CCM waibiana kura, anayedaiwa kuhujumu kura hizo ni katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM

Dec 11, 2010
3,321
6,328
Imeandikwa na Maregesi Paul | Dar es Salaam
Thursday, April 05, 2012

UCHAGUZI wa wabunge wa Bunge la Afrika Mashariki kwa upande wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), umeingia doa. Chanzo chetu cha habari kilichokuwa katika uchaguzi huo, kilisema jana kuwa, uchaguzi huo uliofanyika juzi kwenye Ukumbi wa Karimjee, Dar es Salaam, ulijaa kasoro kwa baadhi ya wagombea kuibiwa kura.

Chanzo hicho kilisema kuwa, mmoja wa wanaodaiwa kuhujumu kura hizo ni aliyekuwa msimamizi wa uchaguzi huo, ambaye pia ni Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Nape Nnauye. Nape alikuwa akisaidiana na kada wa chama hicho, Abdulrahman Kinana.

Chanzo hicho kilisema kuwa, dalili za kuwapo hujuma katika uchaguzi huo, zilianza baada ya wabunge kukataa kura kuhesabiwa chini ya usimamizi wa meza kuu iliyokuwa ikiongozwa na Waziri Mkuu, Mizengo Pinda.

"Mimi nilikuwapo ukumbini na niliingia kama mmoja wa mawakala waliokuwa katika chumba cha kuhesabia kura, kwani nilikwenda kumsimamia jamaa yangu ambaye alikuwa anagombea.

"Kwanza kabisa kabla ya kuingia katika chumba cha kuhesabia kura, kura zilipigwa kama kawaida, zoezi hilo lilipokamilika, ukafika wakati wa kwenda kuhesabu kura.

"Kabla ya hapo, Kinana alisimama na kutueleza kwamba, kura za wagombea zitasimamiwa na meza kuu, aliposema hivyo, wabunge wakalipuka kwa kusema hatutaki na wengine walidiriki hata kuzomea.

"Wakasema wagombea wenyewe wasimamie kura zao au kama kuna wasiotaka kuzisimamia, waweke mawakala kwa sababu meza haiaminiki.

"Baada ya kuvutana kwa muda, ukapitishwa uamuzi, kwamba wagombea ambao wakati huo walikuwa nje ya ukumbi, waitwe ili waulizwe wao wanataka utaratibu gani utumike.

"Walipoitwa, Kinana akaanza kuwaeleza kwamba, hapa kuna mambo matatu, mtu kusimamia kura zake, kuweka wakala au kuamini meza isimamie kura kwa sababu meza inaaminika.

"Alipouliza hivyo, wagombea wakawa kimya, nadhani ni kwa sababu ya ugeni katika masuala hayo.

Lakini mama mmoja nadhani ni yule wanayemuita Shyrose, akasema mimi nitasimamia kura zangu, kisha wengine nao wakaanza kusema watasimamia za kwao na baadhi wakasema wataiamini meza.

"Baada ya hatua hiyo, suala hilo likaonekana kutaka kumalizwa kiaina, sasa Mkuchika akasimama na kuuliza ni utaratibu gani utatumika kuhesabu kura.

"Baadaye ikaamuliwa kwamba, wanaotaka kwenda wenyewe kusimamia kura zao wafanye hivyo, wanaoweka mawakala, wawaweke na wakati huo huo wanaoiamini meza, waiachie itawasimamia," kilisema chanzo hicho.

Kwa mujibu wa chanzo hicho ambacho kiliingia katika chumba cha kuhesabia kura, baada ya kuingia katika chumba hicho, mazingira ya kuhujumiana yalianza, kwani Nape alisimama mbele ya wagombea na kuanza kusoma jina moja moja na kura alizopata mgombea.

"Alipoanza kusoma hivyo, watu wakaanza kulalamika, wakamwambia wataamini vipi kura anazosoma ni za kweli wakati hawaoni anachosoma? Yeye akakataa, akasema ataendelea kusoma tu.

"Alipomaliza kusoma, lawama zikazidi, wagombea wakasema hawakubaliani na matokeo, wakataka kura zihesabiwe upya, lakini yeye akagoma, akasema matokeo yako kama alivyokuwa amesoma awali.

"Wagombea walipoona wanachakachuliwa, vurugu zikaanza, wengine wakaandika barua harakaharaka kwa Kinana ili kumweleza kilichokuwa kikijiri huko ndani.

"Kinana akaamua kuja, alipoelezwa mambo aliyokuwa ameyafanya Nape, akaamuru kura zihesabiwe upya na wakati huo huo, Serukamba (Peter Serukamba, Mbunge wa Kigoma Mjini), Zambi (Godfrey Zambi, Mbunge wa Mbozi Mashariki), Shaha (Abdulkarim Shaha, Mbunge wa Mafia), Martha Mlata (Mbunge wa Viti Maalum) na Mbunge wa Mufindi Kusini, Mahmud Mgimwa, waliingia pia.

"Walipofika, kura zikaanza kuhesabiwa, sasa vituko vikaanza kujidhihirisha kwa sababu baadhi ya wagombea waliokuwa na kura chache, kura zilipohesabiwa kwa mara ya pili wakapata kura nyingi.

"Kwa mfano, kuna mgombea mmoja ambaye awali alikuwa na kura 149, chini ya usimamizi wa Nape, lakini kura ziliporudiwa, amini usiamini, aliambulia kura 40.

