CCM yasema kujivua gamba,vita ya ufisadi viko palepale

BAK

JF-Expert Member
Feb 11, 2007
124,790
288,006
CHASEMA KUJIVUA GAMBA,VITA YA UFISADI VIKO PALEPALE
Neville Meena na Habel Chidawali, Dodoma
Mwananchi

CHAMA Cha Mapinduzi (CCM), kwa mara ya kwanza kimekiri hadharani kuwa mbio za Urais wa mwaka 2015 ni miongoni mwa mambo yanayokitikisa na sasa kinachukua hatua za kuwadhibiti makada wake wenye nia hiyo ili harakati zake zisikiathiri.Kadhalika, CCM kimesema dhana ya kujivua gamba kiliyoiasisi iko palepale na kwamba utekelezaji wake unaanza mara moja kwa kuwachukulia hatua wanachama wake wote wanaotuhumiwa kwa rushwa na ufisadi.

Katibu Mkuu wa CCM, Wilson Mukama aliwaambia waandishi wa habari jana Mjini Dodoma kuwa si vibaya makada wa chama hicho kuanza kufikiria urais wa 2015 lakini tatizo ni njia ambazo zinatumika katika harakati hizo.

“Sisi hatuna shida na watu hao kwa kuwa ni haki yao, lakini lazima watumie njia sahihi ambazo hazitaleta shida kwa chama na tumeona iko haja ya kutengeneza mfumo mzuri wa kupata mgombea urais ambaye hatatokana na fedha isipokuwa akubalike kwa uwezo wake wa kujenga hoja, itikadi yake na kile anachokiamini,” alisema Mukama.

Mukama alikiri kuwa mbali na mbio za urais 2015, pia CCM kinateswa na siasa za makundi ambayo yamekuwa yakitumika kushambuliana, kinyume cha maadili yake.

Alisema CCM kinachukua hatua za kukabiliana na makundi ambayo misingi yake hujengwa katika chaguzi za ndani ya chama, na kwamba watahakikisha hilo halitokei wakati wa uchaguzi wake unaotarajiwa kufanyika mwakani.

“Kwa maneno ambayo tuliyatumia tulisema, hii kansa ya kupangana safu inaweka mtu ambaye hata sifa wala hana habari kabisa na matatizo ya wananchi, wala haumii lakini anapanga safu… lazima tuondokane na kansa hii ili tupate viongozi wanaojali na wanaohangaika na maisha ya wavuja jasho wa nchi hii,” alisema.

Kujivua gamba

Kuhusu suala la kujivua gamba, akimaanisha kuchukua hatua dhidi ya watuhumiwa wa makosa mbalimbali ukiwemo ufisadi na rushwa, Katibu Mkuu huyo alisema kati ya maazimio 26 yaliyotolewa na NEC Aprili mwaka huu, Azimio namba 27 “linahitaji kutekelezwa haraka iwezekanavyo.”

“Dhana hiyo ya kukipatia chama chetu sura mpya ndiyo iliyopewa jina la kujivua gamba na Sekretarieti ya Halmashauri Kuu ya Taifa imekwishatengeneza mpango wa utekelezaji wa uamuzi huo,’’ alisema Mukama.

Alisema katika kikao chake kilichomalizika juzi, NEC imeamua kuwa viongozi wa CCM wanaotuhumiwa kwa ufisadi ndani ya chama walipaswa kujipima na kujitafakari wenyewe na ikibidi wachukue hatua jambo ambalo halijatekelezwa hadi sasa.

Alisema Azimio hilo liliwalenga viongozi katika ngazi zote za chama kuanzia taifa hadi tawi na kilichokusudiwa ni kujenga utamaduni wa kusimamia maadili ya viongozi na wanachama wake.

“Takriban miezi saba baada ya Azimio hilo kupitishwa, bado hatujapata mwitikio wa kuridhisha kutoka kwa viongozi wa ngazi yoyote wa chama chetu ambao ni walengwa wa azimio,’’ alisema na kuongeza:

“Bila shaka sasa wakati umefika wa chama kutekeleza ile sehemu ya pili ya azimio husika kwa kuwawajibisha wahusika, lakini utekelezaji wake hauna budi ufanyike kwa kufuata utaratibu uliowekwa ndani na kanuni za CCM za uongozi na maadili.’’

Msingi wa mpango wa kujivua gamba umejengwa katika azimio la NEC linalosema: “Viongozi wanaotuhumiwa kwa ufisadi watafakari, wajipime na kuchukua hatua wao wenyewe kwa maslahi ya chama, wasipofanya hivyo, chama kiwawajibishe bila kuchelewa.”

Lakini tangu kupitishwa kwa mpango huo Aprili mwaka huu, ni kada mmoja tu, Rostam Aziz aliyechukua hatua za kujiuzulu Ubunge wa Jimbo la Igunga na Ujumbe wa NEC huku wengine wakiwa kimya.

Mukama alisema sehemu ya pili ya azimio hilo inayosema: “Wasipofanya hivyo chama kiwawajibishe bila kuchelewa,” ndiyo msingi wa NEC kurejesha suala hilo kwa Kamati Kuu na kwamba sasa litafanyika katika ngazi zote.
Alisema NEC imeziagiza kamati za siasa kupitia kamati za ulinzi usalama na maadili kwa ngazi zote kuanza mara moja, mchakato wa kutekeleza azimio hilo kwa mujibu wa kanuni na taratibu za chama.

