Burian Balozi mgosi Raphael Haji Lukindo: Alimkosoa hadi Sokoine mbele ya JK Nyerere, ni imara kweli | JamiiForums | The Home of Great Thinkers

Dismiss Notice
You are browsing this site as a guest. It takes 2 minutes to CREATE AN ACCOUNT and less than 1 minute to LOGIN

Burian Balozi mgosi Raphael Haji Lukindo: Alimkosoa hadi Sokoine mbele ya JK Nyerere, ni imara kweli

Discussion in 'Jukwaa la Siasa' started by nngu007, Apr 6, 2012.

 1. nngu007

  nngu007 JF-Expert Member

  #1
  Apr 6, 2012
  Joined: Aug 2, 2010
  Messages: 15,871
  Likes Received: 57
  Trophy Points: 145
  [h=1][/h]
  Godfrey Dilunga
  [​IMG]


  Balozi wa kweli, kipenzi cha Azimio la Arusha  BAADA ya kifo cha Mzee Rashidi Kawawa, aliyepata kuwa Balozi wa Tanzania nchini India, Dk. Ahmed Kiwanuka, Januari 13, mwaka 2010, aliandika tanzia kwenye gazeti hili toleo namba 116, akielezea uadilifu wa Mzee Kawawa.


  Dk. Kiwanuka aliandika; “Maisha ya Mzee Kawawa ni kielelezo cha mtu mwaminifu sana na mwadilifu wa hali ya juu. Uaminifu wake ulikuwa si kwa Baba wa Taifa tu, bali kwa Watanzania na Chama cha Mapinduzi.”

  Nami, kwa kuzingatia nilivyomfahamu (kidogo) Balozi Lukindo, kwa maelezo yake binafsi katika mahojiano yetu yaliyochapishwa kwenye gazeti hili Novemba, 2009, naye pia “maisha yake ni kielelezo cha mtu mwaminifu sana na mwadilifu wa hali ya juu.”


  Wakati fulani, Balozi Lukindo alifika kunitembelea katika Ofisi za Raia Mwema, zilizopo Millenium Business Park, Shekilango, Dar es Salaam.


  Wakati mwingine, alinipigia simu kupongeza makala zangu hasa zenye kupigania uzalendo miongoni mwa Watanzania. Kila nilipopokea simu yake, neno la utanimgosi lilitangulia mazungumzo yetu yaliyokuwa yakitawaliwa kwa hoja nzito kuhusu mustakabali wa taifa. Yeye ni mwenyeji wa Tanga.


  Kwangu, ya kujifunza kutoka kwa Balozi Lukindi aliyefariki Machi 27, 2012 katika Hospitali ya Saisee, India, ni mengi kuanzia mikasa na hata mafanikio yake kazini. Hivyo basi, ingawa mgosi Balozi Lukindo ametangulia, lakini hakuniacha hivi hivi katika safari yangu hii hapa duniani.


  Hata mbele ya kaburi lake, naweza kusimama na kutamka; fair but firmakanielewa na kwa miujiza ya Mwenyezi Mungu, pengine humo humo kaburini akatikisa kichwa kama ishara ya kukumbuka maneno hayo aliyopata kunieleza.


  Fair but firm
  ni maneno ambayo sitaweza kuyasahau maishani mwangu kutoka kwa Balozi Lukindo.


  Ilikuwa mwaka 1960, mgosi Lukindo alipoanza kazi ofisi za wakoloni (kabla ya Uhuru). Siku moja, mkoloni mmoja alimweleza (baada ya kuajiriwa); wewe ni mpole sana, sasa uwe mkali. Naye akamjibu; siwezi kuwa mkali bila sababu.


  Akaendelea kumjibu; jambo (muhimu) kubwa ni mtu kutumia haki na uwe madhubuti...kwa Kiigereza fair but firm (FBF).


  Huu ni ujumbe kwa viongozi, wazee kwa vijana na wananchi kwa ujumla, tutende haki tukibaki madhubuti.


  Ni ujumbe mzito hasa kwa viongozi wa kitaifa, ambao wengi, kama wako fair(watoa haki) basi hawako firm (madhubuti) na kama wako firm, hawako fair.


  Kwangu, Balozi Lukindo ameniachia kanuni mpya ya maisha; fair but firm. Lakini Balozi Lukindo ni nani? Kwa ufupi, hakuwa mwanasiasa. Alikuwa mwanadiplomasia makini, mtetezi wa Azimio la Arusha, mwadilifu na muungwana. Kubwa zaidi, alikuwa Mcha Mungu.  Mgosi
  huyu hakuwa mwanasiasa
  Alinieleza katika mahojiano yetu Novemba 2009; “Mimi si mwanasiasa, ingawa kazi nilizowahi kufanya zinaingiliana na siasa.”


