CCM, CHADEMA, CUF Na Udhaifu Wa Itikadi | JamiiForums | The Home of Great Thinkers

Dismiss Notice
You are browsing this site as a guest. It takes 2 minutes to CREATE AN ACCOUNT and less than 1 minute to LOGIN

CCM, CHADEMA, CUF Na Udhaifu Wa Itikadi

Discussion in 'Jukwaa la Siasa' started by Mchambuzi, Jan 24, 2012.

 1. Mchambuzi

  Mchambuzi JF-Expert Member

  #1
  Jan 24, 2012
  Joined: Aug 24, 2007
  Messages: 4,819
  Likes Received: 1,140
  Trophy Points: 280
  Pamoja na ukweli kwamba vyama vingi vya siasa Tanzania vinaendeshwa kwa mujibu wa Katiba, Kanuni, na Taratibu, pia kuna ukweli kwamba vyama vyote vikubwa – CCM, Chadema na CUF, vina udhaifu mkubwa katika itikadi zao. Kama tutakavyobaini katika mjadala huu, itikadi ndio moyo wa chama ambao unasukuma damu katika viungo vingine vya chama kama vile katiba, kanuni, taratibu, mwongozo, sera na ilani. Mjadala huu utalenga zaidi kwenye vyama vikubwa vitatu vya siasa Tanzania: CCM, Chadema na CUF.

  Ina maana gani kusema Idara za Itikadi, Siasa na Uenezi za CCM, Chadema na CUF zinapwaya?

  1. Tanzania, tuna vyama visivyokuwa na itikadi inayoeleweka na ya vitendo. Mfano, CCM; CCM ilifanikiwa ki-itikadi chini ya mfumo wa chama kimoja kutokana, iliyolenga ukombozi wa nchi na Utaifa (chini ya TANU); baadae siasa ya Ujamaa na kujitegemea ililenga kumwinua mtanzania/mtanganyika. Lakini tangia kifo cha azimio la Arusha mwaka 1992, CCM imekuwa inahubiri itikadi ya Ujamaa, lakini upande mwingine, inatekeleza itikadi ya soko huru, tena bila ya mchujo. Ukosefu wa msimamo kiitikadi ndio tiketi ya Kifo kwa CCM, na wala sio Ufisadi. Tutalijadili hili kwa undani baadae.

  2. Pia tuna vyama vilivyo jizolea umaarufu kutokana na sababu ambazo hazihusiani na UMMA kubaini ubora wa itikadi ya chama baada ya kufananisha na itikadi za chama/vyama vingine vilivyopo. Badala yake, umaarufu wa vyama hivi unatokana na UMMA kuvikubali kwa sababu nyingine nje kabisa ya ubora wa itikadi zao. Mfano mzuri ni umaarufu wa NCCR miaka ya 1990, na ule wa Chadema miaka ya 2000 – hadi sasa. Nimetumia neno ‘jizolea umaarufu’ badala ya ‘jipatia mafanikio’, Kwa sababu, tofauti na ‘mafanikio’ ambayo hutokana na itikadi, mara nyingi ‘umaarufu’ hutokana na vitu vya mpito, na huwa haudumu kwa muda mrefu. Wengi tunakumbuka umaarufu NCCR miaka ya 1990; umaarufu wa Chadema hauna tofauti kubwa sana kwa sababu mafanikio tunayoyaona hayatokani na ubora wake wa itikadi, bali kwa vitu vya msimu tu, ambavyo vinaweza meguka kirahisi. Hili pia tutalijadili zaidi baadae.

  3. Lakini pia, Tanzania tuna vyama vilivyopata mafanikio kisiasa (sio umaarufu) kutokana na itikadi zao. Lakini vyama hivi vina udhaifu mmoja mkubwa juu ya itikadi zao: Itikadi hizi zinaendana na hali halisi ya upande mmoja tu wa jamii badala ya jamii nzima. Mfano, CUF na mafanikio yake visiwani ambayo imekuwa vigumu kuyarudia Bara. Tutalitazama hili pia baadae lakini kwa sasa ni muhimu tu kusema kwamba - mafanikio ya sasa ya CUF visiwani hayana tofauti kubwa na mafanikio ya TANU bara miaka 1960. Kama ilivyokuwa TANU miaka ya 1960, mafanikio ya CUF yanatokana na itikadi inayolenga Utaifa /Ukombozi dhidi ya Utawala wa Bara.

  Pamoja na mafanikio yake visiwani, itikadi ya CUF haina mashiko upande wa bara, na pia haitachukua miaka mingi kabla ya itikadi hii kuishiwa makali hata Zanzibar. Kama ilivyokuwa kwa CCM, CUF nayo itapitia hatua tatu za maisha: (1) Itikadi ya uhuru na Utaifa iliyozaa matunda hadi sasa (2) baada ya utaifa kupatikana, CUF itakumbwa na changamoto za kutekeleza ahadi ilizozitoa wakati wa mapambano ya kudai utaifa kutoka Bara. Hali itazidi kuwa ngumu zaidi iwapo patatokea vyama vingine vya upinzani upande wa Zanzibar (3) Iwapo vitajitokeza vyama vipya vyenye nguvu Zanzibar, itikadi ya CUF itazidi kuishiwa makali kwa kutokana na kushindwa kutekeleza ahadi za ukombozi (kama ilivyotokea kwa CCM), na vyama vitabaki kukosoana huku CUF ikionekana sio lolote/dhaifu, huku vyama vya upinzani Zanzibar vikisahau kabisa kwamba adui yao ni mmoja – wawakilishi wa mataifa tajiri yani - WorldBank na IMF.Hili pia tutalijadili baadae.
  Udhaifu huu wa ki-itikadi ndani ya vyama vya siasa unawakosesha wananchi fursa ya kuunda muono na mtazamo wa kisiasa unaofuatana na imani (za kiitikadi) zinazotambulika, na nyepesi kueleweka au kutofautisha.

