CCM kumeguka ni muhimu kwa Taifa! | JamiiForums | The Home of Great Thinkers

Dismiss Notice
You are browsing this site as a guest. It takes 2 minutes to CREATE AN ACCOUNT and less than 1 minute to LOGIN

CCM kumeguka ni muhimu kwa Taifa!

Discussion in 'Jukwaa la Siasa' started by Mzee Mwanakijiji, Nov 12, 2008.

 1. Mzee Mwanakijiji

  Mzee Mwanakijiji Platinum Member

  #1
  Nov 12, 2008
  Joined: Mar 10, 2006
  Messages: 31,362
  Likes Received: 6,393
  Trophy Points: 280
  Na. M. M. Mwanakijiji (Tanzania Daima)

  CCM KUMEGUKA NI MUHIMU KWA TAIFA

  Na. M. M. Mwanakijiji

  Wakati Baba wa Taifa amesema maneno yale “Upinzani wa kweli utatoka ndani ya CCM” sikuwa nimeyaelewa vizuri. Sasa hivi maneno hayo hata hivyo yanapiga kelele katika mawazo yangu na kuacha mwangwi urindimao katika fikra zangu kila kukicha. Kama tunataka kweli kwenda na kufika kwenye ile nchi ya ahadi mambo kadhaa yanahitaji kutokea yakikihusu Chama cha Mapinduzi.

  La kwanza ni kuwa CCM lazima ishindwe katika uchaguzi mkuu. Chama chochote tawala kinapokaa madarakani kwa muda mrefu kinajenga tabia mbili za hatari; moja ni tabia ya kuzoea na ya pili tabia ya ufisadi. Kwenye tabia ya kuzoea chama tawala kitakuja na kila aina ya mipango mizuri kwenye vitabu na kwenye makaratasi; vitazindua miradi ya kuvutia na kuanzisha kila aina ya kampeni. Matokeo yake chama hicho kinabakia kuwa ni chama cha “uzinduzi”.

  Mara wamezindua barabara, mara wamefungua jengo fulani, mara wamezindua mradi wa visima vya maji n.k Wao sifa yao kubwa iko katika kuzindua vitu na kupiga picha za uzinduzi na kutamba kuwa mradi waliofungua wa wananchi umegharimu kiasi fulani. Na wananchi ambao wamezoea mambo ya kuzindua hujikuta wakisherehekea uzinduzi wa vitu visivyokoma. Hivyo chama kinakuwa na mazoea ya kuanzisha mambo tu. Sasa kuzindua peke yake hakutoshi lazima kuwa na ufuatiliaji endelevu wa yale yaliyozinduliwa.

  Leo hii akipita mtu kufanya tathmini ya miradi mbalimbali ambayo imefunguliwa na serikali (ukiondoa ile ya wafadhili ambayo mara nyingi ina ufuatiliaji wa karibu) utashangaa ji kwa kiasi gani miradi ile imetunzwa kwa kiwango kinachostahili. Hebu mtu atembelee shule tulizozifungua miaka mitatu iliyopita kwa mbwembwe hadi kiongozi mmoja kututambia Bungeni kuwa tunapaa. Je hizo shule leo zinaonekanaje? Je bado zina mabati yote, milango na madirisha?

  Sasa hiyo ni tabia ya mazoea. Yaani chama tawala kinakuwa na mazoea ya kuanzisha mambo bila ya kuyafuatilia ili kuyamaliza au kuhakikisha yanadumu kwa kiwango kinachostahili. Kwa hiyo kinakuwa chama cha mazoea ya mambo yale yale. Ndio maana leo hii maneno ya “kasi mpya, ari mpya, na nguvu mpya” huyasikii tena kwa sababu Chama tawala hakiwezi kuwa na “ari mpya, nguvu mpya, na kasi mpya” kikiwa na tabia ya mazoea!

  Tabia ya pili ambayo inatokana na chama kuwa madarakani kwa muda mrefu ni tabia ya ufisadi. Tabia hii ya pili inatokana na hiyo ya kwanza (ya mazoea). Watumishi waliodumu muda mrefu katika chama tawala wanakuwa na mazoea ya kufanya mambo yale yale kwa mtindo ule ule na ni vigumu sana kwa wao kubadilika. Mazoea haya yanaanza kujenga tabia ya kuanza kutumia madaraka, vyeo, na nafasi mbalimbali kujinufaisha wao wenyewe huku wakiendelea kuzindua miradi mbalimbali kana kwamba wanafanya kitu fulani cha kushangilia. Sasa haina maana kuwa hawafanyi kitu ila kile wanachokifanya na kukitangaza kuwa wanafanya ni kiduchu kweli kulinganisha na kile ambacho wangeweza kufanya au wanapaswa kufanya.

  Sasa huu ufisadi unatokea taratibu kwa sababu kwa vile wamezoeana na wanajuana inakuwa vigumu kweli kwa wao wenyewe kuwajibishana kiasi kinachostahili. Matokeo yake utakuta kuna tabaka la aina fulani la ufisadi unaokubalika katika jamii.

  Mbunge wa Kigoma Kaskazini Mhe. Zitto Kabwe akiandika kwenye mtandao maarufu duniani wa Watanzania wa jamiiforums.com ameelezea kisa cha mzee mmoja ambaye alikuwa anatafuta haki yake kutoka kwenye idara moja nyeti ya serikali (TRA). Mzee huyo baada ya kuhangaika kwa muda mrefu alijikuta kila anakokwenda ili aweze kutatuliwa tatizo lake alihitaji kutoa ahadi kuwa mambo yakimuendea basi “awakatie” watumishi waliomsaidia kitu kidogo.

