CCM wana nia ya dhati ya kuwainua wanawake?

Chesty

JF-Expert Member
Aug 30, 2009
5,778
2,720
MTASHANGAA sana enyi ndugu zangu. Nasikia sasa kaulimbiu imebadilika ghafla. Sasa tunaambiwa kwamba ‘wanawake wanaweza,' utadhani kuna aliyewahi kubisha.

Nasema wacha tu niijadili hii mada kuliko kukaa na kijiba cha moyo.


Chonde-chonde enyi watu msije mkadhani nasema wanawake hawawezi, bali nasema yapo mengi ya kuhoji kuhusu hii hamasa ya dharura waliyopata hiki chama nambari wahedi kuhusu uspika kwenda kwa mwanamama.

Nasema tena msije mkaninukuu vibaya wanakwetu.


Nyote si mnamkumbuka yule mzee wetu wa kasi na viwango? Kwa Kiingereza utaita Mzee Six lakini Kiswahili ita tu Sitta.

Baba wa watu si mliona alivyojituma hadi tukaambiwa amejenga na ofisi ya uspika huko Urambo?


Sasa nasikia kuna watu walimmaindi namna alivyokuwa akisimamia mijada hadi wakati mwingine wakubwa wakajikuta kama wako utupu vile.

Basi wengi tukaanza kusikia mizengwe tangu bunge lililopita kwamba bwana mkubwa aliyekuwa spika alikuwa katika hali ngumu mno kisiasa.


Kuna wakora walidokeza eti ilifikia mahali wakataka kumnyang'anya spika mstaafu kadi yake ya chama ila akanusurika. Hayo tuyaache lakini yalisemwa.

Sasa nasikia alipotangaza nia ya kuendelea kukalia hicho kiti na kuvaa lile joho watu wanaojipanga kwa yao wakaona mambo yatakuwa noma mtu wangu.


Hata ambao hawakutazamiwa nasikia nao wakajitutumua kwenda mbio kutafuta hayo madaraka.


Nasikia utamu wa hicho kiti haukuwa masurufu yanayoambatana nacho bali karata za ukubwa 2015! Mnadhani wansiasa hawaoni mbali?

Tayari washaanza kuunda mitandao mtu wangu. Bwana nani hajui Sitta alivyokuwa mahiri kwenye kiti chake? Wakati tukiambia tumwachie JK amalizie mihula yake yote miwili, ilipofika hapo kwa spika, tukaambiwa wanawake kwanza.


Ebo! Mbona hata kwenye urais hatukuwa hao mama zetu? Huko simo wacha nikimbie enyi wana.


Ingawa sina shaka mna uwezo wa Mama Makinda, lakini siku nyingine tuwe makini wakati wa kutoa majukumu.

Tuangalie uwezo na sio jinsia. Katika hili nasema sina mzaha wala utani. Tukubali kwamba wanawake na wanaume ni sawa hivyo hakuna haja ya kupigia debe jinsia moja kama wote tuko sawa.


Tufike mahali tupambanishe umahiri sio jinsia jamani.

Naapa kujidai kuwapendelea watu wa kike badala ya kuanagalia taaluma ipo siku tutawafanya hawa watu wabweteke.


Mnaonaje kama katika majina matatu yaliyotolewa na hawa nambari wani kugombea uspika wangeweka japo jina moja la mwanaume hasa spika aliyemaliza muda wake?


Ina maana wabunge wetu wangeshindwa kujua bora ni yupi? Ikiwa ni mwanamke wangempa kura, kama sivyo wacha iangukie kwa aliye bora zaidi. Naapa kazi ipo kuliko mnavyodhani.

Najua wengi hampendi hiki nisemacho, ila hiyo ndo habari yenyewe. Miye huko smo tena simo kabisa.


Nasikia hata kwenye kusomea taaluma kuna hicho kitu kinaitwa kuwabeba jinsia ya kike. Ninyi watu mmeacha kufikiri?

Fikiria taaluma kama utabibu ukiamua kumbeba mtu kwa sababu alizaliwa wa kike mbona itakuwa balaa?


Mwadhani malaria itaacha kuwa sugu kwa kuwa tabibu anayeishughulikia jinsia yake ni ya kike?