  Hii ndio sababu kubwa kwanini inakuwa rahisi kwa wananchi kuunga mkono vyama kishabiki zaidi kuliko kutokana na kushiba imani za vyama. Ndio maana, tofauti na nchi zilizokomaa kisiasa, kwa Tanzania, suala la wanachama kuhama hama vyama ni suala la kawaida. Vilevile kwa upande wa viongozi wa vyama, ni jambo la kawaida kuwasikia wanasiasa wa chama kimoja wakitetea wanasiasa wa vyama vingine hata kama wamepewa adhabu kwa kwenda kinyume na katiba na kanuni za vyama vyao (mfano Zitto kuwatetea Kafulila na Hamad).

  Kama Chadema ingekuwa inaendesha siasa za ki-itikadi, jambo hili lisingetokea kwani itikadi ya Chadema na ile ya CUF ni tofauti kabisa. Katika demokrasia iliyokomaa na yenye kuendeshwa ki-itikadi, kitendo cha wanasiasa kuteteana kwa sababu binafsi, au wanasiasa kuhama hama vyama, ni kitendo cha kujimaliza kisiasa. Ni katika nchi kama Tanzania pekee ambapo leo mwanasiasa anaweza jitoa CHADEMA, CCM, au NCCR na kwenda chama kingine bila ya hofu yoyote. Hiki ni moja ya vielelezo vikubwa juu ya udhaifu wa vyama vyetu ki- itikadi. Katika mazingira ya kawaida, kitendo cha kiongozi kuhama chama ni sawa na kukana imani (itikadi) yake na kukumbatia imani (itikadi) nyingine. Kwa mwanachama kufanya hivi sio jambo la hatari sana, lakini ni la hatari sana kwa viongozi.

  Ni mapungufu haya ya ki-itikadi ndiyo hupelekea vyama vyetu kunadi ilani na sera zinazofanana, badala ya kuwa na ushindani mkali wa mtazamo unaotokana na itikadi. Katika siasa za sasa, vyama vyote vinashindana kwenda Ikulu, sio kuleta jambo jipya linalotokana na itikadi zao, bali kutekeleza sera zile zile za soko huria zilizojaa uholela, za WorldBank na IMF, kwa kasi na ufanisi zaidi. Vyama pia vinapoteza muda mwingi sana kushindania yasiyo na umuhimu sana yakiwa yametapakaa (not coherent), kama vile haki za raia, utawala wa sheria, na vita dhidi ya ufisadi. Siasa juu ya masuala haya zimekosa uthabiti (consistency) na kuungamana (coherence) kutokana na udhaifu wa ki-itikadi. Vile vile, kutokana na udhaifu wa ki-itikadi, umaarufu wa vyama mara nyingi (kama sio mara zote), unatokana zaidi na hulka (personalities) za viongozi waliopo katika vyama hivyo, hasa nguvu zao katika jamii wanazotoka, bila ya kujali vyama wanavyotoka au itikadi wanazoziamini.

  Mapungufu ya ki-itikadi yanapelekea vyama kushiriki katika ushindani wa siasa kama vile ni soko la kushindana ubora wa bidhaa. Vyama vinajikita zaidi katika ushindani wa nani ana bidhaa bora zaidi (sera na ilani), kuliko mwenzake, bila ya uwiano na itikadi zao. Vyama vinajali zaidi kuja na bidhaa zinazoendana na mahitaji ya soko kwa wakati huo. Idara za uenezi, siasa na itikadi hazijishughulishi kuzunguka nchi nzima kujenga chama na kusambaza imani (itikadi) zao ili kushawishi wananchi kuwa wafuasi wa kudumu, na pia wawe wapiganaji wa kutetea na kulinda itikadi zao katika maeneo wanayoishi. Nguvu ya chama cha siasa ipo kwenye matawi na mashina, huko ndiko watu wengi wanaishi.

  Lakini cha ajabu ni kwamba, Idara za itikadi, siasa na uenezi, zinatumia muda mwingi kwenye Redio, TV na magazeti kama vile nguvu ya chama ndio zipo huko. Huwa wanakumbuka umuhimu wa matawi na mashina wakati wa uchaguzi tu. Nia ya Mwalimu Nyerere miaka ya 1960, ya kumwachia Kawawa uongozi wa nchi kwa muda na yeye kwenda vijijini ilikuwa ni kujenga chama akisaidiwa na idara ya itikadi na uenezi ya TANU. Aliporudia zoezi hili wakati anawaaga watanzania miaka ya mwisho ya 1990, alielezea kushtushwa kwake na jinsi gani imani ya chama ilivyokuwa ikishuka, kutokana na chama kuzembea kusambaza itikadi kwenye maeneo yanayostahili.

  Kwa Tanzania ya leo, udhaifu huu ndio unaozaa UMMA usiokuwa na msimamo wa kudumu wa kisiasa, na wengine wengi kutoona umuhimu wa kushiriki katika siasa. Wananchi wengi wamechoka na vyama vya siasa, kwani havitekelezi yanayohubiriwa. Isitoshe, mara nyingi, kauli na vitendo vya vyama vilivyopo hupishana, mfano suala la posho za wabunge n.k. Idara za uenezi, siasa na itikadi zimeshindwa kufanya kazi zake kwa ukamilifu, idara hizi mara nyingi uendesha siasa za leo kupinga hili, kesho kuunga mkono lile, ili mradi tu “kujiepusha wasipitwe na masuala ya kupita”. Suala la idara hizi kuja na pre – emptive strategies halipo, na badala yake ni pro-active strategies. Hiki ni kikwazo kikubwa sana kwa ustawi endelevu wa vyama vyetu vya siasa, na demokrasia kwa ujumla.

