Wonderful
JF-Expert Member
- Apr 8, 2015
- 7,347
- 5,985
“NINAFIKIRI miaka 10 niliyoitumikia timu ya Taifa Stars inatosha kiukweli na huu ni muda wangu sahihi wa mimi kustaafu kuichezea timu hiyo.
“Acha niwaachie vijana wengine wanaochipukia waje kuichezea Stars kwa mafanikio makubwa katika kuhakikisha inapata mafanikio katika siku za baadaye.
“Naamini ni maamuzi sahihi kwa wakati sahihi kwangu kutangaza kustaafu kuichezea Stars, ninaamini wapo wachezaji wengi wanaochipukia watakaonirithi mimi na wakongwe wenzangu,” hizo ni kauli za beki mkongwe wa Yanga, Nadir Haroub ‘Cannavaro’.
Cannavaro ambaye alikuwa nahodha wa Taifa Stars kwa miaka kadhaa, amechukua uamuzi huo ikiwa ni siku chache baada ya kuvuliwa unahodha wa kikosi hicho, ambapo cheo hicho kimekabidhiwa kwa Mbwana Samatta anayetarajiwa kutimkia Ubelgiji kwenda kuichezea Klabu ya Genk ya nchini humo akitokea TP Mazembe ya DR Congo.
Katika mahojiano maalum na Cannavaro jijini Dar es Salaam, juzi. Mambo yalikuwa hivi;
Sababu ya kustaafu
“Maneno-maneno naona yamekuwa mengi sana nikiwa naichezea Stars, yalianza mara baada ya mechi ya marudiano ya kuwania kufuzu kucheza Kombe la Dunia dhidi ya Algeria kule kwao.
“Katika mechi hiyo tulifungwa mabao 7-0, kama unakumbuka mechi hiyo muda mwingi tulicheza pungufu baada ya Mudathiri (Yahya) kutolewa kwa kadi nyekundu.
“Kiukweli tulipambana kuhakikisha tunawatoa Algeria lakini ikashindikana, cha ajabu mara baada ya mechi hiyo nilionekana mimi pekee ndiye niliyefungisha, sikujisikia vizuri kwa sababu nilipambana kwa ajili ya taifa langu na mwisho wa siku naonekana si lolote.
Ehee! Amechokwa kumbe
“Kutokana na minong’ono hiyo iliyokuwa inazungumzwa huku wakitaja umri wangu kuwa ni tatizo wakidai nimezeeka, nikaanza kufikiria kuwa inatosha. Nikaanza kupata maoni kuwa niwaachie vijana wenye umri mdogo waendelee kuichezea Stars.
Sakata la kuvuliwa unahodha
“Sing’ang’anii na wala silazimishi kuwa nahodha, kikubwa ninachotaka ni kupewa heshima yangu kwanza kama shujaa niliyeipeperusha vema bendera ya Tanzania kwa mafanikio hayohayo madogo.
“Kiukweli nimepokonywa unahodha bila ya heshima, ninajisikia vibaya kupokonywa unahodha kwa kupitia vyombo vya habari kitu ambacho siyo sahihi, hali hiyo imeshusha heshima yangu kwa kiwango kikubwa.
“Nilitakiwa kupewa taarifa kwa maana ya kupewa barua ya kiofisi na TFF (Shirikisho la Soka Tanzania) na baada ya hapo ingetangazwa kwenye vyombo vya habari, lakini siyo kama hivi ilivyofanyika, mimi nilipata taarifa za kuondolewa unahodha na kupewa Samatta kupitia televisheni kitu ambacho siyo sahihi.
“Nilishangaa utaratibu huo uliotumika, baada ya kupata taarifa hiyo kupitia televisheni, siku iliyofuata ndipo Kocha Mkwasa (Boniface) akanipigia simu na kuniambia kuwa wamempa unahodha Samatta, nikamuitikia tu na kukaa kimya.
“Hivi alivyoondolewa unahodha Maxime (Mecky), Swed (Salum) na Nsajigwa (Shadrack) ni sawa na mimi nilivyoondolewa unahodha? Nimeumia sana, heshima yangu ipo wapi hapo sasa? Licha ya kulitumikia taifa langu kwa nguvu na moyo mmoja, leo naonekana si lolote.
Barua ya kustaafu kupelekwa TFF
“Nimepanga kupeleka barua TFF ya kuwapa taarifa ya kustaafu kwangu kuichezea timu ya taifa, kwa sababu hali inaonyesha kabisa nimechokwa, hivyo acha nijiondoe mwenyewe kabla ya kufukuzwa. Sitaki nistaafu kuichezea Stars kwa dharau kama iliyotokea ya kupokonywa unahodha bila ya kupewa taarifa.
Abaki na Yanga yake
“Nguvu zangu zote nitazihamishia katika klabu yangu ya Yanga. Hivi sasa nimepona majeraha ya enka niliyoyapata nikiwa naitumikia Stars tulipocheza na Algeria, hivyo ninaamini baada ya wiki mbili nitarejea uwanjani,” anahitimisha Cannavaro.
Last edited by a moderator: