CCM huwabadili watakatifu kuwa waovu?

Sababu kuu ya kuipenda JF huwa wana archive posts vizuri kwa reference baadaye. Daaah, safi sana hatimaye mbwa karudia matapishi yake. Huyu huyu Mkumbo alikuwa anatushawishi kipindi tuko wanafunzi UDSM kujiunga na Chadema, leo hii ndo kwishnei.
Mbwa kala mbwa
 
Nimecheka sana, nikasikitika sana. Hii tabia ya kufukua makaburi muache.

Hivi boss wangu Kitila anaweza kupitia uzi huu??

Thanks kwamba JF sio Instagram kwamba unaweza futa sredi zako za Zamani. Ona aibu hii kwa boss wangu.
Hivi haiwezekani kufuta Uzi uliouanzisha? Jamiiforums hapo ndio walipotukomesha.Safi sana Jf
 
Hii theory ikiwa ni ya kweli maanake ni kwamba hata hao wasomi tatizo ni hilohilo mara walipojitumbukiza ndani ya CCM wakaenda na maji, wakapenda uovu, wakautukuza na kuusifu! Mwisho wa siku walionekana watu wa ajabu mbele ya jamii! Mifano ipo tele na kedekede!
Aisee! Hii point Uliyo itoa miaka kadhaa iliyo pita, inakuhusu kabisa hivi leo
 
Sasa nimekubaliana na Ruge......vitu vya kuogopa kwa binadamu ni technology na Mungu. Maandiko huishi. Hebu Propesa wangu Kitila apitie tena hili bandiko lake! Duhhh...
 
Nimekuwa nikiisoma barua ya Butiku, now and then, natafakari mshangao wake kumuona Mkapa alivyobadili baada ya kuukwaa urais. Mshangao wake unaibua maswali mengi ikiwa pamoja na: i) kwamba ina maana huyu bwana pamoja na kuwa karibu na Mkapa ni kweli kwamba hakumjua Mkapa kwa kiasi hicho? au ii) tuseme ni kweli kwamba Mkapa alibadilika baada ya kuingia madarakani kama Rais? iii) na kama hivi ndivyo, kwamba alibadilika, ni kitu gani kilimbadili Mkapa kiasi hicho? iv) Je, kuna wengi tuliokuwa tunawona kuwa ni wazuri lakini ghafla wakabadili baada ya kupata madaraka ya CCM? v) Kingunge na Warioba wanaweza kuwa ni mifano mingine jinisi CCM ilivyowabadili kutoka kuttetea utakatifu hadi kupenda uovu?

Baadhi ya maswali haya yanajibiwa katika makala niliyoandika hivi karibuni na kuchapwa katika gazeti la Tanzania Daima mwanzoni mwa Mwezi huu. Kwa maoni yangu ni kwamba ni vigumu kupambana na madhira katika nchi ile kupitia CCM. Hiki si chombo salala tena cha kusafisha uchafu bali ni agency wa uchafu. Kwa hiyo hatua ya kwanza ya mtu yeyote anayetaka kupambana na matatizo ya nchi yetu ile kwa kupitia siasa ni kuchagua njia ingine mbali na CCM. Butiku naye kwa kuendelea kupiga kelele huku akiendelea kubaki hukohuko anaweza akakuta naye anajichafua. Endelea kusoma na toa maoni yako pia.
________________________________________________________
Jinsi CCM ilivyowabadili watakatifu kuwa waovu

Kitila Mkumbo


NI hivi punde tu nimehitimisha kusoma kitabu kipya kiitwacho “The Lucifer effect: How good people turn evil” kilichoandikiwa na mmoja wa magwiji wa saikolojia ya jamii, Profesa Phillip Zimbardo.
Kwa tafsiri isiyo rasmi tunaweza kutafsiri kitabu hiki kama ‘Athari za Lucifer: Jinsi watu watakatifu wanavyobadilika kuwa waovu’.

Katika kitabu hiki, Profesa Zimbardo kwa kutumia matokeo ya tafiti alizofanya kwa zaidi ya miaka 15, anaeleza jinsi ambavyo mazingira maovu yanavyoweza kumbadilisha mtu aliyekuwa mtakatifu na kuwa mwovu kwa kiwango cha kutisha. Profesa Zimbardo anabainisha mambo matatu kuhusu utakatifu na ushetani.