  Umuhimu wa Itikadi ya Chama

  Kama moyo ulivyokuwa na umuhimu kwa uhai wa binadamu, itikadi ni moyo wa chama cha siasa. Moyo wa chama (itikadi) ndio husukuma damu ili kuviwezesha viungo vingine vya chama (katiba, kanuni, taratibu, mwongozo, ilani na sera), vifanye kazi zake kwa uhakika na ukamilifu. Itikadi utengeneza mtazamo, msimamo, malengo na matarajio kuhusu masuala mbali mbali yanayozunguka maisha ya jamii. Na mitazamo, misimamo, malengo na matarajio haya uhathiri matendo na shughuli za kisiasa ndani ya jamii husika. Wananchi hutegema sana itikadi kama moja ya njia zao kuu za kuwasaidia kuelewa masuala mbalimbali ya kiulimwengu, kwani iItikadi hutoa mwongozo na kusaidia uwepo wa misingi ya kuratibu jinsi gani jamii iendeshe masuala yake ya kisiasa, kiuchumi na kijamii, katika hali ya ufanisi, nidhamu na utulivu.

  Katika dunia ya leo, Itikadi zimegawanyika katika makundi makubwa sita kama ifuatavyo:

  1. Ukomunisti
  2. Ujamaa
  3. Ujamaa wa kidemokrasia/Deocratic Socialism/Social Democrats
  4. Uliberali/Liberal
  5. Conservative Liberals/mchanganyiko wa uhafidhiana na uliberali
  6. Uhafidhiana/Conservative

  Mpangilio huu wa itikadi hutokea kushoto kuelekea kulia (as a continuum) kama ifuatavyo:

  Communism=> Socialism=> Ujamaa wa Kidemokrasia=> Liberals=> Conservative Liberals=> Conservative

  Kwahiyo kwa mfano, itikadi ya kikomunist, na kijamaa zinatambulika kama itikadi za mrengo wa kushoto (leftist), wakati itikadi ya uhafidhiana (conservatism) inatambulika kama itikadi ya mrengo wa kulia (rightists). Katika miaka ya hivi karibuni, itikadi hizi kuu zimezaa itikadi nyingine tatu kubwa ambazo ni: (1) Centre/kati; (2) kati-kulia (centre-right); na (3) kati-kushoto (centre-left); Nitazijadili kwa undani baadae. Vinginevyo, kwa ujumla wake, ukomunisti, Ujamaa na Ujamaa wa kidemokrasia/democratic socialism zinazotambulika kama itikadi za mrengo wa kushoto, wakati uliberali, conservative liberals na conservative hujulikana kama itikadi za mrengo ya kulia.

  Tuzitazame itikadi hizi sita kubwa kwa undani, ili tuzidi elewa itikadi za vyama vya CCM, Chadema na CUF kwa undani zaidi. Ili kurahisisha zoezi hili, nitazigawanya itikadi hizi sita katika makundi makubwa mawili - kundi la kwanza ni lile la itikadi zote za mrengo wa kushoto yani ukomunisti, Ujamaa na Ujamaa wa kidemokrasia/social democrats; Na kundi la pili ni itikadi zote za mrengo wa kulia, yani uliberali, conservative liberals na conservatives. Tuanze na itikadi za mrengo wa kushoto – Ukomunisti, Ujamaa, na Ujamaa wa Kidemokrasia, kwa kufuatana na mpangilio tuliokwisha uona ambao ni:

  Ukomunisti>Ujamaa=>Ujamaa-wa-Kidemokrasia=>Uliberali=>Conservative Liberals=>Uhafidhiana

  Itikadi za mrengo wa kushoto (Ukomunisti, Ujamaa na Ujamaa wa kidemokrasia), asili yake ni Karl Max ambae alidai kwamba Ubepari muundo wa kinyonyaji na kikandamizaji. Wengi wetu tayari tunalielew vizuri suala hili.