  Mzee huyo hakuwa tayari kufanya hivyo. Alipopata nafasi ya kumuelezea Bw. Kabwe juu ya suala lake na Zitto alipoamua kuandika barua kwa Waziri Mkuu, Mzee yule kwa mujibu wa Mhe. Zitto “ akainama na kuniambia, ' Mheshimiwa Zitto (ninamquote hapa maana sipendi kuitwa mheshimiwa) kama ukifanikiwa kunisaidia suala hili, nitakujengea nyumba nzuri Kigoma'”

  Sasa Zitto anaelezea mwitikio wake “Kalamu ilianguka kwa kutetemeka kwa hasira; Mratibu wa Ofisi yetu alikuwa ananiangalia na akitarajia kuachana na Mzee huyu. Nilimtazama Mzee huyu na kumwambia 'Baba, hii ni haki yako huna haja kuinunua. Mimi pia hii ni kazi yangu, ninalipwa kuifanya. Sitaki nyumba yako. Sitaki chochote kutoka kwako”

  Sasa mtu anaweza kuguswa na mwitikio wa Ndg. Zitto lakini ukiangalia vizuri mwitiko wake ulipaswa kuwa hivyo. Lakini kubwa zaidi (tukiamini simulizi la Zitto) ni ujasiri wa Mzee huyo mwenye shida pasipo woga, haya wala kufikiria anachosema kutoa “hongo” namna hiyo. Ukiangalia utaona kuwa katika sehemu nyingi za jamii yetu tumezoea mno vitendo vya ufisadi kiasi kwamba wakati mwingine hata hatufikirii mara mbili. Hii inatokeana na kujengeka katika jamii yetu kwa utamaduni wa kifisadi ambao msingi wake ni utawala wa muda mrefu wa chama kimoja.

  Sasa, ili mambo yaweze kugeuka ni lazima CCM ishindwe uchaguzi mkuu ili hatimaye tuweze kuanza upya kujenga Taifa letu jinsi ile ambavyo tunataka.

  Lakini jambo jingine ambalo linatokana na hilo la CCM kupoteza uchaguzi ni kuwa aidha CCM kama ilivyo ishindwe kwenye uchaguzi huo au ilazimishwe kushindwa toka ndani yake yenyewe.

  Kuilazimisha kutoka nje ni kwa kutokea chama kingine ambacho siyo tu kina sera nzuri lakini wananchi wanaweza kuamini kuwa kinaweza kweli kuchukua madaraka ya nchi na kesho wake wananchi wakaenda zao sokoni, kazini, na shuleni kama kawaida pasipo kukaa na kusikiliza radioni nini kimetokea. Chama hicho kwa sasa hakipo. Kuna dalili kwa mbali tunaweza kuiona lakini kama mwanga wa alfajiri ukimulika toka Mashariki ndivyo chama hicho bado tunakiona kwa mbali lakini bado kikiwa kimetingwa na giza na ukungu wa asubuhi. Bado hakijasimama na kuwa kweli chama mbadala.

  Njia hii ya kuwa na chama mbadala ni bora zaidi na ya kuaminika zaidi kwani italeta nchini siasa mpya ambapo wananchi wanaweza kubadilisha vyama hivi pasipo kuwa na matatizo yoyote au kufikiria mara mbili kwani wanajua vyote viwili vinaweza kuunda serikali na kushikilia nchi. Mfano mzuri ni uchaguzi wa Marekani ambapo chama cha Repablikani kimepoteza nafasi ya Urais, na Mabaraza yake mawili ya Uwakilishi kufuatia ushindi wa Seneta Barack Obama.

  Mara baada ya kutangazwa ushindi huo hakukuwa na uchafuzi wa aina yoyote, mapigano, au mtu kung’ang’ania kuwa yeye ndiyo Rais. Seneta McCain alimpigia simu mshindi na kumpongeza na siku ya Jumatano Rais Mteule Obama (toka chama kimoja) alienda kumtembelea Rais anayemaliza muda wake Bush (toka chama kingine) na kukaa pamoja licha ya maneno makali aliyoyatoa dhidi yake na ambacho yalichochea ushindi wake. Kwanini hilo limewezekana?

  Kwa sababu Wamarekani hawana hofu nani anayechukua madaraka kila baada ya miaka minne kwani wanajua akiwazingua wanamtimua miaka minne ijayo! Katika Tanzania bado hili ni gumu kama tulivyoshuhudia kwa majirani zetu Kenya na Zimbabwe. Hivyo, hili la kuwa na chama mbadala ni muhimu sana kama kweli tunataka kujenga utawala wa kidemokrasia, huu utitiri wa vyama tulionao unapoteza muda, unatawala vipaji, na kamwe hautaleta chama mbadala. Lakini kuombea hilo kwa sasa ni sawa na kusubiri mvua za masika jangwani!

  Ambalo linapaswa kutokea ni kile ambacho kinatokea Afrika ya Kusini sasa hivi. Chama cha Mapinduzi ni lazima kimeguke kama kweli kinataka kurudi kwenye misingi yake na kushiriki upya katika ujenzi wa Taifa jipya la Kitanzani kwani kilivyo sasa kinaenda kwa kuvutana kamba.

  Ili kiweze kumeguka kweli kinahitaji ndani yake watu watakaogongana kimawazo na kimtazamo. Ni lazima utokee mgongano wa kifikra, kiuongozi, na kimwelekeo ili CCM iweze kuwa na kambi kubwa mbili ambazo haziwezi kukaa pamoja na hazipaswi kukaa pamoja. Kule Afrika ya Kusini baada ya kambi ya Zuma kujipanga vizuri na hatimaye kumnyima Mbeki Uenyekiti wa ANC na baadaye kuhakikisha kuwa Mbeki anakuwa dhaifu ndani ya Chama hatimaye waliweza kusababisha Mbeki kuachia ngazi mapema kabla ya muda wake.

