Zanzibar 2020 CCM yawashukuru Wananchi kwa ushindi uchaguzi mdogo

SautiYaMnyonge

JF-Expert Member
May 13, 2018
439
742
CHAMA CHA MAPINDUZI

TAARIFA KWA UMMA

Chama Cha Mapinduzi tunapenda kuwashukuru wananchi wa Jimbo la Konde wilaya ya Micheweni mkoa wa Kaskazini Pemba kwa kuendelea kukiamini chama chetu na kukipatia ushindi wa kishindo katika uchaguzi mdogo wa jimbo la hilo ambapo mgombea wa CCM Ndugu Sheha Mpemba Faki ameshinda kwa kura 1796.

Jimbo hilo lilikuwa upinzani kwa miaka 15 ni Jimbo la tatu CCM kushinda tangu Ndugu Samia Suluhu Hassan Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuchaguliwa kuwa Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi.

Aidha CCM imepata ushindi katika kata 6 Tanzania Bara ambazo ni Mbagala Kuu iliyopo Manispaa ya Temeke mkoani Dar es Salaam, Kata ya Ndirigishi iliyopo wilaya ya Kiteto mkoa wa Manyara, Kata ya Mitesa iliyopo Wilaya ya Masasi mkoa wa Mtwara, Kata ya Gare iliyopo Wilaya ya Lushoto mkoa wa Tanga, Kata ya Mchemo iliyopo Wilaya ya Newala mkoa wa Mtwara na Kata ya Chona iliyopo Wilaya ya Ushetu mkoa wa Shinyanga.

Ushindi huu umetokana na uaminifu na uadilifu wa Chama Cha Mapinduzi katika kuwasikiliza na kuwatumikia wananchi, aidha unatuongezea ujasiri na nguvu zaidi katika kuendelea kuwatumikia watanzania. CCM inaahidi kuendelea kuwatumikia kwa usikivu, bidii kubwa amani na utulivu kwa kuwa tunao uzoefu mkubwa wa kufanya hivyo.

Chaguzi hizi zinaendelea kutoa funzo kwa vyama vya Upinzani nchini kuwa wasiendelee kutafuta mchawi bali wakae chini wajitafakari na wabadili mtazamo wa namna wanavyofanya na kuendesha siasa zao, sivyo kama wataendelea kutegemea siasa za ukosoaji wa makosa ya serikali inayongozwa na CCM kwa kutumia hoja ambazo hazijafanyiwa utafiti wa kutosha basi utawaoandosha katika ramani za siasa nchini.

Chama Cha Mapinduzi kinampongeza Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Menyekiti wa CCM Ndugu Samia Suluhu Hassan kwa usikivu wake kwa wananchi anaowaongoza na kuamua suala hili la TOZO za miamala ya simu kutizamwa upya.

Ameendelea kuwathibitishia watanzania na dunia kwa ujumla kuwa ni kiongozi Imara, mzalendo, shupavu na mwenye dhamira ya kweli kwa watu wake anaowagonza ili kuwatoa na kujikwamua na umasikini.

Chama kinatoa maelekezo kwa Serikali pamoja na kupitia upya tozo hii ya miamala ya simu, lakini pia iandae utaratibu wa kupitia upya sera na sheria ya kodi na kuratibu ubunifu utakaoibua vyanzo vipya vya kodi ili kupunguza mzigo mzito kwa wananchi, ikiwa ni utekelezaji wa Ibara 18 na Ibara 20 ya Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2020 – 2025.

Chama kinawasisitiza wananchi kuendelea kuiamini na kuiunga mkono serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan na kuendelea kuona fahari ya kulipa kodi kwa hiyari na uaminifu kwa maendeleo endelevu ya taifa letu.

KIDUMU CHAMA CHA MAPINDUZI

Shaka Hamdu Shaka
KATIBU WA HALMASHAURI KUU YA CCM TAIFA, IDARA YA ITIKADI NA UENEZI
19 JULAI, 2021.

IMG-20210719-WA0032.jpg
IMG-20210719-WA0031.jpg
IMG_20210719_204659_620.jpg
IMG_20210719_204659_643.jpg
 
0 Reactions
Reply
Back
Top Bottom