  [TABLE]
  [TR]
  [TD]
  [/TD]
  [TD]UKOMUNISTI
  [/TD]
  [TD]UJAMAA
  [/TD]
  [TD]UJAMAA WA KIDEMOKRSIA
  [/TD]
  [/TR]
  [TR]
  [TD]UTAWALA
  [/TD]
  [TD]Mamlaka yote ipo chini ya umma; kuna mwafaka katika jamii kuhusu michakato wa maamuzi mbalimbali.
  [/TD]
  [TD]Masuala ya umma yanaendeshwa kwa “power structure” iliyopo chini ya muundo wa halmashauri, kuanzia ngazi ya chini mpaka taifa.
  [/TD]
  [TD]Masuala ya umma yanaendeshwa na viongozi waliochaguliwa kupitia muundo wa kidemokrasia.
  [/TD]
  [/TR]
  [TR]
  [TD]CHAGUZI
  [/TD]
  [TD]Hakuna chaguzi kwani serikali ya kikomunisti inakubalika na wote.
  [/TD]
  [TD]Ingawa mara nyingi huwa na chama kimoja cha siasa, huwa kunakuwepo na chaguzi za mara kwa mara, hivyo viongozi kuanzia ngazi ya halmashauri mpaka juu hutokana na watu.
  [/TD]
  [TD]Viongozi wa umma hutokana na chaguzi za mara kwa mara zenye uwazi na uhuru kwa wapiga kura;
  [/TD]
  [/TR]
  [TR]
  [TD]SERIKALI
  [/TD]
  [TD]Maisha yote ya jamii, kuanzia utawala, uchumi na maisha binafsi, yapo chini ya serikali.
  [/TD]
  [TD]Kuna za makusudi za kuunganisha serikali na jamii nzima.
  [/TD]
  [TD]Serikali thabiti huitajika ili kuendesha mipango na sera za kugawanya keki ya taifa.
  [/TD]
  [/TR]
  [TR]
  [TD]UCHUMI
  [/TD]
  [TD]Hakuna soko wala ubadilishanaji (exchange) wa aina yoyote; hakuna umiliki binafsi wa mali; bidhaa na huduma zote zinagawanywa sawa katika jamii bila ya ubaguzi wa aina yoyote.
  [/TD]
  [TD]Uwepo wa mishahara isiyotofautiana sana; Pia huduma na bidhaa nyingi kwa umma hutolewa na serikali.
  [/TD]
  [TD]Ubepari unakubalika, na unashamiri kupitia muundo thabiti wa kugawana keki ya taifa na upatikanaji wa huduma bora za kijamii.
  [/TD]
  [/TR]
  [TR]
  [TD]KAZI/AJIRA
  [/TD]
  [TD]Hakuna matabaka ya aina yoyote miongozi mwa wafanyakazi.
  [/TD]
  [TD]Kuna muungano wa tabaka la wafanyakazi; uwepo wa fursa sawa kwa watu wote bila kujali matabaka.
  [/TD]
  [TD]Kuna umoja wa kitabaka miongozi mwa wafanyakazi kupitia taasisi zinazounganisha tabaka hili.
  [/TD]
  [/TR]
  [TR]
  [TD]MAPINDUZI
  [/TD]
  [TD]Kuna mapinduzi yanayolenga kufuta uhaba (scarcity) na pia umiliki binafsi wa mali.
  [/TD]
  [TD]Kuna mapinduzi ya kuangamiza ubwanyenye.
  [/TD]
  [TD]Mapinduzi hayahitajiki kwani ubepari unakubalika hivyo kuendelea kushamiri.
  [/TD]
  [/TR]
  [TR]
  [TD]PROGRAMU ZA KIJAMII
  [/TD]
  [TD]Wananchi hupatiwa huduma zote za msingi na serikali bure, kwa mfano elimu, afya, n.k.
  [/TD]
  [TD]Umiliki wa umma wa njia kuu za uchumi, na matumizi ya rasilimali ya taifa kwa manufaa ya umma pamoja na upatikanaji wa huduma zote za msingi kwa watu wote.
  [/TD]
  [TD]Msisitizo mkubwa ni uwepo wa a “Welfare State”, yenye Social security programs zinazolenga kutoa msaada kwa wote wanaostahili - kama vile huduma ya afya, elimu, makazi, n.k; Pia serikali hugawanya mapato (redistribute income) kwa kutoza kodi za aina mbali mbali kwa lengo la kupunguza tofauti za kiuchumi baina ya matabaka mbalimbali, huku pia ikiweka kinga thabiti kwa watu wasio na ajira, wagonjwa, na wastaafu.
  [/TD]
  [/TR]
  [/TABLE]


  Na sasa tuziangalie itikadi za mrengo wa kulia –Uliberali, Liberal Conservatives, na Conservativesm/uhafidhiana.

  1. Uliberali
  Asili ya itikadi hii ilikuwa ni kupigania haki za watu katika jamii za mataifa ya magharibi yaliyokuwa chini ya tawala za kifalme; tawala hizi hazikutoa haki na fursa sawa za kiuchumi kisiasa na kijamii kwa wananchi. John Locke ndiye (mwanzilishi), na wenzake walidai kwamba – binadamu huru ndio msingi wa jamii imara yenye amani na utulivu; pia walihimiza umuhimu wa kuwepo kwa serikali yenye wajibu wa kulinda haki za msingi za wananchi; harakati hizi ndiyo zilizokuja kuzaa dhana nzima ya demokrasia ya uwakilishi (representative democracy); Baadae harakati hizi ziilichochea kuzaliwa kwa uliberali katika eneo la uchumi, muasisi wake akiwa Adam Smith, ambae alihimiza umuhimu wa serikali kutoingilia shughuli za kiuchumi, kwa mtazamo kwamba, serikali ikiachia shughuli za uchumi zijiendeshe na kujisahisha zenyewe itapelekea ufanisi zaidi katika uchumi. Katika dunia ya leo, Itikadi hii bado ina nguvu kubwa. Kuna jamii nyingi duniani zinazo himiza umuhimu wa serikali kutojiingiza katika shughuli za kiuchumi na kijamii, kwa mfano, serikali kukaa mbali na na utoaji wa huduma za kijamii – afya, elimu n.k; na pia serikali kutoshiriki katika uchumi kupitia mashirika ya umma, na badala yake, mashirika binafsi pekee ndiyo yatawale shughuli za kiuchumi.

  2. Conservative Liberals
  Itikadi hii ni mchanganyiko wa mawazo, sera na imani za uliberali (liberalism) na uhafidhiana (conservatism). Itikadi hii inaunga mkono ulegezaji wa masharti mbalimbali ya kiuchumi na utandawazi (globalization), Pia inaunga mkono sera kali zinazozuia uhamiaji (strict immigration policies). Kiuchumi – itikadi hii inaunga mkono uwepo wa uhuru wa kiuchumi miongoni mwa wananchi, hasa kuwapatia wananchi uhuru wa kujiamulia mambo yao wenyewe. Itikadi hii haijihusishi sana na masuala ya kijamii lakini kila inapobidi kufanya hivyo, huwa na msimamo wa kijamii ulio sawa na ule wa kiliberali (rejea mjadala wa uliberali hapo juu).

