BAK
JF-Expert Member
- Feb 11, 2007
- 124,790
- 288,165
Posted Date::3/31/2008
CCM yashikwa kigugumizi kutoa maamuzi walioba BoT
* Suala la mwafaka labaki kitendawili
* Yatumpia lawama Maalim Seif
* JK abaki na siri yake moyoni
Na Theodatus Muchunguzi, Butiama
Mwananchi
HALMASHAURI Kuu ya Taifa (NEC) ya Chama cha Mapinduzi (CCM) , imeshindwa kutoa maamuzi mazito kama ilivyotarajiwa na Watanzania, kuhusiana na matukio yaliyotokea nchini hivi karibuni, ikiwamo kuwashugulikia wanachama wake, wanaohusishwa na kashfa ya ufisadi.
Vilevile, imeshindwa kushughulikia Muafaka wa kiasiasa visiwani Zanzibar baina ya ya CCM na Chama cha Wananchi (CUF) na badala yake, imerudisha mjadala wake kwa wananchi ili waweze kuamua kwa kupiga kura za maoni.
Watanzania wengi walikuwa na shauku na matumaini kuwa kikao cha NEC kilichofanyika Kijiji cha Butiama, alikozaliwa Baba wa Taifa, Hatati Mwalimu Julius Nyerere kuanzia Jumamosi hadi Jumapili iliyopita usiku, kingetoa maamuzi makubwa na muhimu kama hatua ya kujisafisha kwa umma, kutokana na kashfa hiyo kwa baadhi ya viongozi wake na wa serikali.
Baadhi ya kashfa hizo, ni ya kutoa zabuni kwa upendeleo kwa kampuni hewa ya kuzalisha umeme wa dharura ya Richmond na kuisababishia serikali hasara ya mamilioni ya fedha.
Kashfa hiyo ilimlazimisha aliyekuwa Waziri Mkuu, Edward Lowassa kujiuzulu na kufuatiwa na aliyekuwa Waziri wa Nishati na Madini, Nazir Karamagi na aliyekuwa Waziri wa Afrika Mashariki , Dk Ibrahim Msabaha, Februari 7, mwaka huu, wakati wa kikao cha bungeni kilichofanyika mjini Dodoma.
Lowassa ni mjumbe wa NEC na alikuwa mjumbe wa Kamati Kuu kwa wadhifa wake wakati Karamagi ni mjumbe wa NEC wa Mkoa wa Kagera.
Suala lingine ambalo lililokuwa linasubiriwa kwa hamu kuamuliwa na NEC ni kuhusu makubaliano ya mwafaka baina ya CCM na CUF yaliyofikiwa hivi karibuni, baada ya kudumu kwa takribani miaka miwili chini ya makatibu wakuu wa vyama hivyo, Yusuf Makamba na Maalim Seif Sharrif Hamad.
NEC , pia ilisubiriwa kwa hamu, kuamua na kupitisha azimio kuhusu hoja ya kutaka kutenganisha shughuli za biashara na uongozi ikiwa ni hatua ya kudhibiti ukiukaji wa maadili ya uongozi, lakini haikufanya hivyo.
Akisoma tamko la kikao cha NEC kwa wajumbe wake na waandishi wa habari baada ya kumalizika majira ya saa 5:00 usiku juzi katika ukumbi wa Mikutano wa Joseph Kizurira Nyerere, Makamu Mwenyekiti wa CCM Bara, Pius Msekwa, alisema halmashauri hiyo, iliyakubali kimsingi mapendekezo yaliyomo katika taarifa ya mazungumzo ya muafaka baina ya makatibu wakuu hao.
Hata hivyo, alisema NEC imeazimia kuwa, ikiwa makubaliano hayo yatakubaliwa, yataleta mabadiliko makubwa katika mfumo wa utawala wa Zanzibar na kwa kuliangalia jambo hilo ni lazima wananchi wote wa Zanzibar washirikishwe kuamua kwa kura ya maoni.
Kutokana na hali hiyo, NEC imeigiza kamati ya muafaka ya CCM kurejea tena katika mazungumzo na wenzao wa CUF, ili kuamua jambo hilo.
Hata hivyo, tamko hilo limesema kuwa, NEC imesikitishwa na tabia ya CUF ya kutangaza makubaliano hayo kinyume na makubaliano kati ya vyama hivyo kwa kuwa lilitakiwa kufanywa kwa pamoja baada ya kufikia mwisho.
