'CCM bila rushwa hakuna ushindi'

Josh Michael

JF-Expert Member
Jun 12, 2009
2,523
77
MREMA NAYE ATANGAZA RASMI KUMPIGIA KAMPENI KIKWETE 2010


Waandishi Wetu

MBUNGE wa Moshi Mjini (Chadema), Philemon Ndesamburo ameponda maelekezo ya Rais Jakaya Kikwete kwa wanasiasa kuhusu rushwa kwenye chaguzi akieleza kuwa msimamo wake huo hautekelezeki kwa kuwa CCM bila rushwa, haiwezi kushinda.

Ndesamburo alisema hayo jana alipotakiwa na gazeti hili kutolea maoni kauli ya Rais Kikwete kuwa wanasiasa wanaokusudia kutoa, kuomba au kushawishi rushwa katika uchaguzi ujao, watakiona.

"Hakuna kitu kipya. Hayo ni maneno ya kisiasa. Rushwa zimekuwepo siku zote. Takukuru wamekuwepo wakati wote. Hakuna hata siku moja tumewaona wamekamata mtu kwenye chaguzi," alisema Ndesamburo.

Mbunge huyo ambaye ni mfanyabiashara, alienda mbali zaidi akisema "Bila rushwa CCM haiwezi kushinda kwenye uchaguzi. Hii kupambana na rushwa ni kiinimacho."

Alipotakiwa kueleza mbinu anazozitumia yeye kushinda uchaguzi mwaka 2005 licha ya CCM kugawa rushwa alisema "Nilishinda kwa kura za chuki. Wale wanaopewa rushwa wanawaeleza wenzao hivyo wale ambao hawakupata mgawo, walikasirika na kunipigia mimi."

Alisisitiza kwamba CCM haiwezi kuwahonga wapigakura wote, hivyo anaamini hata akipata mpinzani mwenye fedha kiasi gani kupitia chama hicho tawala, atagonga ukuta tu maana wengi wanampenda yeye kutokana na uchapa kazi wake na isitoshe wapo waadilifu wasiopokea hongo.

Kitendo hicho cha Rais Kikwete kutangaza vita na wanasiasa wanaokusudia kutoa, kuomba au kushawishi rushwa katika uchaguzi ujao, kimeonekana kuwa ni mtihani kwa CCM ambayo sasa imepanga kuendesha semina nchini nzima kwa wanachama wake kuwanusuru.

Juzi Rais Kikwete alisema atasaini kwa mbwembwe sheria ya matumizi ya fedha katika uchaguzi na kuwaonya watakaojihusisha na rushwa katika Uchaguzi Mkuu ujao kwamba, watakumbana na mkono wa dola.

Jana Katibu wa Halmashauri Kuu ya Taifa (Nec) ya CCM, Itikadi na Uenezi, John Chiligati alisema kwamba wana-CCM hawana haja ya kuwa na wasiwasi kwa sababu chama kitawaelimisha kupitia semina mbalimbali.

Chiligati ambaye pia ni Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi alisema mchakato wa semina hizo utaanza kufanywa baada ya Rais Kikwete kusaini sheria hiyo.

Alisema CCM ndiyo iliyofanikisha mpango wa kupitishwa kwa sheria hiyo ya matumizi ya fedha katika uchaguzi na imekusudia kuwaelimisha wanachama wake ili kuepuka lawama kwani, atakayekwenda kinyume na sheria hiyo, asitegemee msaada wa chama.

Chiligati alipuuza madai ya baadhi ya makada wa CCM walioeleza kuwa sheria hiyo itakosa nguvu kwa kuwa ni kawaida kuwa na makambi katika chaguzi akisema, "Kambi huwezi kuzikwepa kwani kila anayetaka kuteuliwa huwa na watu wa kumsaidia, lakini, kinachotakiwa ni pande zote za makambi hayo kuheshimu maadili."

Alisema sheria hiyo pia haiwezi kukosa nguvu kwa sababu ya uwezekano wa kambi hizo kusingiziana kwani dola ipo na ndiyo itakayopaswa kuchunguza kwa ajili ya kujua ukweli.

Chiligati ambaye pia ni Mbunge wa Manyoni Mashariki, alisisitiza kwamba sheria hiyo haiwezi kulea vurugu wakati wa uchaguzi ndani ya CCM bali itakiimarisha umoja na kukikifanya chama hicho kizidi kuwa na nguvu.

Naye Mbunge wa Maswa John Shibuda alisema kwamba sheria hiyo itaisaidia CCM kupata viongozi bora baada ya kuwazuia matajiri wanaotaka kutumia fedha zao kujipatia madaraka ila akaonya kwamba CCM inapaswa kuwa makini na kambi zinazoanzishwa kwa ajili ya uchaguzi huo

Mbunge wa Vinjo, Aloyce Kimaro alisema kwamba sheria hiyo itaisaidia sana CCM kwa sababu kuna baadhi ya viongozi na wanachama wa CCM ambao wamekuwa wakizifanya kura za maoni kama mradi wa kuvuna pesa kutoka kwa wanaowania uongozi.

