Elections 2010 CCM kukaangana wiki ijayo .............

Rutashubanyuma

JF-Expert Member
Sep 24, 2010
214,789
2,000
CCM kukaangana wiki ijayo
Saturday, 04 December 2010 22:39


juzi alikaririwa na gazeti la Mwananchi Jumapili akisema kwamba ndani ya chama hicho hali ni shwari na kwamba hakuna mabadiliko ya uongozi ambayo yanaweza kutokea, lakini ukweli mambo bado yanatokota.

Hatua hiyo ya wanachama kutaka kumbanana inatokana na kuwatuhumu watendaji wa ofisi ya makao makuu kuvuruga mchakato wa umeya katika baadhi ya maeneo yanayohusishwa na vitendo vya rushwa kama ilivyotamgazwa na baadhi ya vyombo vya habari wiki hii.

Jana Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM John Chiligati alisema pamoja na mambo mengine Kamati Kuuya chama itayokutana Ijumaa ijayo, itapitia mapendekezo ya kamati ya maadili na kupitisha rasmi majina ya watakaogombea umeya.
"Kamati Kuu itakayokutana Desemba 10, mwaka huu itapokea mapendekezo ya kamati ya maadili na kisha kupitisha rasmi majina ya wagombea umeya wa CCM," alisema Chiligati.
Katibu mwenezi huyo alisema kwa mujibu wa kanuni na taratibu za chama hicho, kwa kiasi kikubwa CC hufikia maamuzi kulingana na mapendekezo yanayotolewa na kamati ya maadili na kwamba, kamati hiyo tayari imekwisha pokea malalamiko mengi ikiwemo ya wanaotuhumiwa kufanya vitendo rushwa katika mchakato wa umeya.
"Kamati Kuu ndiyo yenye mamlaka ya kuwahoji wote waliotuhimiwa na kisha inatoa mapendekezo yake kulingana na hali halisi ilivyokuwa," alisema Chiligati
Alisema kamati hiyo itakutana kwa siku moja jijini Dar es Salaam na kwamba itajadili ajenda nyingine ambazo hakuwa tayari kuzitaja.
Habari kutoka miongoni mwa wajumbe Kamati Kuu zilisema watendaji na wanachama wengi wa CCM imani yao kwa ofisi ya makao makuu imepungua na sasa wameamua kuwasiliana moja kwa moja na Mwenyekiti wa CCM Taifa, Rais Jakaya Kikwete kueleza tuhuma za rafu zinazofanywa katika mbio za umeya.
Mwananchi Jumapili ilielezwa kuwa kutokana na kuboronga katika Uchaguzi Mkuu uliopita na imani ya wanachama na wanaowania nafasi mbalimbali kupungua kwa sekretarieti ya chama ni moja ya mambo yatakayojadiliwa katika kikao hicho.
Baadhi ya tuhuma ambazo zimeelekezwa kwa baadhi ya watendaji wa chama makao makuu ya chama ni kushiriki kuwabeba baadhi ya wana-CCM ambao wanawania umeya katika Halmashauri za Manispaa za Dar es Salaam ambako tayari wanaotakiwa kupewa nafasi hizo wamejulikana, lakini wanatuhumiwa kutoa fedha ili kufanikisha azma hiyo.
Chanzo chetu cha habari kilisema katika Manispaa ya Kinondoni, mmoja wa wagombea hao, (jina tumelihifadhi) anadaiwa kutoa fedha kwa viongozi wa ngazi mbalimbali ili apewe upendeleo katika kuwania nafasi hiyo na tayari ameanza kupanga safu za viongozi kwa kugawa uongozi wa kamati mbalimbali atakapochaguliwa ikiwa ni fadhila iwapo watampitisha.
Ilibainika kuwa mwezi uliopita kigogo huyo aliitisha mkutano wa madiwani wa CCM kwenye hoteli (jina tunalo) iliyopo Magomeni ambapo muda mwingi ulitumika kumsifia na kumpigia debe na baadaye aliwagawa sh 300,000 kwa kila diwani na chakula cha mchana. (Orodha ya madiwani tunayo).
Habari zaidi zilisema mbali ya fedha hizo, kigogo huyo anadaiwa kwenda Dodoma na kutoa fedha kwa kiongozi mmoja wa mwandamizi wa chama kwa lengo la kutaka amlinde na kumpa upendeleo kwenye kinyanganyiro hicho.
Kwa upande wa Temeke, mmoja wa wagombea anadaiwa kutoa fedha kwa viongozi kuanzia ngazi ya wilaya hadi taifa ili waweze kusaidia kufanikisha azma yake hiyo.
Hata hivyo, washindani wake wamemlalamikia na tayari wameandika barua kwa Mwenyekiti wa CCM Taifa, Rais Kikwete.
