Buriani CCM, salamu nyingi kwa KANU, UNIP

BAK

JF-Expert Member
Feb 11, 2007
124,790
288,005
Buriani CCM, salamu nyingi kwa KANU, UNIP

Samson Mwigamba
Tanzania Daima~Sauti ya Watu

TULIFUNDISHWA katika somo la Kiswahili tulipokuwa darasa la tatu wakati huo, kwamba kuna maneno ya aina tatu yanayotumika tunapoagana.

Tukiagana usiku tunapokwenda kulala tunasema, ‘alamsiki'. Ikiwa kuna mmoja au baadhi yetu wanakwenda safari ya kawaida tu isiyo ya hatari sana, tulifundishwa kuagana kwa kusema, ‘kwaheri ya kuonana'. Na kama ni safari ya hatari ambayo haina uhakika wa kurudi mfano kwenda vitani, tunaagana kwa kusema ‘buriani'.

Mwaka 1978, Mzee Mtwale wa Kijiji cha Namhura jimboni Mwibara wilayani Bunda, hakupata nafasi ya kuagana na kijana wake Mugeta aliyekwenda kulipigania taifa lake dhidi ya nduli Idi Amin Dada mpakani mwa Tanzania na Uganda.

Kijana wake alikuwa amehitimu darasa la 14 la wakati huo na wakati vita inatangazwa alikuwa katika Jeshi la Kujenga Taifa (JKT).

Vijana hawa wasomi wa wakati huo, walichukuliwa kwenda kulipigania taifa lao. Alitokea JKT na kwenda vitani bila ya kupata nafasi ya kuagana na baba yake na kusema buriani.

Siku chache baada ya vita, asubuhi moja majira ya saa tano, gari la Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) liliingia nyumbani kwake.

Mzee Mtwale alikuwa akikamua ng'ombe wake asubuhi ile alipoulizwa na askari walioshuka kwenye lile gari ikiwa hapo palikuwa ndipo nyumbani kwa Mzee Mtwale.

Alipojibu ndiyo, bila ya kumung'unya maneno wala kufumba fumba, askari wale wa JWTZ walimweleza kwamba walikuwa wameleta mwili wa marehemu mtoto wake aliyefia vitani.

Mzee aliruka na kuanguka kule wakati kikontena cha maziwa kikianguka huko. Kilikuwa ni kilio kikubwa kwake kumpoteza kijana wake tegemeo.

Nadhani shida kubwa zaidi ni kwamba hakupata nafasi ya kusema ‘buriani' wakati kijana wake akienda vitani. Angeagana naye hivyo, angelitegemea lolote na hata kifo cha mwanawe kingekuwa ni jambo lililotegemewa na yumkini asingepatwa na mshtuko mkubwa kiasi hicho.

Nisingependa wanaCCM yawakute yaliyomkuta mzee huyu. Mwaka 2005 walipoingia vitani hawakujua kwamba safari yao ilikuwa ni ya vita na kwamba uwezekano wa kufia vitani ulikuwa mkubwa na hivyo walitakiwa waage kwa kusema buriani. Walidhani safari yao ilikuwa ya kawaida tu.

CCM walidhani mambo ni yaleyale. Walifikiri safari ni ile ile ya kuwadanganya Watanzania kwa kauli hewa za "maisha bora kwa kila Mtanzania", "Tanzania yenye neema inawezekana", "Ari mpya, nguvu mpya na kasi mpya" kisha ndani ya safari yao ya miaka mitano ikawa "maisha bora zaidi kwa kila fisadi", "Tanzania maskini zaidi inawezekana", "ufisadi mpya kwa staili mpya na viwango vikubwa zaidi". Na baada ya miaka mitano wanakuja na kauli hewa nyingine na kuzoa kura kwa kishindo. Walikuwa wamekosea.

Mwaka 2005 wakati kampeni zikielekea mwishoni mwishoni, tukiwa nyumbani tunajadili na mke wangu majaliwa ya baadaye ya taifa letu, aliniuliza kwamba ni nini hasa kilichowafanya Watanzania wengi kumshabikia Kikwete (mgombea urais kupitia CCM wakati huo), yule yule aliyetoka CCM ile ile iliyoshindwa kuleta maendeleo yale yale kwa miaka 44 ya uhuru?