  Hakupenda siasa na alinieleza kwa nini. Akasema, kuingia kwenye siasa kama ubunge au waziri haya sipendi, kwa sababu utalazimika kujihusisha na kundi fulani na lazima uunge mkono masuala fulani ya chama chako au kundi lako bila kujali ni sahihi au ni ya makosa.


  “Haya ya kuunga mkono uamuzi wa pamoja hata kama kuna makosa ndiyo unaonitia wasiwasi sana,” kwa hiyo, mgosi hakuwa mwanasiasa na alinieleza, hana kadi ya chama chochote cha siasa.  Alivyokumbuka mkasa wake na Sokoine
  Balozi Lukindo hakuwa mwoga kutoa ushauri hata kama unakinzana na ‘wakubwa’ kiutawala. Hakuwa mnafiki dhidi ya ukweli.


  Alinieleza siku moja walikuwa katika kujadili kuagiza farasi, yeye akiwa Mkurugenzi wa Maendeleo ya Mkoa (RDD) Rukwa.


  Wakiwa katika mkutano na Mwalimu Nyerere Ikulu, Mwalimu akasema (kwa kuchomokea) kwa sababu ya taabu ya usafiri huko mikoani, labda tufanye kwamba mkuu wa mkoa au mkuu wa wilaya ajue kupanda farasi.


  Balozi Lukindo anasema Mwalimu alizungumza kama tahadhari tu, lakini Waziri Mkuu Edward Sokoine baadaye akachukua hilo kama agizo.


  Sokoine akaagiza farasi waletwe Tanzania kutoka Australia, Balozi Lukindo akapinga na kushauri mambo kadhaa. Akasema, farasi ni mnyama anayehitaji maandalizi na matunzo, kwa hiyo wajiandae kwa hayo kwanza. Lakini wenzake wakampinga (akina Kolimba).


  Upinzani ulikuwa mkali dhidi yake, kiasi cha mwenendo wake kiuongozi kutiliwa shaka. Hatimaye farasi wakaagizwa, lakini walikufa kwa kukosekana maandalizi. Huyo ndiye Balozi Lukindo, mzalendo asiyeficha ukweli.


  Siku alipokataa ubalozi

  Aliwahi kunieleza namna alivyoukataa ubalozi ili arudi nyumbani kufanya kazi nyingine.

  Alinieleza; “Nilipokuwa Balozi kule Roma, Italia, mwaka 1974 wengi walidhani Mwalimu Nyerere ameniadhibu kwa kunirejesha nyumbani na kuwa RDD, kwamba kutoka ubalozini nimepangiwa kazi kijijini.


  “Kinyume chake mimi ndiye niliyeomba kurudi nyumbani. Kimsingi, maisha mazuri ya balozi ughaibuni yanatokana na kodi za Watanzania, wakulima wa jembe la mkono na wafanyakazi, kuna tatizo gani mimi kurudi kuwatumikia?


  Namna ilivyokuwa Moscow 1970

  Aliendelea kunieleza; “Ilikuwa mwaka 1970, Marehemu Mloka alipita nilipokuwa Balozi Moscow, nikamwomba nirudishwe nyumbani, akasema sawa.

  Lakini haikuwa hivyo, badala yake nikapelekwa Roma. Nilikuwa Balozi wa kwanza kufungua ofisi ya ubalozi Rome, mwaka 1971.


  Nilipouliza kwa nini sikurudishwa nyumbani nikajibiwa; hatukukurudisha kwa sababu ni mzoefu wa masuala ya ubalozi, kaa huko huko.


  Ilikuwa vigumu kwangu, nilikuwa naona uchungu kwamba kuna ulazima wa kuja kuwatumikia wananchi vijijini, kushirikiana nao kwenye shida na juhudi zao. Hili ndilo lililokuwa linanisumbua.


  Kazi ya Balozi niliizoea na nilitaka kuwa katika mazingira mengine na nimezoea kuishi mazingira yoyote ya maisha bila kuogopa. Kwa kweli nikwambie ukweli tu kilichonituma na kunichoma moyo wangu hadi nihangaike kurejea nyumbani ni Azimio la Arusha.


  Liko kwenye akili yangu kabisa Azimio la Arusha. Mwalimu alipoelekeza watu vijijini, sasa waweze kupata hamasa na wafikie maendeleo nikajiuliza mimi nitawezaje kusaidia kitu hicho?