Nenda kwenye sheria, uhasibu, udereva na kwingine kotekote mnakodhania kuna taaluma.


Badala ya kuwabeba hawa watu wawezeshwe kama tunadhani hawapo sawa.

Lakini kama wapo sawa basi wapambane ili waweze kujivunia mafanikio ya nguvu zao.


Mtashangaa sana lakini mimi ni mmoja wa hao wanaopinga kwa nguvu zote hiki kitu kinachoitwa viti maalum.

Mbona kama ni kuwanyanyapaa mnapowapa viti vya "bure"?

Mnaonaje tukawashauri wakafanya kama walivyofanya wakina Halima Mdee na wenzake wachache?


Kama wanaweza nadhani hawahitaji kubebwa. Simo ila huo ndio ukweli wenyewe na habari ndo hiyo enyi waungwana.

Narudia tena kwamba najua nawaudhi wengi ila wacha tu niropoke mtu wangu.


Nasema turudi tena huku kwenye uspika. Kila kinachosemwa na wanasiasa inabidi ukifikirie mara mbili enyi ndugu kabla hamjapiga makofi.

Nimekutana na mama mmoja anashangilia kweli akisema wanawake wakati huu wamekumbukwa.


Mtanishangaa sana kwa nini nashangaa. Mbona hamfikiri namna halisi ya kuwasaidia kina mama?

Mwadhani kumsaidia mwanamke wa Tanzania ni kuwapa vyeo? Mtashangaa na kushangaa kuhusu maoni yangu lakini wacha tu niyateme.

Ningekuwa mimi nina uwezo wa kumsaidia mwanamke wa Tanzania ningeanza kwa kuhakikisha afya yao hasa wakati wa kujifungua inaangaliwa vya kutosha.


Kwangu mimi ukimhakikishia mwanamke afya yake hapo umemjali kuliko kuwapa uspika au urais au uwaziri mkuu.

Mnashangaa nini? Mmeshakwenda wodi za wazazi mkajionea hali halisi huko? Sizungumzii hospitali kama Aga Khan. Nazungumzia hospitali na vituo vya afya tunavyotumia sisi kina yakhe!


Siku tukiwahakikishia mama zetu kwamba hawatakufa wanapoleta uzima mpya duniani nawaapia hapo hata mimi nitaingia barabarani kuruka ruka kwa kumkomboa mwanamke "kiukweli kweliii." Mtabisha kwa kuwa ninyi ni wabishi tu.


Njia nyingine ya kumkomboa na kumthamini mwanamke wa Tanzania bila kuremba ni kuwapatia huduma ya maji.


Nakumbia yeyote anayetaka kila mwanamke atabasamu, amhakikishie maji. Mnadhani kule kwetu wanajali idadi ya wanawake wanaoitwa waheshimiwa au jinsia ya mtu anayepakia benzi la spika?

Mama yangu anahitaji tu apate chai yake, mlo wake na akiugua apate matibabu. Huko bungeni hata ingekuwa midume yote lakini yeye akapata mahitaji yake ya kimama na kifamilia mnadhani kuna atakayewashangaa?


Leteni ukombozi wa mwanamke kwa kuwapatia mahitaji yao ya kiuhalisia enyi wana.


Kama ni uwakilishi wa akina mama mnaonaje mkahakikisha basi makundi ya akina mama waliopo pembezoni ndio yanawakilishwa bungeni?

Mathalani mwanamke mkulima wa jembe la mkono ndiye anajua taabu na mahitaji ya jamii ya wanawake kuliko "mdada" aliyezaliwa, kusomea na kukulia mjini.


Mnashangaa ninapoongea haya, siyo? Mtajiju lakini Mzee wa Kujitoa angepata nafasi na ikabidi kuwepo nafasi za upendeleo basi angechukua wawakilishi kutoka jamii za kifugaji za wakulima na wanawake wamachinga.


Ukombozi wa kweli wa mwanamke ni kuiwasomesha watoto wa kike halafu waingie wenyewe ulingoni kugombea si kuwapelekea madaraka katika sahani ya dhahabu. Huko kote simo miye!


Source: Tanzania Daima
 
0 Reactions
Reply
Back
Top Bottom