CHADEMA: Kamati iloundwa haifai

Invisible

JF Admin
Feb 26, 2006
16,285
8,340
*Wadai haitakuwa na nguvu za kisheria
*Wasema hawaoni haja ya Zitto kuwamo
*Washauri JK kuunda Tume ya Uchunguzi

VIONGOZI wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) wamesema Kamati iliyoundwa na Rais Jakaya Kikwete kufuatilia sekta ya madini nchini haitawasaidia wananchi kwa madai kuwa zipo kamati nyingi ambazo zilishaundwa katika sekta hiyo lakini hadi leo hakuna ripoti iliyotolewa.

Pia walisema pamoja na Rais Kikwete kuwa na dhamira nzuri ya kuunda kamati hiyo, bado haitakuwa na nguvu kutokana na kwamba imeundwa nje ya Bunge, hivyo kukosa nguvu ya kisheria katika kufuatilia mambo ya madini.

Akizungumza na wanafunzi wa vyuo vikuu vya Dar es Salaam jana katika Maadhimisho ya Kimataifa ya Siku ya Wanafunzi Duniani, Mwanasheria wa CHADEMA Bw. Tundu Lissu, alisema historia inaonesha kuwa zipo kamati nne ambazo ziliundwa kwa ajili ya kushughulikia mambo mbalimbali ya sekta ya madini tangu mwaka 2001, lakini hakuna ripoti ambayo imetolewa na kamati hizo.

Alisema kwa maana hiyo, hata kamati iliyoundwa na Rais Kikwete ambayo inaongozwa na Jaji Mark Bomani, bado wana wasiwasi nayo, kuwa haitaweza kutoa majibu kama inavyotakiwa.

"Binafsi sioni umuhimu wa kuundwa kwa kamati hii, kwa ajili ya kuchunguza mikataba ya madini kutokana na sababu mbalimbali, lakini sababu kubwa hata historia inaonesha, hakuna ripoti au taarifa yoyote ambayo imetolewa kutokana na kamati hizo kuundwa na hii kamati ya Jaji na Zitto ni ya tano," alisema Bw. Lissu.

Alisema sababu nyingine ya kupinga kamati hiyo na kuiona haina umuhimu wowote kwa wananchi, inatokana na baadhi ya wajumbe waliomo ambao wengi wao ni wabunge wa CCM na watumishi wa Serikali, mbali Bw. John Cheyo na Bw. Zitto Kabwe, ambao wanatoka Upinzani.

Vilevile alisema Kamati ambayo ilistahili kufuatilia mambo yanayoendelea katika sekta ya madini, ilipaswa kuundwa na Bunge ambalo lina uwezo wa kisheria na pia lingeipa nguvu Kamati hiyo, kufanya kazi kwa kina ikilinganishwa na Kamati ya Rais Kikwete.

Bw. Lissu alisema kitu ambacho alitakiwa kukifanya Rais Kikwete kabla ya kuunda Kamati hiyo, ilikuwa ni kuliomba Bunge lake liunde Kamati ambayo ingekuwa na nguvu zaidi, kuliko hiyo kwani kamati zote zinateuliwa na Bunge kwa mujibu wa sheria.

"Kama kweli Rais alikuwa na nia ya kutaka kamati yenye nguvu, alitakiwa kuliomba Bunge liiunde au yeye angeunda tume ya kufuatilia matatizo yaliyo katika sekta ya madini. Hivyo kuwapo kwa Kamati hii sasa ni sawa na kiinimacho kwa wananchi," alisema Bw. Lissu na kuongeza:

"Kutokana na Kamati ya Rais kukosa nguvu, sioni hata sababu ya Bw. Zitto kuwamo, kwani ni sawa na kuwa katika ofisi ambayo huna kazi ya kufanya na kibaya zaidi, wajumbe wenzake wengi hawatafanya kazi kama wananchi wanavyotarajia kutokana na wengi wao kuwa maswahiba wa viongozi wanaotuhumiwa kutumia nafasi zao kuingia mikataba ambayo haina manufaa kwa Watanzania," alisema.

Mbunge wa Viti Maalumu, Bi Suzane Lyimo (CHADEMA) alisema Kamati hiyo haina maana kuwapo na inaonesha wazi haitafanya kazi kama inavyotakiwa.

Pia alisema kitendo cha Rais kuunda Kamati, kinaonesha wazi kuwa Waziri wa Nishati na Madini, Bw. Nazir Karamagi, aliliongopea Bunge, kwa kusema mikataba yote ilishapitiwa.

"Kama kweli alisema ukweli kuwa mikataba yote imepitiwa na haina matatizo, kwa nini Rais ameunda Kamati ya kufutalia mikabata hiyo, kwa mantiki hiyo utagundua wazi kuwa wabunge waliongopewa na Bw. Karamagi na kwa maana hiyo, hoja za Upinzani kutaka Kamati Teule, ilikuwa na nguvu na ya msingi kwa manufaa ya wananchi wote," alisema Bi Lyimo.

Hata hivyo, kupitia kongamano hilo, aliwataka wanawake wa vyuo vikuu, kusoma kwa bidii na kuingia katika ulingo wa siasa, ili waweze kutetea haki za wananchi na rasilimali zilizopo.

Mbunge wa Karatu, Dkt.Wilbroad Slaa (CHADEMA), alisema huu ni wakati muafaka kwa wasomi kufuatilia kwa kina mambo yanavyokwenda na kuwa wachambuzi ili kulinusuru Taifa lisifike mahali likapoteza mwelekeo kutokana na viongozi kushindwa kutimiza wajibu wao.

Dkt. Slaa alitumia muda mwingi kuwaeleza wanafunzi hao juu ya ubadhirifu wa fedha aliodai unaofanywa na baadhi ya viongozi wa Serikali na kutumia nafasi hiyo kuwataka wachukie ufisadi kwa vitendo.

"Hivi sasa kuna ufisadi mkubwa unafanyika na watu ambao wataweza kuushughulikia ni wasomi na si vinginevyo, kwani wabunge wameshindwa na ndiyo maana kila siku mambo yote yanakuwa ndioooo...," alisema Dkt. Slaa huku wanafunzi wakimwambia "Why' (kwa nini) endeleaa..."

Dkt. Slaa aliwataka wanafunzi waache kuwa waoga kama walivyokuwa baadhi ya wasomi wanaoogopa kuzungumza ukweli na kuliacha Taifa likielekea pabaya wakati wapo na wanaona mambo yanavyokwenda.

Naye Dkt. Azavel Lwaitama, ambaye ni Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, aliwaambiwa washiriki wa kongamano hilo, kuwa huu ni wakati wa kujadili mambo kwa kina na si kusikiliza fulani kasema nini na mtu kubaki akishangilia.

Alisema suala kubwa lililopo sasa ambalo linatakiwa kufanywa na wananchi wote, ni kusimama imara katika kuangalia mambo kwa undani bila kutoa hukumu.
"Ninachosema ni hivi, huu si wakati wa kusema fikra za Mwenyekiti zidumu, bali ni muda mzuri wa kutafakari mambo ya Mwenyekiti, si kwa sababu unampenda Bw. Zitto au Dkt. Slaa, basi kila kitu anachosema wewe ni kujibu ndiyo bila kufanya uchunguzi," alisema.

Aliwaambia wanafunzi hao kuwa atashangaa kusikia wote waliofika ni wa CHADEMA, kwani kazi kubwa ya wasomi ni kufika katika majukwaa ya kisiasa na kuangalia jinsi wanasiasa wanavyofanya mambo yao na kisha kuyafanyia kazi, kwa manufaa ya Watanzania wote.

Kuhusu ufisadi alisema uwanja huo ni mpana na kuwaambia wanafunzi huo, kuwa hata wao kitendo cha kuiba mitihani ni ufisadi ambao wanaufanya na wanajenga mizizi ya kuwa na viongozi ambao wanapenda kujinufaisha wao, badala ya wananchi wanaowaongoza.

"Hata mkulima anaposhindwa kwenda shamba kwa wakati, naye anafanya ufisadi, hivyo ni kitu ambacho kinatakiwa kuangaliwa kwa umakini zaidi na si kutoa hukumu kwa kumnyooshea kidole mwingine, huku wewe ukijiona uko safi," alisema Dkt. Lwaitama huku wanafunzi wakimsikiliza kwa makini.

Chanzo: Gazeti la Majira
Novemba 18, 2007
 
Mbunge wa Karatu, Dkt.Wilbroad Slaa (CHADEMA), alisema huu ni wakati muafaka kwa wasomi kufuatilia kwa kina mambo yanavyokwenda na kuwa wachambuzi ili kulinusuru Taifa lisifike mahali likapoteza mwelekeo kutokana na viongozi kushindwa kutimiza wajibu wao.
Ungejua wanayofundishwa hapo Chuoni usingesema haya. Wengi wao wanasomea digrii za kuja kuwa mafisadi. Hawasomi ili waje wapate mishahara mikubwa la! ila wanasoma wapate kazi ambayo itawapa mwanya wa kula rushwa full stop.

Kuhusu ufisadi alisema uwanja huo ni mpana na kuwaambia wanafunzi huo, kuwa hata wao kitendo cha kuiba mitihani ni ufisadi ambao wanaufanya na wanajenga mizizi ya kuwa na viongozi ambao wanapenda kujinufaisha wao, badala ya wananchi wanaowaongoza.
Hapo ndio tatizo kubwa lipo Ufisadi unaanzia shuleni na vyuoni. Mawazo yao hata wakiwa shuleni ni kuiba tu.
 
Nawaomba viongozi wa Chadema (Slaa, Zitto, Lissu,n.k) na wengine wote tulio na mapenzi mema na nchi hii kuanza kuelimisha jamii changa (wanafunzi wa primary, nursary, na sekondari kidogo) na hasa wanakijiji wetu waichukie rushwa na ufisadi kwani vyuo vikuu, vyuo, high school, na baadhi ya secondari wamekwisha asilika na huu ugonjwa wa ufisadi na rushwa mawazo yao ni kupata kazi zenye mianya ya rushwa na kutafuna hela za walala puu. hapo ni sawa na kumpa mgonjwa wa ukimwi dawa ya kurefusha maisha. Piganieni hawa ambao hawajaathirika bado wasije wakaambikizwa.
 
msikimbilie vyuoni nendeni vijijini; wekeni mijadala na wanavijiji, wazazi. tutafanikiwa. Waulizeni wasomi kama kuna kazi mbili;

moja ni inahusu manunuzi/procurement/logistic mashahara 500,000na nyingine kuwa plant engineer/IT spe./HR lakini mshahara 900,000 watachagua ipi kama zote pengine anauwezo wa kufanya kazi
 
Back
Top Bottom