  Mwalimu ashangazwa, amkubalia

  Hakuweza kukata tamaa na juhudi zake za kutaka arudishwe nyumbani (Tanzania). alinieleza; “Nilipoona Foreign (Wizara ya Mambo ya Nje) hawanisaidii (kurudi), ilipofika Juni 1974 niliandika barua personally kwenda kwa Mwalimu nakala wizarani, Waziri wa Mambo ya Nje akiwa John Malecela.

  Nasikia Mwalimu alishangaa sana na akawa anajiuliza; balozi anataka kurudi nyumbani? Balozi gani huyu? Lakini mwishowe nilirudi nyumbani, Mwalimu aliniruhusu, nikapigiwa simu kurudi.


  Ni kweli, mwadilifu na mnyenyekevu

  Alizidi kunieleza hali ilivyokuwa katika kurudi kwake Tanzania.

  “Niliporudi tu nilipangiwa Mwanza (RDD) baada ya mwaka nikahamishiwa Rukwa, wakati wananiaga Mwanza, Mwenyekiti wa Chama wa Mkoa (Budodi) alitoa taarifa akisema amekaa na watumishi wa chama na serikali miaka yote hii, na hajawahi kufanya kazi na kuaga mtu ambaye amefikia kiwango cha uadilifu na kufuata miiko ya uongozi kama mimi Raphael Lukindo.


  Nikiwa Chief Protocal, kazi kubwa ni kutengeneza skeleton program halafu nakwenda Msasani, si kweli Mwalimu alikuwa haambiliki, ukimwelesha anakuelewa, wakati fulani nilikuwa nabishana naye kitaalamu kuhusu programu na ikibidi alifuta mawazo yake au mimi kufuta yangu na hivyo kurekebisha programu.


  Mkasa akiwa ubalozini Moscow

  Kutetea nchi ni jambo nililokuwa nalithamini sana. Siku moja kulikuwa na hafla ya mabalozi Urusi. Tulikuwa mabalozi mbalimbali wa nchi za Afrika, tumesimama, tunakunywa na kuzungumza mawili matatu.

  Balozi wa Nigeria wakati ule alikuwa mwanajeshi wa cheo cha kapteni, kwenye Jeshi la Anga la nchi yao. Katika mazungumzo, akawa anamkashifu Rais wa Sierra Leon, Rais gani, anaunga mkono kujitenga kwa Jimbo la Biafra, nilishindwa kumvumilia nikamwambia, unawezaje kumkashifu Rais wa nchi ya Afrika?


  Basi akanigeukia mimi, akamshambulia Nyerere hana shukurani, tulimsaidia katika uasi wa wanajeshi mwaka 1964 lakini hana shukurani anaunga mkono kujitenga kwa Biafra. Alinitibua sana nikawa namfuata kumshambulia, utashangaa yeye ni kapteni wa Jeshi la mimi si mwanajeshi, sikujali hayo.


  Niliona amevuka mipaka, nikamvaa hivyo hivyo anamkashifu Rais wetu? Lakini kwa bahati nzuri alikuwapo Balozi wa Zambia, Paul Saka akatuambia jamani acheni, ilikuwa kati ya 1969 na 1970.


  Niliwahi kukataa kumpa mkono Balozi wa Ureno kwenye sherehe ya kumsalimu Rais wa Italia, Petin. Nilitoa mkono kumsalimu balozi mwenzangu baadaya kujitambulisha, lakini alipojitambulisha ni Balozi wa Ureno tu, nilirudisha mkono wangu. Tanzania ilikuwa inapinga utawala wa Ureno nchini Msumbiji.


  Naam, huyu ndiye mgosi Balozi Lukindo, kipenzi cha Azimio la Arusha, muungwana na mwadilifu. Mshauri asiyechoka na ambaye, siku za miaka ya mwisho ya uhai wake alikuwa akiumia sana na matendo ya ufisadi miongoni mwa viongozi wa kitaifa. Tulimpenda, lakini Mungu amempenda zaidi. Mwanga wa milele umuangazie ee bwana, apumzike kwa amani-ameni.
   
 2. nngu007

  nngu007 JF-Expert Member

  #2
  Apr 6, 2012
  Joined: Aug 2, 2010
  Messages: 15,871
  Likes Received: 57
  Trophy Points: 145
  Kweli, hatuna wanasiasa kama hawa siku hizi, ni imara, hawatikisiki, wanamielekeo ya maana; ndio maana nchi yetu haikuyumba pamoja na umasikini tuliokuwa nao
   
Loading...