Buriani Salim Msoma, msomi makini msomi wa sifa na mjuzi wa Kiingereza kwa kuandika na kuzungumza

Mohamed Said

JF-Expert Member
Nov 2, 2008
15,559
2,000
Salim Msoma kwangu alikuwa kaka, rafiki na pia mwalimu wangu lau kama hili la mwisho naamini hakulijua.

Mimi na yeye tulikuwa tukiandikiana faragha na tukisomana sana katika makala zetu magazetini na kwenye mitandao.

Hapo chini ni barua niliyopokea kutoka kwa Salim Msoma miaka mitano iiyopita akitoa maoni yake kuhusu makala, ''Uchaguzi wa Zanzibar wa Mwaka wa 1961,'' ambamo niliweka nukuu ya Aman Thani akieleza uchaguzi ule jinsi ulivyokuwa.

Wasiomfahamu Salim Msoma ni kuwa Msoma ni katika wanafunzi wasomi makini wa wakati wa mapinduzi ya Afrika miaka ya 1960 kuelekea 1970.

Salim Msoma likuwa mwanachama wa University Students's African Revolutionary Front (USARF) chama ambacho kilianzishwa Chuo Kikuu Cha Dar es Salaam mwaka wa 1967 na wanachama wake walikuja kuacha alama katika historia za ukombozi wa nchi zao kama John Garang na Yoweri Museveni.

Siku moja tukiwa peke yetu Msoma alinidokeza kuwa yeye wakati akiwa mwanafunzi Chuo Kikuu Cha Dar es Salaam alikuwa mmoja wa vijana walioingia Msumbiji kupigana bega kwa bega na FRELIMO dhidi ya Wareno.

Nilipumua kidogo.

Barua hii niliyoitaja hapo juu aliyoniandikia Salim Msoma imekaa Maktaba kama rejea yangu ya kudumu pale nilipotatazika na jambo katika siasa za Zanzibar zinazohusu uchaguzi.

Nakuwekeni hapa barua hii aliyoaniandikia miaka mitano iliyopita ila nanyi mfaidi:

‘’Sheikh Mohamed Said,

Ahsante kwa kutuletea maandishi haya ambayo yanatukumbusha historia ya karibuni ya Zanzibar.

Bila shaka waraka huu umeunakili kutoka kijitabu alokiandika mzee wetu Bw. Amani Thani Fairuz miaka kadha iliyopita na ambacho binafsi nilibahatika kukisoma.

Mimi naomba nitoe maoni ya mawili matatu kuhusu maelezo ya Mzee Amani Thani.

Kwanza nakubaliana nawe kuwa yapo ya kujifunza katika kadhia ya uchaguzi wa Januari na June 1961 Zanzibar khasa tukitilia maanani hali ya kisiasa ilivyo hii leo visiwani.

Lakini ninalotaka kuchangia mimi ni kwamba maelezo ya Mzee Fairuz kama yalivyo maandishi mengine kuhusu mada hii niliyoyasoma yanakuwa na upungufu mmoja.

Nao ni tabia ya kuelezea matukio (facts) bila ya kujadili kwa upana na kutafsiri yaliyo nyuma ya matukio hayo yaani muktadha wake (broad discussion of related issues surrounding the narrated events).

Mfano unapozungumzia suala la kuwepo VITI katika majimbo ya uchaguzi vilivyokuwa vinagombewa na kueleza matokeo ya chama kile kilipata viti kadhaa na kingine kikapata viti zaidi na kushinda bila ya pia kuonyesha TAKWIMU za kura zilizopigwa hakutowi picha sahihi kwa wasomaji kuhusu mfumo mzima wa chaguzi zile.

Hivi leo waandishi mbalimbali wanaeleza na kuonyesha jinsi ukataji wa majimbo (constituencies) ulivyokuwa wa mashaka na hila.

