CCM na Rushwa ni Samaki na maji

Corticopontine

JF-Expert Member
Sep 20, 2019
664
1,272
UKIMKUTA MAMBA NCHI KAVU NI KWA AJILI YA KUOTA JUA NA KUTAGA MAYAI LAKINI ASILI YA MAISHA YAKE NA MAWINDO NI MAJINI:

Ndugu Wana CCM na Watanzania,
Wahenga wa kale walisema, Sikio la kufa huwa halisikii dawa, ni swala la muda tu, na ukitaka kujua ugumu wa kuvunja ndoa ya wana ndoa walioishi kwenye ndoa kwa zaidi ya miaka 30, waulize wana ndoa wenyewe, kwani hata wakiachana huwa wanapeana talaka rejea tu.

Hali ni vivyo hivyo hata kwa mgonjwa aliyeishi na maradhi sugu mwilini kwa muda mrefu, matibabu yake ya kumponya maradhi hayo kikamilifu huwa ni kizungumkuti, na wakati mwingine huweza kuchukua muda mrefu, hususani iwapo maradhi aliyonayo yatakuwa yameshaenea mwili mzima kama vile saratani, ukoma, kifua kikuu, ukimwi na kisukari.

Chama cha Mapinduzi (CCM) ni Chama ambacho kwa zaidi ya miaka 30 iliyopita kilijifungamanisha na rushwa, ufisadi, uporaji wa rasilimali za nchi pamoja na matumizi mabaya ya madaraka. Ni Chama kilichojitoa mikononi mwa wakulima na wafanyakazi kama ilivyokuwa misingi ya kuanzishwa kwake na kikafungamana na wafanyabiashara wenye ukwasi wa fedha.

Ni Chama kilichojitoa kusikiliza na kutatua kero za wananchi na badala yake kikafungamana na wakwepa kodi, majangiri, wahujumu uchumi, na wauzaji madawa ya kulevya. Ni chama ambacho hakikujali tena kutetea maisha ya wananchi wa kawaida isipokuwa kikajifungamanisha na kuabudu wenye fedha.

Ndugu Wana CCM na Watanzania,
Ni ukweli usiopingika kwamba, mwaka 2015 mara baada ya uchaguzi mkuu uliokirudisha Chama hiki madarakani, Mwenyekiti wake mpya hayati Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, licha ya kutambua kwamba hakisafishiki, alijaribu kukirudisha Chama hiki mikononi mwa wanachama wa kawaida kwa mtindo na mbinu za medani kisiasa.

Kwa kutambua kwamba ilikuwa ni vigumu kuitenganisha CCM mtandao, na maovu yaliyoshamiri nchini, ikiwemo mikataba mibovu ya kinyonyaji, yeye alianzisha Chama cha Mapinduzi ndani ya CCM mtandao na kukiita Chama hicho CCM MPYA, TANZANIA MPYA.

Ile CCM ya mafisadi iliyokuwa ikizomewa huko nyuma, aliipa talaka rejea kwa muda. Alichoweza kufanya ni kuhakiki mali na rasilimali za Chama zilizokuwa zimehodhiwa mikononi mwa wajanja wachache kwa kuunda tume, ambapo kutokana na unyeti wa taarifa ya uhakiki huo, aliogopa kuiweka hadharani kwa wanachama na watanzania.

Ndugu Wana CCM na Watanzania,
Kupitia kaulimbiu ya CCM MPYA, TANZANIA MPYA, Chama hiki kiliweza kurudisha matumaini ya wanachama na wananchi waliokuwa wamekata tamaa, na wakaanza kukipenda, wakiwemo waliokuwa wamekimbilia upinzani kurejea kwa mtindo wa kuunga mkono juhudi.

Kazi kubwa iliyofanyika kwa miaka mitano ni viongozi wa Chama na serikali kuzunguka nchi nzima kusikiliza na kutatua kero mbali mbali zinazokabili wananchi ikiwemo vitendo vya dhuluma pamoja na ukosefu wa haki katika vyombo vya maamuzi, bila kusahau migogoro ya ardhi iliyokuwa imekithiri kila konabya nchi.

Ni kupitia utendaji huu wa CCM MPYA + TANZANIA MPYA kuwajali watu wa maisha ya chini wakiwemo machinga, mama lishe na baba lishe, Chama kilipendwa, serikali ilipendwa, zomea zomea ya mafisadi hao ikaisha na ushindi wa asilimia 84.6 kwenye uchaguzi wa 2020 ni kielelezo cha imani waliyokuwa nayo wananchi kwa CCM.

Ndugu wana CCM na Watanzania,
Wahenga wa kale walisema, ng'ombe wa masikini huwa hazai, na akizaa, ndama anakufa.

Hivyo ndivyo ilivyotokea kwa Chama cha Mapinduzi. Baada ya Mwenyekiti wake kufariki, matarajio ya wengi yalikuwa ni kwamba Chama kitaendeleza mazuri yaliyofanywa kwa miaka mitano (5), badala yake leo tunaambiwa tajiri ndiye amechaguliwa kuwa Mwenyekiti wa Kanati ya fedha na uchumi ndani ya Jumuiya ya Vijana ya Chama cha Mapinduzi.

Maana yake ni kuwa, Mamba aliyekuwa nchi kavu akiota jua na kutaga mayai, kwa sasa amerejea majini kuliko asili ya maisha na mawindo yake. Kumbuka wakati CCM mtandao ikiwa madarakani, mweka hazina wake mkuu alikuwa mfanya biashara mwenye ukwasi mkubwa wa fedha, ambaye bila woga alidiriki kujimilikisha mali za Chama na kuwa mali zake ikiwemo luninga ya Channrl ten, radio ya Magic fm na mtambo wa kuchapisha Magazeti. Huwezi kuitenganisha CCM mtandao na vitendo vya dhuluma, wizi, ufisadi, uporaji rasilimali za nchi.

Kinachoendelea kwa sasa ndani ya serikali na CCM mtandao ambayo imerudi madarakani ni kuhakikisha kwamba, wafuasi wa CCM mpya + Tanzania mpya wanafyekelewa mbali. Huu ndiyo wakati tunaposhuhudia teuzi kwa ajili ya kuondoa wanaoonekana kuwa kikwazo cha upigaji dili hata kama utendaji wao una tija kwa taifa na kuweka watu wapya.

Tangu CCM mtandao iliporejea madarakani tarehe 19th March 2021, hakuna tena ziara za kusikiliza na kutatua kero za wananchi, hakuna tena ziara za kukagua miradi ya maendeleo ya kimkakati. Kipaumbele si kusimamia shughuli za maendeleo bali ni kupanga safu ya 2025.
 
zomea zomea ya mafisadi hao ikaisha na ushindi wa asilimia 84.6 kwenye uchaguzi wa 2020 ni kielelezo cha imani waliyokuwa nayo wananchi kwa CCM
HAKUNA UKWELI HATA KIDOGO KWENYE AYA HII.KAMA CCM ILIPENDWA,YALE MABEGI YA KURA FEKI YALIKUWA YA NINI?
 
🗣️ Regacy!! Ohhh! Mataga kama hamridhishwi na CCM ya sasa, si muanzishe chama chenu kipya ili muienzi Legacy ya Hayati?

Hivi huku kulia lia kwenu kutawasaidia nini? Iwapo hamchukui hatua?
 

Similar Discussions

Back
Top Bottom