CCM Zanzibar sasa washiriki maandamano ya CUF

BAK

JF-Expert Member
Feb 11, 2007
124,792
287,994
Date::1/16/2010
CCM Zanzibar sasa washiriki maandamano ya CUF
ccmzenji.jpg

Maelfu ya wafuasi wa chama cha CUF na CCM Zanzibar wakijumuika katika maandamano ya kuunga mkono kauli ya katibu mkuu wa CUF Maalim Seif Sharif Hamad ya kutaka uchaguzi mkuu visiwani humo usogezwe mbele, Maandamano hayo yalianza katika uwanja wa Maisara na kuishia kiwanja cha Demokrasia Kibanda Maiti jana.*Seif asema Wazanzibari waachiwe Zanzibar yao

Salma Said, Zanzibar

CHAMA cha Wananchi(CUF) jana kilifanya maandamano makubwa yaliyowashirikisha wanachama wa CCM mjini Zanzibar, kuunga mkono maridhiano yaliyofikiwa kati ya Rais wa Serikali ya Mapindizi (SMZ), Amani Abeid Karume na Katibu Mkuu wa CUF Maalim Seif Sharif Hamad Novemba 5, mwaka jana.

Maandamano hayo yalianza saa 2:00 asubuhi katika Viwanja vya Maisara na kuishia Uwanja wa Demokrasia Kibanda Maiti Mkoa wa Mjini Magharibi, yalipambwa na rangi za bendera za vyama vya CCM na CUF pamoja na picha za Maalim Seif na Rais Karume.

Katika maandamano hayo baadhi ya wanachama wa vyama hivyo walibeba mabango yenye ujumbe mbalimbali mengine yakisomeka "Ahsante Rais Karume, ahsante Maalim Seif, tumesamehe na tutasahau, kwa maslahi ya wazanzibari tupo tayari kwa lolote, asiyeitakia mema Zanzibar ni hasidi wa Wazanzibari."


Mengine yalikuwa na ujumbe uliosema: "Kujiamulia sio kuamuliwa, maslahi ya Zanzibar ni makubwa kuliko chama, Zanzibar ni moja ya Waunguja na Wapemba, Zanzibar ipo juu ya CCM na CUF, kuungana sio kutengana, hatima ya Wazanzibari itaamuliwa na Wazanzibari wenyewe zama za giza zimekwisha tukishirikiana, pasipo na mapenzi hakuna maendeleo na viongozi tusipoteze nafasi ya kuwaunganisha Wazanzibari."


Vile vile, ngoma ya mpwaka choka (beni) ya wana CCM kutoka Miembeni na Jang'ombe Mitaa yenye wanachama wengi wa CCM ilichangamsha maandamano hayo. Hii ni mara ya kwanza kwa wana CCM kushiriki maandamano ya CUF tangu kuanza kwa mfumo wa vyama vingi nchini.

Kabla ya maridhiano hayo, wafuasi wa vyama hivyo walikuwa wakiishi kwa uhasama na mara nyingi zilitokea vurugu baina yao zilizoambatana na umwagaji damu.

Mbali ya ngoma hiyo, zumari likiongozwa na Kikundi cha Mji Mkongwe ambako ndio ngome kubwa ya CUF, walipita huku wakionesha manjonjo yao kwa Maalim Seif na wimbo wao maarufu wa 'Yaa Habibi Seif'.

Wimbo maalumu wa taarabu uliotungwa hivi karibuni kwa ajili ya maridhiano ulioimbwa na Mzanzibari Abdallah Issa (Super Star) nao uliibua shangwe kubwa kutoka kwa maelfu ya watu waliohudhuria maadamano hayo.


Kufanyika kwa maandamano hayo kumetokana na kongamano lililofanywa juzi la CUF ili kujadili mustakabali wa hali ya kisiasa na kujenga Zanzibar mpya yenye maridhiano.

Nguvu ya mshikamano visiwani humo tangu kufikiwa kwa maridhiano ya viongozi hao wawili, ilionekana pia Ijumaa wiki hii katika sala ya pamoja ambapo mamia ya Wazanzibar walijitokeza kutoka vyama vyote.


Akisoma risala ya mikoa mitatu ya Unguja, katika maandamano hayo, Mohammed Kombo alisema maridhiano yaliyofikiwa yanaweza kutoa suluhisho la viongozi kuliko uchaguzi ambao wanaamini umechafuliwa.