Kwanza, anabainisha kuwa dunia wakati wote ina watu wa aina mbili - yaani watu walio watakatifu na waovu. Pili, ukuta kati ya utakatifu na uovu unapenyeka. Tatu, inawezekana kwa malaika kuwa shetani, na mashetani kuwa malaika!
Kwa mujibu wa Profesa Zimbardo, dawa ya kupambana na uovu katika jamii, si kupambana na waovu, bali kupambana na mazingira yanayosababisha watu wafanye uovu. Ndiyo kusema kuwa hata kama mtu atakuwa mtakatifu namna gani kuna uwezekano mkubwa wa mtu huyo kuchafuka kama atawekwa katika mazingira machafu.

Profesa Zimbardo anahitimisha kitabu chake kwa kutoa tahadhari kuwa ili kuyashinda mazingira ya uovu katika jamii, kunahitajika wajitokeza watu jasiri (heroes). Hata hivyo Profesa Zimbardo anakiri kuwa katika jamii mara nyingi watu jasiri ni wachache mno na nguvu zao huonekana tu pale ambapo jamii huwaunga mkono katika jitihada zao za kupambana na mfumo unaojenga na kulinda watenda maovu. Bila jamii kuwaunga mkono watu jasiri, juhudi za watu hawa huonekana kama za kujikweza na zisizokuwa na manufaa yoyote katika jamii.

Kwa bahati mbaya au nzuri nimemaliza kusoma kitabu hiki katika kipindi ambacho nchi yetu ipo katika mkanganyiko mkubwa kuhusu usafi na uadilifu wa viongozi wetu tuliowakabidhi mamlaka na madaraka ya kuongoza nchi. Nimehusisha maudhui ya kitabu hiki na tuhuma nzito za ufisadi zilizotolewa na viongozi wa upinzani dhidi ya viongozi kadhaa wa serikali. Nimehusisha pia maudhui ya kitabu hiki na juhudi za baadhi ya watu wanaoheshimika katika jamii yetu za kujaribu kuwasafisha waliotuhumiwa na kuwabeza wale wanaoibua tuhuma za ufisadi.

Nitawatolea mifano watu wawili ambao ni Kingunge Ngombale-Mwiru na Jaji Joseph Sinde Warioba, ambao wote kwa muda mrefu wamejijengea heshima kubwa katika jamii yetu.

Mzee Kingunge alikuwa mtu wa kwanza kujitokeza katika kujaribu kuwasafisha viongozi waliotuhumiwa kuhusika na ubadhirifu wa mabilioni ya pesa kwa kutumia nafasi za uongozi tulizowakabidhi.

Majibu ya Kingunge yalikuwa rahisi kabisa; kwamba tuhuma za wapinzani hazikuwa na ukweli wowote, bali “jitihada ya kutaka serikali iondoke kwenye mstari wa kushughukia maendeleo ya wananchi, ihangaike na tuhuma za hewani.” (Mwananchi, Septemba 19, 2007, uk. 2). Mzee Kingunge alikwenda mbali zaidi kwa kusema: “Nongwa iliyopo ni kuona maendeleo yanakua kwa kasi. Angalia shule tunazijenga kwa kasi na sasa tunageukia kwenye zahanati, sisi kwetu haya ni maendeleo na dunia inaona na kutusifu, lakini kwa wenzetu hawa ni nongwa” (HabariLeo, Septemba 19, 2007, uk.2).

Hili la kwamba maendeleo yanakua kwa kasi na kwamba wapinzani wanaona nongwa linahitaji makala nyingine. Lakini inatosha tu kusema kuwa inawezekana Kingunge na viongozi wenzake wanaishi dunia nyingine.

Kama kweli serikali ya leo inaleta maendeleo makubwa kama anavyodai Kingunge, wananchi wasingewazomea mawaziri katika mikutano ya hadhara na Waziri Mkuu asingeitikiwa na wananchi kwa kusema “ovyo” aliposema pale alipotarajia aitikiwe “oyee” katika ziara zake huko mikoani.

Bahati mbaya kwake Kingunge alitoa kauli zake hizi kabla hata hajasoma kwa kina tuhuma zilizotolewa na wapinzani kama alivyokiri mwenyewe pale aliposema “tunangoja tupate nyaraka zao tutajibu tuhuma zote”. (Mwananchi, Septemba 19, 2007, uk. 2).

Kwa hiyo kimsingi Kingunge aliamua kuzungumzia jambo asilolijua na kusahau usemi maarufu wa Rais mstaafu Mzee Mkapa, ambaye Kingunge alikuwa mshauri wake mkuu, ya kwamba huna haki ya kulizungumzia jambo ambalo hujalifanyia utafiti. Kibaya zaidi, jambo alilokuwa analizungumzia ni kutetea tuhuma zinazohusu uchafu.