  3. Conservatives/wahafidhiana
  Asili ya itikadi hii ni harakati za kupinga mapinduzi ya kumwondoa mfalme wa Ufaransa katika karne ya kumi na nane. To conserve maana yake ni ‘kuhifadhi’, hivyo conservatives hawaamini katika mabadiliko au uharibifu wa desturi/utamaduni. Edward Burke ni muasisi wa itikadi hii; yeye alipinga mapinduzi ya kumwondoa mfalme wa ufaransa kwa mtazamo kwamba kitendo hicho kitaharibu desturi, imani na taasisi zilizojengwa kwenye jamii kwa muda mrefu ambazo ni muhimu katika maisha ya watu. Katika siasa za leo, wahafidhiana wanapinga ushiriki wa serikali katika uchumi kwa madai kwamba, umaskini ndani ya jamii ni matokeo ya serikali kuingilia maisha ya wananchi kwani kitendo hiki hulea watu wavivu, na kuua dhana ya uchapa kazi na uwajibikaji katika jamii. Badala yake, wahafidhiana wanahimiza kila mtu kujipatia riziki yake kwa jasho lake, na sio kusubiri serikali kupitia huduma za kijamii, social security, n.k. wahafidhiana pia wanapinga uwepo wa mashirika ya umma katika uchumi, na badala yake wanahimiza uchumi uendeshwe na mashirika binafsi.

  Kama tulivyoona awali, itikadi hizi sita zkubwa baadae zilizaa itikadi nyingine tatu: Centre/kati; kati-kulia (centre-right); na kati-kushoto (centre-left). Tuzitazame na hizi:

  Ukomunisti>Ujamaa=>Ujamaa-wa-Kidemokrasia=>Uliberali=>Conservative Liberals=>Uhafidhiana

  1. Itikadi ya Mrengo wa Kati (Centre) – Huu ni mrengo kati ya Uliberali na Ujamaa wa kidemokrasia. Chadema inatamka hii kama itikadi yake kama chama. Kwa kawaida, Itikadi ya mrengo wa kati (centre) inaamini na kuunga mkono mambo makuu yafuatayo:
  · Ongezeko la kodi linaloenda sambamba na ongezeko la vipato vitokanavyo na shughuli za uchumi (progressive taxation); Umiliki binafsi wa mali; Uhuru na haki ya wananchi mbele ya sheria; Uliberali wa kiuchumi na uliberali wa kijamii.

  Uliberali wa kiuchumi kwa maana ipi:
  · Kuwapatia wananchi uhuru wa kujiendeshea shughuli zao bila ya kuingiliwa na serikali; Umiliki wa mali binafsi; Serikali kuratibu/rekebisha (regulate) uchumi, lakini wanapinga serikali kukwaza uhuru wa biashara na ushindani katika soko; wanaunga mkono sera za serikali za kuondoa ukiritimba binafsi (private competition) kwa imani kwamba ukiritimba huu unaumiza wananchi maskini;

  Uliberali wa jamii kwa maana ipi?
  · Haki ya kijamii na uhuru kwa watu wote; Wajibu wa serikali kuinua hali za maisha ya wananchi kwa njia kama vile – ajira, afya, elimu, huku haki za wananchi zikizidi kuimarishwa.

  2. Mrengo wa Kati - Kulia (centre-right) – huu ni mrengo uliopo katikati ya Uliberali na Conservative Liberals.
  · Kwa ujumla, itikadi hii inaunga mkono kanuni nyingi za soko huru; lakini vilevile inapinga serikali kujiingiza kupita kiasi kwenye shughuli za kiuchumi (kupitia mashirika ya umma); inapinga serikali kujingiza kupita kiasi kwenye utoaji wa huduma za kijamii (kama vile afya na elimu); na inaunga mkono umiliki wa mali binafsi;

  3. Mrengo wa Kati – Kushoto – huu ni mrengo uliopo kati ya Ujamaa wa Kidemokrasia na Ujamaa.

  Mrengo huu unaamini katika yafuatayo:

  · Jamii endelevu na serikali endelevu; Uliberali wa kijamii (rejea hapo juu), na siasa za kijani (green politics); pia ina amini katika mchanganyiko wa sekta ya umma na sekta binafsi kuendesha huduma za kijamii kama vile elimu, afya n.k; Uwepo wa social security ya kutosha kwa wananchi wanaostahili tu (sio katika kiwango cha Ujamaa na Ukomunisti) ili kupunguza kasi ya umaskini na kulinda ‘vipato’ vya wananchi wanaioshi katika mazingira ya uzee (wastaafu), wagonjwa, walemavu na wasio na ajira; mrengo huu pia una amini katika haki na fursa sawa kwa wote; inaunga mkono uwepo na umuhimu wa taasisi za serikali zinazoratibu sekta binafsi kwa nia ya kutetea wafanyakazi na walaji (consumers), kwa kuhakikisha uwepo wa vyama vya imara vya wafanyakazi, na pia ushindani wa haki (fair competition) katika soko; pia wanaunga mkono ongezeko la kodi linaloenda sambamba na ongezeko la vipato katika uchumi, lengo kuu likiwa kukusanya kodi ya kutosha ili isaidie kutoa huduma muhimu za kijamii kwa wale wanaostahili.

