'CCM bado imevaa mfumo wa ufisadi'; Msekwa asema kinachowaumiza ni mbio za urais 2015 | JamiiForums | The Home of Great Thinkers

Dismiss Notice
You are browsing this site as a guest. It takes 2 minutes to CREATE AN ACCOUNT and less than 1 minute to LOGIN

'CCM bado imevaa mfumo wa ufisadi'; Msekwa asema kinachowaumiza ni mbio za urais 2015

Discussion in 'Jukwaa la Siasa' started by nngu007, Apr 15, 2011.

 1. nngu007

  nngu007 JF-Expert Member

  #1
  Apr 15, 2011
  Joined: Aug 2, 2010
  Messages: 15,871
  Likes Received: 56
  Trophy Points: 145
  *Kiongozi UVCCM adai utawasaidia waliotemwa kuibuka
  *Msekwa asema kinachowaumiza ni mbio za urais 2015


  SIKU chache baada ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) kufanya kile kinachoitwa ni kujivua gamba, imeelezwa kuwa hatua hiyo haitasaidia, kwani 'imeondoa
  watu badala ya mfumo dhaifu' ambao ndiyo jamvi la mafisadi ndani ya chama na serikali yake.

  Imeelezwa kuwa pamoja na CCM kutaka baadhi ya watuhumiwa wa ufisadi katika kashfa mbalimbali ambazo zimekuwa zikiitikisa nchi kwa muda mrefu sasa, wajirekebishe au kukaa kando, bado wanaweza kutumia mfumo dhaifu uliolea ufisadi kwa muda mrefu, hata kama wako nje, kwani 'watu hao wana vibaraka na mawakala wao katika maeneo mengi nchini'.

  Hayo yalisemwa jana na Mjumbe wa Mkutano wa Wilaya Umoja wa Vijana wa CCM, Moshi Vijijini, Bw. Paul Makonda alipozungumza na waandishi wa habari kuhusiana na hatua hiyo ya CCM, ya kuteua wajumbe wapya wa Kamati Kuu (CC) na sekretarieti, baada ya wale wa awali kujiuzulu.

  Alipobanwa na waandishi wa habari, wakitaka kujua kundi lipi analitumikia kati ya yaliyopo ndani ya CCM, alisema kuwa anatumwa na wananchi wasiokuwa na sauti, wanyonge, wasiosikika, walioko vijijini, baadhi yao wakiwa ni wana-CCM, ambao wakati mwingine si rahisi kuvifikia vyombo vya habari na kupaza madai yao dhidi ya matatizo yanayoikabili nchi na chama chao.

  Huku akitaja majina ya baadhi ya watuhumiwa wa ufisadi, Bw. Makonda alisema kuwa wametumia mwanya wa mfumo huo wa ufisadi kushawishi uteuzi wa mawaziri, wakuu wa mikoa, wakuu wa wilaya na nafasi nyingine mpaka ngazi za chini ambao ni watiifu kwao, hivyo wanaweza kuwatumia kadri wanavyotaka, kwani 'ni mawakala na vibaraka wao'.

  Akizungumza kwa ujasiri, Bw. Mkonda alisema kuwa anatumia nafasi yake hiyo pamoja na ile ya Mjumbe wa Mkutano wa UVCCM Mkoa wa Kilimanjaro kutoa maoni yake, ambapo alisema kuwa Mwenyekiti wa CCM, Rais Jakaya Kikwete anastahili pongezi kwa uamuzi huo mgumu wa Dodoma.

  "Tumpongeze Rais Jakaya Kikwete kwa uamuzi mgumu, ambao kabla haukutarajiwa na yeyote awe mwanachama au si mwanachama. Uamuzi wa kuvunja sekretarieti ya chama siyo tu ulikuwa mgumu, bali athari zake hata sasa itakuwa ngumu kuchukuliwa na wahusika na washirika wao. Haya ndiyo maamuzi ambayo wanachama wanaweza kuandamana kuyaunga mkono.

  "Hata hivyo kilichofanyika ni mkakati wa kujinusuru, ambapo sasa Sekretarieti mpya chini ya Katibu Mkuu Bw. Wilson Mukama inalo jukumu la kuhaulisha haiba ya chama iliyopauka machoni pa Watanzania na miongoni mwa wanachama na kuelekeza katika mkakati wa ushindi endelevu, kwa kukibadilisha chama kutoka utendaji kwa uzoefu, kwenda utendaji wa kitaalamu unaozingatia nyakati tulizonazo.

  "Yaliyotokea Dodoma ni katika juhudi za chama kujinasua na mtego wa kuporomoka kwenye siasa za Tanzania na kimataifa...sasa ni wakati wa kuondokana na utendaji mazoea na kwenda kisayansi...kilichotokea ni kuondoa watu dhaifu na si kuondoa mfumo dhaifu, uliojengeka kwa kipindi kirefu ambao ulisababisha watu wenye uroho. Walioamua kuweka mustakabali wa taifa rehani kwa maslahi yao binafsi kuigeuza nchi kuwa jamvi la mafisadi.

  "Ni mfumo huu dhaifu uliopelekea uimarishaji wa watu badala ya kuimarisha mifumo ya utawala, siasa, demokrasia na haki za binadamu, utawala wa sheria na ushiriki wa wananchi katika kujiletea maendeleo," alisema Bw. Makonda kwa kirefu, akiongeza kuwa haitoshi kuwaondoa akina Andrew Chenge, Edward Lowassa na Rostam Aziz.

