Buriani Ali Abdul Mufuruki, Mhandisi mwenye mapito mengi kwenye Biashara

Zitto

Former MP Kigoma Urban
Mar 2, 2007
1,562
10,880
Buriani Mzee Ali Abdul Mufuruki, Mhandisi Mwenye Mapito Mengi Kwenye Biashara

“Zitto mnahitaji mgombea Urais anayeijua sekta binafsi vizuri asaidie kuijenga Tanzania, ongea na Ali Mufuruki agombee Urais” yalikuwa maneno kutoka kwa mmoja wa rafiki zangu, mwaka Jana katikati ya sakata la zao la Korosho. Nikamjibu kuwa Ali hawezi kukubali. Yeye ni Mfanyabiashara. Hata hivyo katika mazungumzo mbali mbali na watu wangu wa karibu Ali amekuwa akiibuliwa.

Nakumbuka tulipopewa changamoto ya kuunda Baraza la Mawaziri linaloweza kuendesha Nchi CCM ikiondoka madarakani, Ali Mufuruki tumekuwa tukimtaja kama Waziri wa Fedha. Hivi ndio namna Ali Mufuruki amekuwa akijadiliwa pengine bila hata yeye mwenyewe kujua kuwa alikuwa akijadiliwa. Siku moja nilipokutana naye Nairobi, nikamchokoza hilo la Urais, akacheka sana. Akaniambia hayo ni mambo ya wengine. Mimi Mfanyabiashara na ninasaidia nchi kupitia Biashara.

Ali Abdul Mufuruki ametangulia mbele ya Haki. Kwa wengi wetu ni msiba wa ghafla kwani hivi karibuni ameonekana akiendelea na shughuli zake kama kawaida. Mara ya mwisho nimemwona katika mjadala alioufanya AzamTV akiwa vizuri tu (kwa macho ya mwanaadamu). Hata hivyo sisi sote ni wake Allah na kwake tutarejea. Ali ametangulia kwa Mola wetu na Leo Watanzania wanamuaga kwa heshima zote anazostahili.

Mwaka 2019 umekuwa mwaka wa majonzi sana. Wafanyabiashara wakubwa wawili nchini wamefariki bila kumsahau ndugu Ruge Mutahaba ambaye naye kwa hakika alikuwa katika’ligi’ za Ali na Mzee Mengi Lakini kwa namna yake ya kukuza vipaji na kujenga himaya ya Habari na Burudani. Ali Mufuruki sio tu alikuwa Mfanyabiashara bali alikuwa Mfanyabiashara Mtanzania ambaye njia yake ni mafunzo makubwa sana kwa wengi.

Ninaamini kuwa Ali ameacha mapito yake kwenye maandishi na hivyo Watu wengi na hasa kizazi kijacho wataweza kujifunza kutoka kwake. Septemba 30, 2019 Ali aliniandika ujumbe wa simu kuwa “nina mradi wa Kitabu changu na nataka nitulie kuhakikisha kuwa ninamaliza kitabu hiki ifikapo mwakani”. Allah alikuwa na mipango yake amemchukua kabla ya mwaka kuisha. Nataraji familia itaweza kumaliza mradi huu ili vizazi vimsome Ali na mapito yake mpaka kuwa Mfanyabiashara mkubwa nchini na mtu mwenye heshima tele.

Hata hivyo Ali alikuwa na maono ya mbali na ameandika maono yake hayo kwenye Kitabu chake (pamoja na wenzake) kuhusu Viwanda. Kitabu hicho “Tanzania’s Industrialisation Journey 2016-2056:

From an Agrarian to a Modern Industrialized State in 40 Years” kina mawazo mazuri sana ya kuisaidia nchi yetu kutoka hapa ilipo na kuwa Taifa lenye maendeleo ya Watu wake.