  Kwa leo naomba niishie hapa ili kupunguza urefu wa uzi huu ambao tayari umepitiliza. Ila ningependa kumalizia kwa kusema kwamba - ni muhimu kwa vyama vyetu vya siasa kuamka na kuchagua itikadi zilizokuwa ‘relevant’ na mazingira ya nchi na kuondokana na siasa za kubahatisha. Siaza za ki-itikadi zitavipatia vyama vyetu vya siasa mafanikio ya kudumu, na maisha marefu, badala ya umaarufu wa muda mfupi kama ule uliotokea kwenye chama cha NCCR, mzimu ambao pia unaviwinda vyama vya Chadema na CUF hivi sasa, huku CCM ikiwa imeshafikia katika hatua ya mwisho kabisa ya maisha yake. Ni muhimu wananchi kushiba itikadi za vyama. Ni muhimu kuanza kuwavutia wananchi kwa sababu nje ya personalities za viongozi wa vyama, au kelele za ufisadi ambazo hazina mashiko ya ki-tikadi. Pa ni muhimu nitamke kwamba kwa hali ya sasa ya udhaifu ki-itikadi ndani ya vyama vyetu vikubwa, sio CCM, CHADEMA, CUF, au NCCR, ambavyo vina majibu ya kumnyanyua mtanzania kutoka katika umaskini. Kinachoendelea sana sana ni mbio za vyama hivi kukimbilia Ikulu ili kuwa watekelezaji wazuri zaidi kuliko wenzao, wa sera za soko holela zinazolazimishwa kwetu na WorldBank na IMF.

  Lakini vyama vya siasa Tanzania bado vina nafasi nzuri ya kurekebisha mapungufu yote haya. Kwa CCM ambayo ndio chama tawala, ni lazima sasa itambue kwamba Ujamaa wa Marxist – Lenin ulishaanguka zaidi ya miaka 20 iliyopita, lakini haina maana kwamba Ujamaa umefeli. Ujamaa wa Kidemokrasia kama ule uliopo katika nchi za Sweden na nyinginezo ndio njia sahihi ya CCM kuifuata ki-itikadi. Nje ya kufanya haya, CCM haina mbadala mwingine zaidi ya KUFA, kwani kitaendelea kushindana na vyama kama Chadema katika sera zile zile, tofauti kubwa ikiwa, mmoja yupo madarakani, mwingine ni mpinzania. Kwa Chadema na CUF, ingawa wana declare itikadi zao kuwa ni mrengo wa kati (Chadema) na Uliberali (CUF), vyama hivi bado vina mapungufu makubwa ki-itikadi, ambazo nitazijadili siku ningine. Poleni na pia samahanini kwa uzi mdefu.
   
 2. Ericus Kimasha

  Ericus Kimasha Verified User

  #2
  May 31, 2013
  Joined: Oct 27, 2006
  Messages: 488
  Likes Received: 126
  Trophy Points: 60
  Hii makala ingekuwa imesomwa vyema katika wakati wake, ingelichangia kuokoa kodi zetu zilizotumika kuwalipa posho watunga sheria jana pasipo kufanya kazi. Inasikitisha kwamba Makala za uchambuzi wa maana na muhimu kama hizi watu hatupendi kuzisoma na badala yake tunabaki kupelekwa na upepo wa matukio. Tubadilike!

  Asante sana Kaka Mchambuzi
   
 3. Eistein

  Eistein JF-Expert Member

  #3
  May 31, 2013
  Joined: Nov 24, 2011
  Messages: 1,107
  Likes Received: 7
  Trophy Points: 135
  shukrani mchambuzi.
   
 4. Steven Robert Masatu

  Steven Robert Masatu Verified User

  #4
  May 31, 2013
  Joined: Aug 7, 2009
  Messages: 2,395
  Likes Received: 729
  Trophy Points: 280
  Forbidden truth!!!. Mkuu hii kitu kama tungeipitia mapema pale mjengoni tusingeshuhudia ule mnyukano, na inaonekana umeipost humu JANUARY 2012. Aisee nani aliificha hii mada?
   
 5. Kibanga Ampiga Mkoloni

  Kibanga Ampiga Mkoloni JF-Expert Member

  #5
  May 31, 2013
  Joined: Aug 9, 2007
  Messages: 14,583
  Likes Received: 1,675
  Trophy Points: 280
  Lakini sijaona akizungumzia uhusiano wa USHOGA na ULIBERALI.
   
 6. mdeki

  mdeki JF-Expert Member

  #6
  May 31, 2013
  Joined: Mar 28, 2011
  Messages: 3,303
  Likes Received: 39
  Trophy Points: 145
  Ukweli mtamu huu

  Sent from my BlackBerry 8520 using JamiiForums
   
 7. Maundumula

  Maundumula JF-Expert Member

  #7
  May 31, 2013
  Joined: Nov 4, 2010
  Messages: 7,055
  Likes Received: 74
  Trophy Points: 145
  Siku hizi hamna vyama vya left and right kila mtu ajavuta kati kati ambapo ndio wapiga kura wamejaa.
   
 8. M

  Magesi JF-Expert Member

  #8
  May 31, 2013
  Joined: Jul 10, 2012
  Messages: 2,590
  Likes Received: 1
  Trophy Points: 0
  Mchambuzi heshima kwa mkuu nadhani kuna haja sasa CUF wamwombe radhi Wenje na watanzania kwa ujumla.
   
 9. M

  Magesi JF-Expert Member

  #9
  May 31, 2013
  Joined: Jul 10, 2012
  Messages: 2,590
  Likes Received: 1
  Trophy Points: 0
  Rudi tena kuisoma mkuu kwenye maswala ya kijamii.
   