Na je, Mungu hawaonei Watanzania huruma na kuamua kufanya kitu ili wachaguliwe viongozi wapya wenye mtazamo mpya na wenye nia na uchungu wa dhati wa kuwatoa Watanzania kwenye lindi kubwa la umaskini? Majibu yangu yalikuwa hivi:

"Mungu anawaonea huruma sana Watanzania. Lakini hawezi kulazimisha kuzigeuza nia zao kwa uwezo alio nao. Anaweza tu kuwafunulia wazi hali halisi na kuwaacha wafanye uchaguzi. Wala hatafanya kazi kwa miujiza kama ile aliyoifanya kwa vizazi vya kale ili waamini. Sitegemei kama kuna siku atashusha roho mtakatifu kama alivyofanya siku ya Pentekoste.

Kwamba itokee ghafla siku moja kabla ya kupiga kura na bila kuwapo kwa jambo lolote, viongozi wa vyama vya upinzani wajazwe roho mtakatifu na kuanza kuzungumza kwa lugha ngeni, lakini kila Mtanzania akisikia kwa lugha yake mwenyewe? Kwanba ghafla Freeman Mbowe, Ibrahim Lipumba, Dk. Willibrod Slaa, Hamad Rashid Mohamed, Augustine Mrema, John Cheyo, Zitto Kabwe, Wilfred Lwakatare, James Mbatia, Dk. Sengodo Mvungi, Anna Komu na wengineo wengi wanazungumza kwa lugha ngeni, lakini Wajita wanawasikia wakiongea kwa Kijita, Wasukuma wanasikia wakiongea Kisukuma, Wachaga wanasikia ni Kichaga kinaongewa, Wazaramo nao wanasikia Kizaramo, vivyo hivyo kwa Waha, Wanyakyusa, Wagogo, Wamasai na Waarusha, Wadengereko, Wasambaa, Wangoni, na makabila yote ya Tanzania.

Wote wasikie kwa lugha yao viongozi hawa wa upinzani wakizungumzia uchafu wa chama tawala halafu eti kwa mwujiza huo ndipo sasa wakubali na kuing'oa CCM siku ya uchaguzi. La Hasha! Lakini binafsi naona kitu kimoja ambacho Mungu amekiruhusu kwa kusudi la kuwasaidia Watanzania. Amewaacha waleweshwe na mvinyo ulioandaliwa na wanamtandao, yakiwemo baadhi ya magazeti na kufikia kuamini kwamba Kikwete ni chaguo la Mungu.

Watanzania wamejenga matumaini makubwa juu ya ‘malaika' huyu na hakika hawataamini macho, masikio na fikira zao pale ‘kiumbe' huyu anayeonekana kama kashushwa kutoka juu atakaposimikwa kuwa kiongozi wa taifa hili.

Na ni baada ya yeye kuvurunda, ndipo Watanzania wataamka na kugundua kwamba hakuna ‘chema' kilichosalia ndani ya kapu hili liitwalo CCM.

Na hapo ndipo kifo chake kitakapokuwa kimewadia. Kwangu mimi CCM inapoelekea kushika madaraka ya nchi hii tena, nawaaga kwa kusema ‘buriani' Ni maneno niliyoyasema mwaka 2005 ambayo bado naamini yatatimia. Ni wakati huo kwa mara ya kwanza nilitamka neno ‘buriani' kwa Chama Cha Mapinduzi.

Leo natumia kalamu hii kuwakumbusha wanaCCM wote kwamba walisahau kuaga buriani. Nachelea kusema tusipowakumbusha sasa wataanguka na kuzimia pale chama chao tegemeo kitakapokufa.

Wataruka na kuanguka kule wakati ‘vijikontena' walivyotunza ‘vijisenti' walivyovikamua kwenye EPA, Richmond, Dowans, IPTL na kwingineko vikianguka huko.

WanaCCM, chama chenu kiko taabani. Kinaelekea kule kule ilikokwenda KANU ya Daniel arap Moi, Malawi National Congress ya Kamzu Banda, UNIP (United National Independency Party) ya Kenneth Kaunda, na vinginevyo.

Vipimo vinaonyesha wazi kwamba virusi vya UKIU (Ukosefu wa Kinga ya Ufisadi), vimeenea mwili mzima wa chama kuanzia kichwani (Makao Makuu) hadi nyayoni (kwenye mashina). Napenda niwakumbushe kwamba hapo chama kilipofikia hakuna kinga wala tiba tena labda mjaribu kubadilisha kabisa damu (total blood transfusion) ambapo unaondoa damu yote mwilini yenye virusi na kuweka damu safi.

