CCM yataka kuimarisha uhusiano na vyama vya upinzani

Mtu wa Pwani

JF-Expert Member
Dec 26, 2006
4,184
671
jee wapinzani wako tayari kwa mashirikiano haya?

au wataona kuwa wanategwa maana wao kila kitu waoga wanaogopa kivuli chao


source majira
Kikwete: Huu ni mwaka wa kushirikiana na wapinzani

Na Maalum, Pemba

MWENYEKITI wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Rais Jakaya Kikwete, ameutangaza mwaka huu wa 2008 kuwa mwaka wa kuimarisha ushirikiano kati ya CCM na vyama vya upinzani nchini.

Pia Mwenyekiti huyo wa CCM amewakumbusha viongozi wa CCM kuhusu wajibu wao kwa wananchi kama unavyotamkwa katika Ilani ya Uchaguzi wa mwaka 2005 wa chama hicho.

Alisema kwamba suala la viongozi wa umma kuonekana wala rushwa na wakosefu wa uadilifu, linasumbua na kuikera jamii.

Hayo ni baadhi ya majukumu saba ambayo Mwenyekiti huyo wa CCM alisema ndiyo ya msingi ya chama hicho kwa mwaka huu.

Majukumu mengine ni pamoja na kuendelea kutekeleza Ilani ya Uchaguzi ya CCM, Kuimarisha uhusiano kati ya CCM na vyama vingine vya siasa, Maandalizi ya CCM ya Uchaguzi wa Serikali za Mitaa, Kushiriki katika uboreshaji wa Daftari la Wapigakura, Kuendelea kusimamia maadili ya viongozi na uongozi, Uchaguzi wa jumuia, na Kutekeleza mradi wa kuimarisha Chama.

Akihutubia katika Sherehe za Kuadhimisha Miaka 31 tokea kuzaliwa kwa Chama cha Mapinduzi leo kwenye Uwanja wa Gombani, Chake Chake, Pemba , Mwenyekiti huyo wa CCM alisema kuwa uhusiano wa vyama una sura mbili ; ushindani na ushirikiano. CCM ilizaliwa Februari 5, mwaka 1977.

Aliwaambia maelfu ya wananchi kwenye uwanja huo: “ Mwaka huu ni mwaka wa kuimarisha mahusiano baina ya Chama chetu na vyama vya upinzani nchini. Kwenye kuendesha mfumo wa siasa za vyama vingi, kuna sehemu mbili. Sehemu ya kwanza ni ushindani na sehemu ya pili ni ushirikiano.”

Aliongeza: “Ushindani ni wakati wa uchaguzi na uchaguzi unapokwisha kwa kuwa wote tunajenga nchi moja, hatua inayofuata ni ushirikiano.”

“Kuimarisha ushirikiano na mahusiano baina ya CCM au Serikali na vyama vya upinzani imekuwa dhamira yangu tangu mnipe heshima ya kuliongoza Taifa letu mwaka 2005,” amesema Mwenyekiti huyo.

Aliwakumbusha wananchi hatua ambazo yeye amezichukua kuelekea katika kutimiza azma hiyo, ikiwa ni pamoja na kuunda wizara mahsusi katika ofisi yake, kwa ajili ya kujenga, kuimarisha, kukuza na kudumisha ushirikiano kati ya vyama vya siasa.

Pia alikumbusha kuwa alilisemea jambo hili katika hotuba yake ya Mwaka Mpya kwa Taifa, usiku wa Desemba 31, mwaka jana.

“Ningependa CCM ioneshe uongozi kwenye suala hili na pia kuonesha njia kwamba siasa za upinzani hazina maana ya uadui, chuki na kutokushirikiana," alisema Mwenyekiti huyo.

Alisema kuwa ushirikiano wa vyama unaweza kudumishwa na kuimarishwa, kupitia taasisi mbili yaani Bunge, na Kituo cha Demokrasia Tanzania kinachoongozwa na Mwenyekiti wa chama cha upinzani cha UDP, Bw. John Cheyo. Serikali inatoa bajeti ya kuendesha kituo hicho kila mwaka.

Mwenyekiti huyo pia alitumia nafasi ya sherehe hizo kufanyika Pemba ambako, kwa muda mrefu, uhusiano kati ya CCM na chama cha CUF umekuwa siyo mzuri, kuelezea maendeleo ya mazungumzo ya mwafaka kati ya vyama hivyo viwili.

“Moja ya dhamira ya mazungumzo yanayoendelea sasa baina ya CCM na CUF ni kubadilisha aina ya mahusiano kati ya vyama hivi viwili, yatoke kuwa mahusiano ya chuki, uhasama na uadui, yawe mahusiano ya kupingana kwa hoja, na kushirikiana katika kuijenga Zanzibar na Tanzania kwa jumla pale uchaguzi unapokwisha.”

Aliongeza; “Dalili zinaonyesha kwamba mazungumzo haya yatafanikiwa katika azma hii adhimu. Tumefika pazuri, Lakini mara nyingi katika mazungumzo kama haya, mwisho ndipo panakuwa pagumu kidogo,lakini tutafanikiwa.”

Kuhusu wajibu wa viongozi wa CCM kwa wananchi, alisema kuwa wajibu huo unaainishwa katika sura ya tisa ya Ilani ya CCM.

Alisema kuwa Ilani ya CCM inawataka viongozi wa chama hicho kuongoza kwa kuonesha mifano.

Alisisitiza: “Tunapopiga vita rushwa, inapendekeza zaidi sisi wenyewe tukiwa waadilifu. Tunapohimiza mapinduzi ya kilimo, basi tuwe na mashamba ya mifano. Ilani inawahimiza viongozi na wanachama wa CCM kuwa mfano wa kuigwa kwa uchapakazi na kujitegemea katika maisha.”

Kuhusu uadilifu na vitendo vya rushwa, Mwenyekiti huyo alisema kuwa suala hilo limeainishwa katika Ibara ya 110 ya Ilani ya CCM.

“Kwa maana hiyo, hatua ambazo Serikali na CCM imekuwa ikizichukua katika kupambana na rushwa, wizi na ubadhirifu, ikiwemo kwenye suala la Benki Kuu, ni utekelezaji thabiti wa maagizo ya Ibara ya 110 ya Ilani ya CCM,” alisema.

Kuhusu kauli yake ya majuzi juu ya umuhimu wa viongozi kutengenisha uongozi wa umma na shughuli za biashara, Rais Kikwete alisema kuwa hatua zitachukuliwa kuweka taratibu wa kutelekeza jambo hilo .

“Katika nchi kama yetu, baada ya kuondoa masharti ya uongozi ambayo yalikuwa na misingi ya kijamaa, panahitajika pawepo masharti mwafaka yanayoendana na mfumo wa uchumi wa soko tunaoufuata sasa.Wenzetu kama sisi wanao utaratibu unaoitwa kwa Kiingereza “Blind Trust,” alisema na kuongeza:

“Yaani wakati ukiwa kwenye nafasi ya uongozi wa umma, hujihusishi moja kwa moja na shughuli za biashara. Unakabidhi shughuli hizo kwa wadhamini wanaoziendesha kwa niaba yako.”

Aliongeza: “Haki zako zinahifadhiwa mpaka siku ukiacha uongozi wa umma, unachukua na kuendelea. Ni utaratibu mzuri ambao unasaidia kumwondolea kiongozi migongano ya kimaslahi na kutiliwa shaka na jamii kuhusu uadilifu wake.”
 
Back
Top Bottom