Hali ni hivyo hivyo kwenye Manispaa ya Ilala ambako mmoja wa madiwani aliyepita kwa shida huku akilalamikiwa na wananchi wengi kiasi cha baadhi kurudisha kadi za chama, ameandaliwa kushinda.
Kwa nafasi ya Meya jiji la Dar es Salaam ambako mmoja wa watu wanaowania nafasi hiyo (jina tunalo) anadaiwa kugharamia tafrija ya mmoja wa mawaziri baada ya kuteuliwa hivi karibuni ili kuweka mazingira ya kuteuliwa kuwania nafasi hiyo ya juu jijini.
Waziri huyo (jina tunalo) aliangusha tafrija kubwa baada ya kuteuliwa kwa mara nyingine kuingia katika baraza jipya la mawaziri.
Mbali ya sakata la umeya kuitesa CCM pia hata uteuzi wa viti maalumu vya udiwani bado malalamiko yanazidi kuongezeka katika maeneo mbalimbali nchini.
Naye Habel Chidawali anaripoti kutoka Dodoma kuwa; Viongozi wa CCCM wilaya ya Mpwapwa wanatarajia kufikishwa mahakamani wakati wowote kujibu tuhuma za kuvuruga matokeo ya kura za udiwani wa viti maalumu.
Hilo limetokana na chama hicho kupitisha jina la mtu aliyeshika nafasi ya tatu katika matokeo hayo kwa kile kilichoelezwa kuwa ni kiongozi wa Umoja wa Wanawake wa chama hicho (UWT) ngazi ya wilaya.
Majina ya madiwani wa Viti Maalumu yalirudishwa mwishoni mwa wiki baada ya kusubiriwa kwa muda mrefu kutoka Tume ya Taifa ya Uchaguzi na kwamba wanatarajia kuapishwa wakati wowote pamoja na madiwani wa kata.
Rehema Zahai ambaye alikatwa jina lake na kurudishwa jina la Katibu wa UWT wa wilaya ya Mpwapwa alisema kuwa yuko tayari kwenda mahakamani ili kutafuta haki yake kama imeshindikana kupatikana kupitia vikao vya chama.
"Ni kweli mimi nimekatwa jina langu bila hata ya sababu zozote na limerudishwa jina la mtu wa tatu kitu ambacho najiuliza kuwa mimi ninakosa hata huyu wa pili naye anakosa, haiwezekani kuna mchezo umechezwa, lazima nipiganie haki yangu maana najua kilichofanyika," alisema Zahai.
Habari ambazo Mwananchi Jumapili imezipata na kuthibitishwa na viongozi wa CCM ngazi ya wilaya zimeeleza kuwa katika kura za udiwani wa viti maalumu Tarafa ya Mpwapwa, Rehema alipata kura (196) akifuatiwa na Josephine Chilolose (132) huku Katibu wa UWT wilaya ya Mpwapwa Christina Mbeleselo akipata kura 12 lakini jila lake ndilo lililoteuliwa.
Katibu wa UWT Wilaya ya Mpwapwa ambaye pia ni Diwani mteule, Christina Mbeleselo alisema wanaopaswa kuulizwa kuhusiana na kukatwa jina hilo ni jumuiya hiyo ngazi ya Mkoa.
"Ni kweli mimi nilishika nafasi ya tatu na Zahai aliongoza katika kura, lakini nasema kuwa hayo yote mimi sikuyafanya ila akaulize mkoani ambako majina yanapangwa kwa alfabeti inawezekana ndiyo maana hakuteuliwa, lakini kweli aliongoza tena kwa kura nyingi tu," alisema Mbeleselo.
Mwenyekiti wa UWT Mkoa wa Dodoma Fatuma Tawfiq hakuwa tayari kulizungumzia sakata hilo hata alipotumiwa ujumbe mfupi kwa njia ya simu alijibu kuwa yuko kwenye kikao.
"Ni kweli nilikuwa nakata simu yako kila ulipopiga kwani tangu wakati huo mimi niko kwenye kikao na bado tunaendelea," ilisomekana sehemu ya ujumbe mfupi aliotuma kwa Mwandishi.
Katibu wa CCM Mkoa wa Dodoma, John Balongo aling'aka na kusema kuwa lazima aliyeongoza ndiyo ateuliwe, haiwezekani mtu kuongoza halafu anaachwa na anateuliwa mtu mwingine.
"Mimi niko Dar es Salaam narudi kesho (leo) lakini mwambieni huyo mama sikuwa na taarifa hizo, najua waliochanganya madiwani UWT mkoa na hilo limetuvuruga sana lazima tutengue uteuzi huo," alisema Balongo.
 

Toa taarifa ya maudhui yasiyofaa!

Kuna taarifa umeiona humu JamiiForums na haifai kubaki mtandaoni?
Fanya hivi...

Umesahau Password au akaunti yako?

Unapata ugumu kuikumbuka akaunti yako? Unakwama kuanzisha akaunti?
Contact us

Top Bottom