CCM wajiandae kukubali matokeo na wasije kuwa ndio chanzo cha umwagikaji damu nchini. | JamiiForums | The Home of Great Thinkers

Dismiss Notice
You are browsing this site as a guest. It takes 2 minutes to CREATE AN ACCOUNT and less than 1 minute to LOGIN

CCM wajiandae kukubali matokeo na wasije kuwa ndio chanzo cha umwagikaji damu nchini.

Discussion in 'Uchaguzi Tanzania' started by Ujengelele, Oct 8, 2010.

 1. U

  Ujengelele JF-Expert Member

  #1
  Oct 8, 2010
  Joined: Jan 14, 2008
  Messages: 1,256
  Likes Received: 0
  Trophy Points: 0
  Dk. Slaa alipaswa kumpa pongezi Lt. Jen. Shimbo

  Lula wa Ndali-Mwananzela
  Oktoba 6, 2010

  BAADA ya Luteni Jenerali Abdulrahman Shimbo kutaka vyama vya siasa viwe tayari kukubali matokeo ya uchaguzi ili kuepusha vurugu, baadhi ya viongozi wa vyama vya siasa na asasi za kijamii wamekuja juu wakimlaumu kuwa Jeshi linaingilia mchakato wa kisiasa kitu ambacho si kizuri katika demokrasia.
  Hisia za watu wengi bila ya shaka zimechukulia kauli ya Lt. Jenerali Shimbo kuwa ni ya kisiasa na ilikuwa ina lengo la kukisaidia Chama cha Mapinduzi (CCM).

  Mawazo haya bila ya shaka yamechangiwa kwa kiasi kikubwa na taarifa zilizoandikwa na baadhi ya magazeti wiki iliyopita yakidai ya kuwa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kiko tayari kumwaga damu ili kulinda kura na hivyo kuashiria kuwa kama matokeo hayataenda wanavyotaka wao basi “nguvu ya umma” itatumika kushinikiza serikali.

  Ni katika maudhui haya kauli ya Shimbo kuwa “hakuna damu itamwagika” inaendana kabisa na habari hizo za wiki iliyopita na hivyo kimantiki ilihusishwa na kujaribu kuwaambia wapinzani kuwa wakishindwa basi wakubali na wasilete vurugu kwani “vyombo vya usalama” viko tayari kukabiliana na vurugu zozote nchini.

  Waliochukulia tafsiri hii kwa kweli siwalaumu kwani inaendana kabisa na mtiririko wa matokeo hadi hivi sasa hasa tukizingatia kuwa watawala wetu walioshindwa ndio wamekuwa wakianza tena kuwatisha wananchi kuwa upinzani ukishika madaraka (wakiwa chama tawala) basi kutatokea vurugu.

  Nimewasikia baadhi yao pole pole hasa maeneo ya vijijini na mipakani wakianza tena ulaghai wao wa kuwatisha watu kwa yale yaliyotokea “nchi jirani” na hivyo kuwataka Watanzania waendelee kuchagua chama tawala kwani ndicho chenye “dhamana” ya kulinda amani, umoja na utulivu.

  Wakijua kuwa muda wao wa kuendelea kushikilia usukani unakaribia kwisha na usirudi, wameanza tena kuitia neno la “umwagikaji damu” na kutaka kuhusisha hilo na haki ya wananchi kuipinga serikali yao na kukataa utawala wa kujipandikiza.

  Katika msingi huo basi kauli ya Shimbo kwa haki kabisa ilionekana kukibeba chama tawala. Lakini kwa mtu yeyote makini ambaye angeweza kuchukua muda kidogo kuitafakari kauli hiyo ataona kuwa kauli hiyo haiwahusu wapinzani hata kidogo na kama kweli Shimbo alikuwa amekusudia kutuma ujumbe basi kwa kweli alikuwa amepiga simu isiyopokelewa na kupata ujumbe “the number you are trying to call is not reachable - namba unayopiga haipatikani kwa sasa!” Kweli kabisa kama namba aliyotaka kuipata ni ile ya wapinzani na hususan CHADEMA basi kwa kweli namba hiyo ni noti richebo!