Mapitio ya Kitabu hicho yaliyofanywa na Andrew Coulson ( https://ceo-roundtable.co.tz/wp-content/uploads/2018/08/Tz-Industrialisation-Book-Review.pdf ) yanakupa ufupisho mzuri sana wa Kitabu hicho. Ali alikuwa anapigia chepuo TANZANIA kuwa Dola la Maendeleo (developmental state) na hasa umuhimu wa Tume ya Mipango ya Taifa. Bahati mbaya sana Serikali ya Awamu ya Tano imevunja Tume ya Mipango.

Ni nadra sana hapa Tanzania na labda Afrika nzima Mfanyabiashara kama Ali Mufuruki kusisitiza umuhimu wa utamaduni wa Taifa katika kile alichoita ‘National Exceptionalism‘ ikiwemo mavazi, chakula, historia yetu, ushairi nk. Ali anaona utamaduni ni zaidi ya kutambulisha nchi, ni Biashara. Wakati nadurusu hotuba ya Mwalimu Nyerere ya Desemba 10, 1962 nilikuta anavyosisitiza kuhusu Utamaduni wa Taifa alipokuwa anaeleza sababu za kuunda Wizara ya Utamaduni. Miaka 55 baadaye Ali Mufuruki, Mfanyabiashara sio Mwanasiasa, aliandika kukumbusha namna Utamaduni ni Mali. Bahati mbaya sana hatukumsikiliza Mwalimu Nyerere na sidhani kama tumemsikiliza Ali Mufuruki. Muhimu ni kuwa wote wameandika.

Nimesoma andiko la shahada ya Uzamivu la Chambi Chachage ambamo Ali Mufuruki amezungumzwa katika Sura ya Tano na Sita. Chambi ameeleza kwa ufasaha sana kukua kwa Ali Mufuruki kama Mfanyabiashara kuanzia chini kabisa mpaka mafanikio aliyoyapata. Natamani sana Chambi azalishe Eneo hili kama makala kwa Umma badala ya andiko la kitaaluma. Watanzania na Waafrika watajifunza jambo kubwa sana kutoka kwa Ali.

Kwamba Ali alikuwa mtumishi wa Shirika la Umma liitwalo NECO (Shirika la Uhandisi la Taifa), baada ya kutoka masomoni Ujerumani, akaamua kustaafu akiwa na miaka 30 tu na kuanzisha kampuni yake binafsi mwaka 1988 nchi ikiwa na Uchumi hodhi wa dola, huo ni ujasiri ambao wengi wetu hatuna. Kwamba aliweza kupenya katika ushindani wa Biashara ya teknolojia mpaka kupanua Biashara kwenye maeneo mengine kama maduka ya nguo na majengo hadi kuwa utajiri wake ni simulizi yenye mafunzo makubwa.

Ali ameacha mchango Mkubwa sana kwa Tanzania haswa kwa Shirika letu la Ndege , ATCL. Ali alipoingia Kama Mwenyekiti wa Bodi wa ATCL mwaka 2002 Nchi yetu ilimiliki 51% ya Hisa za Shirika, lakini alipotoka mwaka 2007 Nchi yetu ilimiliki 100% ya Hisa za ATCL. Pamoja na kuwa kinara wa Sekta Binafsi nchini, Ali aliona Ubinafsishaji wa ATCL ulishindwa kulifufua Shirika hilo, hivyo aliamua kulirudisha limilikiwe na umma, Japo alipinga namna ATCL inayomilikiwa kwa 100% na umma namna inavyoendeshwa, kwa kuwa aliona uendeshaji husika hautaongeza tija na ubunifu, na ungeturudisha kwenye matatizo yaliyopelekea ATCL ibinafsishwe. Ushauri wake hatujausikiliza.

Kitendo chake hiki akiwa Mwenyekiti wa Bodi ya ATCL ni ishara ya imani yake ya “Dola la Kimaendeleo la Tanzania”, na kwamba tunapaswa kurekebisha mapungufu ya Ubinafsishaji nchini, maoni ambayo pia Rais Mkapa (ambaye Ubinafsishaji ulifanyika chini yake) ameyatoa kwenye kitabu chake kilichotoka karibuni.

