CCM ni vululuvululu | JamiiForums | The Home of Great Thinkers

Dismiss Notice
You are browsing this site as a guest. It takes 2 minutes to CREATE AN ACCOUNT and less than 1 minute to LOGIN

CCM ni vululuvululu

Discussion in 'Uchaguzi Tanzania' started by mrefu36, Aug 19, 2010.

 1. mrefu36

  mrefu36 Member

  #1
  Aug 19, 2010
  Joined: Aug 16, 2010
  Messages: 60
  Likes Received: 2
  Trophy Points: 15
  CCM ni vululuvululu


  na Waandishi wetu, Thomas Nyimbo atua CHADEMA


  [​IMG] BAADA ya kuelemewa na malalamimiko kutoka kwa wanachama wake huku wengine wakipandishwa kizimbani baada ya kuhusishwa na vitendo vya rushwa, Chama Cha Mapinduzi (CCM) kimetangaza ‘vita’ dhidi ya wanachama wake watakaogeuza kampeni zijazo kuwa uwanja wa mapambano.
  Kauli hiyo imetolewa na Katibu wa Itikadi na Uenezi wa chama hicho, Kapteni John Chiligati, alipokuwa akichukua fomu baada ya kuteuliwa na chama chake kuwania ubunge katika Jimbo la Manyoni Mashariki.
  Alisema hatua hiyo itasaidia kurejesha nidhamu na kuwa chama cha kuigwa na vyama vingine, ikizingatiwa kimeshika dola.
  Hata hivyo, Chiligati ambaye alikuwa akizungumza kwa niaba ya mgombea wa ubunge wa Jimbo la Manyoni Magharibi, John Lwanji, aliahidi kuyatekeleza maadili yote yaliyopo kwenye kitabu cha maadili kwa madai kwamba ndiyo yaliyokubaliwa na vyama vyote vya siasa.
  Kwa mujibu wa Chiligati, kila chama kina wajibu wa kuwadhibiti wanachama wake ambao wanakiuka maadili ya uchaguzi, unaosababisha uchaguzi huo kutokuwa huru na wa haki na kwamba kinachotakiwa ni kudumisha amani na kuhakikisha wanapatikana viongozi bora.
  Kwa upande wake msimamizi wa uchaguzi wa Wilaya ya Manyoni, Bi Fortunata Mallya, aliwatahadharisha wagombea hao kutoweka saini kwenye fomu ya maadili ya zoezi zima la uchaguzi. MWANZA

  Mwandishi Wetu, Sitta Tuma, anasema Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU), mkoani Mwanza, imeanza kuwaita na kuwahoji wagombea ubunge wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), mkoani hapa, ambao wameteuliwa na chama hicho kugombea nafasi hiyo.
  Wagombea ubunge hao (majina yao tunayo), wanadaiwa kutoa rushwa na matumizi ya mali za serikali wakati wa mchakato wa kura za maoni ndani ya chama hicho tawala.
  Imeelezwa kwamba mmoja wa wagombea hao ambao wamebanwa na TAKUKURU yumo mbunge anayetetea nafasi yake hiyo, ambaye wakati wa mchakato wa kura za maoni alikuwa anakabiliwa na upinzani mkali jimboni mwake.
  Taarifa zilizoifikia Tanzania Daima, zilieleza kwamba wagombea hao wamehojiwa na ofisi ya TAKUKURU mkoani hapa kwa siku mbili tofauti, ambapo mmoja wao alihojiwa juzi Jumanne na mwingine aliitwa na kuhojiwa jana.
  Kwa mujibu wa taarifa hizo, wagombea ubunge hao ambao wameteuliwa kugombea ubunge katika majimbo yao katika Uchaguzi Mkuu uliopangwa kufanyika Oktoba 31, mwaka huu, huenda wakafikishwa mahakamani kujibu mashitaka dhidi yao.
  “Mpaka leo (jana), kuna wagombea wawili wa nafasi ya ubunge walioteuliwa wamehojiwa kuhusu tuhuma za kutoa rushwa na mambo mengine, mmoja alihojiwa jana (juzi) na mwingine leo (jana). MAFIA