Imebainika majimbo yaliyokuwa na wafuasi wengi wa ASP yalitengewa viti vichache wakati majimbo yalokuwa na watu kidogo wa ZNP yalipewa viti vingi.

Ujanja huu ambao Waingereza wanauwita 'gerrymandering' ndio hatimae uliwapokonya ushindi halali ASP na kutulea mabalaa na maafa visiwani.

Wasomaji lazima waelimishwe kuwa miongoni mwa sababu za kufanyika Mapinduzi Zanzibar ni hili la kunyimwa kwa hila na ujanja haki yao ASP ya kuunda na kuongoza serikali.

Jengine ninalotaka kulieleza kwa mnasaba huu huu wa kujadili mambo badala ya kuyataja tu kijuu juu ni kitendo cha Sheikh Mohamed Shamte kujitoa ASP mwaka 1960.

Bw. Fairuz ameeleza haelewi sababu za Mzee Shamte kujitoa ASP.

Lakini kadri ya muda ulivyopita imebainika wazi kuwa ZPPP kilikuwa ni chama kilichotokana na tawi lililokuwa la Shirazi Association huko Pemba.

Mara zote imekuwa ikitolewa picha potofu kuwa Waswahili wa Zanzibar waliojitambulisha kwa jina la Shirazi Association walikuwa ni kitu kimoja (homogeneous).

Kumbe hali ni tofauti kabisa.

Washirazi wa Pemba na hata baadhi ya wale wa Unguza wamekuwa wakati wakiwemo ndani ya chama cha ASP wakipinga kile walichokihisi ujenzi wa uhusiano wa karibu kati ya ASP na TANU.

Shamte aliwakilisha hisia hizo na alikuwa hamuamini kabisa Julius Kambarage Nyerere kinyume na alivyokuwa Mzee Karume.

Na Mzee Shamte alipohisi huu usuhuba wa Nyerere na Karume unazidi kushamiri ndipo akagombana na Mzee Karume na kuamua kujitoa ASP.

Lakini kuna jambo jengine ambalo ZNP hawakupenda kuliongea.
Nalo ni kwamba huyu Mzee Shamte hapo mwanzoni alikuwa hawaamini pia Waarabu!

Inaelezwa kuwa katika mwaka ule (1959) ambao Mzee Karume kwa shinikizo la PAFMECA alianza kuhutubia mikutano kupitia jukwaa moja na Sheikh Ali Muhsin, Shamte alikuwa ni ‘’diehard,’’ mmoja wapo aliekasirishwa ndani ya ASP.

Cha kustaajabisha ni kumuona mtu yule yule alokuwa akipinga kumuona Karume akiwa pamoja na Ali Muhsin alikuja baadae kuunda Umoja na huyohuyo Ali Muhsin kuanzia uchaguzi wa 1961 na hatimae akapewa Uwaziri Mkuu ndani ya Serikali ya Uhuru 1963!
Haya ndio mambo ambayo waandishi kama Bw Fairuz wanapaswa kuyasema kwa uwazi zaidi.

Wasalam.’’

Huyu ndiye Salim Msoma msomi aliyejiamini kutokana na ukweli alioujua na wala hakuona muhali kuueleza.

Ninazo barua na makala zake nyingine nyingi ambazo kwangu ni ''Masterpiece'' na nimezihifadhi sehemu maalum.

Moja ya barua hizi ni aliyomwandikia Rais Hussein Mwinyi alipochukua uongozi wa Zanzibar kama Rais.

Hii ni barua aliyoniandikia itaishi miaka 100.

Tanzania imepoteza msomi makini ambae wengi walinufaika na fikra zake.

Buriani kaka na rafiki yangu Salim Msoma msomi wa sifa.

Allah amfanyie wepesi safari yake.

Amin.