  Kama kina Zuma walitarajia Mbeki angeondoka kimya kimya walifanya makosa na matokeo yake mashabiki wa Mbeki wameamua kujimega kutoka ANC na kuunda chama kingine cha kisiasa. Sijui ni kwa kiasi gani chama hicho kitakuwa na nguvu katika siasa za Afrika ya Kusini kwani yawezekana kukawa na mambo ya kikabila au majimbo ndani yake lakini kwa vyovyote vile kunailazimisha ANC aidha kubadilika au kujikuta inabadilishwa.

  Hilo ndilo linalohitajika kutoka ndani ya Chama cha Mapinduzi. Hata hivyo haliwezi kutokea hadi pale baadhia ya “vigogo” wa chama hicho hasa wakongwe au wale ambao wamejikuta wakiwekwa pembeni kutokana na misimamo yao watakapoamua kujitoa ndani ya chama hicho na kuanzisha chama kingine. Hili litawezekana tu pale ambapo wakongwe walioko CCM watakapotambua mioyoni mwao kuwa CCM siyo mama yao. Pale watakapotambua kuwa wanaweza wasife wana CCM lakini watakufa wakiwa ni Watanzania!

  Sasa hivi heshima kubwa ambayo baadhi yao wanayo (kama alivyosema Mzee Kawawa miaka ile) ni kuhakikisha kuwa wanakufa wakiwa wana CCM pia. Wengine kati yao wameapa kabisa kuwa liwalo na liwe wao ni “wana CCM mpaka kufa”. Nakumbuka wengine wetu tuliimba nyimbo za “naapa naahidi mbele ya Chama, Mapinduzi nitakulinda mpaka kufa”. Lakini ahadi hiyo ni ya uongo kwani utii na mapenzi yetu kama raia wa taifa letu hayawezi kamwe kuwa kwa mtu, idara, taasisi au chama cha kisiasa. Mapenzi na utii wetu wa kwanza na wajuu zaidi ukiondoa ule ulioko kwa muumba wetu ni kwa nchi yetu.

  Wazo hili litakapoingia ndani ya viongozi wa CCM hasa wale ambao kweli wanaamini mabadiliko yanahitajika haitawachukua muda kuamua kujitoa ndani ya CCM na kuanza harakati za kuleta mabadiliko ya kweli.

  Hili hata hivyo haliwezi kuwa jambo la mtu mmoja mmoja kama ilivyokuwa kwa Ndg. Mrema (mwenyekiti wa sasa wa TLP). Kujiondoa kwa mtu mmoja ndani ya CCM haitoshi inabidi kundi zima la wana CCM mahiri na mashuhuri liamue kujitoa ndani ya chama hicho kama ishara ya kuchoshwa na mambo yalivyo lakini pia kama alama ya kutaka kuanza upya.

  Tatizo kubwa la mpango huo ni kuwa kuna dalilii kuwa wale watakaotoka yaweza kuwa ni wale ambao tayari wamekataliwa na wananchi na hawana ule “ujiko” wa kisiasa au mtaji wa kisiasa wa kuwaweza kufanya kuwa na nguvu nchini. Lakini endapo watakaotoka ni wale ambao wananchi wamewaona ni watetezi wao, wapiganaji wao, au kwa namna fulani wanasimamia maslahi ya Taifa basi CCM itakuwa kweli imepata mpasuko unaostahili.

  Kumeguka huko kwa CCM kutasababisha mgongano wa kifikra katika Taifa, mgongano ambao utachuja makapi na nafaka na kuchuja viongozi uchwara na wenye masihara kutoka katika viongozi walio bora. NI mgongano ambao mbegu zake tumekuta tukizipanda taratibu.

  Hata hivyo, ili mgongano huo na mpasuko huo utokee unahitajika ujasiri wa kweli wa maamuzi. Lakini kitakachosababisha hasa mpasuko huo ni pale ambapo serikali ya CCM itakapoamua kuruhusu wagombea binafsi nchini.

  Hakuna kitu ambacho kinaitisha CCM na watawala wake kama wagombea huru. Wagombea huru wasiofungamana na chama chochote ni tishio kubwa kwa CCM kuliko upinzani uliopo sasa. Sababu kubwa ni kuwa wagombea huru hawafungwi na nidhamu ya chama fulani au woga kwa “mwenyekiti wa chama”. Wao wanafungwa na wapiga kura wao. Ni kwa sababu hiyo CCM imejitahidi sana kukwepa kuruhusu wagombea binafsi kwa sababu endapo watafanya hivyo watakuwa wameamua kutumia mafuta yao wenyewe kukaangwa.

  Hata hivyo naamini kabisa ya kuwa ni kwa maslahi ya Taifa wabunge wa CCM waiteke hoja ya wagombea binafsi na kuilazimisha kwa nguvu ya kisheria. Kama serikali yenyewe haitaki kuleta mswaada wa mabadiliko hayo ya sheria wakati umefika kwa mbunge mahiri wa CCM kuleta mswada binafsi wa kuleta mabadiliko hayo. Sababu kubwa ni kwamba, wakileta mabadiliko ya sheria hiyo ni wazi kuwa wabunge wengi waliopo sasa ndio watakuwa wa kwanza kufaidika nao hasa kama CCM itaendelea kutumia mfumo wake wa kura za maoni na maamuzi ya Kamati Kuu katika kutafuta wagombea wake.

  Vinginevyo, bado ninaamini ya kuwa kumeguka kwa chama cha Mapinduzi ni muhimu kutokea ili hatimaye Taifa letu liweze kuanza upya safari ya maendeleo. Sababu kubwa ni kwamba CCM imetawala muda mrefu na haiwezi kubadilika au kujibadilisha. CCM imeendelea kutawala kwa kawaida huku ukifanya mazingaombwe ya kuonesha inabadilika kumbe inabakia vile vile; na CCM hata kama ikipigiwa mbiu ya mgambo haiko tayari kujisafisha na kuleta mabadiliko ya kweli ya Taifa kwa kadiri ya kwamba hali iliyopo inainufaisha yenyewe.

