Ccm majeraha matupu

AMARIDONG

JF-Expert Member
Jun 24, 2010
2,502
177
HALI ya wasiwasi imezidi kutanda miongoni mwa watu wa Wilaya ya Tandahimba, yakiwa ni matokeo ya makovu ya uchaguzi wa ubunge, yaliyompa ushindi mgombea wa CCM.Hata hivyo ushindi huo ulipingwa vikali na aliyekuwa mgombea wa chama cha CUF akiungwa mkono na wananchi wa jimbo hilo, jambo ambalo lilisababisha vurugu zilizowalazimisha FFU kuingilia kati.Habari za awali zilisema wananchi katika baadhi ya vijiji, walilazimika kuhama makazi yao na kujificha maporini, wakihofia kukamatwa kwa tuhuma za kuhusika katika vurugu hizo.

Habari zilisema baadaye hali ilirejea kuwa ya kawaida.Lakini ingawa leo ni siku 29 tangu uchaguzi mkuu umalizike, bado kuna taarifa za uwezekano wa kufanyika vurugu nyingine kutokana na madai ya kuwa matokeo ya uchaguzi huo, yachakachuliwa.

Hali kadhalika, hisia za kulipiza kisasi zilizotokanana watu kujeruhiwa na kupoteza mali wakati wa vurugu zilizotokea mara baada ya kutangazwa kwa matokeo ya kura Novemba mosi mwaka huu.

Nyumba tisa zilichomwa moto mara baada ya kutangazwa kwa matokeo hayo na miongoni mwa watu walioathirika ni vikongwe, Fatuma Hamisi (88) na Rehema Alimited (82), ambao ni wajane na sasa hawana mahali pa kuishi.

Katika uchaguzi huo, uliokuwa wa vuta nikuvute, Tume ya Taifa ya Uchaguzi, ilimtangaza Juma Njwayo wa CCM kuwa mshindi baada ya kupata kura 34,154 dhidi ya Katani Ahmed wa CUF aliyepata kura 33,116.

Matokeo hayo yanapingwa vikali na wafuasi wa CUF ambao wanadai kwamba mbinu za uchakachuaji wa kura zilitumika kumpa ushindi, mgombea wa CCM, ambaye kwenye uchaguzi huo alikuwa anatetea nafasi hiyo.

Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Mtwara, Stephen Buyuya, alithibitisha kuwa vurugu kubwa zilitokea wilayani Tandahimba mara baada ya kutangazwa kwa matokeo ya kura.

Alisema vurugu hizo zilikuwa kuba zaidi katika Kata ya Kitama, ambako Katani wa CUF anaishi.

Buyuya alisema polisi walilazimika kutumia nguvu za ziada kwa kupiga mabomu ya machozi na kuwakamata baadhi ya vijana, waliohusika katika vurugu hizo.

Hata hivyo, baadhi ya viongozi wa CUF na baadhi ya wakazi wa Kata ya Kitama, walisema wanaopaswa kulaumiwa kuhusu vurugu hizo ni polisi na Mkuu wa Wilaya ya Tandahimba, Husna Mwilima, ambaye anadaiwa kutumia vyombo vya dola ili kulazimisha wananchi wakubali matokeo.

Katibu wa CUF, katika Kata ya Kitama, Hassan Lipili alisema wakati ukusanyaji wa kura ukifanyika, mkuu huyo wa wilaya, alikutana na Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya ya Tandahimba, ili kupanga namna ya kuwadhibiti wafuasi wa CUF mara baada ya kutangazwa kwa matokeo.

Lipili pia alisema baadhi ya nyumba zilichomwa na polisi wakati wakirusha mabomu ya moto mitaani ili kuwahofisha wananchi wa Kitama na kusababisha wengi wao, kukimbia makazi na kujificha misituni.

Baba wa mgombea wa CUF, ambaye ni kada wa CCM, aliyewahi kushika nyadhifa mbalimbali ndani ya chama hicho, Juma Katani alisema mkuu huyo wa wilaya ndiye aliyechochea vurugu hizo.

Katani ambaye aliwahi kuwa kiongozi wa CCM ngazi ya tawi na Mwenyekiti wa Wazazi Wilaya ya Tandahimba, alisema Mwilima alikutana na mgombea wa CUF, viongozi na kuamuru wakubali matokeo kwa maelezo kuwa mgombea wa chama hicho cha upinzani ‘hana uwezo’ wa kuwa mbunge kwa vile ‘bado ni mtoto’.

