SoC 2022 Bustani ya Botanic na Zoolojia, chachu ya ufaulu kwa masomo ya sayansi

Stories of Change - 2022 Competition

Seif Al-jahury

New Member
Aug 3, 2022
1
1
BUSTANI YA BOTANIC NA ZOOLOJIA, CHACHU YA UFAULU KWA MASOMO YA SAYANSI


1660333258739.png


Kuhusu Bustani ya Botanic.

Katika miaka ya hivi karibuni, watafiti na watunga sera kote ulimwenguni wamezidi kutoa wito wa umakini zaidi kuwekwa juu ya elimu kupitia kujifunza kwa vitendo katika mazingira ya nje ya darasa, wakitaja faida nyingi na umuhimu wa wanafunzi kujifunza kwa vitendo tofauti na wakati wakiwa darasani.
Matokeo muhimu ya tafiti yanaonyesha kuwa wanafunzi wa shule kutembelea katika mazingira yaliyo nje ya shule kama vile makumbusho ya sayansi, bustani za mimea na mbuga za wanyama ni muhimu katika kukuza uelewa wao na maslahi ya masomo ya sayansi.
Kwa sababu ya upotevu wa baadhi ya spishi za mimea na wanyama kwa kasi isiyo na kifani, na kusababisha kupungua kwa huduma za mfumo wa ikolojia, na karibu theluthi moja ya spishi za wanyama na mimea ulimwenguni zinakabiliwa na tishio la kutoweka kutokana na shughuli nyingi zinazofanywa na binadamu zikiwemo:

 • Uvunaji kupita kiasi.
 • Mbinu haribifu za kilimo
 • Ukataji ovyo wa misitu
 • Uchomaji moto wa vichaka na mapori
 • Ukuaji wa miji
 • Uchafuzi wa mazingira ya fukweni na baharini sambamba na uvuvi usio salama
 • Mabadiliko ya matumizi ya ardhi
 • Spishi vamizi za kigeni
 • mabadiliko ya hali ya hewa duniani na mengineyo.
Kutokana na sababu nilizotaja hapo juu ambazo hupelekea kupotea kwa spishi za mimea, wadudu na wanyama, na kutokana na kuwepo kwa uhitaji mkubwa wa spishi za wadudu, mimea na wanyama kwa ajili ya kufanyia mitihani ya vitendo (practical Examinations) kwa wanafunzi wa shule za sekondari nchini Tanzania kila ifikapo mwishoni mwa mwaka, tunahitaji tena kwa umuhimu wa kipekee kujenga eneo kubwa la uhifadhi litakalokuwa na seksheni zenye mkusanyiko wa viumbe mbalimbali vya majini kama vile tilapia, wadudu wa porini kama vile mijusi, panzi na panya, wanyama kama vile nyoka na baadhi ya mimea ili kukuza mbinu shirikishi za elimu na vitendo vya kisayansi kwa wanafunzi wa shule za sekondari za Tanzania, taasisi za elimu ya juu hususani walio katika nyanja za afya na masomo ya mazingira, pia walimu na watafiti mbalimbali watanufaika.