  Kwa sababu tukiangalia vipimo vyote vya kiakili na kihistoria tunaweza kusema pasipo shaka kuwa ujumbe wa Lt. Jenerali Shimbo unahusu CCM na ni CCM peke yake. Ukiangalia kwa karibu utaona kuwa masuala ya kutokubali kushindwa na mambo ya kumwaga damu hayahusiani hata kidogo na chama hata kimoja cha upinzani. Si CUF, TLP, NCCR-MAGEUZI au CHADEMA ambao wanahusishwa na yote mawili kwa wakati huu. CUF labda kwa upande fulani wana historia ya kukataa matokeo na kutokuwa tayari kumtambua mshindi lakini kwa upande wa Bara vyama vyote vya upinzani havijahusishwa na tuhuma hizo mbili za kukataa matokeo au kuanza kumwaga damu.

  Hata hivyo, ni CCM peke yake katika vyama vya siasa nchini ambayo ina historia ya kutokuwa tayari kukubali kushindwa na vile vile kwa kutumia serikali yake na wakati mwingine mashabiki wake imehusishwa na umwagikaji wa damu nchini.

  Wakati vyama vingine vyote vya kisiasa nchini vimesema wazi kuwa endapo uchaguzi utakuwa huru na wa haki kabisa na ukaonekana hivyo basi vitakubali kushindwa mgombea wa CCM wa nafasi ya Urais bado hajatoa kauli kama hiyo hadharani kulihakikishia Taifa kuwa endapo atashindwa basi atakubali kushindwa.

  Tatizo la kutokutoa msimamo huo ni kuzirusha roho za mamilioni ya Watanzania hasa wakiwa wanajua historia ya eneo letu la Afrika ambapo watawala wa muda mrefu huwa hawashindwi kirahisi.
  CCM wamejifunza katika makosa ya Kenneth Kaunda (Zambia) na Daniel arap Moi (Kenya) na kwa hakika hawataki hilo litokee Tanzania. Hawako tayari kuona kuna uwezekano kuwa wanaweza kushindwa hivyo hawataki kabisa kutumia kauli ya kuonyesha kukiri uwezekano wa kinadharia kuwa wanaweza kushindwa.

  Sasa, katika siasa hakuna ubaya kwa mtu kujiamini kuwa “atashinda” hiyo ni sehemu ya siasa; lakini katika siasa za kitaifa ambapo maisha na hisia za watu zinakuwa juu ni muhimu kwa wanasiasa kutuliza wananchi kwa kuwahikikishia kuwa endapo wao wananchi watawakataa katika sanduku la kura, basi watakubali hukumu hiyo ya wananchi. CCM bado katika ngazi ya urais haijafikia uwezo huu wa ukomavu. Bado wanaona kuwa Urais ni kama sehemu ya CCM na kwamba CCM bila Urais haiwezekani. Kumbe, kwa kutokuwa tayari kukubali uwezekano huo wa kidemokrasia kutokea, CCM inaonekana kujiandaa kung’ang’ania urais kwa nguvu yoyote ile.

  Hapa ndipo kauli ya Mnadhimu Mkuu wa Jeshi inapoonyesha nguvu yake. Kwa vile chama pekee cha kisiasa ambacho mgombea wake hajatoa kauli ya kuonyesha kuwa tayari kukubali maamuzi ya kukataliwa na wananchi ni CCM basi kauli ya “vyama vikubali matokeo” inahusu zaidi mgombea huyo kuliko Dk.Slaa, Profesa Ibrahim Lipumba au mgombea mwingine wa Urais. Kumbe moja kwa moja kauli ya Shimbo inamlenga Kikwete, mgombea wa CCM na kwa namna fulani kumuweka katika nafasi ya kumtaka atoe kauli yenye kulihakikishia Taifa kuwa endapo atapoteza urais basi ataheshimu matokeo hayo.

  Sote tunajua hilo haliwezekani kutokea; Kikwete hawezi kutamka hadharani kuwa akishindwa ataheshimu maamuzi ya wananchi. Hili linatuleta kwenye jambo jingine lile la pili, kumwagika damu.
  Katika historia yetu ya kisiasa ya karibuni ni uongozi wa CCM na serikali yake, makada wake na mashabiki wake ndio wamehusishwa na vitendo vya umwagikaji wa damu nchini. Kuanzia mauaji ya Mwembechai, mauaji ya Pemba na vipigo vya wana CHADEMA kule Kiteto, dalili zinaonyesha kuwa CCM haichelewi kutumia vyombo vya dola kuzima upinzani wa kisiasa.

