CCM and its Leaders Hypocrisy Can Not Go Unnoticed! Historia Itatuhukumu

Elly B

JF-Expert Member
Jan 11, 2011
1,194
906
YAPO mambo ukiyasikia ama kuyaona kutoka kwa wanasiasa na watawala wetu fulani ambao taifa linawaamini kuwa wanayo busara ya hali ya juu, unaweza kuangua sio tu kicheko bali kilio cha uchungu!

Watanzania wamewasikia baadhi ya wanasiasa na watawala wakifura kwa nguvu na hasira kwa madai kwamba, Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere ametukanwa na kukashifiwa na wanasiasa wa vyama vya upinzani.

Wakasikika wakisema kuwa kunena kwa lugha ya matusi na kashfa dhidi ya Baba wa Taifa, ni utovu wa nidhamu kubwa na ni ishara ya kutomuenzi Mwalimu Nyerere.

Sitaki kutaja majina ya watawala waliofoka, lakini nikiri kwamba nimeshangazwa sana na ‘ujasiri' na ‘ufuasi' bandia ulioonyeshwa na baadhi ya watawala tuliowasikia.Wapo wengi wanaojidai na kulitumia vibaya jina la Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere kwa kuwa sio kweli kwamba ni watetezi wa kweli wa kiongozi huyo wa kwanza wa taifa letu.Mmoja wa watawala wanaojitapa kwamba ni muumini wa Mwalimu Nyerere, anasutwa na historia ya maisha yake kisiasa, ambayo kwa ubovu wake alilazimika kuwa mbali na Mwalimu.

Watanzania wanajua ni wangapi wanaojitapa kuwa wafuasi wa Mwalimu waliomkimbia wakati wa uhai wake na kujiunga na vyama vya upinzani. Huku bado tunakumbuka namna walivyokuwa wakiisema CCM kwa ubaya wake tangu enzi ya TANU na kwa maana hiyo, uongozi wa Mwalimu.Watanzania wanatambua bado jinsi viongozi hao walivyozunguka kila kona ya nchi wakiishambulia CCM ya Mwalimu na hawakurejea hadi walipohakikisha amefariki!

Leo watu hao wanapofura na kulipuka kwa hasira; tuwaulize, uzuri wa Mwalimu kwao umeanza lini? Wao walipomshambulia wakati ule, walikuwa raia wa nchi gani?

Lakini tuwe wakweli mbele za Mungu. Hivi leo ni wanasiasa wangapi ndani ya CCM wanao ujasiri wa kusimama hadharani na kusema wanamuenzi kwa dhati na kwa vitendo Mwalimu Nyerere?

Wangapi wasimame tuwaone ndani ya CCM na hata nje anayeweza kujigamba kwamba ni ishara ya mtu anayeyaendeleza mema ya Mwalimu. Je, Mwalimu alimpa mwanae yupi ama mkewe uongozi wa juu ndani ya CCM? Mwalimu Nyerere aliwahi kumiliki miradi gani ya kiuchumi kiasi cha kuonyeshwa vidole kila kona kama walivyo watawala wengi wa sasa? Nani leo ndani ya CCM anaweza kusema hajawahi kula rushwa, na anaendesha siasa zake bila unafiki na kujikomba kwa umbea na majungu? Kama kweli watawala wetu wanajidai kumuenzi Mwalimu, ilikuwaje basi asimame na kuwasuta hao hao wanaojidai kuwa wafuasi wake kabla hajafa?