Hii itamaanisha kuondoa uongozi wote wa chama kuanzia juu hadi chini na kuweka viongozi wapya wanaotoka katika jamii ya kawaida ya wakulima na wafanyakazi ambao hawajaathirika kwa vyovyote na virusi vya ufisadi. Kwa bahati mbaya sana, hii oparesheni haijawahi na haiwezi kufanyika hapa nchini kwa sasa.

CCM ikiwa vitani askari wake wameanza kunyoosheana mitutu ya bunduki na panga zikatazo kuwili. Wamekuwa kama Wafilisti niliowahi kuwazungumzia huko nyuma wakiwa ndani ya kambi yao usiku wakijiandaa na vita dhidi ya Waisrael.

Ghafla wanasikia sauti kubwa ya matarumbeta yapigwayo na Waisrael (wapinzani, wanahabari na wanaharakati mbalimbali) na kushtushwa na miale mikali ya mienge yao ndani ya kambi.

Wafilisti wanadhani Waisrael wameshaingia ndani ya kambi yao na kila mmoja wao anaponyanyuka anadhani yule aliye jirani naye ni Muisrael. Hivyo ananyoosha upanga na kukata kumbe akikata Mfilisti mwenzake hadi wakamalizana.

WanaCCM wanamalizana. Kila anayeshtuka mambo yake yakiwa yameanikwa, anadhani mpinzani ni mwanaCCM mwenzake. Anajibu mapigo kwa kuanika mambo ya yule anayemhisi na hata kupambana naye kwa njia nyingine.

Watashtuka ifikapo asubuhi na kujikuta wamemalizana huku wanamapinduzi wa leo tukitangaza ushindi na kusherehekea kifo cha ‘joka mla watu'.

Hivi sasa wanarusha makombora hata bila kujua wanayaelekeza wapi. Mwulize Anna Abdallah kwamba alikuwa akimwelekezea nani mashambulizi wakati akichangia mjadala wa bajeti bungeni? Mzee Malecela naye juzi aliibuka na kudai kwamba eti kashfa za EPA ziliibuliwa na Dk. Raphael Chegeni, yule Mbunge wa Busega (CCM).

Mara hapo hapo anadai anayestahili sifa ni Rais Kikwete aliyemtimua kazi Gavana aliyekwisha kujiuzulu na kwenda kumficha yeye na hata kifo chake huko Marekani. Rais ambaye hadi leo hataki kuitoa ripoti yote ya wakaguzi wa Ernst & Young kuhusu mabilioni ya EPA, hataki kuwatimua Mwanasheria Mkuu na Mkuu wa TAKUKURU kama alivyoagizwa na Bunge, hataki mafisadi walioiba mabilioni ya EPA watajwe na kukamatwa, hataki ‘mabest' wake waliohusika na kashfa ya Richmond waguswe. Tumsifu kwa lipi? Kwa maoni yangu, hayo yote yalinenwa na wahenga kwamba "mfa maji haachi kutapatapa". Waacheni CCM watapetape, lakini kifo chao ni hakika. Ujumbe kwetu ni mmoja tu, kwamba tuzidishe mashambulizi maana ushindi unakaribia.

Wakati umewadia ambako tutaishuhudia CCM ikiwa ndani ya jeneza lililopakwa rangi ya kijani kibichi. Siku hiyo inakuja mbio na wenye macho msisubiri kuambiwa mtazame. Ila kwa wanaCCM wenyewe hili bado ni fumbo. Hawana habari, wanaendelea kukamua ng'ombe wao madini, misitu, mikataba mibovu, utawala mbovu, ufisadi wa kutisha, na wengineo. Maziwa yanaendelea kuingia vyomboni mwao chururu chururu, si ndo ndo ndo.

Makamanda tunaolibeba jeneza la CCM tusichoke. Twende nalo huko huko Mtera (2010) bila kuchoka. Na tutakapofika wala hatuhitaji lugha ya mafumbo mafumbo (ya kuwanyima wabunge wengi na kuwapa urais) la! Tutawaambia ‘live' kama wale wanajeshi kwamba tumeleta mwili wa marehemu CCM (kuwanyima udiwani, ubunge na urais) aliyefia kwenye vita dhidi ya maisha bora kwa kila Mtanzania.

Hatutajali jinsi mafisadi walioshikilia chuchu za ng'ombe wao akina EPA, Richmond, IPTL na wengine watakavyoruka na kuanguka anguko kuu kuliko lile la Mzee Mtwale. Tutawasaidia kuchimba kaburi na kuizika CCM.

Najua huu utakuwa ujumbe mchungu zaidi kuwahi kutolewa kwa chama hiki kikongwe na wenyewe wakisoma watatamani ‘waikolimbe' kalamu hii isiandike tena. Lakini kalamu hii haiwezi kuuficha ukweli huu. Kiapo chake ni kusema ukweli, tena ‘ukweli uchi' (naked truth) siku zote.

Na wakati mkiwa mmekunja nyuso zenu kwa hasira dhidi ya kalamu hii, yenyewe inawaaga : "Buriani CCM, salamu nyingi kwa KANU, UNIP na wengineo huko mwendako."

smwigamba@yahoo.com
0713 953761
 
what a wishfull thinking!
aisee hapa kazi ni kubwa, kenya pamoja na fujo yote, lakini si unaona mafisadi wao bado wapo tu? wanabadili majina ya vyama na kuendelea.
 
Ni makala iliyosheheni ujuzi mkubwa wa kalamu,ni makala ya kusisimua inayovuta hisia na kukaribisha tumaini lililopotea. kama mwandishi alivyosema hiyo ndiyo naked truth! Nachukizwa kuona masuala mazito ya taifa hili hayatolewi majibu. Hakuna mtu yoyote awaye anayeweza kuyatolea bold statement zaidi ya Jakaya Mrisho Kikwete,asipoyatolea maamuzi maana yake ni kukitia kitanzi chama cha mapinduzi.binafsi nisingefurahi kuona CCM ikipatwa na yale yaliyowakuta UNIP,KANU na MNC lakini kama hatua mahsusi hazitachukuliwa sasa (wakati wa ku-act ni sasa) basi nachelea kukubaliana na mwandishi huyu kwamba hiyo ndiyo itakuwa-fate ya chama cha mapinduzi.JK do something kukinusuru chama,historia isije ikakuhukumu kama ulivyowaambia wazee wa Dar es Salaam baada ya EL kujiuzulu.
 
Nafikiri ni ujumbe Mzuri sana ambao unatuelekeza kuitimisha chama cha mapinduzi kilichokufuru kwa kila hari na mali ndani ya nchi yetu. Nafikiri wananchi tuko tayari kukipeleka kitakapotaka tukizike, hila ningeomba kiandike usia.

Hapa kimefikishwa na Jemedari wetu Rais mpendwa sana JK ambaye ameweka historia kabambe ya kushindwa kufukuza MAFISADI badala yake ameweka mkakati madhubuti ya kuwasafisha. Nafikiri watanzania tuna akiri za kutosha hivyo ni matumaini yetu kuwa ama chama kitose mafisadi wanaokichafua au kikubali kizikwe na mafisadi wakiwa ndani yake.

Nina uhakika mafisadi hawatakaa wakasimama walikofikia panatosha.
 
Mazingaombwe CCM, utabiri wa Nyerere waja

Evarist Chahali, Uskochi Juni 25, 2008
Raia Mwema~Muungwana ni Vitendo

NIANZE makala hii kwa kuvishukuru vyombo kadhaa vya habari vya kielektroniki (radio na televisheni) ambavyo kila asubuhi vinatusomea vichwa vya habari vya magazeti ya siku husika.

Kwa wengi wetu, utaratibu huo unatusaidia sana kufanya maamuzi ya gazeti lipi la kununua siku hiyo na si kupoteza fedha ya ngama kununua gazeti ambalo kila wiki linahangaika kuwasafisha mafisadi.

Hata hivyo, pamoja na utaratibu huo mzuri wa vyombo hivyo vya habari, bado kuna tatizo kwa baadhi ya watangazaji ambao huwa na wakati mgumu kutafsiri vichwa vya habari vya magazeti ya Kiingereza.

Sawa, hii ni lugha ya kigeni na wenye kuimudu ni wachache. Zaidi, kwa sie tunaoishi kwenye chimbuko la lugha hiyo, yaani Uingereza, tunashuhudia baadhi ya wenyewe wanavyoiboronga kama ambavyo baadhi ya wenzetu wanavyokuwa na wakati mgumu kuongea lugha yetu ya Taifa. Lakini kwa nini watangazaji wanaoelewa kwamba kimombo ni mgogoro kwao wasiombe kufanyiwa tafsiri sahihi ya vichwa hivyo vya habari mapema kabla ya kujiadhiri "laivu" kwa wasikilizaji wao? Uzembe wa aina hii unapaswa kukomeshwa mara moja.

Lakini pengine uzembe huu unachangiwa na hadhira ya vyombo hivyo vya habari. Hivi inaingia akilini kweli kuona takriban kila kituo cha runinga kinajibidisha kuonyesha tamthilia fulani ambazo wahusika wanazungumza Kispaniola halafu tunasikilizishwa maneno ya Kiingereza? Hivi kweli hakuna tamthilia nzuri zaidi ambazo wahusika wanazungumza Kiingereza, kwa mfano, na hivyo mtazamaji haiishii kuona midomo ikikinzana na maneno yanayotamkwa na waigizaji husika?

Nadhani ili kuondokana na maudhi ya aina hii kuna umuhimu kwa wasanii wetu kujitahidi kutengeneza tamthilia za Kiswahili zitakazoonyeshwa kila siku mithili ya Isidingo.



33.jpg

MBUNGE Peter Serukamba

Baada ya angalizo hilo, napenda kuonyesha mshangao wangu kwa Watanzania hawa: Peter Serukamba, Alhaji Adam Kimbisa na mkongwe Kingunge Ngombale Mwiru. Kwa mujibu wa vyombo mbalimbali vya habari, wanasiasa hawa na wengineo walisimama kidete katika kikao kilichopita cha NEC ya CCM huko Dodoma kuwatetea watuhumiwa wa ufisadi.

Kabla ya kujiingiza kwenye siasa,Alhaji Kimbisa alikuwa kiongozi wa chama cha Msalaba Mwekundu, ambacho kinafahamika kwa jitihada zake za kuokoa maisha kwa wahanga wa majanga kama njaa, mafuriko, kimbunga, vita, nk. Alipoingia kwenye siasa niliamini kabisa kwamba angeendelea na ile spirit ya kuwasaidia wahanga ambayo ndiyo sifa kuu ya Red Cross.

Kwa mantiki hiyohiyo, nilitarajia mwanasiasa huyu angekuwa mstari wa mbele kama akina Anne Kilango kutetea maisha wa Watanzania wenzake yanayohatarishwa na mafisadi.

Nadhani Mheshimiwa Serukamba alipokuwa akitetea watuhumiwa wa ufisadi hakuwa anawakilisha mawazo ya maelfu ya wana-Kigoma waliomtuma akatetee maslahi yao. Ni kweli kwamba itapofika mwaka 2010 Watanzania wataiuliza CCM pamoja na mambo mengine, kuhusu maji, barabara na maisha bora, lakini kwa hakika hawatasahau kuuliza kwa herufi kubwa kwa nini chama hicho kimeendelea kuwalea watuhumiwa wa ufisadi kana kwamba hiyo ndiyo sera yake kuu?

Serukamba anapaswa kufahamu kwamba mengi ya matatizo yanayolikabili jimbo lake na maeneo mengine ya nchi ni matokeo ya ushenzi wa wanaharamu wachache wasio na uchungu na nchi wanaotafuna utajiri na raslimali za Taifa kwa ulafi mkubwa. Hawa si watu wa kutetewa hata kidogo na laiti kama Edward Sokoine angekuwa hai, basi wangekuwa magerezani kwa tuhuma za uhujumu wa uchumi.

34.jpg

Kingunge


Kuna wakati huwa napata shida kuamini kuwa Mzee Kingunge wa sasa ni yuleyule aliyekuwa swahiba wa Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere, mwanasiasa ambaye hadi mauti yanamkuta alipambana kwa nguvu zake zote dhidi ya unyonyaji, ukandamizaji na uwezekano wa kuwapo jamii yenye wachache wanaokula na kusaza huku wenzao wakiwa hawana uhakika wa japo mlo wa siku moja.

Kama Kingunge huyu ndiye yuleyule aliyekuwa karibu na Nyerere basi angekuwa mstari wa mbele kutaka hatua kali zichukuliwe dhidi ya mafisadi badala ya kuwatetea au kukaa kimya .

Tatizo kubwa la siasa za Afrika ni kuendesha mambo kiushikaji kana kwamba nchi ni kijiwe fulani cha kahawa. CCM inafahamu bayana kwamba Watanzania wamechoshwa kuona nchi yao inatafunwa na mchwa wachache ambao nadhani wanapaswa kuchunguzwa na Idara ya Uhamiaji kufahamu kama ni wazawa halisi wa nchi hii kwani matendo yao yanafanana kabisa na maadui wa nje wa ustawi wa Taifa.