Mbunge wa Urambo Magharibi, Lucas Selelii amemtaka Rais Kikwete kuchukua hatua za mfano ili kuwakomesha wanaojihusisha na ununuzi wa kura katika chaguzi.

"..Rais asiishie tu kutangaza vita, aonyeshe vitendo kwa kuchukua hatua za mfano na hapo wenye tabia hizo chafu watakoma. Wakiona mwenzao fulani katupwa jela wataogopa, lakini si kwa maneno tu," alisema Selelii na kuongeza:

“ Wakati sasa umefika kwa rais kuwa mkali zaidi kuhusu masuala hayo. Tazama kwa mfano sasa watu wanagombania majimbo utazani yao, wanamwaga fedha hata kabla ya kampeni. Wanatoa wapi fedha hizo, kama kusaidia kwa nini wasisaidie miradi ya maendeleo ya jimbo. Rais aongeze ukali kwa hili achukue hatua.”

Mwanasiasa mkongwe nchini, Peter Kisumo alipongeza hatua ya Rais Kikwete kusimama kidete kuhusu kuhakikisha matumizi ya rushwa na hongo yanakomeshwa kuanzia Uchaguzi Mkuu utakaofanyika Oktoba.

Hata hivyo, Kisumo ambaye pia ni Mwenyekiti wa Baraza la Wadhamini wa CCM alitahadharisha kuwa itakuwa ni makosa makubwa utekelezaji wa suala hilo kuachiwa Takukuru wenyewe.

Kisumo alitoa kauli hiyo jana katika mahojiano maalumu na Mwananchi, huku akisisitiza kuwa itakuwa ni kosa kubwa kama Watanzania, vyama vya siasa na vile vya kiraia vitaibebesha mzigo Takukuru yenyewe.

"Vita hii aliyoitangaza Rais wetu isiachiwe Takukuru na asasi za kiraia pekee kwamba ndizo zipambane na rushwa hapana…CCM nacho kinatakiwa kuonyesha mfano wa kivitendo kuanzia chaguzi zake za ndani,"alisema.

Kisumo alisema suala la baadhi ya Watanzania kuwaomba rushwa wagombea au wagombea wenyewe kutoa takrima kwa wapiga kura ni jambo linalotaka sasa kuwa utamaduni wa Mtanzania jambo alilosema ni la hatari.

Mwanasiasa huyo alisema ipo mifano nchi nzima hivi sasa ya wanasiasa wanaotaka kuwania ubunge hususan kupitia CCM kuwaita viongozi mbalimbali kuanzia ngazi ya mashina na kata na kuwakirimu ili wawafanyia kampeni.

"CCM kina wafuasi wengi na ndicho kinachosikilizwa na Watanzania wengi sasa tukionyesha mfano wa kumuunga mkono Rais nina hakika anachokisimamia Rais kitatekelezeka na katika hili, tuache unafiki,"alisisitiza Kisumo.

Kisumo alitolea mfano wa tukio la mwaka jana huko Mwanga la baadhi ya wanawake kutaka mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM (NEC), Anne Kilango Malecela awalipe nauli na posho ni dalili kuna tatizo ndani ya CCM.

Mwanasiasa huyo alisema kama sheria hiyo mpya itapokelewa kikweli kweli na Watanzania na viongozi wa kisiasa ana imani kuwa Taifa la Tanzania litapata viongozi waadilifu na hata suala la ufisadi litatoweka.

Alisema kuwa Tanzania inakosa viongozi waadilifu kutokana na mfumo wenyewe wa kupata viongozi hao kuwa na matatizo kutokana na kuruhusu kuwepo kwa mianya ya wagombea wanaonunua uongozi kwa fedha.

"Tukiruhusu tupate viongozi wanaonunua uongozi tutakuwa ni taifa la hovyo ….tusiruhusu kuwa na viongozi ambao ni criminal minded (wenye mawazo ya uhalifu) na kwa kweli kwa hili namuunga mkono rais,"alisema Kisumo.

Mwenyekiti wa Taifa wa TLP ambaye tayari ametangaza kugombea ubunge katika jimbo la Vunjo, Augustine Mrema alisema kama mgombea wa CCM atakayesimamishwa hatajihusisha na rushwa, anaamini atashinda.

"Mimi naunga mkono mkakati wa Rais Kikwete na naomba Takukuru wakafungue kitua chao kule Vunjo, naamini watasaidia wananchi wengi wanaonipenda niwe mbunge wao wasirubuniwe," alisema Mrema.

Alielezea kufurahishwa na mkakati wa Kikwete, akisema atakapokuwa kwenye kampeni za kuwania jimbo hilo atawataka wapigakura waelekeze kura zao Rais kwa Kikwete.

Kwa mujibu wa Rais Kikwete juzi kupitishwa kwa sheria hiyo mpya ni jambo la kihistoria na ni hatua ya kimapinduzi kwa kuwa itasaidia kudhibiti rushwa na kuzuia taifa lisifike mahali pabaya.

Alibainisha kwamba, hali inaonyesha kuwa mbaya zaidi sasa kutokana na rushwa katika uchaguzi kuanza kuwa tatizo kubwa, hususani katika mchakato wa kuchagua wagombea wa chama wakati wa kura za maoni.