Kitu ambacho Kingunge hakukijua ni kuwa kwa kutetea uchafu naye alikuwa anajichafua na kubadili milele nafasi yake katika jamii kutoka kuwa mtu anayeheshimika kwenda kuwa kitu kingine kabisa ambacho bila shaka sasa anakijua!

Pengine aliyeiweka nafasi yake ya kijamii katika utata mkubwa zaidi ni Jaji Joseph Sinde Warioba. Mzee Warioba naye amejikuta akijaribu kuwasafisha waliotuhumiwa kwa kauli za kujichanganya.

Warioba alikaririwa na magazeti ya tarehe Septemba 28, 2007 akitoa kauli zilizolenga bila mafanikio kuwasafisha viongozi wa serikali wanaotuhumiwa kushiriki katika ubadhirifu.

Katika mkutano wake na waandishi wa habari, Warioba alizungumzia mambo mawili makubwa. Kwanza aliwataka viongozi wa kisiasa (nafikiri aliwalenga zaidi wale wa upinzani) kujadili matatizo ya wananchi na kwamba viongozi wa sasa wamekuwa mstari wa mbele kuzungumzia masuala ambayo hayamsaidii mwananchi kujikwamua na umaskini.

Kwa maneno mengine, anachotwambia Warioba ni kuwa ufisadi na rushwa si matatizo ya wananchi yanayokwamisha juhudi zao za kujikwamua na umaskini.

Hii ni kauli ya ajabu na inatosha tu kusema kuwa ni ya ajabu bila kutoa maelezo yoyote kwa sababu naamini hata yeye Warioba aliporudi nyumbani na kuisoma kauli yake kesho yake atakuwa alijilaumu na hakuamini macho yake kwamba aliitoa yeye!

Ajabu nyingine katika kauli ya Warioba ni pale alipojaribu kuonyesha kuwa tuhuma za ufisadi zilizoibuliwa na wapinzani hazina maana kwa kuwa tu si mpya.

Hii pia ni hoja dhaifu kwa sababu tatizo haliwezi kuacha kuwa tatizo kwa sababu tu eti si jipya. Tatizo linakwisha kwa kutatuliwa na sio kwa kuwa kuukuu. Kauli ya pili ya Warioba iliyopewa uzito katika magazeti ni ile iliyohusu kumhusisha Rais wa nchi na tuhuma za ubadhirifu. Warioba aliwataka viongozi wa upinzani waache kumkejeli Rais anayebeba nembo ya taifa letu. Nami nakubaliana na Warioba kuwa si jambo linalopendeza kuona Rais anakejeliwa.

Hata hivyo, nitumie nafasi hii kumuweka sawa Warioba kuwa suala hapa si kuacha kumkejeli Rais na viongozi wengine wa serikali, bali ni hao viongozi wakiongozwa na Rais anayebeba nembo ya taifa letu kuacha kujiweka katika hali ya kukejeliwa. Labda mzee Warioba atusaidie. Hivi kwa mfano, ni nini hasa maana ya Rais kutangaza hadharani kuwa anawajua wala rushwa na kwamba ana majina ya watu wanaofanya biashara ya mihadarati na kisha kukaa kimya bila kuchukua hatua zozote?

Mzee Warioba atusaidie pia; ni nini hasa tafsiri ya Rais kuwaacha madarakani watu ambao wana tuhuma nzito kwa kiwango cha Gavana wa Benki Kuu na Waziri wa Nishati na Madini? Mimi ninaamini kuwa kukaa kimya bila kuwachukulia hatua watu ambao wewe mwenyewe umesema unawajua kuwa ni wala rushwa ni kuiweka nafasi yako katika hali ya kukejeliwa.

Dawa ya kukwepa kejeli si kuwakemea wale wanaokukejeli, bali ni kuhakikisha kuwa huiweki nafasi yako katika mazingira ya kukejeliwa kwa kuchukua hatua zinazostahili pale watendaji wako wanapofanya mambo yatakayosababisha wewe ukejeliwe.

Mzee Kingunge na Warioba inabidi wajiulize kama kweli haya wanayoyasema wapinzani hayana maana, inakuwaje wao wahamaki na wananchi wahamasike kuwaunga mkono wapinzani kwa kiwango tulichokishuhudia? Pengine swali kubwa ambalo inabidi tulijibu ni kuwa iweje watu waliokuwa wanaheshimika katika jamii kwa kiwango cha Kingunge na Warioba wafikie hatua ya kutokuona kuwa tuhuma za ufisadi si jambo la maslahi kwa wananchi?