  Ndio maana utaona kuwa mambo yanayohusu CCM wako tayari kuyadili kwa kina kuyachukulia hatua madhubuti lakini yanapokuja yale yenye umuhimu kwa Taifa inabidi hadi watu waandamane. Hebu fikiria suala la EPA peke yake hadi watu kufikishwa mahakamani imechukua miaka miwili, na hapo kesi haijaanza.

  Na hapo hatujaanza kuangalia suala la Meremeta, Mwananchi Gold, Deep Green Finance, Kagoda, Rada, Malori, Helikopta, Majengo ya BoT n.k Kama jambo moja tu limechukua miaka miwili haya yote yakijakumalizwa kuna wengi wetu hapa tutakuwa tumeshaondoka katika ulimwengu huu na wajukuu zetu wakiandalia kuhangaika nayo! Kwa kadiri tunakubali na kushangilia mazingaombwe tunayoyaona ndivyo hivyo na wenyewe hawaoni haraka ya kufanya jambo lolote kwa sababu wamezoea jinsi ilivyo.

  Lakini vyovyote vile ilivyo, kama kweli Tanzania inataka kupati nafasi ya kufanikiwa na kuanza kuelekea nchi ile tuitamaniyo, CCM kama ilivyo sasa haistahili kuendelea kuliongoza Taifa letu baada ya 2010. Aidha wanyang’anywe Urais (kama ilivyotokea Afrika Kusini, au wanyang’anywe Bunge (kama ilivyotokea Kenya), au wanyang’anywe vyote viwili (kama ilivyotokea Marekani). Kuwaachia waendelee walivyo sasa, ni kuwapa baraka ya kutudumaza.

  Niandikie: mwanakijiji@mwanakijiji.com
   
 2. Field Marshall ES

  Field Marshall ES JF-Expert Member

  #2
  Nov 13, 2008
  Joined: Apr 27, 2006
  Messages: 12,659
  Likes Received: 69
  Trophy Points: 0
  Wananchi wa Tanzania tunatakiwa kupigania mabadiliko ya katiba ya Jamhuri, CCM sio tatizo, tatizo ni katiba yetu ya chama kimoja ambayo imekua ikitumika under system ya vyama vingi vya siasa, ni kosa moja kubwa ambalo mpaka leo viongozi waasisi wa Upinzani wetu Tanzania, wameshindwa kulikubali kuwa walilifanya mwanzoni.

  Wa-Tanzania hatuwezi kuhubiri mabadiliko kwa kutegemea dhana ya CCM kumeguka, tunatakiwa kutegemea vyama vyetu vya upinzani CCM haiwezi kumeguka na haitakuja kumeguka, not in our life time infact tunapoanza ku-preach haya ya kumeguka kwa CCM ni dalili tosha za kukubali kutupa taulo la kushindwa na kukubali kwamba CCM haiwezekaniki mpaka ijikate yenyewe.

  Wananchi wa Tanzania, tulilie mabadiliko ya katiba tu, kwa sababu as long as rais mwenyekiti wa CCM ana madaraka aliyonayo sasa, CCM haitakuja kumeguka, hao wakuimegua CCM sasa hivi wengi wana tuhuma nzito sana za uhalifu, na wanajua siku wakitoka tu watatinga kwenye mkono wa sheria, dawa ni kubadili katiba ili kupunguza nguvu kubwa alizonazo rais wa jamhuri, ili kuleta utawala wa respect kwa the rule of law, mengine yote yatajiweka sawa.

  Kwamba eti wazee wa CCM watajitoa ndani ya CCM, hiyo pia ni ndoto maana wengi wao sasa hivi wanategemea pension ya serikali ya CCM, kwa hiyo kama dhana ya kutukomboa ni hii ya kumeguka kwa CCM, tumekwama as a nation!

  Lakini kwamba eti CCM itameguka, hapana haitakuja kutokea na hii katiba ya Jamhuri tuliyonayo.
   
 3. Mzee Mwanakijiji

  Mzee Mwanakijiji Platinum Member

  #3
  Nov 13, 2008
  Joined: Mar 10, 2006
  Messages: 31,362
  Likes Received: 6,393
  Trophy Points: 280
  Katiba itabadilishwa vipi na CCM hii hii; kama kulililia mabadiliko ya Katiba mzee si NCCR ilipoanza ilikuwa na lengo kubwa la kuleta mabadiliko ya Katiba? Suala la kulilia Katiba mpya mbona limesemwa sana?

  Hata hiyo Katiba mpya kama kweli tunataka iwe ni Katiba ya wananchi kweli, haiwezi kutokea kwa kadiri ya kwamba CCM bado iko ilivyo. Katiba mpya haitakuja hadi wabunge wa CCM watakapoamua wao kuidai na hivyo kusababisha mmeguko (kati ya wale wanaotaka Katiba mpya na wale wanaooona Katiba iliyopo inafaa).

  Hata sisi wananchi tulie vipi kutaka Katiba mpya haitatokea kwa kadiri ya kwamba CCM bado ni moja. So, it begs the question.... kipi kitangulie? Katiba mpya ili isababisha mgawanyiko CCM, au Mgawanyiko CCM ili usababishe Katiba mpya?
   