CCM inaweza kuwadanganya Watanzania wachache kwa muda fulani kwamba tuhuma za ufisadi dhidi ya baadhi ya viongozi wake ni uzushi tu. Inaweza pia kuwadanganya Watanzania wote kwa muda fulani kwamba masuala ya Richmond, EPA na maskandali mengine ni porojo tu za kisiasa. Lakini kamwe haiwezi kuwadanganya Watanzania wote kwa muda wote kwamba chama hicho si kichaka kinacholea mafisadi, maana isingekuwa hivyo basi kisingeruhusu watu kama (Mwanasheria Mkuu) Johnston Mwanyika na (Mkurugenzi mkuu wa TAKUKURU) Edward Hosea waliotajwa bayana kuwa na mapungufu yaliyosaidia kufanikiwa kwa ujambazi uliofanywa na matapeli wa Richmond wakabidhiwe jukumu la kuchunguza wizi wa EPA .

Na wala haiwezi kuudanganya umma wa Watanzania kwamba waliolazimika kujiuzulu kutokana na kuhusishwa kwao na utapeli wa Kampuni ya Richmond walifanya hivyo kulinda maslahi ya Taifa. CCM isiwafanye Watanzania ni wajinga kiasi hicho wakati wanakumbuka vizuri jitihada zilizokuwa zikifanyika kila vilipojiri vikao vya Bunge kuhakikisha kuwa suala la Richmond halijadiliwi katika chombo hicho cha kutunga sheria?

Wakati fulani nilipata fursa ya kuzungumza na mzee mmoja anayezijua vyema siasa za nchi hii na alinifahamisha kwamba unapoona watu wazima waliokabidhiwa dhamana ya kuwakilisha wananchi wanafikia hatua ya kuumbuana hadharani basi ni dhahiri kwamba kuna matatizo makubwa ndani ya chombo kinachowaunganisha.

Unajua laiti baadhi ya vikao vya CCM vingekuwa vinaonyeshwa laivu, watayarishaji wa michezo ya kuigiza wangepata washiriki lukuki wa kuunda ze komedi kadhaa kwani katika vikao hivyo mambo mengi ni ya nyodo, ubabaishaji, vijembe, wajumbe wa Zanzibar kumaka wanaposkia Mwenyekiti kataja umeme, na mazingaombwe mengine.

Japo wenyewe CCM wanajigamba kwamba ni magwiji wa demokrasia, kiasi kwamba si ajabu kwa kiongozi mmoja kusema hili na mwingine akatamka lile, tunayoshuhudia hivi sasa ndani ya chama hicho kikongwe ni dalili kwamba kimeishiwa na mbinu za kuwatumikia waliokikabidhi dhamana ya kuwaongoza.

Nidhamu ndani ya chama hicho imeshuka zaidi ya ilivyo kwenye vijiwe vya karata tatu. Ukiona watu wenye akili timamu wanatishiana maisha kwa vile tu baadhi yao wanajikomba kwa mafisadi huku wengine wakikumbuka wajibu wao kwa taifa lao basi ujue utabiri wa Nyerere kwamba upinzani wa kweli utazaliwa kutoka ndani ya CCM yenyewe unakaribia kutimia.

Zamani tulisikia kuna makundi ya wanamtandao na wasio-wanamtandao. Baadaye tukasikia kuna wanamtandao-maslahi na wanamtandao-upuuzi-gani-sijui. Sasa tunashuhudia wana-CCM wanaokumbatia mafisadi na wana-CCM walioamua liwalo na liwe lakini lazima kieleweke kwa mafisadi kuadabishwa na hatimaye nchi kunusurika.

Nimeona kwenye gazeti moja kwamba kuna jitihada za kuwadhibiti akina Kilango, Aloyce Kimaro. Tatizo ni kwamba hao ni wawakilishi tu wa mamilioni ya Watanzania wenye mawazo kama yao. Kuwadhibiti hao wachache hakutaweza kuwa salama ya mafisadi kwani tayari wazalendo hao wameshazaa "Vilango" au "Vimaro" lukuki wasio tayari kuzibwa midomo kwa kisingizio cha kujenga mshikamano ndani ya chama huku wananchi wakiteseka.



Barua-pepe: epgc2@yahoo.co.uk
Blogu: http://chahali.blogspot.com
 

Similar Discussions

Back
Top Bottom