“Sasa tunajiuliza, kama huyo mgombea wa CUF hana umri wa kuweza kuwa mbunge, Tume ya Uchaguzi iliwezaje kupitisha jina lake. Hili ni jambo la kushangaza kwa DC kusema hilo. Na hili lilitoa picha ya wazi kwamba CCM walimnyanga'anya ushindi," alisema Mzee Katani.

Mzee Katani alisema mgombea huyo wa CUF ana umri wa miaka 31 na alishuhudia mwanaye akiteswa na polisi pamoja na wafuasi wengine wa chama hicho, siku ambayo polisi waliendesha msako wa kamatakamata.

Mwananchi lilipowasiliana na mgombea huyo, alisema alikuwa jijini Dar es Salaam kwa matibabu kwani katika tukio hilo aliumizwa mbavu na kuvunjwa mkono wa kushoto.

Katani pia alisema wazee wa Kata ya Kitama wamemzuia asiende kijijini kwao kwa sababu hali aliyonayo ya kuonekana ana POP mkononi inaweza kuchochea hasira zaidi kwa wakazi wa Kitama wanaodai kuwa wamenyang'anywa ushindi.

Katani alisema ana mpango wa kupinga matokeo hayo mahakamani na kuwashtaki askari polisi waliompiga, ambao alisema anawafahamu wote kwa majina.

Mwananchi lilipowasiliana na Mwilima Alhamisi iliyopita, ili kufafanua kuhusu shutuma zinazomkabili, alisema asingeweza kuzungumza na mwandishi wa habari hizi kwa sababu hakuweka miadi ya kukutana naye.

Hata alipoambiwa na mwandishi wa habari hizi kwamba alikuwa tayari kumfuata siku yoyote ambayo angeipanga, alisema ana ratiba ndefu na asingeweza kusema mara moja bila kuichunguza kwa makini hivyo akaahidi kumpigia simu baadaye kumjulisha.

Mwananchi liliwasiliana naye mwishoni mwa wiki iliyopita lakini aliendelea kusisitiza kuwa hana nafasi na wala hayuko tayari kuwasiliana baadaye kwa njia ya simu.

Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Tandahimba, Abdalah Njovu, alipinga vikali kuwepo kwa uchakachuaji wa matokeo, ili kumpendelea mgombea wa CCM na kwamba hata matokeo ya udiwani yanadhihirisha kwamba chama hicho tawala kilishinda kihalali.

"Ni kweli kwamba mgombea wa CUF alionekana kufanya vizuri katika kata tisa wakati wa CCM naye alifanya vizuri katika kata 21. Hivyo hivyo katika udiwani CCM ilishinda kata 21 na CUF kata tisa,” alisema Njovu.

Njovu alikiri kwamba kuwa kulikuwa na vurugu na kwamba dalili zilianza kujitokeza baada ya wafuasi wa CUF kumiminika kwa wingi kwenye ofisi za Halmashauri ya Tandahimba, wakisubiri matokeo yatangazwe.

Kuhusu fujo zilizotokea kipindi hicho cha uchaguzi, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mtwara, alisema polisi walikwenda baada ya kusikia kuwa, nyumba zinachomwa moto

Buyuya alisema askari walipofika katika Kata ya Kitama, walishambuliwa kwa mawe, huku baadhi ya vijana wakijitokeza hadharani na kutamba kuwa wanasubiri polisi waishiwe risasi ili wawakamate na kuwakata shingo.
Alisema watu wanaodhaniwa kuwa ni wafuasi wa CUF, walipoona polisi wameingia katika eneo hilo, walifunga barabara zote kwa magogo, ili kuwafanya polisi washindwe kuondoka.

Kamanda huyo alisema askari polisi katika eneo hilo, walishuhudia baadhi ya nyumba zikiwaka moto, kitendo kilichowalazimisha kuanza kuwasaka wahalifu na kufanikiwa kuwatia mbaroni watuhumiwa 30.


Alisema hata hivyo watu 17 waliachiwa huru baada ya kuwahoji na kubainika kwa hawakuhusika katika vurugu hizo na kwamba wengine 13 wanatarajia kuwafikisha mahakamani.

Hata hivyo baadhi ya vijana katika kata ya Kitama walisema bado wanaishi kwa wasiwasi kufuatia vitisho kwamba polisi bado wanaendesha msako.