Kauli hiyo ya kukilalamikia CUF, imetokana na uamuzi wa Hamad kutangaza baada ya mazungumzo ya mwafaka kukamilika kuwa miongoni mwa mambo yaliyokubaliwa katika mazungumzo yao ni mgawanyo wa madaraka, kwa chama kitakachoshinda uchaguzi kuchukua nafasi ya urais na kingine wadhifa wa waziri kiongozi.
Wakati Hamad anatangaza makubaliano yaliyofikiwa kuhusu mwafaka, CCM kilisema suala hilo lingepelekwa katika kikao cha NEC kupata baraka na ni miongoni mwa ajenda zilizoandaliwa.
Kuhusu azimio la kutenganisha shughuli za biashara na siasa, NEC imeagiza serikali zote mbili kutunga sheria ya kufanya hivyo t kwa viongozi walioko ndani ya vyombo vya dola.
Utaratibu wa kuchanganya nafasi za uongozi na biashara umekuwa ni chanzo cha migongano ya kimaslahi, na ukiukwaji wa maadili na miiko ya uongozi, hivyo Halmashauri Kuu ya Taifa imeazimia kuondoa upungufu huu, ilieleza sehemu ya tamko hilo na kusisitiza kuwa:
Halmashauri Kuu ya Taifa imezingatia kwamba uongozi katika chama si kazi ya kujipatia riziki, japo zipo baadhi ya kazi za uongozi zenye mishahara; hivyo imesisitiza kwa mara nyingine tena kwamba kiongozi wa chama lazima awe na shughuli halali inayompatia kipato cha kuendesha maisha."
Tamko linaitaka CCM ijiimarishe katika taswira yake ya asili kama chama chenye viongozi waadilifu, kinachojali maslahi ya watu na hasa jukumu lake la kutetea wanyonge.
Msekwa, alisema viongozi watakaobainika kuvunja miiko ya uongozi wachukuliwe hatua mara moja na Kamati za Maadili za ngazi zote zitekeleze majukumu yake ipasavyo na kwa nguvu mpya.
Kikao cha NEC hakikutoa tamko lolote kuhusu hatua za kinidhamu dhidi ya watuhumiwa wa kashfa ya Richmond. Badala yake tamko hilo limesema halmashauri hiyo kwa kuzingatia hoja zilizojadiliwa bungeni kutokana na taarifa ya Kamati Teule iliyoongozwa na Mbunge wa Kyela, Dk Harrison Mwakyembe, imeona wananchi wanachukia maovu, hususan wizi, ubadhirifu na rushwa miongoni mwa viongozi na watumishi wa umma.
Hivyo basi, Halmashauri Kuu ya Taifa imewasisitiza viongozi wa chama na serikali wasiwe sehemu ya maovu, kufanya hivyo kunajenga chuki kwa chama na serikali zake. Aidha, zichukuliwe hatua thabiti kupambana na maovu katika jamii mara yanapojitokeza.
Pamoja na hayo, NEC imesisitiza kuwa Bunge kama chombo cha kusimamia serikali katika utendaji wake, halina budi kuwa mstari wa mbele kukemea maovu yaliyofanywa na viongozi, watumishi wa umma na vyombo vya umma.
Msekwa aliongeza kusema kuwa, halmashauri hiyo imesisitiza kuwa, mfumo, utaratibu na madhumuni ya kuwapo kwa Kamati ya Wabunge wote wa CCM yazingatiwe na itumike kuzungumza na kuelewana hasa kuhusu masuala makubwa yanayowasilishwa Bungeni.
Tamko halikuzungumzia chochote kuhusu kashfa kuhusu ufisadi wa wizi wa Sh 133 bilioni kutoka katika Akaunti ya Malipo ya Nje (EPA) ya Benki Kuu ya Tanzania (BoT).
Wakati Mwenyekiti wa CCM, Rais Jakata Kikwete akitangaza kumalizika kwa kikao hicho na kuwaita waandishi wa habari kuingia ukumbini kusikiliza tamko, wajumbe wa NEC walilipuka kwa nyimbo za kukisifia chama hicho na Kikwete.
Kikwete aliufunga mkutano huo kwa kuwaeleza wajumbe kuwa watakutana Mei, mwaka huu, kujadili jambo alilosema ni la siri aliyowaeleza Jumamosi. Hata hivyo hakufafranua.