  Mwandishi Wetu, Andrew Chale, anaripoti kuwa katika hali isiyo ya kawaida, wanachama wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Wilaya ya Mafia, mkoani Pwani wapo njia panda ndani ya chama hicho kufuatia kutopatiwa ufumbuzi juu ya mgombea wao aliyeshinda kura za maoni na badala yake Halmashauri Kuu (NEC), ikampitisha mgombea mwingine.
  Wakizungumza kwa nyakati tofauti kwa njia ya simu, kundi la wanachama wa CCM wilayani hapa, walipinga hatua ya NEC kuondoa jina la Omary Kimbau, aliyeshinda kwa kupata kura 1,803 huku mpinzani wake ambaye alikuwa mbunge wa jimbo hilo, Abdul Shaha, akipata kura 1,798.
  Katika kile kilichoonekana kamati hiyo kucheza mchezo mchafu, wanachama hao walidai walitakiwa kupewa maelezo ya kina, kwani wao walimchagua kwa moyo mmoja katika kura za maoni, lakini walikata jina lake na kumpitisha mgombea mwingine.Mbali ya hilo, baadhi ya wanachama kutoka kata za Kilindoni, Ndagoni, Kigani, Bweni na Mburani, wameamua kuweka mgomo baridi ili kushinikiza uongozi huo kutoa majibu ya kina na ya msingi juu ya kukatwa kwa jina la Kimbau na kisha kulipachika jina Shaha.
  Hata hivyo, alipotafutwa Kimbau kuzungumzia suala hilo, hakuwa tayari kuongelea suala hilo na kumtaka mwandishi wa habari hizi akamuulize Katibu Mkuu wa CCM, Yusuph Makamba.
  Kutoka Morogoro, Mwandishi Wetu Joseph Malembeka, anaripoti kuwa wakati jana ilikuwa siku ya kurudisha fomu za kugombea ubunge, wagombea Amani Mwaipaja wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) na Abdulahaziz Abood wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), juzi walijikuta wakipishana kwenye mlango wa Tume ya Uchaguzi ya Taifa (NEC) mkoani hapa bila kusalimiana.
  Pasipokuwa na wapambe wala shamrashamra, wagombea hao wanaofikisha idadi ya wagombea tisa jimboni humo, walijikuta wakipishana kimya kimya, mmoja akitoka na mwingine akiingia katika ofisi hizo zilizopo ofisi za manispaa mjini hapa.
  Akizungumza na waandishi mara baada ya kuchukua fomu hizo, Mwaipaja ambaye ni mwanasheria na mwanaharakati wa kutetea haki za binadamu, aliitaka NEC kuacha ubabaishaji katika kutatua mapema kasoro za uchaguzi.
  Wakati huo huo, Katibu wa CHADEMA Mkoa wa Morogoro, Abel Luanda, aliwaambia waandishi mjini hapa kuwa chama hicho kinatarajia kusimamisha wagombea katika majimbo yote 10 ya mkoa huo.
  Kutoka mjini Moshi, Mwandishi Wetu Charles Ndagulla aripoti kuwa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Kilimanjaro, kinasaka ‘dawa’ ya kumaliza tofauti za kisiasa baina yake na kada wake, Athuman Ramole, aliyeongoza kura za maoni kuwania ubunge wa Jimbo la Moshi Mjini na baadaye jina lake kuondolewa na Halmashauri Kuu ya chama hicho (NEC).
  Juzi chama hicho kiliitisha mkutano na waandishi wa habari na ‘kumshinikiza’ Ramole abadili msimamo wake wa kutomuunga mkono Justin Salakana ambaye alipitishwa na NEC kuwania ubunge jimbo hilo, akitokea nafasi ya tatu.
  Katika mkutano huo ambao Katibu wa CCM Mkoa wa Kilimanjaro, Steven Kazidi, anadaiwa kumbembeleza Ramole aliyeshinda kura za maoni kwa kupata kura 1,554 atangaze kumuunga mkono Salakana ambaye anadaiwa hana mvuto kwa siasa za Moshi Mjini.
  Salakana ambaye mwaka 1995 alikuwa mbunge wa Jimbo la Rombo (CHADEMA) na baadaye kuangushwa na Basil Mramba mwaka 2000, alishika nafasi ya tatu kwa kupata kura 1,152, nyuma ya Thomas Ngawaiya, aliyepata kura 1,539, kuteuliwa kwake kumezusha hali ya kushangaza kwa wana CCM wa Jimbo la Moshi Mjini.
  Huko Iringa, Mwandishi Francis Godwin anaripoti kuwa hatimaye aliyekuwa mbunge wa jimbo hilo aliyebwagwa kwenye kura za maoni, Monica Mbega, jana alijitokeza kuchukua fomu za kuwania kiti hicho kwenye Ofisi ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) mkoani hapa.