Nikiwa Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Mahesabu moja ya kazi niliyokutana nayo ilikuwa ni kurejesha heshima ya Benki Kuu baada ya ufisadi mkubwa wa EPA. Gavana Ndulu alifanya kazi kwa karibu nami katika kuhakikisha Bunge linasaidia kuzuia EPA nyengine kutokea. Wakati huo wote Ali alikuwa kwenye Bodi ya Benki Kuu. Mara kadhaa nilipokutana naye amekuwa akiniambia namna kipindi kile tulisaidia BoT kutimiza wajibu wake. Waliofaidika na EPA walikuwa mstari wa mbele kutaka Ndulu ashindwe kazi, PAC haikukubali na Ali alikuwa msaada mkubwa kwangu katika changamoto hii. Ali alitumikia Benki Kuu kwa weledi wa hali ya juu sana.

Maisha ya Ali ni mafunzo. Namna alivyoshirikiana na Mkewe, Bi Saada Ibrahim katika kukuza Biashara zao ni ushuhuda wa namna Ali alivyoishi na kuthamini nafasi ya Mwanamke katika Jamii. Ni Mfano bora kwetu tuliobaki duniani.

Mungu ampe Subira Saada na watoto katika wakati huu mgumu sana kwao

Mola amlaze Pema Ali Abdul Mufuruki

Kabwe Z. Ruyagwa Zitto

Kiongozi wa Chama, ACT Wazalendo

Disemba 10, 2019
 
Wakati mnamwagia sifa wekeni hapa pia alifanya nini, achievements zake kibiashara kwa nchi, kwanza ningependa kujua aliajiri Watanzania wangapi, pili alichangia kwa kiasi maendeleo ya TZ kama Mfanyabiashara?

Nilichokiona kuna watu wanapenda sana kujikweza klk uhalisia, mbona akina Bakhresa, Dewji, Patel wameajiri maelfu ya Watanzania na wanachangia kiasi kikubwa sana Uchumi wa Tanzania lkn hawajikwezi kila mahali?

Binafsi sijawahi kukutana na Mtanzania aliyeajiriwa na Mufuruki lkn nakumbana na wengi kila siku wanaofanya kazi Azam industries au Dewji.

Mswahili akipata kidogo matako hulia mbwata!
 
Marehemu Ali alikuwa na ndoto ya kuwa mwenyekiti wa sekta binafsi, lakini nafaisi ilipo patikana mwaka 2018, alifuatwa na Sembeye kuombwa kugombea nafasi hiyo AKAKATAA NA KUSEMA SIO SASA NINA MAMBO MENGINE YA KUFANYA kauli hii kaongea Simbeye kwa uchungu sana mpaka amelia.

Lazima kuna kitu Ali alimwambia hasa kwa kuwa utawala wa awamu hii umeamua kuwatesa matajiri, akaona asiwe sehemu ya kuwafanya waishi kama mashetani, maskini Ali alijua sekta inaenda kufa na hakutaka imfie yeye. Halafu mtu anaandika amesikitishwa sana na kifo cha mtu alietaka awe shetani. Unafiki.
 
Barbarosa, Mufuruki ni kati ya Watanzania wachache walioweza kuweka chachu ya kimawazo katika jamii. Kubadilisha mawazo ya watu kunaweza kuwa muhimu kuliko kuajiri watu.

Kwa mfano, wakati vijana wengi "wasomi" walipokuwa wamejikita kutafuta kazi za ofisini, huku wakiacha fursa za biashara kwa sababu ni kazi zilizo chini ya hadhi zao, Mufuruki aliwaasa kuachana na usomi wa kufa na tai shingoni wakati fursa za biashara kuchakalika zipo.

Yeye mwenyewe kama mtu aliyesomea Uinjinia na kujikuta kawa mfanyabiashara ni mfano.

Tulihitaji kusikia maneno hayo kutoka kwa mfanyabiashara maarufu.

