CCM: Kutoka Tingatinga Hadi Shokamzoba... ( Makala, Raia Mwema)


M

maggid

Verified Member
Joined
Dec 3, 2006
Messages
1,084
Points
1,500
M

maggid

Verified Member
Joined Dec 3, 2006
1,084 1,500
Na Maggid Mjengwa,


ASKOFU Desmond Tutu alipata kuyasema haya;


“ Kuna tofauti ya kimsingi kati ya kuwa huru na kuwa katika hali ya kukandamizwa. Kuwa huru ni pamoja na kupata huduma za msingi za kijamii; kuwa na ajira, maji ya bomba, umeme, makazi bora na huduma za msingi za afya. Kuna maana gani basi ya kuwa huru wakati ubora wa maisha ya watu haujaimarishwa? Kama sivyo, hata kura nazo hazina maana yeyote!” – Desmond Tutu ( William Gumede; Thabo Mbeki And The Battle For The Soul Of The ANC, Uk. 67)Na mwanafasihi Mtanzania Profesa Kezilahabi anayesema haya: “ Siku hiyo ikifika utaona ishara itakayokuongoza. Utakapofika pale ambapo kila binadamu lazima afike utajua hukukosea; kwani njia ya kwenda huko inajulikana kwa wote na inakwenda moja kwa moja bila kupinda.


Huna haja ya kusoma kitabu chochote kupata maelezo ya kwenda huko wala hakuna haja ya kusikiliza mahubiri. Hakuna utalaamu unaohitajika , maana utajikuta umefika. Utakapofika utamkuta amekaa peke yake akiwatazama wale wengine . Hao wengine utawatambua maana ni ndugu zako wote.Wengi kati yao ndio wale waliokuwa askari wa mwanga. Wale ambao hutaweza kuwatambua atakutambulisha kwao, na wewe utachukua nafasi yako. Usistuke utakaposikia majina yao; maana, wengi kati yao wana majina makubwa. Utawakuta wanafanya jambo fulani. Wewe pia fanya kama wao bila kuuliza , bila manung’uniko, na usikate tamaa. Kwa sasa hivi subiri ishara” ( E. Kezilahabi, Nagona)Na kwa masikio yangu, nilipata kumsikia Philip Mangula akiyatamka haya mwaka 2007; “ Isifike mahali CCM ikatangaza tenda za uongozi!” Ilikuwa ni kwenye Ukumbi wa Mikutano wa St. Dominic, Iringa, Septemba 10, 2007. Ni kwenye Mkutano wa CCM Mkoa wa Iringa.

Hiyo ilikuwa ni kauli nzito kutolewa na aliyekuwa Katibu Mkuu wa zamani wa CCM. Mangula aliyatamka hayo wakati akitoa hotuba ya kushukuru wajumbe. Alishindwa nafasi ya Uenyekiti wa Mkoa, na aliambulia kura 332.


Leo ndani ya CCM Mangula amepewa nafasi ya Umakamu wa Mwenyekiti wa CCM, Bara. Na majukumu makubwa mawili ya Makamu ni haya; Mosi, kumshauri Mwenyekiti, Pili, kusimamia maadili. Na tayari Mangula ametamka, kuwa ndani ya miezi sita atakuwa ameshakisafisha chama chake. Swali; Je, atawageukia pia ‘ waliomdhalilisha kisiasa’ pale Ukumbi wa St. Dominic Iringa mwaka 2007?


Naliona tatizo linaloikabili CCM kama Chama cha siasa. Limewasahau wale ambao Askofu Tutu amewazungumzia; ni umma uliochoshwa na malumbano ya kisiasa yasiyoisha, ambayo, msingi wake ni vita vya wenyewe kwa wenyewe ndani ya chama. Vita vya kuwania nafasi za juu za uongozi. Umma, ambao kwao wao lililo la msingi ni kuhakikishwa wanapata huduma muhimu za msingi, kama vile ajira, elimu, maji ya bomba, makazi bora, huduma za afya na mengineyo. Umma unahitaji kutoka kwa wanasiasa, kauli zenye kuwatia matumaini ya baadaye. Kauli zenye kuashiria, kuwa mwenye kuzitoa amedhamiria kutatua matatizo yao ya kimsingi.