Buyuya alisema kuna uwezekano wa kuwatia mbaroni watu wengine kwa sababu bado upelelezi unaendelea.

CCM yadaiwa kutonesha majeraha ya uchaguzi
Katika hatua nyingine, kitendo cha CCM wilayani humo kufanya mkutano wa ndani katika Kata ya Kitama, kimetafsiriwa na wafuasi wa CUF kuwa ni kuendelea kutonesha makovu yaliyotokana na uchaguzi uliopita.

Baadhi ya wafuasi na viongozi wa CUF , wamedai kuwa kitendo hicho ni kinyume na makubaliano ya wakazi wa eneo hilo na vyombo vya dola kwamba hawatafanya mikusanyiko yoyote ambayo inaweza kusababisha hisia za kuzusha tena machafuko.

Makubaliano kati ya wakazi wa eneo hilo na polisi, yalifikiwa katika mkutano uliofanyika Novemba 4 mwaka huu, huko Kitama, baada ya kutokea kwa vurugu za kisiasa.

Hata hivyo, CCM wilayani humo, imedai kuwa mkutano huo ulikuwa maalumu kwa ajili ya kuwapa pole watu waliopoteza mali na kuchomewa nyumba, wakati wa vurugu hizo.

Viongozi na wafuasi wa CUF, ambao hadi sasa wanashikilia msimamo kwamba mgombea wao alinyang'anywa ushindi na kupewa mgombea wa CCM, walisema mkutano huo wa chama tawala uliofanyika wiki iliyopita, ulizusha wasiwasi mkubwa na hata baadhi ya watu kutaka kuuvamia ili kuusambaratisha.

Katibu wa CUF, (Lipil) alisema viongozi walifanya kazi ya ziada ya kujaribu kuwatuliza wafuasi wao waliokuwa na hasira, ili wasiingilie mkutano wa CCM na kuzusha machafuko mengine.

"Kufanyika kwa mkutano huo kumesababisha hali ya wasiwasi lakini sisi kama viongozi, tulijaribu kuwaambia wafuasi wetu wawe watulivu. Lakini CCM hawakupaswa kufanya kikao hicho wakati huu ambao polisi wamewataka wananchi kuwa watulivu, na kutokuwa na mikusanyiko inayoweza kusababisha uvunjifu wa amani," alisema Lipili.

Habari zilisema mkutano huo ulimhusisha pia Mwenyekiti wa CCM wilaya, Alhaji Dadi Mbuki, ulijadili mambo kadhaa zikiwemo sababu za chama hicho tawala, kupoteza kiti cha udiwani katika kata hiyo.

Katibu wa CCM wilaya ya Tandahimba, Mohamed Shaban alisema mkutano huo haukuwa wa ndani na kwamba ulikuwa wa wazi na ulikuwa maalumu kwa Mwenyekiti wa CCM wilayani hapa, kuwakabidhi Sh 400,000 waathirika.

Kamanda wa polisi Mkoa wa Mtwara, Stephen Buyuya alisema kwamba tangu walipofanya mkutano wa pamoja na wananchi hali ya amani imerejea na hawajapata taarifa zozote za kuwepo kwa hali ya kuzusha tena uhasama
 
Maskini ahmed katani kijana wa miaka 31 aliyepokwa ubunge wake na CCm halafu viongozi wa kitaifa wa KAFU wanashabikia Maalim Sheif kuwa makamu peke yake!! hawajui kuwa nguvu ya chama iko kwa wabunge. Hakuna kiongozi yeyote aliyekwenda huko kumsaidia huyu kijana!! CUF ni chama cha kufa tu!
 
Maskini ahmed katani kijana wa miaka 31 aliyepokwa ubunge wake na CCm halafu viongozi wa kitaifa wa KAFU wanashabikia Maalim Sheif kuwa makamu peke yake!! hawajui kuwa nguvu ya chama iko kwa wabunge. Hakuna kiongozi yeyote aliyekwenda huko kumsaidia huyu kijana!! CUF ni chama cha kufa tu!

cuf kimeshakufa siku hizi kinaitwa CCM B
 
''kutukana na msimamo wetu(cuf) mpya unaotokana na malidhiano ya zanzanzibar, naomba kuondo jina lango kwenye kinyang'anyiro cha naibu spika'' habib mnyaa. Kauli hii ni tosha kujua msimamo wa cuf kuwa ni kopo na mfuniko na ccm.
 
0 Reactions
Reply
Back
Top Bottom