Alisema NEC iliagiza kazi hiyo kufanyika haraka bila kuchelewa na baada ya kukamilika kwa kazi hiyo, taarifa zipelekwe kwenye vikao vya kikatiba vya uamuzi kwa hatua za utekelezaji.

Alisema chama hicho kitahakikisha kwamba ajenda hiyo haitekwi na makundi yanayokinzana na kwamba lengo zima ni kuhakikisha kwamba CCM kinaongeza uwezo wa kusimamia mambo yake na Serikali zake zote.

“Lazima kifike mahali (CCM), kiwe na uwezo wa kuzisimamia na kuhakikisha kwamba Serikali zinatekeleza matakwa ya wananchi na siyo vinginevyo, ndiyo maana watu wanajiunga na vyama kwani huwa wanatarajia watapata utetezi,” alisema Mukama.

Kuhusu vurugu na migomo ya vyuo vikuu CCM kiliagiza Serikali kuchukua hatua za haraka kukabiliana na hali hiyo na kuitaka kusimamia sheria inayokataza uendeshaji wa shughuli za kisiasa katika taasisi za elimu nchini. Kimetaka wanafunzi na watumishi wabanwe ili waendeshe shughuli hizo nje ya taasisi husika.

Kuhusu suala la Nishati nchini, Mukama alisema NEC imeiagiza Serikali kuhakikisha kuwa inapunguza bei za mafuta na hasa ya taa ambayo yanatumiwa na wananchi wengi wenye kipato cha chini.

Juzi, Mawaziri Wakuu wa zamani, Edward Lowassa na Frederick Sumaye, waliwashambulia kwa maneno makali wajumbe wawili wa Sekretarieti ya CCM kwamba wamekuwa wakikivuruga chama na kusababisha mgawanyiko uliopo kwa jinsi ambavyo wamekuwa wakisimamia mpango wa kujivua gamba.

Lowassa aliyejiuzulu Uwaziri Mkuu, kutokana na kashfa ya Richmond ndiye aliyekuwa wa kwanza kuzungumzia suala hilo wakati wa mjadala wa hali ya siasa, pale alipowataja Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Nape Nnauye na Naibu Katibu Mkuu wa chama hicho, Tanzania Bara, John Chiligati kwamba wamekuwa wakitukana watu ovyo kwa fedha wanazopewa na CCM.

Kwa mujibu wa taarifa hizo, Lowassa alitumia zaidi ya dakika saba kumshambulia Nape kwamba amekuwa akifanya mambo nje ya utaratibu na kwamba mwenendo huo umekuwa ukikibomoa chama badala ya kukijenga.

Sumaye alisimama na kuhoji sababu za chama hicho kunyamazia ukiukwaji wa taratibu ambao umekuwa ukifanywa na watendaji hao.
 
Hawa magamba ni wasanii wa hali ya juu. Kujivua gamba ilikuwa ni kauli ya kuwapa siku 90 Lowassa, Rostam na Chenge wajivue madaraka na kujiondoa chamani vinginevyo watafukuzwa. Sasa gamba wameshindwa kulivua wanakuja na usanii mwingine na kubadilisha kauli....Dah! Siku 90 zimekuwa miezi 7 na magamba bado yanapeta tu ndani ya chama!!!!
 
Inasikitisha kuwa baadhi ya Wanachama wa Chama FODODO baada ya kushabikia waendesha bidii wa chama fulani kudumisha fikra za KUJIVUA GAMBA ziendelee kwa kuwa wao ndio walioasisi kazi hiyo chini ya LIST OFA SHAME.Ajabu baadhi yao humu ndani wamegeuka kasuku wa kutetea bidii ya MAFISADI kuendelea KUPETA NDANI YA CCM, wakati chama chao ndio walikuwa waasisi wa kupigia kelele MAFISADI kupitia LIST OF SHAME YA PALE JANGWANI.

Hakika kwa Mwenye Akil timamu na anaipenda Nchi ni HATARI KUBWA sana KUENDELEA kushadadia uwepo wa MAFISADI ndani ya MFUMO [SYSTEM] kwa tiketi ya CCM.

Kwa kuwa kuingia kwao kwa mbinu za uchafu ndio hivyo hivyo na kwa style hiyo hiyo ya KIHUNI NA UCHAFU watafuta vyama vya UPINZANI na hivyo kulipoteza TAIFA katika msimamo na njia yake ya KUJENGA DEMOKRASIA YA KWELI NA USTAWI WA TAIFA kwa njia sahihi.
 
Huu ni mziki w nzi chooni...wadanganyika na waliwao ni sisi sisiii kumpokanya mtu mpini wakati tuko kwenye makali lazima tuwe Bruce Lee,lazivyo watatutafuna hadi mifupa kama kuku wa kisasa na uongo wao.Eee Mola tusaidie sisi wajawako tupate awezae kutuvusha mto huu wenye mamba {CCM}.Tumebanwa hatusogei washibao ni washache..:ballchain:
 
Tutarajie kuachishwa kazi kwa viongozi/watendaji wengi wa ngazi za chini wa ccm na huu utakuwa mpasuko mkubwa zaidi kwani kutakuwa na vilio nchi nzima wakilalamika kutolewa kafara. Pia hili likitokea litasaidia watz kujitoa kwenye makucha ya ccm.
 
Back
Top Bottom