Buriani Captain Malik, "Encyclopedia" ya historia ya mpira wa Tanzania

Mohamed Said

JF-Expert Member
Nov 2, 2008
20,900
30,235
CAPTAIN MALIK ENCYCLOPEDIA YA HISTORIA YA MPIRA WA TANZANIA

Jina lake ni Captain Malik na Mji mzima wa Dar es Salaam ukimjua kwa majina yake haya mawili.

Hii ilikuwa Encyclopedia ya historia ya mpira wa Tanzania.

Leo Kamusi Kubwa hii imefunga kurasa zake na hazitafunguka tena.

Zimebaki kumbukumbu.

Captain Malik kafariki leo nyumbani kwake Mtoni.

Hatuna pa kwenda kuuliza ni kwa kiasi gani Asante Kotoko ilikuwa inaiogopa Yanga au kwa nini Hamisi Kibunzi na Arthur Mambeta wakipendeza sana pale katikati ya uwanja wakati wa Sunderland (Underline) na kule Yanga (Kuala Lumpur) Abdulrahmani Juma na Mohamed Msomali walikuwa makini zaidi wanapocheza na wachezaji hawa.

Au kwa nini Celebic akiwaamini sana Athmani Kilambo na Mohamed Chuma kuzuia mashambulizi ya kina Jonathan Niva wa Kenya na John Kadu wa Uganda wakati wa Gossage Cup kuelekea Challenge Cup.

Captain Malik ni mtu maarufu sana kwa watu wa Dar es Salaam hasa wa kizazi cha miaka ya 1950 nyuma kidogo na mbele kidogo ya hapo.

Captain Malik yuko katika orodha yangu ya watu ambao nimefahamiana nao na wamenishangaza kwa akili zao nyingi walizojaaiwa na Allah kiasi kuwa unapozungumza nao haukuchukui muda kutambua kuwa huyu si mtu wa kawaida ambae unaekutana nae Karikaoo kila uchao.

Mara moja akili yako inatambua kuwa huyu ni mtu mwenye kipaji ambacho si cha kawaida. Katika orodha hii yangu nitawataja wachache na nawataja kwa kuwa tayari wameshatangulia mbele ya haki – Peter Colmore, Jim Bailey, hawa ni Wazungu Colmore ni Mkenya mwenye asili ya Kiingereza, na Bailey ni Kaburu wa Afrika Kusini na mwingine ni Sheikh Ali Muhsin Barwani, Mzanzibari.

Kaka yangu Captain Malik leo kifo chake kimemungiza ndani ya orodha yangu hii.

Captain Malik katika ujana wake miaka ya mwishoni 1950 na kuanzia 1960 alikuwa akicheza mpira Young Africans ya Dar es Salaam akiwa nahodha na hapo ndipo alipopata jina lake hili la ‘’Captain,’’ ambalo limemganda hadi anaondoka duniani.

Captain Malik ananiitikadi mimi kama mdogo wake nami siku zote amekuwa kaka yangu na kwa kweli si mimi tu, sisi wengi tuliokulia Kariakoo tunamuheshimu Captain Malik kama kaka yetu mkubwa.

Iko siku nimemkuta Capatain Malik katika kizingiti cha Msikiti wa Manyema baada ya Sala ya Alasiri anavaa viatu aondoke. Baada ya mazungumzo nikamuomba nimpige picha na akanikubalia na ndiyo hiyo picha hapo juu. Nina picha nyingi sana nimempiga Captain Malik wala hazina idadi. Huyu kwangu alikuwa mtu ‘’special,’’ akili kubwa sana.

Captain Malik Allah amempa kile Wazungu wanakiita, ‘’Photographic Memory,’’ yaani kipaji cha kukumbuka kwa usahihi kabisa kila kile ambacho jicho lake limeona kuanzia tarehe, majina, mahali na yote yaliyokuwapo kwa wakati ule.

Athmani Kilambo alikuwa mchezaji wa Yanga na pia timu ya taifa ya miaka ya mwanzoni 1960 akicheza nafasi yoyote ya ulinzi na alitokea Bagamoyo akiwa kijana mdogo labda miaka 20 hivi.

Captain Malik ndiye aliyempokea Yanga na kumkabidhi jezi kucheza mechi yake ya kwanza Ilala Stadium. Huu ukaja kupelekea usuhuba mkubwa baina yao uliodumu nusu karne hadi alipokufa Kilambo.