 4. Field Marshall ES

  Field Marshall ES JF-Expert Member

  #4
  Nov 13, 2008
  Joined: Apr 27, 2006
  Messages: 12,659
  Likes Received: 69
  Trophy Points: 0
  Wananchi wa Tanzania tukitaka ibadilishwe inaweza kubadilishwa, so far hatujataka au kuamua on a serious tone kwamba tunataka kubadilishwa kwa katiba, hawa watuhumiwa wa EPA wako kizimbani kwa sababu ya pressure yetu wananchi na sio kwa bahati tu.

  Lowassa aliondoka kwenye power sio kwa bahati mbaya ilikuwa ni pressure yetu wananchi, tatizo tulinalo wananchi wa Tanzania ni moja tu ni wepesi wa kuridhika na machache tu, huwa hatudai mpaka mwisho.

  Kwenye la katiba viongozi wetu wa upinzani walituangusha toka mwanzoni kwa sababu ya tamaa ya madaraka, yaani tamaa mbele mauti nyuma walifikiri kwamba ni kweli wananchi walikuwa wamechoshwa na utawala wa Mwalimu, walifikiri kwamba ni kweli wananchi wamechoshwa na utawala wa CCM, hawakujua kwamba vile vilikuwa ni vilio tu vya wananchi wachache ambao sio hata wapigakura, hata wafadhili wetu ambao ndio walioikaba koo CCM kukubali vyama vingi vya siasa walishangazwa sana na vyama vipya kutolilia kubadilishwa kwa katiba kwanza kabla ya anything.

  The Scandnavians, ambao ndio hasa waliokuwa the big push behind kuanzishwa kwa upinzani, ndio hasa wa kulaumiwa zaidi kwani na wao walidhani kuwa wananchi wengi hawaipendi CCM, halafu the biggest mistake of all the players wa Upinzani na hawa wafadhili, ilikuwa ni kuwa-underestimate CCM of what they will do under a threat ya kukosa mlo, sasa tuko kwenye worse political situation kuliko tulipokuwa bila upinzani.
   
 5. Mzee Mwanakijiji

  Mzee Mwanakijiji Platinum Member

  #5
  Nov 13, 2008
  Joined: Mar 10, 2006
  Messages: 31,362
  Likes Received: 6,393
  Trophy Points: 280


  tutake vipi na tutumie tone gani kuonesha kweli tunataka?

  Lowassa hakuondoka kutoka na pressure ya wananchi aliondoka in spite of JK and as strategic move on his part. Angetaka kukaa angeendelea na wala wasingefanya lolote.


  Wananchi sasa hivi unafikiri wamebadilika? Miaka mitatu tu iliyopita kwa kutumia Katiba hii hii waliweza kuipa CCM ushindi mkubwa kweli, unafikiri wanahusisha matatizo yaliyopo na Katiba iliyopo?


  Tatizo la Katiba mpya Tanzania siyo wapinzani, siyo wafadhili, na siyo wananchi; Tatizo la kupatikana Katiba mpya Tanzania ni CCM. We deal with CCM we get new constitution; may be not as simple as that lakini hatuwezi kuwa na Katiba mpya bila kushughulikia the CCM factor.
   
 6. Field Marshall ES

  Field Marshall ES JF-Expert Member

  #6
  Nov 13, 2008
  Joined: Apr 27, 2006
  Messages: 12,659
  Likes Received: 69
  Trophy Points: 0
  Lakini CCM haiwezi kubadili katiba bila kushinikizwa na sisi wananchi, katiba ya sasa inawaruhusu wachache ndani ya CCM kuendelea na mlo, sasa CCM haiwezi kubadili katiba yenyewe ili hao wachache wakose mlo,

  Tatizo linakuja ni kama wananchi tunaelewa kinachoendelea, kwa sababu tukikazania dhana ya kumeguka kwa CCM, hivi mkuu unajua CCM wanaweza kujimegua kwa magirini na wakaendelea kupeta, kama walivyokubali kuanzishwa kwa upinzani, huku wakijichomeka kwa siri kwenye hivyo vyama,

  Naomba kumaliza kwa kusema hivi tuwe waangalifu na what we are crying for, tumeshafanya makosa ya kutosha, sasa umefika wakati tuwe waangalifu ili tusiwe tunarudia tena makosa yake yale na wananchi wa Tanzania, tujifunze kulilia ishus mpaka mwisho, badala ya kukubali kudanganywa mara kwa mara na viongozi wetu na majibu nusu nusu.

  Anyways ni mawazo yangu tu machache.

  Thanxs And Out!
   
 7. Mzee Mwanakijiji

  Mzee Mwanakijiji Platinum Member

  #7
  Nov 13, 2008
  Joined: Mar 10, 2006
  Messages: 31,362
  Likes Received: 6,393
  Trophy Points: 280


  Utaona nimelielezea hilo pia, kwa maana kwamba kumeguka peke yake haitoshi ni nani amemeguka kwangu ndilo muhimu kwani kama watu kutoka CCM wapo wametoka na tumewaona. We need more than tokens of change!

  hamna neno..
   
 8. Madela Wa- Madilu

  Madela Wa- Madilu JF-Expert Member

  #8
  Nov 13, 2008
  Joined: Mar 24, 2007
  Messages: 3,074
  Likes Received: 35
  Trophy Points: 135
  Limetumika neno kumeguka na si kuimega.
  Biskuti imemeguka.
  Nimeimega Biskuti.
  Gema limemeguka.
  Tumelimega gema.
  CCM itameguka.
  Tutaimega CCM.
  Kumeguka ni kitendo chenye uhusiano na nguvu ya ndani inaathirika kutokana udhaifu unaojengeka ndani kwa ndani na kuleta mgawanyiko.
  Kumega ni kitendo chenye uhusiano na nguvu kutoka nje yenye uwezo wa kuidhofisha nguvu ya ndani na kuleta mgawanyiko.