Na katika siasa kuna Uongozi na Utawala. Kazi ya chama cha siasa ni kuongoza, hivyo basi, kuisimamia Serikali kutekeleza majukumu yatakayoupa umma nafuu ya maisha. Na kazi ya utawala ni ya Serikali, kwa kusimamiwa na Chama cha Siasa. Tatizo ni pale Chama cha siasa kinapochukua jukumu la kutawala badala ya kuongoza.


Huko nyuma CCM ilikuwa kimbilio la wanyonge. CCM ilichukua jukumu lake la kuongoza, kuisimamia Serikali.

CCM ilipata kuwa na Makamu Mwenyekiti aliyekuja pia kujulikana kama ‘ tingatinga’- Ni John Malecela. Hakika, CCM haikuhitaji ‘ tingatinga’ bali uongozi utakaousimamia Serikali katika kutekeleza majukumu yake, na wanasiasa wa aina ya akina Malecela walipaswa kwenda kwa wananchi kuwaeleza kwa hoja kile ambacho CCM, kama chama kinafanya katika kuisimamia Serikali na matunda yaliyopatikana. Ni kutokana na kutolitambua jukumu hilo la chama cha siasa, haikuwa ajabu kuona hata ‘ tingatinga’ nalo ‘likatitia’ kisiasa. John Malecela alishindwa hata kwenye kura za maoni jimboni kwake.

Nionavyo, uteuzi wa Philip Mangula unaweza kuiletea tija CCM kama Mangula atachukua jukumu la kuwa ‘ Shoka Mzoba’ la kisiasa ndani ya CCM. Mangula atakayechukua jukumu la kuweka uwiano wa mitikisiko ya ndani ya chama inayotokana na vita ya kuwania uongozi, na kwa sasa, kuelekea 2015. Mangula ambaye hatasikiliza umbeya wa kisiasa bali vithibitisho vya madai yanayotolewa na pande zinazosigana kwenye chama chao. Maana, hata kwa maslahi ya nchi yetu, ni heri kuwa na CCM yenye makundi yenye kuwania Urais 2015 kuliko CCM yenye magenge yenye kuendesha biashara ya ‘ Siasa za reja reja ama ‘siasa za mafungu’ – Retail politics.


Ni kwenye ‘ Siasa za mafungu’ ndipo utawakuta wana-CCM wenye kudhani wao ni wasafi na wenzao ni wachafu. Wakati, kimsingi, jamii nzima kwa sasa ni kama imeoza kimaadili. Leo utawakuta wala rushwa CCM, na hata kwenye vyama vya upinzani. Utawakuta makanisani, misikitini na hata kwenye sekta ya michezo.


Kinachohitajika ni mkakati wa kitaifa utakaohakikisha, uko twendako tunapunguza idadi ya viongozi wa kisiasa, kijamii na hata kimichezo watakaoingia kwa nguvu za fedha, hivyo basi, nguvu ya rushwa. Kama alivyopata kutamka Mwalimu kwenye Kitabu Chake; Uongozi wetu na Hatma ya Tanzania – Rushwa ni kama kansa kwenye jamii yetu. Hivyo basi, ni tatizo la kimfumo zaidi kuliko la baadhi kwenye jamii.


Tunafanyaje basi , kama Taifa kuweka mazingira ya kupunguza, ama kumaliza rushwa kwenye chaguzi zetu? Itaendelea juma lijalo.

0712 95 61 31 / 0788 111 765/ 0754 678 252 http: //mjengwablog.com
 

Forum statistics

Threads 1,296,628
Members 498,713
Posts 31,254,170
Top