"Mwingine chini ya usimamizi wa Nape alikuwa na kura 32, lakini ziliporudiwa mgombea huyo akazoa kura 136.

"Si hilo tu, kuna dada mmoja alikuwa akimsimamia ndugu yake, kura za kwanza alikuwa amepata kura 114, ziliporudiwa akapata kura 126, lakini matokeo yakabadilishwa kwamba amepata kura 107, wakati yeye mwenyewe alikuwa akihesabu kura hizo.

"Sasa angalia haya madudu, wao wanasema chama kiko imara, uimara wake uko wapi, mambo yanapelekwa kienyeji na ndiyo maana hata wabunge tulipoulizwa mwanzoni kama meza inaweza kusimamia kura tulikataa, kwa sababu sisi wenyewe hatuaminiani.

"Pamoja na kwamba washindi wameshapatikana, bado tunasema uchaguzi haukuwa huru na wa haki, yaani mtu kama Nape anaingia katika uchaguzi akiwa na watu wake, huu siyo utaratibu kabisa, chama tunakiua wenyewe," kilisema chanzo chetu.

Nape alipozungumza na MTANZANIA kwa simu jana, alisema uchaguzi ulikwenda vizuri tangu kura zilipopigwa hadi uhesabuji wa kura, ingawa kulitokea kasoro ndogondogo ambazo ni za kawaida.

"Nadhani mmelishwa stori kwa sababu mimi na Kinana ndiyo tuliokuwa wasimamizi wa uchaguzi huo, uchaguzi ulikwenda vizuri na hata kura zilipohesabiwa kwa mara ya pili, washindi waliokuwa wameshinda awali ndiyo hao hao walioendelea kushinda.

"Kwa hiyo mtu anaposema hayo, anadanganya kwa sababu hakuna aliyelalamika, lakini kama kuna ambaye hakuridhishwa na matokeo angegomea matokeo.

"Pamoja na hayo sishangai malalamiko haya kuletwa kwenu kwa sababu najua aliyeyaleta anajua mtayaandika kwa ajili ya kumwandika Nape vibaya," alisema Nape.


Source: Mtanzania
 
Kazi kweli kweli! Sijui kama wale nadhani wanafaa watapita!!!!???
 
Duh hata wao kwa wao hawaaminiani! Nadhani wanajua ambacho huwa wanafanya huko kwenye kura majimboni ndio maana hawaaminiani!

Inaonekana wamezoea kuzomea yaani hata wakiwa peke yao wanazomeana kumbe!
 
Fanya editing, miandishi imesongamana utadhani foleni za Dar....thread haina mvuto wa kusoma, hata kama siyo mwandishi wa Habari lakini kugandanisha sentesi hakukubaliki.
 
Sasa mbona chanzo chako akikueleza iliishia wapi mbona hatukumfahamu aliyeshinda kialali??
 
Hiyo ndiyo CCM mbona hayo ndiyo maisha siku zote kwenye chaguzi!!!
 
CCM ni Janga la kitaifa. Huu wizi wa kura upo ndani ya damu. Wametuibia wapinzani sasa tumewastukia wanakwenda kuwaibia ndugu zao wenyewe. Kweli huu ni mwanzo wa mwisho kwa Magamba.
 
Duh hata wao kwa wao hawaaminiani! Nadhani wanajua ambacho huwa wanafanya huko kwenye kura majimboni ndio maana hawaaminiani!

Inaonekana wamezoea kuzomea yaani hata wakiwa peke yao wanazomeana kumbe!
Imebidi nicheke tu na hii comenti yako mkuu! Wezi siku zote huwa hawaaaminiani hata iweje?
 
Mimi ningepigwa na bumbuwazi ikiwa uchaguzi ungekwenda pasi kupindisha uhalisia. Kwa Si Si Em wizi kwao ni sera hivyo ni lazima isimamiwe katika kutekelezwa. Na kama hamuamini subirini muone kura za JK zitakavyochakachuliwa wakati atakapopigiwa kura kuchaguliwa M/Kiti wa Chama - Taifa. Teh! Teh! Teh! Teh! Teh! Teh! Teh! Teh! Teh! Teh! Teh!
 
Kwa nini member wengine mnakopi habari yote halafu unaandika mistari miwili tu, wengine tunatumia simu mnatujazia nafasi.
 
Duh hata wao kwa wao hawaaminiani! Nadhani wanajua ambacho huwa wanafanya huko kwenye kura majimboni ndio maana hawaaminiani!

Inaonekana wamezoea kuzomea yaani hata wakiwa peke yao wanazomeana kumbe!

Mkuu Kimbunga,

Kila siku huwa nakuona unaegemea kwenye utetezi wa hawa jamaa .... sasa angalia namna wanavyotiana aibu mbele ya wananchi. Wangekuwa ni wapinzani wanalalamika, utasikia kwamba wapinzani kazi yao ni kulalamika kwamba wameibiwa kura.

Hii ni aibu kubwa sana wabunge kukosa imani na Waziri Mkuu, Mjumbe wa Kamati na Katibu Mwenezi wa CCM ... sasa kama hao hawaaminiki, nani anaaminika ndani ya CCM? Si ajabu hata wajumbe wa CC huwa hawamuamini JK!

Kaazi kweli kweli!
 
Nape namwaminia kwa kujenga hoja za uongo, kuna tetesi ya kuwa amesomea masters ya kujenga hoja za uongo Muzumbe University.
 
Back
Top Bottom