Kikwete ambaye alikuwa akizungumza kwa furaha aliwaagiza makamanda wa Takukuru kuanza kujipanga kufanya kazi ya kudhibiti wanunua uongozi na kubainisha kuwa tayari kuna wagombea wameshaanza kupita mitaani wakigawa mipira na wengine kukarabati ofisi za CCM.

"Anzeni sasa kujipanga kuifanya kazi hiyo kwani naambiwa wanunuaji wa uongozi wameshaanza, wengine wanapita na kugawa mipira na wengine wanakarabati majengo ya ofisi za CCM.

Sheria inaruhusu kudhibiti rushwa kabla na wakati wa kura za maoni ndani ya vyama vya siasa na wakati wa uchaguzi, nawaomba muanze kufuatilia na kuchukua hatua zipasazo," aliongeza.

Akielezea kuhusu na sakata la rushwa katika uchaguzi, Rais Kikwete alisema: "Rushwa kubwa kwenye uchaguzi ipo wakati wa kura za maoni katika vyama pengine hata kuliko wakati wa uchaguzi wenyewe na kuahidi kuwa yeye kama rais yuko tayari kufanya kila linalowezekana ili kuiwezesha Takukuru kufanikisha kazi ya kudhibiti vitendo hivyo na kuwataka waanze kazi hiyo sasa.

Aliasa kuwa rushwa katika uchaguzi imeanza kukomaa na iwapo hatua hazitachukuliwa, una hatari itageuza uongozi kuwa bidhaa ya kununuliwa kama shati, au njugu jambo ambalo alisema ni hatari kwa vile hata mwendawazimu akiwa na fedha anaweza kuununua.
Habari hii imeandaliwa na Leon Bahati, Exuper Kachenje na Daniel Mjema, Mos
 
Huyu jamaaa, baada ya kwenda nje kwa mara ya 35 hivi (tangu ashike nchi) kutembeza bakuli anatoa maagizo hata mtoto wa mika 7 anajua kuwa ni vumbi la macho.

ni dhahiri hakuna kingine anachojua, au anachoweza isipokuwa kila kukicha kiguru na njia -- bakuli mkononi kwa matokeo yasiyoonekana.

Kibaki, pamoja na matatatizo yake mengine, "siyo Matonya" kamwe yeye huenda nje kwenye mikutano tu. kule hakuna matatizo ya umeme, ambao pia ni bei chini kuliko hapa, bajeti hugharamiwa na serikali yake kwa asilimia 95 (JK ni asilimia 65 tu, asilimia 35 ni za kuomba-omba.

Na usisasahau Kenya haina madini kabisa -- hapa yako bwerere wakuja hujitwalia watakavyo -- pamoja na michanga. Hata kuwaambia wafukie basi mashimo wanawaogopa!

Eti sasa Takukuru wapambane na rushwa! Rushwa gani hiyo mpya? Maana rushwa zote ziko tangu zamani na Hosea hataki katakata kuzishughulikia. Yule Vijisenti anapeta tu, magego nje. Yeye na Hosea wanatuona wote WaTZ na majuha.

Ndiyo, majuha, kwani kama BAE wamekiri kosa la kulainisha viganja vya viongozi wa hovyo kama akina Vijisenti, hivi kweli wanapata wapi jeuri, au nafasi ya kutufanya Watanzania mabwege?

anachofanya Hosea ni mauzauza tu, wala hakieleweki -- si kazi yake kujua BAE walikiri vipi na makubaliano yao na SFO yalikuwa vipi. Mradi Watanzania walihujumiwa, na waliyohujumu walishatajwa na SFO, kuna nini tena Hosea anasubiri? Kamata, Vijisenti, Dr Rashidi pelekaa mahakamani kwa ushahidi huo huo iliopo. Kwa Vijisenti, moja ya "counts" katika charge sheet yake iwe ile ya kufungua akaunti nje ya nchi bila ya kibali cha BoT.

Na Hosea, ziko wapi zile kesi tatu za vigogo mlizokuwa mnazitaja wewe na JK kwamba zingetinga mahakamani? Ni miezi kadha imepita sasa Watz hawazioni, ilikuwaje?

Tafadhalini sana, iko siku Watz watachoka kufanywa majuha. Hivi CCM isipofanya rushwa katika uchaguzi, wakale wapi? Haiondoki hiyo chini ya utawala wa CCM!
 
Kuna ulazima wa kurekebisha hata sheria ya Ruzuku ya vyama, hata kurudisha mali zote za CCM kwenye Serikali na pia kama kweli anataka kufanya hivyo, Huwezi kuwa na chama ambacho kinapata Bilioni 1 kwa mwezi ukashindana na Mtikila ambaye hana Ruzuku, CCM wanajua kuwa hiyo ndio nguzo muhimu sana ila ni dhambi kubwa sana kuona hivyo, Rushwa CCM ni ngumu sana kuondoka, maana kuna mauza uza kibao bado yanaweka kando lengo nzima la sheria yenyewe,
 
Back
Top Bottom