Mwalimu Nyerere alishuhudia jinsi CCM ilivyobadilika na kuwa mzigo kwa nchi yetu na pia tishio kwa usalama wa taifa. Bado Watanzania hawajasahau namna Mwalimu baada ya kuona kuwa CCM inaelemewa na ‘uchafu', Mwaka 1993 alichapisha kitabu kiitwacho ‘Uongozi Wetu na Hatima ya Tanzania'. Mwalimu bila kutafuna maneno aliandika, nanukuu: "Chama Cha Mapinduzi, kwa sababu ya uzito wa historia yake, hadhi ya jina lake, mfumo wa wavu wake, mazoea ya watu, na ubovu wa vyama vya upinzani, kinaweza kuchaguliwa na Watanzania, pamoja na kansa ya uongozi wake. Au watu wanaweza wakachoka, wakasema, ‘potelea mbali' wakachagua chama chochote, ilimradi tu watokane na kansa ya uongozi wa CCM." Mwalimu Nyerere akaongeza kwa ukali kwamba, nanukuu: "Hainifurahishi kuyasema haya, lakini uhai wa nchi yetu unataka yasemwe. Nilisema awali kwamba kansa ya uongozi ndani ya Chama Cha Mapinduzi isingekuwa ni jambo la kutisha sana kama tungekuwa tumeanza kuona chama kizuri cha upinzani kinachoweza kuiongoza nchi yetu badala ya CCM"

"Ubovu wa uongozi ndani ya CCM ndio uliofanya nikapendekeza tuanzishe mfumo wa vyama vingi. Nilitumaini kuwa tunaweza kupata chama kingine kizuri ambacho kingeweza kuiongoza nchi yetu badala ya CCM; au ambacho kingekilazimisha Chama Cha Mapinduzi kusafisha uongozi wake, kwa kuhofia kuwa bila kufanya hivyo kitashindwa katika uchaguzi ujao. Lakini bado sijakiona chama makini cha upinzani; na wala dalili zozote za kuondoa kansa ya uongozi ndani ya CCM." Mwisho wa kunukuu.

Leo hii hakuna anayekana kwamba ndani ya CCM kumeoza kwa rushwa, majungu na ufisadi. Leo hii Watanzania wanashuhudia watawala wao wakitukana watu waziwazi bila aibu wala woga.Watanzania hawakuwahi kusikia enzi ya utawala wa Mwalimu, mwanasiasa na kiongozi anamwita mwanasiasa mwenzake mbwa, na mwingine akaruka na tusi la nguoni lisiloandikika na bado akashangiliwa kwa makofi! Wakati wa Mwalimu Nyerere Watanzania wanasiasa wa ovyo kiasi hiki wangeishia kizuizini. Badala yake, wanaojidai kumuenzi Mwalimu wamezawadiwa vyeo vikubwa, hata kuwa mawaziri. Je, huko ndiko kumuenzi Mwalimu?

Watanzania tunashuhudia rasilimali zikiporwa ovyo na kutoroshwa nje ya nchi. Watu wanatajwa kwa majina. Kwamba fulani ndiye kafanya hivi na wengine wanaweka wazi ushahidi walionao. Badala ya kuchukua hatua za kisheria, watawala wanaotamba kumuenzi Mwalimu wamesimama kuwatetea!

Ni wale wale wanaojidai kumuenzi Mwalimu Nyerere wanakiri kuwa makampuni yao yalihusika kutorosha nyara za taifa, lakini hawako tayari kuwajibika. Enzi ya Mwalimu mtu wa aina hii asingethubutu kusimama na kujifanya ni mzalendo wa kweli na mwenye uchungu wa taifa hili. Angeishia kizuizini tu!

Asimame mwanasiasa anayelia na kujifanya anampenda Mwalimu Nyerere aseme lini wakati wa utawala wake, Mwalimu aliwahi kuzomewa ama waziri wake kurushiwa mawe na wananchi? Leo Watanzania wanashuhudia ndani ya CCM watu wakiitana mizigo. Wakishutumiana kwa uzembe, wizi na ubadhilifu. Lakini wako wapi? Wamechukuliwa hatua gani? Wamewajibishwa na nani? Je, Watanzania wanafanywa wajinga kiasi cha kuchezewa akili namna hii?