 10. Azizi Mussa

  Azizi Mussa Verified User

  #10
  May 31, 2013
  Joined: May 9, 2012
  Messages: 7,633
  Likes Received: 2,280
  Trophy Points: 280
  Mkuu; ni watu wachache sana wanaoelewa maandiko kama haya ambayo MCHAmuzi kaweka hapa na ndio maana pia unaona vitu kama hivi ima asichangie mtu, au wachangiaji wake huwa wachache sana. Mara nyingi watu hawapendi kusoma mada za kufikirisha sana kwani kufikiri ni kazi pevu ambayo wengi hawaipendi.
   
  Last edited by a moderator: Jan 4, 2016
 11. m

  mokti Member

  #11
  May 31, 2013
  Joined: Sep 20, 2012
  Messages: 70
  Likes Received: 2
  Trophy Points: 0
  Nakubaliana na wewe kuhusu umuhimu wa itikadi kama roho ya chama cha siasa. Changamoto zilizopo katika vyama vyetu inawezekana inatokana na yafuatayo: (i) Moja ni kukosa wataalamu wa siasa wa kuongoza vyama husika katika mfumo ambao utakuwa endelevu;
  (ii) Mbili malengo ya viongozi wetu wengi wa vyama vya siasa wanajali zaidi maslahi binafsi na kwamba vyama vinakuwa ni ngazi tu ya kupandia kufikia malengo yao; (iii) wananchama nao hawana uelewa mkubwa wa kuweza kupambanua mambo husuan umuhimu wa Itikadi na uhai wa chama; na (iv) gharama kubwa ya kuelimisha na kuhamasisha wananchama ku "own" Itikadi ya chama na kuiendeleza.

  Kutokana na hali hii, ndiyo maana vyama vyetu huchukua njia rahisi ya kuwashawishi wanachama kukipenda chama ntindo wa "fanatism" kama walivyo mashabiki wa timu za mpira ambao hata timu ikidorora bado wanaweka matumaini kwa timu yao. Na ndiyo maana hata viongozi wakihama kutoka chama kimoja kwenda chama kingine inaonekana ni kama mchezaji wa mpira kahama kutoka timu moja kwenda timu nyingine. Aidha, kutokana na gharama ndogo ya kuendeleza utaratibu huu, nachelea kusema kwamba hali hii itaendelea kwa miaka mingi ijayo. Ni vyema kutambua pia kwamba kwa viongozi wengi wa vyama, hali hii iliyopo inawapa uchawishi wa kuendeleza mfumo huu kwa kuwa kwao hawana kikubwa cha kupoteza.
   
 12. Mchambuzi

  Mchambuzi JF-Expert Member

  #12
  May 31, 2013
  Joined: Aug 24, 2007
  Messages: 4,819
  Likes Received: 1,140
  Trophy Points: 280
  Mokti,

  Naunga mkono hoja zako kwenye bandiko namba 11 hapo juu, lakini nina reservation kwenye eneo moja: Binafsi naamini kwamba wananchi wanaendesha maisha yao ya kila siku kufuatana na itikadi mbalimbali, kwa mfano vijijini na mijini, wapo wahafidhiana, wapo waliberali, wapo wajamaa, lakini tatizo ni kwamba tu vyama vya siasa nchini vimekosa umakini ku exploit suala hilo;ningependa kusikia mtazamo wako juu ya hili;

  Sent from my BlackBerry 8520 using JamiiForums
   
 13. Red Giant

  Red Giant JF-Expert Member

  #13
  Apr 17, 2015
  Joined: Mar 9, 2012
  Messages: 9,507
  Likes Received: 6,008
  Trophy Points: 280
  huu uzii umenielimisha sana.
   
 14. Pascal Mayalla

  Pascal Mayalla JF-Expert Member

  #14
  Apr 17, 2015
  Joined: Sep 22, 2008
  Messages: 24,593
  Likes Received: 18,589
  Trophy Points: 280
  Mkuu Red Giant, asante kuuibua uzi huu hadi sisi tumeona!. Kiukweli Mkuu Mchambuzi,

  ni teacher, tutor or lecture angepaswa kufundisha somo la political science kwenye vyuo vyetu vikuu!. Just imagine uzi ulioshiba kama huu, umepandishwa tangu 2012, leo hii ndio post no. 14!.

  Pasco
   
 15. u

  uaminifukazi JF-Expert Member

  #15
  Apr 17, 2015
  Joined: Oct 22, 2014
  Messages: 1,437
  Likes Received: 286
  Trophy Points: 180
  Kuna watu watakuja kuukandia kwan unawakosoa.
   
 16. TEKNOLOJIA

  TEKNOLOJIA JF-Expert Member

  #16
  Apr 17, 2015
  Joined: Jan 6, 2014
  Messages: 4,306
  Likes Received: 752
  Trophy Points: 280
  Well thought out analysis. Tatizo halipo kwa Vyama vya siasa tu,bali lipo ktk mfumo wa kisiasa tuliouchagua mara baada ya Uhuru.Siasa huathiri kila kitu ktk maisha yetu ya kila siku,ELIMU na SIASA YA CHAMA KIMOJA vikiwemo.Tulifundishwa mashuleni kuutukuza UJAMAA na kuuchukia UBEPARI.Mara baada ya kuingia ktk mfumo wa vyama vingi,mabadiliko ktk mfumo wa ELIMU ilikuwa ni lazima,Elimu ambayo ingetoa fair and equal analysis of varieties of ideologies and give the people the freedom to choose from. Hii ingesaidia to sensitize people to the ideologies hence make it ease for them to know where they belong politically. Kwa sasa ni ngumu kwa vyama vya siasa to drum up the support based on ideology kwasababu people are not fully aware of ideology issue
   
 17. Pascal Mayalla

  Pascal Mayalla JF-Expert Member

  #17
  Apr 17, 2015
  Joined: Sep 22, 2008
  Messages: 24,593
  Likes Received: 18,589
  Trophy Points: 280
  Mkuu Mchambuzi,
  kwanza asante kwa nondo kama hizi!, pili naomba ufanye mapitio baadhi ya nyuzi zako kama rejea kuelekea October, especiall ule uzi wa CHADEMA: Tujadili Utayari wa Kutawala Nchi 2015 ambao hata sijui kwa nini umefungwa!.

