CCM ilijibwetesha kwa wenye fedha, Rais na serikali waje kiubunifu zaidi

Phillipo Bukililo

JF-Expert Member
Dec 29, 2015
18,487
13,612
Marehemu Mwalimu Nyerere hakupenda kuona rundo la wafanyabiashara wakijitokeza kwenye mikutano ya CCM, miaka ile wakati ameng'atuka, huku mara moja moja akiitwa kushiriki mikutano hiyo.

Ilimkera sana kuona kuwa chama ambacho alishiriki kwa nguvu nyingi katika kuhakikisha kinavaa sura ya utaifa na kinajitegemea licha ya hali ya maisha kubadilika kila kukicha, kinageuka tegemezi kwa watu ambao utajiri wao umejaa chembe chembe za kutokuwepo na uaminifu.

Azimio la Zanzibar la mwaka 1992 halikuja na madhara ya kuua moyo wa ujamaa uliokuwepo ndani ya nafsi za baadhi ya watanzania peke yake, bali ikajengekea tabia ya wafanyabiashara kuabudiwa. Nyakati hizo ndipo Yanga na Simba zikaanza kuwakubali wafadhili, ambao hawakusita kuwaahidi wachezaji magari na nyumba iwapo timu zingeweza kutwaa kombe fulani.

Kuanzia hapo muelekeo ukaanza kupotea. Tajiri mwenye fedha akawa mtu muhimu na ndani ya siasa za ndani za CCM, hata kama fedha yake ina uhusiano na hali ya kuwa haramu. CCM ikakubali kujibwetesha kwa wenye fedha, na wao wakautumia vizuri udhaifu huo. CCM ikageuka kichaka kibaya sana kilichojaa wafanyabiashara wanaojua viilivyo namna ya kutumia fursa iliyojitokeza kwao.

Leo hii Rais John Magufuli na serikali yake wanajaribu kujivua utando mkubwa sana wa wenye fedha, ambao kwa takriban miaka ya 24 wamekuwa na jukumu fulani la kukibeba chama.

Hii ni vita ambayo ushindi wake utaweza kupatikana ikiwa asilimia kubwa ya wanaCCM na wananchi kwa ujumla watakubali kuwa kujitegemea ni kitu kinachowezekana, bila hata ya mwenye fedha kugongewa mlango wa nyumba yake ili aweze kuombwa kufadhili mikutano ya chama.

Waliozoea kumfuata tajiri fulani, wanakumbushwa kwamba kujibwetesha kwa nia ya kupata fedha kunaambatana na kuuza utu pamoja na rasilimali za nchi. Hakuna kitu fulani cha kipekee walichonacho hao matajiri walioutengeneza utajiri wao kwa mgongo wa huruma ya chama kikubwa cha siasa.

Hakuna maana ya nchi kutumia fedha nyingi sana katika kusomesha watanzania wengi halafu vyama vya siasa vikabakia kuwa tegemezi kwa nguvu ya fedha ya wachache. Mbadala wa utegemeaji wa fedha za wachache upo, na chama cha siasa haswa CCM watakuwa wamejivua utando wa utumwa na kubakia huru. Jambo ambalo lilimfanya JKN akawa mnyonge baada ya kung'atuka CCM.
 
Asante! Asante! Ujumbe umesheheni yote ambayo pengine ningependa kusema laiti ningekuwa na uwezo wako wa kuchambua. Turudi zama za nzige, walisema kwetu. Tujifunze.
 
Back
Top Bottom