  Mbega ambaye alikuwa na wapambe wachache ambao walitinga katika ofisi za msimamizi huyo wa uchaguzi wa Jimbo la Iringa Mjini, Teresia Mahongo, majira ya saa 6 mchana huku wakiwa na magari takriban matano, pia alimpongeza Frederick Mwakalebela kwa kutangaza kukubali uamuzi huo.
  Mbega aliwaomba wagombea wengine kujitokeza kumpa ushirikiano ili aweze kushinda katika jimbo hilo, huku akigoma kutangaza sasa kama ataendelea kugombea milele katika jimbo hilo.
  Mbega ambaye ni Mkuu wa Mkoa wa Kilinanjaro, alisema kuwa alichokifanya Mwakalebela kutangaza kutoa ushirikiano kwake ni busara ya hali ya juu, ambayo inapaswa kuigwa na wana CCM wengine badala ya kuendelea kuweka makundi ndani ya chama.
  Katika hatua nyingine, aliyekuwa mshindi katika kura za maoni katika Jimbo la Njombe Magharibi, Thomas Nyimbo, ambaye alifanyiwa mizengwe na Halmashauri Kuu ya CCM (NEC) baada ya kuenguliwa jina lake, jana alichukua rasmi fomu ya kuwania ubunge kwa tiketi ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), huku wana CCM wakimsindikiza.
  Nyimbo ambaye amechukua fomu yake jana, anatarajia kuirejesha leo, amesema hana sababu ya kuiacha nafasi hiyo ambayo amepewa na wananchi wa CCM wa jimbo hilo, badala ya kupewa mtu ambaye si chaguo lao.
  “Nawaomba sana wana CCM ambao waliniona kuwa nafaa kuogonza jimbo hili kunipa ushirikiano ndani ya CHADEMA ambacho pia ni chama bora nchini na chenye sera za kweli za kuikomboa nchi hii …kutoka kwa CCM ambao wameendelea kuendekeza chuki na ubinafsi na kuchukia watu wenye uwezo wa kuongoza nchi na kuwataka wale ambao wataishia kusema ndiyo mzee kwa kila jambo…sipendi kwa sasa kuzungumza sana kwani nguvu yangu na mapenzi ya wana Njombe Magharibi yataonekana Oktoba 31,” alisema Nyimbo.
  Naye Msajili wa Vyama vya Siasa, John Tendwa, ameeleza kusikitishwa kufuatia kundi la watu linalodaiwa kuwasilisha malalamiko kuhusu uamuzi wa Kamati Kuu (CC) na Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM (NEC), kumteua Waziri wa Fedha, Mustafa Mkulo, kuwa mgombea wa ubunge katika Jimbo la Kilosa na kuwataka wazee hao kuacha kutumia ofisi yake kuwasilisha majungu.
  Tendwa alisema amesikitishwa kuona suala la Waziri Mkulo ambaye ni mbunge aliyemaliza muda wake katika jimbo hilo, likiibuka kwa kasi siku za hivi karibuni, baada ya maamuzi ya CCM yaliyofanywa mjini Dodoma.
  Akizungumza na Tanzania Daima mjini Dar es Salaam jana, Tendwa alilalamikia taarifa zilizochapishwa na gazeti moja la kila siku (si Tanzania Daima) kwamba amepokea malalamiko hayo na kuahidi kuyafanyia kazi kulingana na sheria za nchi. “Na hata kama kuna mamlaka hizo, ofisi yangu si miongoni mwazo, hivyo ninapenda kutoa taarifa rasmi kwamba wanaofanya hivyo wanaweza kuwa ni wale walioshindwa katika kura za maoni, hivyo kutaka kupenyeza maneno kwa mamlaka za serikali. “Nimeanza kubaini kwamba hawa jamaa wanaweza kuwa ni wale waliojeruhiwa na kura za maoni na wanadhani muhimu kwa sasa ni kutafuta mahala ambapo Waziri wa Fedha na Uchumi anaweza kuwekewa pingamizi la kikatiba na kuenguliwa mara moja,” alisema Tendwa.
   
 2. M

  Mutu JF-Expert Member

  #2
  Aug 19, 2010
  Joined: Mar 30, 2008
  Messages: 1,333
  Likes Received: 6
  Trophy Points: 0
  mshike mshike kweli ,hebu wataalam wa mabo wanaoweza kusheheresha katika habari ya Mustafa Mkulo hapo wafanze hivyo tafadhali maana kunaviungo vinakosekana kupata kunoga na kueleweka.Swala lake ilmefika kwa Tendwa likilalamikiwa kivipi?
   
Loading...