CCM Inakabiliwa na Changamoto ya Kukosa Viongozi Wawili... Litaathiri Utendaji wa Samia?

Mzee Mwanakijiji

Platinum Member
Mar 10, 2006
33,475
39,988
Na. M. M. Mwanakijiji

Pamoja na kuwa Taifa limepoteza Rais wake kufuatia kifo cha Rais John Pombe Magufuli Chama cha Mapinduzi kinakabiliwa na changamoto ambayo kama chama hakijawahi kuipitia. Kwa mara ya kwanza Chama cha Mapinduzi hakina Mwenyekiti wake na hakina Katibu Mkuu wake. Ikumbukwe kuwa aliyekuwa Katibu Mkuu Dk. Ally Bashiru aliteuliwa na Rais Magufuli wiki chache nyuma kuwa Katibu Mkuu kiongozi kufuatia kifo cha Balozi John Kijazi. Na wiki si nyingi Mwenyekiti wa CCM ambaye ni Rais alifariki dunia na hivyo kufanya Chama cha Mapinduzi kikose viongozi wawili muhimu sana ambao wanahitajika katika utendaji wa chama.

Ikumbukwe kuwa chini ya Ibara 115 ya Katiba ya CCM Katibu Mkuu pamoja na majukumu mengine ana kazi zifuatazo:
(2) Atakuwa Katibu wa Mkutano Mkuu wa CCM wa Taifa, Halmashauri Kuu ya CCM ya Taifa, na Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya CCM ya Taifa.
(3) Atakuwa ndiye Mtendaji Mkuu wa CCM na atafanya kazi chini ya uongozi wa Halmashauri Kuu ya CCM ya Taifa.
(4) Atakuwa na wajibu wa kuitisha Mikutano yote ya Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya CCM ya Taifa, Halmashauri Kuu ya CCM ya Taifa na Mkutano Mkuu wa CCM wa Taifa. (5) Ataitisha na kuongoza vikao vya Sekretarieti ya Halmashauri Kuu ya CCM ya Taifa kwa madhumuni ya kushauriana, kuandaa agenda za Kamati Kuu, na kuchukua hatua za utekelezaji wa maamuzi ya CCM.
(6)Atakuwa ndiye Mkurugenzi wa Uchaguzi wa Chama nchini

Hivyo kifungu kidogo (4) kinahusika kwani ndiye anatakiwa kuitisha vikao mbalimbali. Lakini pia kazi zake nyingine kuendelea katika kifungu kidogo cha (7) cha Ibara hiyo hiyo ni kuwa:
(7) Kazi na majukumu ya Katibu Mkuu wa CCM:-
(a) Kuratibu kazi zote za Chama Cha Mapinduzi.
(b) Kusimamia kazi za Utawala na Uendeshaji katika Chama.
(c) Kufuatilia na kuratibu masuala ya Usalama na Maadili katika Chama.
(d) Kusimamia Udhibiti wa Fedha na Mali za Chama.

Lakini pia inaweza kutolewa hoja kuwa wapo Manaibu Katibu Wakuu (wa Bara na Visiwani). Hata hivyo Katiba ya CCM - kwa maoni yangu - haijatoa nafasi ya kukaimisha madara yote ya Katibu Mkuu kwa Manaibu wake kwani hata wao wanaweza kupangiwa au kupewa majukumu mengine na Katibu Mkuu. Hivyo, ni wazi ipo haja kubwa ya kupatikana kwa Katibu Mkuu.

Lakini zaidi ni wazi kuna haja ya kuwa na Mwenyekiti. Hii ni mara ya kwanza kwa CCM kutokuwa na Mwenyekiti wake. Japo kwenye Urais wa nchi Katiba ya nchi imeweka utaratibu unaotakiwa kufuata kumpata anayemrithi ikitokea kwamba Rais hayupo tena madarakani lakini kwenye CCM utaratibu wake hauko wazi sana. Mara zote huko nyuma toka Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere CCM imekabidhiana Uenyekiti kutoka mmoja kwenda mwingine na hata ilipotokea Mwenyekiti hakuwa Rais kwa wakati mmoja utaratibu uliwekwa wazi kuwa ni utamaduni wa CCM kuwa Rais anayetokana na chama chao ndio pia atakuwa Mwenyekiti wa CCM. Hii ndio sababu ya Nyerere kuamua kumwachia Mwinyi na hata baadaye Jakaya kumwachia Magufuli.

Lakini kwa vile nafasi hii iko wazi kwa sababu Mwenyekiti wa CCM Taifa amefariki basi ni wazi kuwa haja ya kuitisha vikao na taratibu zifuatwe. Bahati Mbaya Katibu Mkuu naye hayupo! Ikumbukwe kuwa Mwenyekiti wa CCM anachaguliwa na Mkutano Mkuu wa CCM na kwa vile nafasi iko wazi kwa sababu ya kifo ni wazi Mkutano Mkuu Maalum (usio wa kawaida utaitishwa). Hii ndio sababu labda ya Manaibu Wenyekiti wa CCM - Bara na Visiwani kukutana japo sijui ni kwa kiasi gani maamuzi yao yanafuata katiba hasa ukiondoa ukweli kuwa hakuna Katibu Mkuu ambaye ndiye mtendaji mkuu. Ni wazi kati ya mambo mengine CCM watatakiwa wakae chini waangalie mapungufu ya Katiba yao kwa sababu wanaweza kujikuta wanaliingiza taifa katika mgogoro wa kisiasa usio wa lazima hasa endapo Rais Samia Suluhu Hassan hatopewa Uenyekiti wa CCM mapema zaidi iwezekanavyo.

Kwa maoni yangu Mkutano Mkuu Maalum wa CCM unatakiwa uitishwe mapema zaidi. Japo mkutano wa kawaida unatakiwa utolewa taarifa si chini ya miezi mitatu kabla ya mkutano huo; mkutano "maalum" unaweza kuitishwa mapema zaidi na ninaamini hili ndilo litakalofuata. Ni muhimu na muhimu sana kuwa Mama Samia Suluhu Hassan apewe Uenyekiti wa CCM haraka iwezekanavyo kwani kuacha nafasi hii iwe na ombwe ni kusababisha mianya ya kisiasa isiyo ya lazima. Hii ni muhimu ili pia apate nafasi ya kupendekeza jina la Katibu Mkuu wa CCM ambaye atakuwa ataingia na kuziba pengo la Dkt. Bashiru. Sijui kama Bashiru angependa kurudi alikotoka (kuwa Katibu Mkuu) au Rais ataona anamfaa kama Katibu Mkuu Kiongozi. Hili tutasubiria tulione.
 
Sidhani kama ni sahihi kusema hakuna Katibu Mkuu, Bashiru bado ni KM wa CCM hadi pale atakapochaguliwa mwingine vivyo hivyo Polepole ni katibu mwenezi CCM hadi pale atakapochaguliwa mwingine.
 
Back
Top Bottom