  Pasco
   
 18. Mchambuzi

  Mchambuzi JF-Expert Member

  #18
  Apr 18, 2015
  Joined: Aug 24, 2007
  Messages: 4,819
  Likes Received: 1,140
  Trophy Points: 280
  Mkuu Pasco,

  Nashukuru na nitafanya hivyo. Vinginevyo it is very interesting kuona kwamba chama cha Zitto na wenzake akina Kitila Mkumbo, kwa maana ya chama cha ACT kimeamua kufuata itikadi ambayo niliijadili humu miaka mitatu iliyopita (2012). This ideology can work na kuwakomboa wananchi wanyonge walio wengi, lakini kwa bahati mbaya sana, kiongozi mkuu wa ACT Zitto na wenzake hawana uwezo wa kutekeleza itikadi hii kwani ACT imeundwa kuua upinzani kwa manufaa ya CCM. ACT haijaundwa kwa manufaa ya wanyonge. Kwa maoni zaidi, tafadhali fuatilia uzi ufuatao ambapo pia tunayachambua masuala haya kwa kina:

  https://www.jamiiforums.com/great-thinkers/656568-duru-za-siasa-chama-cha-act-mpini-wa-ccm-kumaliza-upinzani-12.html#post12472490

  cc Mag3, Mkandara, Nguruvi3, Jasusi, Tumaini Makene, Mwita Maranya
   
  Last edited by a moderator: Jan 4, 2016
 19. M

  Mkandara Verified User

  #19
  Apr 18, 2015
  Joined: Mar 3, 2006
  Messages: 15,443
  Likes Received: 132
  Trophy Points: 160
  Mkuu shukuran kuwa ukurasa mmoja isipokuwa swala la UJAMAA litakuwa tata nchini kwa watu wote kwa sababu ni gumu sana utekelezaji wake haswa katika wakati huu. na mkanganyiko unaanzia na UJAMAA wenyewe utaupa sura gani kisiasa maana ukweli ni kwamba UJAMAA wetu ni UHAFIDHINA. Unapotaka Kulinda, kuenzi na kutukuza mila na desturi za Kiafrika - UBANTU ina maana wewe ni mhafidhina na wale wanaotaka mabadiliko ya Kimila aidha kwa kupenda mambo mapya au kudai haki zitokanazo na matamanio katika maisha yao ndio Liberali.

  Sasa itatakiwa ACT wajipambanue vizuri, aidha UJAMAA wao ni huo wa UNYERERE kufuata misingi ya Ujamaa wa Muafrika ambao watu wote sawa, huishi kama ndugu na hukabiri matatizo yao pamoja katika mgawanyiko wao wa kimila katika maisha yao yatokanayo na nguzo kuu za Ukulima, Uvuvi, ufugaji, na wafanyakazi. Hivyo siasa za ACT lazima zijikite katika mambo hayo na kuendeleza imani ya kwamba Uti wa mgongo wa uchumi wetu ni KILIMO.

  Hivyo kama kweli ACT imeundwa kuua Upinzani basi tutafakari malengo ya Upinzani juu ya Itikadi zao maana nijuavyo mimi Chadema wao ndio Liberali na CCM ni Utawala wa Kiumla maana wametuonyesha wazi kwamba hawawezi kusimamia Ujamaa walokuwa wakiutangaza. Kina Mtatiro nako porojo nyingi lakini sijawasikia wakitetea yale mambo yanayosimamia itikadi yao.

  Na yawezekana kabisa ACT wakawa kama CCM lakini hatuwezi wapima kwa sababu ya UKAWA maana UKAWA sio Umoja wa Upinzani wala sio umoja unaounda Upinzani isipokuwa ni watu waloafikiana juu ya Katiba Mpya. Wamekubali kugawana majimbo na kuweka mgombea mmoja mmoja kila jimbo pale wanapoona cjhama kinakubalia hivyo hakuna ushindi hapa bado wanagawana zile asiliia zao za mwaka 2010 ili kura zilizochukuliwa na mwenza zimuongozee mgombea mmoja dhidi ya CCM.

  Sasa maadam hakuna Umoja katika Utawala isipokuwa kumpokonya CCM madaraka hilo lawezekana ikiwa tu mahesabu yataonyesha kwamba kama mwaka 2010 pasipo Upinzani jimbo fulani lingekuwa na chama cha pili. lakini pia wamesahahu ya kwamba tunaingia Uchaguzi mpya kwa kutumia sheria zile zile za mwaka 2010 ambazo ndizo chanzo na sababu ya Upinzani kushindwa. Hapa wame overlook the main problem, maana bado Mahakama, NEC, TISS, POLISI ni vikwazo vilivyowamaliza mwaka 2010 sio wapigaji kura.
   
 20. Mchambuzi

  Mchambuzi JF-Expert Member

  #20
  Apr 22, 2015
  Joined: Aug 24, 2007
  Messages: 4,819
  Likes Received: 1,140
  Trophy Points: 280
  Kwa hoja hii, sielewi kwanini haukubali hoja kwamba ACT ametibua Safari Ya UKAWA Ya matumaini Kwa kuamua kuitikia ccm.
   
Loading...