  Kwa hiyo kumeguka kwa CCM si jambo litokanalo nda Dua zetu bali ni matokeo ya Uchoyo, Pupa na Uroho wa kila kitu ndani ya CCM.

  Falme nyingi Duniani, hata zile zenye nguvu nyingi mno za ajabu kama Rome empire ziliangamia kutokana na kumeguka na si kumegwa, kumegwa kilikuwa ni kitendo cha mwisho baada ya zenyewe kumeguka.

  Kwa kipindi kirefu,Rushwa uongo na upendeleo ulitumika kuwahadaa mamilioni ya Watanzania ili kuiweka CCM madarakani .
  Rushwa, udanganyifu na upendeleo vimeshindwa kabisa kabisa kutumika katika kujenga safu za uongozi ndani ya CCM.
  Rushwa za wazi katika Chaguzi za ndani za CCM, Upendeleo wa wazi katika kuteua wagombea na taarifa zilizoshehena uongo ndani ya vikao vya CCM vimegeuka kuwa Kansa ya kisiasa isiyo na tiba zaidi ya kifo.
  Kwa hiyo CCM itameguka au ni muhimu kumeguka
  Mkuki siku zote ni mtamu kwa nguruwe tu.
   
 9. J

  Jasusi JF-Expert Member

  #9
  Nov 13, 2008
  Joined: May 5, 2006
  Messages: 11,484
  Likes Received: 165
  Trophy Points: 160
  CCM imeshameguka. Kinachosubiriwa ni confirmation of the fact.
   
 10. M

  Mama JF-Expert Member

  #10
  Nov 13, 2008
  Joined: Mar 24, 2008
  Messages: 2,858
  Likes Received: 20
  Trophy Points: 0
  okay, shibuda apendekezwe kuwa mwenyekiti ccm b, lowassa, katibu na rostam mweka hazina.
   
 11. Field Marshall ES

  Field Marshall ES JF-Expert Member

  #11
  Nov 13, 2008
  Joined: Apr 27, 2006
  Messages: 12,659
  Likes Received: 69
  Trophy Points: 0
  Kumeguka kwa CCM, hakuwezi kuwa a strategy ya kusubiriwa na sisi wananchi as our last hope au resort, katika kuleta mabadiliko muhimu kwa taifa letu, CCM are too smart kwa this kind of strategy kwa sababu ndani ya chama hawana uroho, they share whatever they have equally, under ufalme wa rais wetu wa jamhuri ambaye ana madaraka ya ajabu sana, that is a problem,

  I mean kuimba maneno ya kushujaa ni one thing na realities za siasa bongo ni absolutely another story, unahitaji kuwa na hela nyingi sana kumeguka, walionazo sasa hivi huko ndani ya CCM wote wana tuhuma za uhalifu, wanakingiwa kifua na nguvu za ajabu kutokwenda kwenye sheria, na rais wetu ambaye ni mwenyekiti wa CCM.

  Dhana ya kumeguka kwa CCM haiwezi kuwa a political strategy ya kutuokoa wananchi, ni mabadiliko ya katiba peke yake ndiyo yanayoweza kutuokoa Tanzania, then ndio CCM inaweza kumeguka lakini as long as mwenyekiti wa CCM ana power aliyonayo sasa, ninasema kwamba haitakuja kutokea under our watch, yaani kumeguka kwa CCM na tukizidi kuulilia wanaweza kuutengeneza huko mmeguko.

  Wananchi wengi wanakuja hapa JF kutafuta hope, sasa tukianza kuwaambia kuwa the last hope tuliyonayo ni kumeguka kwa CCM, maana yake tunawaambia nini masikini hawa wananchi?
   
 12. Shadow

  Shadow JF-Expert Member

  #12
  Nov 13, 2008
  Joined: May 19, 2008
  Messages: 2,908
  Likes Received: 71
  Trophy Points: 145
  Unajua ukiangalia constitution making Tanzania unaweza kulia. Katiba ya sasa ni ya CCM na ilipitishwa na Kamati kuu ....soma hotuba ya waziri mkuu wa wakati huo Nd. E.M. Sokoine. Kwa hiyo katiba si ya wananchi bali ni ya CCM na inalinda mpaka sasa hivi maslahi ya CCM. Na namashaka hata kama chama kingine kikiingia na kuonja utamu wa hiyo katiba kama wataweza kuanza mchakato wa kuibadili( angalia mifano mingi tu Africa tukianza na jirani Kenya)

  Viongozi kama sokoine ni wachache .. wanasiasa wa bongo wengi 'wajanja wajanja' na hawako katika kuleta mabadiliko ya kweli.

  Tanzania inahitaji vuguvugu la kweli na damu kama ya hayati Sokoine...wengi walipo ni blah blah
   
 13. Mag3

  Mag3 JF-Expert Member

  #13
  Nov 13, 2008
  Joined: May 31, 2008
  Messages: 9,094
  Likes Received: 6,188
  Trophy Points: 280
  Kusema kweli kisiki kilichoziba njia kuelekea kupatikana kwa katiba mpya ni CCM na ili tufikie huko tunakokwenda ni lazima kisiki hiki king'olewe. Hata hivyo wakati nakubaliana na Mwanakijiji kuwa CCM lazima imeguke kwanza, natofautiana naye kwa namna ya hilo kuwezekana. Tukisubiri imeguka yenyewe, kitu ambacho sina uhakika nacho, hatutakuwa tumesafisha njia na si ajabu atakayebaki madarakani akaleta zengwe kubwa zaidi. Lakini kama ikilazimishwa kumeguka, kitu ambacho nakubaliana nacho moja kwa moja, hawatapata muda wa kutosha wa kujipanga.