Na je, ni kitu gani kimewapata watu hawa hata watoe kauli ambazo zinasababisha mkanganyiko katika jamii badala ya suluhu na amani kama tulivyowazoea?

Je, hawa watu wamebadilika au mazingira yamewabadilisha kutoka umalaika kwenda u-Lucifer?

Kwa kutumia mantiki iliyomo katika maudhui ya kitabu cha Profesa Zimbardo, ni wazi kuwa hawa wenzetu ni waathirika wa mazingira waliomo ambayo ni CCM. Chama hiki (CCM) kimechafuka kwa kiwango ambacho kila apitaye humo lazima achafuke.

Haishangazi kuona kuwa watu ambao kabla ya kuingia CCM walikuwa wanaonekana kuwa watu wema wanaoweza kuisaidia jamii katika kujikwamua na matatizo yake ukiwamo umaskini, lakini walipoamua kufanya hivyo kupitia CCM wakajikuta ama wanachafuka kama wenzao waliowakuta humo au wanashindwa kufurukuta.

Nani angejua kuwa ingefika wakati Kingunge na Warioba wangetoa kauli ambazo hata mtoto wa shule ya msingi anazishambulia na kuzizomea?

Kinachowaponza ndugu zetu hawa ni mazingira waliyomo; maadamu wamechagua kubaki katika mazingira machafu hawatakwepa kuchafuka! Vilevile tumewashuhudia watu waliokuwa wanaheshimika kwa usafi kutokana na kuchukia rushwa na ufisadi, lakini walipopata uongozi kupitia CCM wakabadilika ghafla na kuanza kutamani utajiri wa haraka na kuupata utajiri huo kupitia ufisadi na rushwa hiyohiyo waliyokuwa wanaichukia.

Ndio kusema basi tatizo hapa si hao watu wanaofanya ufisadi; tatizo ni hayo mazingira yanayowafanya wapende ufisadi yaani CCM. Kwa hiyo juhudi za kweli za kupambana na ufisadi huo si tu kupambana na hao mafisadi, bali lazima ihusishe pia kupambana na mazingira yanayosababisha hao watu wapende vitendo vya ufisadi. Katika mapambano haya tuna habari mbaya na njema.

Habari mbaya ni kwamba mapambano dhidi ya mazingira yanayofanya watu wafanye ufisadi ni magumu na ya hatari. Lazima wapatikane watu wachache jasiri ili waongoze mapambana haya. Habari jema ni kwamba tayari wameshajitokeza watu wenye ujasiri wa kupambana na ufisadi katika jamii yetu. Hata hivyo, juhudi za hawa majasiri haziwezi kufua dafu kama hawataungwa mkono na jamii nzima hasa pale watu wanaokubalika kwa kiwango cha kina Warioba watajitokeza kuwabeza watu hao na kutetea mazingira ya ufisadi.

Kwa hiyo, natoa wito kwa wananchi kuwaunga mkono sana kina Dk. Slaa na wenzake kwa juhudi wanazofanya katika kuibua na kuwaumbua mafisadi. Uungwaji mkono wa majasiri hawa usifanyike tu katika mazungumzo ya vijiweni, majumbani na maofisini. Kuna haja ya kuunga mkono juhudi zao kwa njia ya vitendo kama vile maandamano. Hata hivyo niseme tena kuwa juhudi za kupambana na fisadi moja moja ni mkakati wa muda mfupi ambao hautarajiwi kumaliza kabisa hili tatizo ambalo sasa ni kama kansa katika nchi yetu.

Mkakati wa muda mrefu wa kutokomeza hii kansa ya ufisadi lazima uwe ni kuyamaliza mazingira yanayosababisha watu kuwa mafisadi; mazingira haya ni CCM.

Ndiyo kusema tunapoendelea na mapambano haya kwa sasa tutambue kabisa kuwa dawa ya kweli ya ufisadi na uchafu mwingine katika nchi yetu ipo katika uchaguzi wa 2010.

kitilam@yahoo.com
0754 301908
cc: Mwenyekiti wa Chama Kongwe
Mtaa wa Lumumba.
Jionee majembe yako!
 
'Nimeamua kurudi upinzani ili nitubu nisije nikafa nikiwa ccm nikaenda motoni' By Hayati..... (nimemsahau jina alikufa miezi 3 iliyopota kama sikosei)
 
wakati huo huo upinzani hasa Chadema hubadili waovu kuwa wasafi, ukiwa na ovu lolote wewe kimbilia huo, it is a perfect cover...
 
Back
Top Bottom