Enzi ya Mwalimu hatukusikia waandishi wakipigwa na kung'olewa meno na macho. Pamoja na kuambiwa kuwa alikuwa ‘dikteta' nani aliumizwa kijinga? Nani alitekwa na kuponea chupuchupu kisa tu kasema ukweli? Nani hakumbuki jinsi Mwalimu huyo huyo alivyokubali kujiuzulu kwa mzee Mwinyi baada ya kutokea mauaji ya wananchi kule Shinyanga? Leo yametokea mauaji ya kijinga na kizembe kiasi kikubwa. Badala ya kuwajibika kama ishara ya utawala unaofuata nyayo za Mwalimu, Watanzania wameshuhudia sio tu hakuna aliyewajibika, bali mtu anapandishwa cheo kikubwa na kusifiwa kwa ‘kazi njema'. Kumuenzi gani huko? Watawala wanamchezea nani akili?

Mwalimu Nyerere alisomesha watoto wake hapahapa nchini. Wakatibiwa hapa hapa nchini. Leo mtoto wa waziri gani anasoma shule zetu za akina ‘Kanumba'?

Kama wanamuenzi, ilikuwaje wasirudishe Azimio la Arusha? Si wanataka kumuenzi? Wamepora nyumba za serikali na wakajiuzia kwa bei ya kutupwa. Kibaya zaidi, nao wakawauzia matajiri wa kigeni ambao wamejenga mahekalu na wanayapangisha kwa mamilioni ya fedha? Mwalimu aliuza nyumba ipi ya serikali? Alijipatia nyumba ipi maana tunajua aliondoka madarakani bila nyumba.Tuwaulize hawa wanaoringa kumuenzi mwalimu, nani aliwaruhusu waziuze? Ndiko kumuenzi huko?

Ndiyo maana nikasema, kuna mambo yanafanywa na watawala yanachefua, yanaudhi na yanaweza kukufanya sio ucheke bali kulia kwa uchungu!


Makala hii imechapishwa katika gazeti la Tanzania Daima la 24/04/2014
 
Ccm ya sasa hivi imejaa watu wa kukurupuka na wavivu wa kufikiri..hawawezi kukaa chini na kufikiri sawasawa
 
Ccm ya sasa hivi imejaa watu wa kukurupuka na wavivu wa kufikiri..hawawezi kukaa chini na kufikiri sawasawa

Sitaki kuamini kuhusu uwezo mdogo wa kufikiri, nadhani ni kuendekeza njaa na maslahi binafsi kwa gharama za wananchi maskini.
 
Ccm ya sasa hivi imejaa watu wa kukurupuka na wavivu wa kufikiri..hawawezi kukaa chini na kufikiri sawasawa
Utasema mengi lakini mwishowe kwa sababu ya kutoelewa kwao wataishia kusema "umewatukana waasisi".
Picha hata ya kuchora inaongea maneno zaidi. only intelligent people will understand.jpg

 
Sitaki kuamini kuhusu uwezo mdogo wa kufikiri, nadhani ni kuendekeza njaa na maslahi binafsi kwa gharama za wananchi maskini.

Sidhani kama CCM hawajui watendalo. Sidhani kama hawajui kuwa wanaiba, sidhani kama hawajui kuwa wanafanya ufisadi na ten percent, sidhani kama hawajui ni nani anauwa tembo na nani anauza madawa ya kulevya. Siamini kama hawajui wanawaumiza watanzania na wanaipeleka nchi ndiko kusiko.

Ila watakuja kukiri kwamba walijua yote haya pale wakati utakapofika, changes are innevitable!
 
Sidhani kama CCM hawajui watendalo. Sidhani kama hawajui kuwa wanaiba, sidhani kama hawajui kuwa wanafanya ufisadi na ten percent, sidhani kama hawajui ni nani anauwa tembo na nani anauza madawa ya kulevya. Siamini kama hawajui wanawaumiza watanzania na wanaipeleka nchi ndiko kusiko.

Ila watakuja kukiri kwamba walijua yote haya pale wakati utakapofika, changes are innevitable!

Naisubiria hiyo siku. Kwa sababu nitapenda kuona wanawajibishwa kwa maouvu yao.
 
Back
Top Bottom