  Hivyo kwa vile tayari tunajua kuwa CCM haiwezi kusema hadharani kuwa itakuwa tayari kukubali matokeo ya hukumu ya wananchi, tunabakiwa na hofu ya jambo moja tu nalo ni kuzima kwa nguvu mwamko wa wananchi pale watakapoona matokeo ya uchaguzi yanaanza kumuonyesha Dk. Slaa kuwa anashinda. Hapa tuna la kusema kuhusu Tume ya Uchaguzi.

  Kumwagika damu kule Kenya wakati wa Uchaguzi wao Mkuu au hata kule Zimbabwe, kulitokana kwa kiasi kikubwa na kukosekana kwa uhuru wa Tume za Uchaguzi. Kwa upande wa Kenya hasa, tume ya Uchaguzi ilijikuta inasukumizwa na upande wa Mwai Kibaki ili wamtangaze Rais mara moja wakijua kuwa kwa kufanya hivyo hakuna mahakama yoyote ambayo ingeweza kuhoji jambo hilo.

  Matokeo yake walimtangaza mbio mbio na kuwahi kumwapisha usiku wa manane! Kilichofuata sote tunakijua, kwani si jeshi wala polisi walioweza kuzuia munkari wa watu walioona kuwa wamedhulumiwa haki ya kumchagua mtu wanayemtaka yaani kwao Raila Odinga.

  Picha hii ya Kenya inacheza cheza katika fikra za watu wengi sasa hivi, kwani tunaona dalili ile ile ikianza kutengenezwa Tanzania. Tume ya Uchaguzi haijaweka wazi utaratibu wake wa kukusanya na kutangaza matokeo ya Urais ili kuondoa utata wa wizi au kuchakachuliwa kwa matokeo. Utaratibu wa watu wachache ndani ya tume kupokea matokeo kutoka kwa maafisa wa uchaguzi (Returning Officers) na baadaye kuyajumlisha na kuyatangaza kutazua vurugu. Ni mtindo uliojengwa katika msingi ya usiri na haki ya watu wachache kujua suala zito la kitaifa.

  Ni kwa sababu hiyo nina mapendekezo mawili:
  Kwanza, Tume ya Uchaguzi iweke utaratibu wa kupokea matokeo ya majimboni wazi, hadharani na mbele ya waangalizi wa ndani na wa nje na matokeo hayo yakiwa yanajumlishwa kwa kadiri yanavyokuja hadharani. Hii itawahakikishia wananchi kuwa matokeo yanavyokujwa ndivyo yanavyotangazwa na idadi inaonekana kwa kadiri inavyokwenda hadi mwisho.

  Njia hii ndiyo inatumiwa na nchi nyingi za kidemokrasia ili kuondoa uwezekano wa matokeo kupikwa mahali fulani. Hivyo, kama Kikwete amepata kura 610,000 hadi saa tatu usiku na Dk. Slaa kura 700,000 (au kinyume chake) basi Tume isianze kuingiwa na kiwewe iendelee kukusanya matokeo na kama tunavyojua ikifika hadi asilimia kama sabini hivi ya kura zote kuwa zimehasabiwa basi mshindi atakuwa amepatikana. Kwa kufanya hivyo, Tume ya Uchaguzi inajiweka katika mazingira ya kutokuwa mshirika wa kusababisha vurugu nchini.

  La pili, hata hivyo, linatokana na hilo la kwanza. Kwa vile tunajua kuwa kuna uwezekano bado wa matokeo kuvurugwa wakati yanaripotiwa kutoka vituoni kwenda kwa wasimamizi wa uchaguzi au kutoka kwa wasimamizi wa uchaguzi kwenda Tume basi ipo haja ya kuhakikisha kuna chombo huru cha pili ambacho nacho kitakuwa kinakusanya matokeo hayo hayo moja kwa moja (live) na kuyajumlisha kama Tume inavyofanya japo yale ya Tume ndiyo yatakuwa rasmi.

  Katika mpangilio wa namna hiyo Msimamizi wa Uchaguzi akitoa ripoti yake kwa Tume basi anatoa pia kwa chombo hicho huru na idadi hizo lazima zilingane. Mwisho hesabu za Tume ya Uchaguzi zilingane na zile za hicho chombo huru kingine. Nina uhakika kutakuwa na vyombo vya habari navyo ambavyo vitakuwa vinakusanya matokeo yake vile vile.