  Kuna njia mbili za kukisambaratisha kigenge hiki. Kwanza ni kwa kuwaandama bila kuchoka na bila kuwaonea haya hasa pale wanapoharibu. Kuwapigia kelele wezi, wala rushwa, wahujumu uchumi, mafisadi n.k. bila kurudi nyuma kila dakika, kila saa na kila siku. Kwa njia hii tunakata mizizi ya kisiki na lazima kuna siku wachache wao kama wamo hawatakubali kukaa kimya na tutakuta mnara wa Babeli ukianguka peke yake. Hata aliye na roho ya paka ataanza kukosa usingizi kwa nguvu na wingi wa sauti za wazalendo.

  Njia ya pili ni kwa kuwaeleza wananchi ubovu wa hii katiba unaowawezesha wachache kuitafuna nchi bila woga wa kuchukuliwa hatua. Nawapongeza Chadema kwa operation sangara lakini katika harakati zao za kujitangaza wakipe umuhimu kilio cha mabadiliko ya katiba. Huko vijijini watanzania hawaijui katiba, wanajua tu fulana na kofia za CCM - waelezeni ubovu wa katiba tuliyo nayo na nani ni kisiki kinachokwamisha katiba mpya.

  Ni afadhali mara mia kuwa na mtu dikteta kuliko kuwa na chama dikteta. Chama dikteta huwa ni kimbilio la watu wenye hulka sawa na hujenga taswira ya kuhodhi malmaka na kulindana na kwa sababu hii huweza kumeza mihimili mingine ya dola kama mahakama na bunge. Historia inatufundisha vita dhidi yake ilivyo ngumu na mara nyingi mwarobaini yake huwa ni mapinduzi ambayo matokeo yake ni umwagaji wa damu - tuiombee nchi yetu isifikie hapo.
   
 14. Z

  ZeMarcopolo JF-Expert Member

  #14
  Nov 13, 2008
  Joined: May 11, 2008
  Messages: 13,589
  Likes Received: 480
  Trophy Points: 180
  Mnataka CCM imeguke mara ngapi? au eleezeeni asilimia ya kumeguka mnayoitaka ili mridhike kuwa imemeguka. Je kuondoka kwa Mrema, Seif Sharif Hamad, Lipumba, Mbowe, Cheyo, Mbatia , Kitila Mkumbo na wengine toka CCM sio kumeguka??? kama kumeguka huko hakujazaa matunda yanayozungumziwa na mwandishi wa thread hii, je ni kumeguka gani tena kwingine anakokuzungumzia. Tatizo sio CCM, CCM kama chama cha siasa is doing the very right thing. Kama kuna tatizo baso tatizo hilo ni kwa vyama vya upinzani. Ukisema CCM ijitoe yenyewe madarakani, indirectly unasema kuwa vyama vya upinzani vimeshindwa kuwaconvince watanzania kuwa vina uwezo wa kusimamia utawala wa nchi. Hivyo basi kitendo cha CCM kujimegua kwa makusudi kitakuwa ni usaliti kwa watanzania ambao mpaka sasa wamedhihirisha kuiamini CCM zaidi ya vyama vyote vingine vilivyopo.
   
 15. Nemesis

  Nemesis JF-Expert Member

  #15
  Nov 13, 2008
  Joined: Feb 13, 2008
  Messages: 3,841
  Likes Received: 1,101
  Trophy Points: 280
  mama umenivunja mbavu duu! Shibuna awe chairman wa CCM b tehe tehe tena katibu Lowasa aisee!. Shibuda siyo fisadi ila amejiweka kama kituko ndani ya CCM hivyo hawawezi kumpa nafasi hiyo. Lowasa ni fisadi hivyo hawawezi kukaa meza moja na Shibuda. Lowasa anajua kwamba Shibuda hata laza hata neno moja, mipango yote ya ufisadi itawekwa wazi. Zaidi ya haya Shibuda haaminiki ndani ya CCM.

  Pia Shibuda hajawahi kufanikiwa mipango yake ya kuwa kiongozi wajuu katika CCM, hata nafasi yake ya ubunge sioni kitu kikubwa anachokifanya. Hiyo CCM b ikitaka kufanikiwa inatakiwa iwe na madume kama Nape au Mwikabwe waliogoma kumpikia chai Nchimbi.
   
 16. Madela Wa- Madilu

  Madela Wa- Madilu JF-Expert Member

  #16
  Nov 14, 2008
  Joined: Mar 24, 2007
  Messages: 3,074
  Likes Received: 35
  Trophy Points: 135
  Katiba hiyo hiyo ilikuwepo wakati;
  Dr Slaa anashinda ubunge.
  Tarime manispaa inaongozwa na Chadema.
  Kabwe anashinda jimboni kwake Kigoma.
  Chadema kuibuka kidedea jimboni Tarime.
  Kisiwa cha Pemba kinachukuliwa na wawakilishi wa CUF.
  Lowasa analiwa kibano cha Nguvu kwa shinikizo liloanzia nje ya CCM.

  Hiyo katiba ni kizuizi lakini si jiwe la kutulemea, la sivyo hakuna mbunge kutoka vyama vya upinzani angetamba.
  CCM wakitanguliza Fedha na wewe ukatanguliza fedha ni lazima utaliwa mzima mzima.

  Kuapa kwamba CCM haiwezi kulala ngoma tukiwa hai, eti mpaka katiba ibadirishwe ni dalili ya kujidharau kifikra zaidi kuliko kutishika na nguvu za CCM.
  Kuna Makburu kibao waliapa Mandela kamwe hawezi toka jela akiwa hai au akiwa na jeuri yake yote mfukoni. Mandela yuko nje kifua mbele na jeuri yake yote, Wao ni Historia Mandela anadunda hata hivi niandikapo habari hizi.