  Alisema kuwa kwa muda mrefu chama hicho kimejikita katika kuangalia matokeo kama njia ya kujihalalisha machoni pa watu na kuwatambia wapinzani, badala ya kuangalia mfumo unaokiwezesha kupata matokeo, hivyo kimeshtuka baada ya 'kuvuliwa nguo sehemu nyeti na wapinzani', kwa kushindwa katika maeneo aliyodai yalikuwa muhimu na ngome ya CCM, kwenye uchaguzi uliopita.

  Kijana huyo ambaye alionekana kutoa maelekezo kwa sekretarieti mpya ya CCM, alisema kuwa kinatakiwa kujifanyia marekebisho ya kimfumo ndani ya chama, kuufanya utafiti wa mwelekeo wa kisiasa kuwa ndiyo kipaumbele cha ofisi ya katibu wa uenezi na itikadi, kutumia mifumo ya kisasa ya mawasiliano kutoa taarifa kwa haraka, bila kuwa na milolongo ya kusubiri vikao halali.

  Akiwageukia wenzake wa UVCCM, ambao katika mkutano wa kwanza aliwapatia siku saba wajiuzulu akiwatuhumu kwenda kinyume na katiba na kanuni za CCM, alisema sasa yuko katika mchakato wa kuandaa UVCCM nyingine, ambayo amesema itaitwa UVCCM-Maadili, ambao uko mbioni kumalizika na kuwasilishwa mezani kwa katibu mkuu mpya.

  Alisema kuwa anatumia haki ya ibara ya 15 katika katiba ya CCM kuunda UVCCM-Maadili, akiwataka vijana wengine wanachama wa CCM, wanaotaka kuitumikia nchi kwa uadilifu, kujitokeza na kumuunga mkono katika mchakato huo, akisema UVCCM iliyopo imeshindwa majukumu, badala yake viongozi wake wamekuwa vibaraka na mawakala wa mafisadi.

  Pia alitoa madai mazito kwa mmoja wa makada wa chama hicho, wanaotuhumiwa kwa ufisadi, Bw. Rostam Aziz, akitaka aondolewe katika chama, pamoja na viongozi wa UVCCM, Mwenyekiti Beno Malisa, James Millya, Hussen Bashe na Martine Shighela, ambao alidai ni vibaraka wake, akisema mwenendo wao umeharibu chama na ustawi wa taifa kwa ujumla.

  "CCM imetoa siku tisini kwa wale wenye tuhuma za ufisadi, walojihusisha na DOWANS, KAGODA, na mambo mengine yaliyoaibisha nchi na kushusha haiba ya chama mbele ya wapiga kura. Huu ni muda mrefu mno kwa watu kama hawa. Wanaweza kutumia muda huo kufanya mambo ya ajabu kabisa. Hivyo wao wenyewe wachukue hatua hizo mapema."

  Bw. Makonda aliongeza kuwa iwapo Bw. Lowassa aliwahi kujiuzulu katika kashfa ya Richmond, mapema wakati bunge likiendelea na mjadala, basi anatakiwa kufanya vivyo hivyo katika hatua hii, pamoja na watuhumiwa wengine wote.

  Msekwa ataja kinachotuumiza

  Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Tazania Bara, Bw. Pius Msekwa amsema kuwa miongoni mwa mambo ambayo yanakiumiza chama hicho ndani kwa ndani ni mbio za urais katika uchaguzi wa mwaka 2015.

  Msekwa aliyasema hayo jana wakati akizungumza kwenye hafla fupi ya kutambulisha Sekretarieti ya Halmashauri Kuu ya CCM taifa iliyochaguliwa hivi karibuni mjini Dodoma baada ya chama hicho ujivua gamba' na kujiuzuku kwa ile ya awali.

  Msekwa alisema kuwa hivi sasa ndani ya chama hicho yapo makundi ya vinara wanaowania urais ambayo yamewagawa wanachama wa chama hicho na hali hiyo imekuwa ikiathiri umoja na mshikamano ndani ya chama kwa kiwango kikubwa.

  Alisema kuwa umoja na mshikamano ndani ya chama ni nguvu kubwa inayowahakikishia ushindi katika mashindano na vyama vingine, hivyo tatizo hilo la vinara kuwagawa wanachama ni kubwa na linaathiri chama kwa kiwango kikubwa, hivyo chama hakina budi kulitafutia ufumbuzi wa haraka.

  Akifafanua zaidi, alisema kuwa kiini kikubwa cha tatizo hilo ni utaratibu wa kupata wagombea wa CCM ambao unatumika hivi sasa kulingana na kanuni za uchaguzi wa kuingia katika vyombo vya dola zilizopo.

  Kufuatia hali hiyo, Bw. Msekwa alisema kuwa NEC imefanya mageuzi kwa kuelekeza utafutwe utaratibu bora zaidi wa kupata mgombea urais kwa tiketi ya CCM ambao utalenga kuzuia matumizi makubwa ya fedha kwa nia ya kununua kura za wajumbe wa vikao vya uchujaji na vya uteuzi wa mwisho katika mchakato huo.

  Naye Katibu Mkuu mpya wa chama hicho, Bw, Wilson Mukama alisema kuwa yaliyofanywa na chama hicho ni maamuzi ya kimapinduzi na wala hayapunguzi heshima ya chama hicho, hivyo wana-CCM hawapaswi
  kukaa kama kuku katika tenga, watembee kifua mbele kwani chama chao kimeimarishwa.

  Mukama alisema kuwa mageuzi yaliyofanyika ndani ya chama si ya kujipodoa bali ya kukijenga upya ili kiweze kuleta ari mpya kwa wanachama wake na kuahidi kuwa kazi ya sekretarieti hiyo mpya wajiandae kuona matokeo mazuri.

  Imeandaliwa na Tumaini Makene, Dar; na Pendo Mtibuche, Dodoma
   
Loading...