waliokuwepo eneo la tukio wakiongozwa na Mkuu wa Kituo cha Polisi Ndago, zimekuwa zikihusishwa na kifo cha kiongozi mmoja wa UVCCM, aliyekutwa amefariki eneo jirani, baada ya mkutano wa CHADEMA kumalizika.
Aidha kauli ya Mwenyekiti wa CCM, Rais Kikwete imefumbua fumbo juu ya mazingira ya utata yanayozunguka kifo cha kada wa CHADEMA, Mbwana Masoud, kilichotokea Igunga baada ya uchaguzi mdogo, ambaye alikutwa ameuwawa kinyama baada ya kutekwa na kuteswa na vijana wa CCM waliopewa mafunzo ya kufanya kazi hizo katika makambi ya Ulemo, Iramba, Singida.
Itakumbukwa kuwa wakati wa uchaguzi mdogo wa Igunga, CHADEMA kilibaini na kuwasilisha ushahidi polisi ukidhihirisha pasi na shaka kuwa CCM walikuwa wameanzisha makambi wakiwafundisha vijana mbinu za kijeshi kwa nia ya kuteka, kutesa na kuua wanachama na viongozi wa CHADEMA. Vyombo vya dola, wakiwemo polisi na usalama wa taifa, walihusika kutoa mafunzo kwa vijana hao wa CCM.
Upo uthibitisho mkubwa, kama ambavyo umeelezwa na Katibu Mkuu Dkt. Slaa mara kadhaa sasa akimtaka Rais Kikwete kama mwenyekiti wa CCM atoe ufafanuzi, kuwa chama chake kimeingiza silaha za moto bila kibali na kuwapatia vijana wake katika mafunzo kwenye makambi maeneo mbalimbali nchini.
Tangu utolewe ushahidi huo, kwa kutaja aina ya bunduki, namba yake, uwezo wa kubeba risasi na ilikotengenezwa, mbali ya polisi kushindwa kufanya uchunguzi ili kuwaambia Watanzania kwa nini CCM wanaingiza silaha nchini, Mwenyekiti wa CCM, Rais Kikwete ambaye pia ni Amri Jeshi Mkuu, ameshindwa kutoa ufafanuzi wowote, hali ambayo inahatarisha ulinzi na usalama wan chi.
Tunaweza kutaja matukio mengi ambayo kauli ya Rais Kikwete imefunua ukurasa mpya wa kilele cha ushahidi namna ambavyo kuna ushirika kati ya CCM, serikali yake na vyombo vya dola, hasa Jeshi la Polisi, kushughulikia vyama vya upinzani, hususan CHADEMA kwa kuteka, kutesa na kuua raia wasiokuwa na hatia, lengo kubwa ikiwa ni kutimiza matakwa ya propaganda za CCM kuwa CHADEMA ni chama cha vurugu.
Lakini hapa tunaweza kutaja mengine machache. Matukio yote ya chaguzi ndogo na kwa kuanzia uchaguzi wa Kiteto, Busanda, Biharamulo, Igunga, Arumeru Mashariki na chaguzi za juzi za kata 29, upo ushahidi wa wazi namna ambavyo CCM wanashirikiana na polisi, mmoja akimtumia mwenzake kufanikisha malengo ya kisiasa kama ambavyo Rais Kikwete amethibitisha.
Matukio yote hayo hasa katika chaguzi ndogo za ubunge, ambapo viongozi wa CCM na polisi wameshambulia, wameteka na wametesa wanachama na viongozi wa CHADEMA katika shughuli halali za kisiasa, ushahidi wake umewasilishwa polisi kwa ajili ya uchunguzi na sheria ichukue mkondo wake, lakini mpaka sasa hakuna hatua wala taarifa zozote za maana. Hivyo kauli ya Rais Kikwete imefumbua fumbo na sasa Watanzania wanajua zaidi.
Hitimisho.
Watanzania wanajua kuwa matukio ya vyombo vya dola kuhujumu wapinzani na wakosoaji wa serikali ya CCM, kwa nia ya kuilinda CCM, yameanza kwenda mbali ya CHADEMA, kwa sababu sasa hata mtu, watu au makundi mbalimbali ya kijamii ambayo yanaonekana kutoa mawazo mbadala, kudai haki na uwajibikaji yameanzwa kuandamwa. Mifano mizuri hapa ni kufungiwa kwa Gazeti la Mwanahalisi na kutekwa na kuteswa kwa kiongozi wa madaktari, Dkt. Steven Ulimboka.
Rais Kikwete aoneshe dhamira yake kwa kutekeleza barua ya Mwenyekiti wa CHADEMA, Freeman Mbowe, aliyemwandikia kutaka matukio yote ambayo vyombo vya dola, wakiwemo polisi, wametumika kuteka, kutesa na kuua kwa malengo ya kisiasa ya kupambana na wakosoaji wa CCM na serikali yake, vifanyiwe uchunguzi huru, kwa kuunda Tume ya Kimahakama/Kijaji ili ukweli ujulikane na haki ionekane ikitendeka badala ya kutoa lugha ya kisiasa kwa nia ya kujikosha mbele ya umma, lakini nyuma ya pazia CCM na polisi, wanakaa na kupanga mikakati inayopelekea kudhulumu haki na roho za Watanzania.
Aidha, wakati uchunguzi huo ukifanyika, watuhumiwa wote, wakiwemo viongozi wa CCM, serikali na watendaji wa Jeshi la Polisi waliokubali kutumika, hata kuvunja haki za binadamu, katiba na sheria, wanawajibika kwa wao kujiuzulu au kufukuzwa kazi na Rais Kikwete.
Imetolewa leo Novemba 16, 2012, Dar es Salaam na;
Wilfred Lwakatare
Mkurugenzi wa Ulinzi na Usalama CHADEMA