  Katapila lilishindwa kuundoa ule mbuyu pale ST Peter, lakini ukimpa kazi hiyo mkata kuni yeyote yule bandu bandu ya shoka siku saba nyingi,mbuyu ule utakuwa historia kama historia nyingine zote.
   
 17. Mzee Mwanakijiji

  Mzee Mwanakijiji Platinum Member

  #17
  Nov 14, 2008
  Joined: Mar 10, 2006
  Messages: 31,362
  Likes Received: 6,393
  Trophy Points: 280
  Ndio maana naamini CCM itafungwa magoli kwenye uwanja wao, sheria zao, mpira wao, na refa pia wao!!
   
 18. E

  Englisher Member

  #18
  Nov 14, 2008
  Joined: Nov 13, 2008
  Messages: 19
  Likes Received: 2
  Trophy Points: 0
  This is brilliant ideas MKJJ! Infact all innocent people in CCM we just consider them as wafisadi. If they rel mean it, that leadership is for people let them quit being CCM members.

  cheers
   
 19. Bongolander

  Bongolander JF-Expert Member

  #19
  Nov 14, 2008
  Joined: Jul 10, 2007
  Messages: 4,882
  Likes Received: 47
  Trophy Points: 135
  Kuna possibility kubwa kuwa kumeguka kwa CCM kunaweza kuwa kusambaratika kwa Tanzania. Sasa inategemea kama hilo litakuwa ni neema au laana. Bado mpaka sasa sijaona ubaya mkubwa wa katiba kama watawala wangekuwa na nia thabiti ya kuendeleza taifa. Katiba yetu imetoa means and ways kwa watawala kutumia kila kinachoweza kutumika kuliletea maendeleo taifa. Inampa Rais,Waziri,Mkuu wa Mkoa na mkuu wa wilaya nguvu zote zinazohitajika ili kuweza kufanya kazi. Kama kweli wangekuwa na nia thabiti ya kuendeleza nchi na kutumia madaraka kwa niaba ya wananchi basi nina hakika Tanzania ingekuwa mbali.
  Tatizo lililopo ni kuwa taasisi zote nyeti Tanzania kama Umoja wa wazazi na Jeshi zimekuwa zina-serve interest za CCM, na sio interest za Taifa. Interest za taifa zinachukua nafasi ya tatu. Kama issues zinagusa interest za wanaCCM wenyewe basi wanatumia vyombo vyote kulinda hizo interest. Katiba inatoa loop holes hizo. Chama chochote ambacho hakiko madarakani sasa hakitapenda katiba ya sasa lakini kikiingia madarakani hakitakubali ibadilishwe na hakitaweza kutawala bila katiba inayowafanya wao miungu watu. Bado hatujafikia hatua ya nchi kama Israel, ambapo IDF, Kidon na Mossad ni idara ambazo hazina uhusiano hata kidogo na Likud,Labour wala kadima. Tanzania ni other way round.
  Ikibadilishwa katiba ndio mwisho wa CCM, na inawezekana pia kuwa ndio mwanzo wa kusambaratika kwa Tanzania. Hayo ni maoni yangu tu yanaweza kuwa challenged.
   
 20. M

  Mkandara Verified User

  #20
  Nov 14, 2008
  Joined: Mar 3, 2006
  Messages: 15,443
  Likes Received: 132
  Trophy Points: 160
  Jamani tusiwe vipofu ktk hoja ambayo ni muhimu..Field marshall Es kasema ukweli mtupu ambao hauhitaji maelezo mengi..
  Kama CCM ni kisiki itakuwaje mtu usubiri hadi kimeguke!.. hali hiyo itatokana na kitu gani? tusubiri hali ya hewa ya ukame ama!..
  Kama alivyosema kuanzishwa kwa vyama vya Upinzani kulitokana na Ulazima uliotakiwa toka nchi za nje na CCM walijenga vyombo hivi kuuhadaa Ulimwengu.. Mrema na Seif Sharrif walitoka wakiwa na uhakika na nafasi za juu zenye posho na mshiko safi kama vile wako CCM.. tatizo lilikuja tu pale tamaa za kibinadamu zilipoingia kwa hawa jamaa. Mrema aliona upenyo wa kuweza kushinda Uchaguzi, akafanya kweli nje ya makubaliano.. Seif Pia aliona upenyo wa kuchukua Uongozi Zanzibar, CCM wakabadilisha Uwakilishi ktk serikali ya Muungano...Bahati yake ni kwamba hadi leo jhii bado ni tishio kubwa kwa CCM lakini wmeshamtafutia dawa..
  CCM haiwezi kumeguka kirahisi wakubwa zangu kwani kila mkulu alipo ndani ya CCM anakatiwa chake kisawasawa, huku nje hakuna nuru na wale wote waliojaribu kujimegua wamerudi wenyewe..
  Wee fikira tu majuzi Kikwete amekebehi UJAMAA wakati huu ndio mwongozo wa chama chake na Imani ya chama inasema - Ujamaa na kujitegemea ndiyo njia pekee ya kujenga jamii ya watu walio sawa na huru!..
  Lakini la kuchekesha viongozi wote ndani ya chama walimpigia makofi na kumshangilia wakati akikitukana chama chake mwenyewe akitumia neno Upinzani..Na ajabu kubwa ni kwamba Upinzani hawakurudisha majibu.
  Mkuu wangu kisiki hiki hakiwezi kuondoka bila zana maalum za kung'oa visiki na watu wenye moyo na imani kubwa isiyofungamana na woga wa Uchawi..
  CCM sio tu kisiki cha mkorosho, hiki ni kisiki sawa na ule mbuyu wa St. Peters, njia panda kwenda Masaki.
  Tumejenga barabara kuuzunguka, measure zetu ni kutazama kama uwezekano wa usafiri bado unawezekana bila kukiondoa kisiki hicho..
   
Loading...