Ccm,chadema wavutana mbele ya makamu wa rais,chadema wasema ccm wanateka mkiutano ya serikali

kamandamakini

Senior Member
Feb 17, 2012
165
137



MVUTANO
mkubwa unaotokana na itikadi za kisiasa, umeibuka mbele ya Makamu wa Rais Dk.Mohamed Gharib Bilali kati ya Chama cha Mapinduzi (CCM) na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) muda mfupi baada ya Mbunge wa Jimbo la Iringa Mjini, Mch.Peter Msigwa,

Kupanda juu ya jukwaa lililoandaliwa kwa ajili ya Dk. Bilali kuwahutubia wananchi, akiituhumu CCM mkoani humo kwamba mara zote imekuwa ikipora mikutano ya serikali hasa wanapokuwapo viongozi wa kitaifa, kwa kuweka bendera zake na kuipamba mikutano hiyo kwa sare za CCM pasipo kujali mikutano hiyo inawahusu wananchi wote na siyo chama cha Mapinduzi.

Baada ya kauli hiyo, Msigwa aligeuka nyuma ya jukwaa hilo na kumwomba Dk.Bilali, na yeye awasilimu wakazi wa mji wa Iringa kwa salaam za Chadema, kwa kuwa wao hawakupata nafasi ya kuweka bendera zao wala kuvalia mavazi ya Chadema katika mkutano huo.

Mvutano huo, uliibuka wakati wabunge na viongozi mbalimbali wa mkoa wa Iringa walipokuwa wakiitwa kutoa salaamu, ndipo Mch.Msigwa alipoombwa na Mkuu wa Wilaya ya Iringa,Kapt. Mstaafu Asseri Msangi kupita mbele ili awasalimu wananchi wa Manispaa hiyo.

Alipomaliza kutoa tuhuma hizo, Msigwa alimwomba Makamu wa Rais, amruhusu kuwasalimu wananchi kwa falsafa ya chama chake na ndipo alipokunja ngumi na kuwasalimu wananchi hao kwa salaam ya ‘Peoples Power’ huku wananchi waliokuwa wamefurika katika uwanja wa Mwembetogwa wakilipuka kwa sauti kubwa ya Power, Power!

Muda mfupi baada ya salaam hizo,mbunge huyo alimweleza Makamu wa Rais na ujumbe wake kwamba kwa kuwa na yeye (Msigwa) ni Mwenyekiti wa Chadema Wilaya ya Iringa, angeamua kuwaambia wananchi wake wabebe bendera zao au kuvalia kombati za chama chake ingekuwa balaa.

“Kama na mimi ningewatuma wananchi wangu wabebe bendera au kuvalia mavazi ya chama (Kombati) ingekuwa balaa lakini naomba niwasalimu wananchi wangu kwa salaamu ya chama chetu…’Iringa, Peoplesssss,wananchi wakaitika Power! huku wakinyoosha vidole viwili juu jambo ambalo lilimlazimu Msigwa kuwaambia wananchi hao, nawaombeni sasa, mumsikilize mheshimiwa Makamu wa Rais,”alisema mbunge huyo.

Hali hiyo haikuwapendeza viongozi wa CCM jambo ambalo lilimlazimu Katibu wa Chama hicho mkoa wa Iringa, Mary Tesha kupanda jukwaani na kutoa ufafanuzi kuhusu bendera tatu za chama hicho zilizokuwa zikipepea uwanjani hapo sambamba na bendera ya taifa.

“CCM Oyeee! Mheshimiwa Makamu wa Rais siyo kweli kwamba tumekuwa tukiteka ziara wala kuipora mikutano ya serikali kwa kuweka bendera zetu. Hata mheshimiwa mbunge (Msigwa) anajua kwamba Makamu wa Rais amekuja kukagua miradi inayotekelezwa kwa ilani ya CCM…Hii ni fahari kwetu na lazima na sisi tuwepo kwa kishindo,”alisema katibu huyo akijibu kauli iliyotolewa na mbunge wa Iringa mjini (Chadema).

Alipomaliza kumjibu Mch. Msigwa, Tesha kabla ya kushuka jukwaani, aliwataka wanachama wa CCM wawachague viongozi waadilifu wa chama chao katika uchaguzi mkuu wa chama hicho ambao umeanza nchini kote kwa kuchukua fomu katika ngazi za mashina,tawi na Kata.

Hata hivyo,katika hali isiyo ya kawaida wakati mbunge huyo akitumia salaam ya Peoples Power, Dk.Bilali alikuwa mtulivu na hakuonekana kuvurugwa na falsafa hiyo hata wakati alipopanda jukwaani kuwahutubia wananchi wa Manispaa ya Iringa waliofika kumsikiliza.
MAKAMU WA RAIS AZUNGUMZIA ELIMU

Katika mkutano huo, Dk.Bilali alisema kuwa serikali imekusudia kufikia malengo yake hadi ifikapo mwaka 2015 kwa kuhakikisha kuwa idadi ya watoto wa shule wote wanaozaliwa wawe wamepata elimu ya msingi kwa asilimia 60.

“Na hapa nataka nisisitize kwamba ukimsomesha mtoto wa kike umesomesha familia lakini ukimsomesha mtoto wa kiume umemsomesha mmoja…Lengo letu ni kuhakikisha kwamba ifikapo mwaka 2015 asilimia 60 ya watoto wanaozaliwa wapate elimu ya msingi,”alisema Dk.Bilali

Aidha,alisema kuwa katika kukabiliana na changamoto ya makali ya mgawo wa umeme na usambazaji wake,serikali imepata kiasi cha dola bilioni moja za kimarekani kutoka katika nchi wahisani kwa ajili ya kukabiliana na hali hiyo.

NAWASILISHA.
 

Attachments

  • IMG_1045.jpg
    IMG_1045.jpg
    70.1 KB · Views: 39

Similar Discussions

0 Reactions
Reply
Back
Top Bottom