Mimi nimemfahamu Kilambo tayari keshakuwa mchezaji maarufu kabisa akijulikana ndani na nje ya Tanganyika wakati ule, mchezaji mwenye umbo kubwa lakini mwepesi na hodari wa ‘’sliding tackles,’ kiasi akiwamudu vilivyo wachezaji wakali wa enzi zile.

Kilambo alipatapo kunambia siku moja kuwa yeye wagomvi wake walikuwa wachezaji wa Kenya hasa Wajaluo kwa kuwa wakitumia nguvu sana katika uchezaji wao.

Kilambo anasema Kocha wao wa timu ya taifa ya Tanganyika Myugoslavia Celebic akijua mchezo wa Kenya wa kutumia nguvu na alikuwa katika Gossage Cup akimpanga Kilambo beki wa kulia na Mohamed Chuma beki wa kushoto na hawa wote walikuwa, ‘’hard tacklers,’’ wana uwezo mkubwa sana wa kupambanisha chuma kwa chuma. Kilambo anasema washambuliaji wa Kenya wakiwaogopa sana wao.

Turudi kwa Captain Malik.

Captain Malik siku moja kanichekesha sana kiasi cha kutokwa na machozi. Anasema siku hizo Kilambo mgeni Dar es Salaam na Yanga bado hajawa, ‘’senior player,’’ bahati mbaya timu imeingia uwanjani Ilala Stadium yeye kachelewa na alipofika lango kuu askari wakakataa kumpitisha ingawa aliwaambia kuwa yeye ni mchezaji wa Yanga.

Ikabidi Captain Malik afatwe ndani ili aje langu kuu kumtambua Kilambo na kumuingiza ndani awahi kuvaa jezi na kuingia uwanjani. Captain Malik anasema kamkuta Kilambo nje pembeni katoa macho kajikunyata hajui nini la kufanya.

Captain Malik ni ‘’Encyclopedia,’’ ya historia ya mpira Afrika ya Mashariki na hasa Tanzania.

Ana hazina kubwa sana ya historia na matokeo muhimu ya mchezo huu ndani ya Yanga, Simba wakati ule ikiitwa Sunderland, Cosmopolitan na club ndogo za mjini kama African Temeke Good Hope, Liverpool, Kahe Republic, Rover Fire na nyingine nyingi za mitaani.

Siku zote kila fursa ilipotokea niliandika kuwa Itafaa sana kama Tanzania Football Federation (TFF) watafute muda wazungumze na Captain Malik wapate historia za viongozi wa mpira waliopita kama marehemu Kitwana Ibrahim. kiongozi wa Yanga maarufu sana Kondo Kipwata, Patron wa Simba Habib Segumba akijulikana kama ‘’Underline,’’ au manahodha waliopita wa timu ya taifa kama Captain Ayub Mohamed, au ‘’strikers’’ wa kutisha kama Yusuf Mwamba au wachezaji waliocheza timu ya taifa katika umri mdogo sana kama Hemed Mzee, mchawi wa chenga, Mbwana Abushiri akijulikana kama ‘’Director,’’ wapigaji penalty na ‘’free kicks,’’ waliokuwa wakiogopewa kama Hemed Seif, magolikipa hodari wa ‘’diving,’’ kama Kitwana ‘’Popat’’ kabla hajaacha kuccheza golini na kwenda kucheza mbele na kuwa mshambuliaji hodari na Hatibu Mtoto.

Picha hii Kitwana yuko hewani ilipigwa na ikatoka katika magazeti yote.

likuwa picha nzuri sana ya ‘’action.’’ Captain Malik anayajua yote haya na katika uhodari wake atakupangia timu yote ya Kenya na Tanganyika kutoka kichwani. Nilitaka TFF imtafute Captain Malik awarithishe hazina yake na faida kubwa sana ya kumbukumbu ingekuwa imehifadhiwa. Lakini ajizi nyumba ya njaa.

Captain Malik alikuwa na mengi katika suala la uchawi katika mpira katika enzi zao, ‘’Benchi la Ufundi,’’ na atakupa na majina ya ''mafundi'' wenyewe na walikokuwa wakiwatoa na nini walikuwa wakifanya.

Captain Malik atakupa na majina ya vijana waliokuwa wakitumwa kufanikisha mambo haya kabla ya mechi kubwa ya Simba na Yanga labda jana yake usiku wa kuamkia mechi na siku ya mechi wakati timu zinajitayarisha kuingia uwanjani.