NI YAPI MADHUMUNI YA KUJENGA BUSTANI YA BOTANIC NA ZOOLOJIA?
 • Bustani hii ya mimea na wanyama, kwa kimombo (Botanical and Zoological Garden) itakua ni sehemu ambayo imetengwa maalumu kwa ajili ya ukusanyaji, uhifadhi na maelezo ya aina mbalimbali za mimea na wanyama na majina yao halisi na ya kisayansi.
 • Eneo litakusanya spishi za wanyama na mimea na majina yao ya kawaida (common names) pamoja na majina yao ya kisayansi (scientific names) ikiwa ni pamoja na maelezo ya maandishi kwa kila spishi ili kurahisisha shughuli za kujifunza kwa wanafunzi na watafiti.
 • Bustani hi inatarajiwa kupunguza tishio la kutoweka kwa spishi za mimea na wanyama kutokana na shughuli mbali mbali za kibinadamu. Shughuli hizi ni kama vile uvunaji kupita kiasi na unyonyaji kupita kiasi wa spishi za mimea na wanyama, mbinu haribifu za kilimo na misitu, kuongezeka kwa ukuaji wa miji, athari za kimazingira, mabadiliko ya hali ya hewa duniani na mengineyo.
 • Vile vile bustani hii itatumika kwa ajili ya kufanyia tafiti mbali mbali za kisayansi. Eneo lote la bustani litatumika na watafiti mbalimbali wakiwemo wa mazingira na afya ikiwa ni pamoja na kutumia maabara itakayokuwepo ili kurahisisha ufanisi wa tafiti hizo.
 • Maonyesho ya wanyama, wadudu na bustani za mauwa. Eneo hili litakua na utaratibu maalum wa kuwaruhusu wananchi wasiokuwa wanafunzi kuja kujionea bustani za mauwa, mimea ya dawa, aina mbalimbali za wadudu, wanyama na samaki kwa lengo la kujifunza.
 • Uchunguzi wa vitendo vya kisayansi kwa wanafunzi, watafiti wa kada za afya na mazingira. Eneo la bustani litakua na chumba maalumu cha maabara ya sayansi ambacho kitakua na vifaa vyote vinavyohitajika. Chumba hiki kitatumika kwa ajili ya kufanyia mazoezi ya vitendo kwa wanafunzi huku wakitumia spishi za mimea na wanyama zinazozalishwa hapo hapo.
 • Sehemu ya mapumziko na kivutio cha watalii. Bustani hii itakua ni sehemu ya watu kupumzika hasa siku za sikukuu na mahala penye mandhari nzuri kwa wageni hasa kutokana na uwepo wa bustani za mauwa ya kupendeza yenye rangi za kuvutia, harufu nzuri na aina tofauti za wanyama na wadudu. Hii itachangia pia kuongeza pato la Taifa na kupunguza tatizo la ajira kwa vijana nchini Tanzania.
 • Bustani hii itakua ni sehemu ya uhakika ya upatikanaji wa mimea inayotumika kama dawa za kienyeji (herbal plants). Ukusanyaji wa mimea ya dawa kama vile kivumbasi, mitunguja, michaichai, miarobaini, mirihani, mipatakuva na mengineyo utasaidia kupunguza tatizo la kutoweka kwa dawa za mitishamba.
Bustani hii inaweza kuwa na mkusanyiko wa mimea maalumu ya aina tatu, ambapo kila aina moja katika makundi haya itapandwa sehemu maalum na tofauti na nyengine bila maingiliano. Aina hizo ni kama zifuatazo:
 • Mimea inayotumika kwa ajili ya mitihani maalumu ya vitendo kwa wanafunzi wa shule za Sekondari.
 • Mimea inayotumika kwa ajili ya dawa za kienyeji (herbal plants)
 • Mimea inayotumika kama bustani za mauwa kwa ajili ya urembo na kivutio (flower garden)
Bustani hii ya Botaniki itakua na mkusanyiko maalum wa wanyama na wadudu kama vile mijusi, nyoka, panya, sungura, paka, vyura, tilapia, mende, vipepeo, majongoo, panzi, kima na wengineo.
Mfano wa mchoro wa bustani hii ni kama ufuatao:

1660333432099.png


Kutokana na kuongezeka kwa tishio a kutoweka kwa spishi za wanyama na mimea na kusababisha kupungua kwa mfumo wa ikolojia, hali ambayo pia hupelekea kuwa na uhitaji mkubwa wa spishi za mimea na wanyama kwa ajili ya kufanyia mitihani ya vitendo ya wanafunzi wa kidato cha sita na nne kila ifikapo mwishoni mwa mwaka. Hivyo basi, kuna haja kubwa ya kuanzishwa Bustani ya Botaniki na Zoolojia sehemu yoyote ndani ya Tanzania ili kupunguza tatizo la upotevu wa mimea, wanyama na wadudu hasa wanaotumika katika mitihani ya vitendo ya masomo ya sayansi na mazingira.

Natoa wito kwa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania hasa kwa kushirikiana na Baraza la Mitihani la Taifa (NECTA), wizara ya Elimu, Taasisi za Elimu ya juu pamoja na taasisi binafsi kuwa kuna kila sababu ya kuanzisha bustani ya mimea na wanyama ambayo itakua ndio mkombozi wa uzalishaji wa spishi za wanyama na mimea kwa ajili ya mitihani ya vitendo mashuleni na vyuo vya kada za afya. Hii itapelekea wanafunzi kuzidi kuyapenda masomo ya sayansi kwavile watapata fursa ya kutembelea bustani hii na kufanya mazoezi ya vitendo, hivyo kuongeza ufaulu katika masomo ya sayansi.Imeandikwa na

Mwalimu Seif Mohammed Said
+255774370828
Zanzibar.
 

Attachments

 • 1660333318035.png
  1660333318035.png
  45.4 KB · Views: 4
Upvote 1
1 Reactions
Reply
Top Bottom