"Aliyeanzisha maridhiano ndio aendelee nayo, asipewe mtu mwingine kwani anaweza kuacha njiani au kuyaharibu kwa makusudi kwa lengo la kuwaacha Wazanzibari katika giza kama miaka ya nyuma," alisema Kombo.


Akizungumza katika mkutano huo, Katibu Mkuu wa CUF, Maalim Seif alisema yeye na Rais Karume hawatarudi nyuma katika kuwaangusha Wazanzibari kwa kuwa wana nia safi juu ya suala hilo na kwamba, Wazanzibari wamejenga matumaini makubwa kwao.


"Mimi ni CUF kindakindaki na mheshimiwa Karume ni CCM kindakindaki; lakini tumeamua kufanya maridhiano kwa maslahi ya Wazanzibari na haturudi nyuma," alisema Maalim Seif. Alisema kutokana na maridhiano hayo kumekuwepo na mbinu za watu fulani aliowaita wasioitakia mema Zanzibar ambao wanataka kutumia nafasi ya kuwagawa Wazanzibari kwa vyama vyao vya siasa, jambo ambalo alisema halitawezakana na kuwataka wananchi hao wakatae kugawanywa kwa kuwa wametoka mbali katika misukosuko ya kisiasa.


Alisema kwa kuwa Rais Karume ndiye muasisi wa maridhiano anapaswa kuendelea nayo kwa hali yoyote na asijaribu kumuachia mtu mwengine ambaye anaweza kuyaharibu njiani kwa maslahi yake na kuongeza kwamba, Rais Karume akubali maombi ya Wazanzibari.


"Rais Karume ndiye uliyeanzisha maridhiano haya, tena unataka tumpe mtoto nani? Tumpe mwanga? Atamuua…sisi wenyewe tunapaswa kumlea mtoto huyu, hatuwezi kuwapa hawa watu wenye kutia tia maneno; eti wanataka urais.

Hapana ni sawa na wanga watamuua…rekebisha katiba tupate kumlea mtoto wetu," alisema Maalim.


Seif alisema kutokana na maridhiano hayo Watanzania wote kwa ujumla wangefurahi na kuunga mkono kama alivyoonyesha Rais Kikwete.


Alisema ameshangazwa na watu wenye kutilia shaka na kuanza kuleta chokochoko za kutaka kuwagawa Wazanzibari.

"Namshukuru Rais Kikwete, amefahamu na ametuunga mkono na ameahidi kuwa atatumia njia zote kutusaidia katika kuyaunga mkono maridhiano haya.


Mimi nawashangaa hawa wengine ambao wameanza maneno, mimi nilidhani watu wenye akili wote watayaunga mkono; lakini bahati mbaya wanatumia vyama kutaka kutugawa tena, tusikubali kurudi huko tulipotoka jamani," alisisitiza Maalim Seif.


Baadhi ya wanasiasa wakiwamo wasomi kutoka Tanzania bara wameibuka kupinga mapendekezo ya Rais Karume kuongezewa muda yaliyotolewa wiki hii na Maalim Seif.

Juzi Katibu Mkuu wa CCM, Yusuf Makamba alionyesha wasiwasi kuhusu mshikamano unaozidi kukua kati ya Maalim Seif na Rais Karume na akayaponda mapendekezo kumwongezea muda rais wa Zanzibar.


Pia Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, John Chiligati alipinga mapendekezo hayo na kusema rais anayekuja ataendeleza maridhiano yao.


Maalim Seif aliwaomba wananchi kuunga mkono kusogezwa mbele uchaguzi wa Zanzibar ili kuweka mazingira mazuri ya kuingia katika uchaguzi katika hali ya amani na maridhiano hasa kwa kuzingatia chaguzi zote zinazofanyika huwa zinakumbwa na malalamiko na misuguano isiyo ya lazima ambayo matokeo yake husababisha chuki, uhasama na mauaji.

"Uchaguzi ni sumu ya umoja wa Wazanzibari, uchaguzi ni farka ya kutufarakanisha na yeyote anayetaka uchaguzi sasa hatutakii mema anataka kutuua tunakwenda katika uchaguzi tunapigana, tunauana hiyo ni kwa faida ya nani? Hapana tunataka tukifanya uchaguzi uwe safi" alisema Maalim.
 
wazanzibar na Sharif wao wanachekesha, jinsi wanavyotumia hoja dhaifu kulazimisha mambo.
 

Similar Discussions

0 Reactions
Reply
Back
Top Bottom