  Hivyo kuwa na nyavu tatu za namna hiyo kunasaidia kuondoa uwezekano wa watu kugomea matokeo hasa kama yanakusanywa, kuhesabiwa na kutangazwa wazi. Nje ya hapo usiri wowote ule utasababisha tetesi na uzushi wa hapa na pale na matokeo yake kutakuwa na vurugu. Naamini Tume ya Uchaguzi ikipendekeza mfumo wa namna hii ambao hauhitaji gharama yoyote ya ziada, basi sehemu ya kuhesabu kura na kutangaza matokeo nayo itakuwa huru na ya haki.

  Lakini kwa vile CCM haijawa tayari kukubali matokeo na kwa kuwa ndio pekee wenye historia ya kutumia nguvu ya vyombo vya dola kwa sababu za kisiasa ni wazi kuwa kauli ya Shimbo basi inahusu CCM zaidi na ninaamini ni kauli ya kuungwa mkono.

  Lakini zaidi naamini ipo haja ya kuwataka CCM watoe kauli hadharani kama watakubali matokeo yoyote yale au la kwani ukimya wao ndio unachochea hisia kuwa ni wao wanaojipanga aidha kukataa matokeo au kusababisha vurugu endapo mgombea wao ataonekana kushindwa.

  La maana ni kwa vyombo vyetu vya usalama kuwa tayari kutekeleza wajibu wao wa kikatiba ambao ni kuhakikisha kuwa amani na utulivu unakuwepo na kama kutakuwa na upingaji wa kisiasa wa matokeo basi vihakikishe yote yanafanyika kwa amani na si kujaribu kuua mbu kwa mzinga! Isije kuwa tukajikuta wanaosababisha umwagikaji damu ya Watanzania si wanasiasa bali ni wanajeshi.

  Ninatoa wito wa dhati kabisa kuwa Jeshi la Wananchi liache kabisa kujishughulisha na mchakato wa uchaguzi na badala yake wawe makambini kuwa tayari kumsalimu amiri jeshi mkuu.

  Kazi ya ulinzi na usalama wa raia katika mazingira ya kawaida ya kisiasa hata kama ni ya uchaguzi ni kazi ya Polisi na hadi hivi sasa sijasikia kama Jeshi letu la Polisi limeshindwa kazi.

  Ninafahamu kuwa katika mazingira fulani fulani JWTZ linayo haki ya kikatiba kutoa msaada lakini hadi sasa sijaona ulazima huo kwani hatujamsikia Inspekta Jenerali wa Polisi Said Mwema akisema kuwa Jeshi la Polisi limezidiwa nguvu na linahitaji msaada wa Jeshi.

  Isije kuwa kwamba ni kweli kauli ya Shimbo haikutolewa kwa ajili ya vyama “vyote” bali kwa ajili ya wapinzani tu. Kama hiyo ndiyo ilikuwa nia yake kuwatisha wananchi kuwa wasipinge kile watawala wamekiamua basi atakuwa amekosea.

  Shimbo na wenzake wenye magandwa ya jeshi letu wasijidanganye kuwa ati wataweza kuzima fikra za mabadiliko kwa kutumia mizinga na kwa kutumia bunduki kuzinyamazisha sauti za mabadiliko. Vyombo vya usalama visijidanganye kuwa vinaweza kufanya mbinu mbalimbali na kuhakikisha kuwa kiu ya mabadiliko inapotoea katika mioyo ya Watanzania. Ndugu zangu hakuna pingu za kutosha kuyafunga mawazo huru na hakuna magereza ya kutosha kufunga wana mabadiliko.

  Mbinu ya vyombo vya dola kutumia nguvu kuzima mabadiliko zimeshaonyeshwa mara kadhaa kushindwa. Zimeshindwa Zimbambwe, zimeshindwa Ukraine, zimeshindwa Kenya, zitaendelea kushindwa kwani kila zama zina mashujaa wake na kila shujaa ana ujumbe wake.


  Vinginevyo, nawashauri CCM waanze kufanyia kazi ushauri wa Luteni Generali Shimbo ili wajiandae kukubali matokeo na wasije kuwa ndio chanzo cha umwagikaji damu nchini.
   
 2. Rutashubanyuma

  Rutashubanyuma JF-Expert Member

  #2
  Oct 8, 2010
  Joined: Sep 24, 2010
  Messages: 158,613
  Likes Received: 419,233
  Trophy Points: 280
  Hapo umegusa donda ndugu ulipobainisha ya kuwa:-

  Tunamtaka JK naye ajitokeze hadharani na kuthibitishia yu tayari kukubali matokeo yoyote yatakayotangazwa na tume ya uchaguzi
   
Loading...