Mfanyabiashara mwenye biashara kubwa anaweza kulipa kodi kubwa na kuajiri watu wachache wenye mishahara mizuri, wakati mfanyabiashara mwenye biashara ndogo anaweza kuajiri watu wengi bila mshahara na alipe kodi ndogo.
 
Nilisoma andiko lake moja ambalo Ally alikua anapinga bomoabomoa ya nyumba za mabondeni.

Alidadavua ni namna gani binadamu anatakiwa kuishi na maji na kuonesha mifano namna ya wenzetu wanavo fanya ku-deal na tatizo la maji, ambalo huwasumbua sana walalahoi. Nilimpendaje!

Inna lilah wa inna illah rajuhun.
 
Mufuruki ni kati ya Watanzania wachache walioweza kuweka chachu ya kimawazo katika jamii. Kubadikisha mawazo ya watu kunaweza kuwa muhimu kuliko kuajiri watu.

Kwa mfano, wakati vijanabwengi "wasomi" walipokuwa wamejikita kutafuta kazi za ofisini, huku wakiacha fursa za biashara jwa sababu ni kazi zilizo chininya hadhi zao, Mufuruki aliwaasa kuachana na usomi wa kufa na tai shingoni wakati fursa za biashara kuchakalika zipo.

Yeye mwenyewe kama mtu aliyesomea Uinjinia na kujikuta kawa mfanyabiashara ni mfano.

Tulihitaji kusikia maneno hayo kutoka kwa mfanyabiashara maarufu.

Mfanyabiashara mwenye biashara kubwa anaweza kulipa kodi kubwa na kuajiri watu wachache wenye mishahara mizuri, wakati mfanyabiashara mwenye biashara ndogo anaweza kuajiri watu wengi bila mshahara na alipe kodi ndogo.

Unataka kuniambia Marehemu Ally hakuwahi kuajiliwa kwenye maisha yake?

Kama amewahi kukaa kwenye hii mifumo yetu basi kuwa tajiri sio kazi kubwa sana na wala sio issue.

Hatuwezi kuwaambia vijana wa kitanzania wakajiajiri huku asilimia kubwa wanaosema maneno hayo mitaji yao wameipata baada ya kuajiliwa na kukaa kwenye system kwa miaka mingi..
 
Wakati mnamwagia sifa wekeni hapa pia alifanya nini, achievements zake kibiashara kwa nchi, kwanza ningependa kujua aliajiri Watanzania wangapi, pili alichangia kwa kiasi maendeleo ya TZ kama Mfanyabiashara? Nilichokiona kuna watu wanapenda sana kujikweza klk uhalisia, mbona akina Bakhresa, Dewji, Patel wameajiri maelfu ya Watanzania na wanachangia kiasi kikubwa sana Uchumi wa Tanzania lkn hawajikwezi kila mahali?
Binafsi sijawahi kukutana na Mtanzania aliyeajiriwa na Mufuruki lkn nakumbana na wengi kila siku wanaofanya kazi Azam industries au Dewji.

Mswahili akipata kidogo matako hulia mbwata!
Wewe kwako watu wa maana ni wahindi na Waarabu, tulishakudharau siku nyingi Mhindi koko wewe!
 
Neno la chuki kwa namna hiyo ni kimbilio la mtu asiye na hoja.

Wenye kusikia wote wamesikia Jiwe alisema malaika wataishi kama shetani.

Jiwe kaipa familia yangu nyumba ya serikali iliyokadiriwa kuwa ya dola milioni tatu Oysterbay.

Hicho ndicho alichonifanya Jiwe.

Siandiki kwa chuki, naandika kwa principle.
Mimi sio mgeni kwa huo uandishi wako, naamini kuna jambo la chini ya kapeti ambalo wadau humu jukwaani hawalifahamu.

Huwa unatumia maneno fulani yanayozidi mtazamo wa principle, yanakuwa makali sana.
 
Back
Top Bottom