Miaka ile Kariakoo walikuwa wakiishi wenyewe wenyeji, bado hawajahama kuyapisha maghorofa. Siku ya meshi ya Yanga na Simba pale Mnadani. Mtaa wa Mafia na Msimbazi washabiki wa timu hizi watawasha vitezo na kuchoma ubani toka asubuhi na bendera zinakuwa zimepandisshwa za Yanga na Simba zikipigwa na moshi wa ubani.

Captain Malik atakutajia hadi majina ya hawa washabiki wakubwa wa sifa. Hali ya mji inakuwa imebadilika toka asubuhi washabiki wa Mnadani wanashambuliana kwa maneno makali makali ya kuvunjana nguvu kuwa nani atatoka mshindi jioni ile.

Wakati ule mechi hizi zinachezwa Ilala Stadium. Captain Malik atakupa majina ya wakata tiketi wa Ilala Stadium.Kwa leo ukitazama unajiuliza watu wailiweza vipi kuenea uwanja mdogo kama ule. Captain Malik kayashuhudia haya yote kwa macho yake na si kama mchezea pembeni bali akiwa amevaa rangi za Yanga kama mchezaji.

Buriani kaka yetu Captain Malik umeondoka na historia yako umetuacha masikini tukibakia na kumbukumbu zako siku ulizokuwa ukitupandisha mori na simulizi zaoko ambazo hatukuchoka kuzisikiiza.

Allah akufanyie wepesi katika hii safari yako.

Amin.

image_2020-11-11_205206.png
 
Pole sana Mohamed kwa msiba huu. Enzi zake pia kulikuwa na mchezaji mwingine mahiri akiitwa CHENJA; huyu alikuwa askari polisi! Chenja alikuwa wa Temeke sio Kariakoo!
 
Pole sana Mohamed kwa msiba huu. Enzi zake pia kulikuwa na mchezaji mwingine mahiri akiitwa CHENJA; huyu alikuwa askari polisi!! Chenja alikuwa wa Temeke sio Kariakoo!
Bulesi,
Ahsante sana.
 
Na wewe mzee wangu ALLAH amekujaalia kipaji kikubwa sana cha uandishi. Aina ya uandishi wako inavutia na haichoshi.

Uwe pole kwa msiba.

ALLAH amjaalie kauli thabiti marehemu.

Sisi sote ni wa ALLAH nasi kwake tutarejea.
 
Hivi hakuna namna serikali zetu zikawa na taratibu ya kuwafaa hawa watu ambao waliliwakilisha vyema taifa?
 
Pole sana Mohamed kwa msiba huu. Enzi zake pia kulikuwa na mchezaji mwingine mahiri akiitwa CHENJA; huyu alikuwa askari polisi!! Chenja alikuwa wa Temeke sio Kariakoo!!!
Nafuu hujamtaja majina yake ya kwanza, kwakuwa kama ni Mkristo utagombana na huyu Mzee sasa hivi.

Ndio maana hapo majina ya kikristo aliyoyataja ni ya hao wazungu wawili tu.

Means Tanganyika haikuwa na mchezaji Mkristo wakati huo hata mmoja kote Simba na Yanga?

Mkiwa mnamsoma huyu Mzee inawapasa kuijua sababu ya kupost, Mimi nilishamsoma saikolojia yake katika mada zake huyu Mnafiki.

Kuna ujumbe alikuwa anatoa hapa kinafiki

Pia kuweni makini na Uongo alio nao.
 
Nafuu hujamtaja majina yake ya kwanza, kwakuwa kama ni Mkristo utagombana na huyu Mzee sasa hivi.

Ndio maana hapo majina ya kikristo aliyoyataja ni ya hao wazungu wawili tu.

Means Tanganyika haikuwa na mchezaji Mkristo wakati huo hata mmoja kote Simba na Yanga?

Mkiwa mnamsoma huyu Mzee inawapasa kuijua sababu ya kupost, Mimi nilishamsoma saikolojia yake katika mada zake huyu Mnafiki.

Kuna ujumbe alikuwa anatoa hapa kinafiki

Pia kuweni makini na Uongo alio nao.
Huyo anatoa historia ya mji wa dsm ambao wakazi wake kiasili ni wa pwani ambao majority ni waislamu siyo ajabu kutokuwa na watu wa dini zingine,
 
Back
Top Bottom