245173967_1041554096591968_4644165893572051849_n.jpg
 

bagamoyo

JF-Expert Member
Jan 14, 2010
13,575
2,000
Salim Msoma likuwa mwanachama wa University Students's African Revolutionary Front (USARF) chama ambacho kilianzishwa Chuo Kikuu Cha Dar es Salaam mwaka wa 1967 na wanachama wake walikuja kuacha alama katika historia za ukombozi wa nchi zao kama John Garang na Yoweri Museveni.

More info :

University Students' African Revolutionary Front​


University Students' African Revolutionary Front
The University Students' African Revolutionary Front (USARF) was a political student group formed in 1967 at the University of Dar es Salaam in Tanzania. The group, which engaged in study and activism and held regular meetings on Sundays, featured many students who would go on to become influential politicians. USARF was composed of students from Kenya, Zambia, Malawi, Zimbabwe, Ethiopia, Sudan, Tanzania, Uganda and elsewhere in Africa. President of Uganda, Yoweri Museveni was elected its chairman for the whole time he was at university. John Garang, another former USARF member, was the vice-president of Sudan until his death in July 2005. The group identified closely with African liberation movements, especially FRELIMO in Mozambique.
Alumni
Uganda

*Yoweri Museveni
*Eriya Kategaya
*James Wapakhabulo
*Joseph Mulwanyamuli Ssemwogerere
*John Kawangaall
Tanzania
*Charles Kileo
*Salim Msoma
*Adam Marwa
*Patrick Quoro
*Andrew Shija
Malawi
*Kapote Mwakasungura
Sudan
*John Garang
References
* [http://www.statehouse.go.ug/president.php?category=The President Uganda State House website]
 

Uzalendo Wa Kitanzania

JF-Expert Member
Mar 8, 2020
1,169
2,000
"MSOMI WA SIFA NA MJUZI WA KIINGEREZA KWA KUANDIKA NA KUZUNGUMZA"

Mzee Mohamed, unamaanisha kujua kiingereza ni sifa kuu ya Usomi?!
 

Sesten Zakazaka

JF-Expert Member
Sep 10, 2017
10,136
2,000
Sheikh Mohamed,

Huyu Salim Msoma ni ndugu yake Abdulghani Msoma? Yule aliyewahi kua mwalimu/kocha wa vilabu kadhaa vya soka Visiwani na Bara?
 

Mohamed Said

JF-Expert Member
Nov 2, 2008
15,559
2,000
Unatuelimisha sana na Makala zako hapa jukwaani na ndiyo maana baada ya kuzisoma huwa tunaenda kutafuta cha ziada sisi tulio wanafunzi wenye kutaka kujua zaidi baada ya professor Mzee Mohamed Said kutoa lecture hapa jukwaani.
Bagamoyo,
Sote ni wanafunzi nami umenielimisha kwa taarifa hiyo.
 

Teknologist

JF-Expert Member
Oct 20, 2018
1,142
2,000
"MSOMI WA SIFA NA MJUZI WA KIINGEREZA KWA KUANDIKA NA KUZUNGUMZA"

Mzee Mohamed, unamaanisha kujua kiingereza ni sifa kuu ya Usomi?!
Ndiyo, ni sifa kuu ya usomi
unamuuliza kama unabisha au unataka kujua ya kuwa mjuzi wa kiingereza pia ni usomi
Kuna;
Bachelor of Arts (BA) in English
Masters of Arts MA in English
Phd in English

Na pia naamini kuna viwango hivi vya usomi kwa Kiswahili....
 

Nyati dume

JF-Expert Member
May 20, 2021
213
500
Kuna elimu kubwa nimeipata hapo ya kueleza matukio bila kujadili kwa upana na kutafsiri yaliyo nyuma ya matukio hayo.

RIP comrade Msoma.
 

Toa taarifa ya maudhui yasiyofaa!

Kuna taarifa umeiona humu JamiiForums na haifai kubaki mtandaoni?
Fanya hivi...

Umesahau Password au akaunti yako?

Unapata ugumu kuikumbuka akaunti yako? Unakwama kuanzisha akaunti?
Contact us

Top Bottom