Bungeni kwawaka moto, ripoti za kamati zaibua mjadala mkali!

Arusha Mambo

Senior Member
Jan 27, 2011
174
150
Wabunge wameanza kikao cha Jioni kujadili taarifa za Kamati tatu za Bunge, Kamati ya Hesabu za Serekali, Mashirika ya Umma na Serekali za Mitaa. Jumla ya Wabunge 51 wameomba kuchangia.
================================

KATIKA hatua isiyokuwa ya kawaida, Mbunge wa Mbozi Mashariki, Godfrey Zambi (CCM) amesema Chama Cha Mapinduzi (CCM) kinaweza kuanguka katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015, kutokana na kukithiri kwa vitendo vya ubadhilifu wa mali ya umma serikalini.

Zambi alikwenda mbali zaidi na kudai kuwa anashangaa kwa nini Waziri Mkulo bado yuko ofisini licha ya tuhuma nzito zinazomkabili.
Zambi aliyekuwa akichangia hoja ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali, alisema ubadhirifu wa kutisha uliofanywa na Wizara ya Fedha na taasisi nyingine za serikali unakiweka rehani chama hicho katika Uchaguzi Mkuu ujao na akadai hatashangaa kikishindwa.

Kauli ya mbunge huyo ilionekana kuwashitua baadhi ya wabunge wa CCM, lakini ikapokewa kwa shangwe kubwa na wabunge wa upinzani.
Zambi aliungana na Mbunge mpya wa Arumeru Mashariki, Joshua Nassari, ambaye alionesha kushangazwa kwake na utendaji wa serikali ambayo imekaa kimya ikiwaachia mafisadi kupora mali ya umma bila kuchukuliwa hatua zozote za kisheria.

Mbunge huyo alidai kuwa ni jambo la kushangaza kuwa hadi sasa Waziri Mkulo bado yuko ofisini pamoja na tuhuma nzito zinazomkabili.
Akizungumza kwa kujiamini, Zambi alisema Wizara ya Fedha inanuka ubadhirifu na kutaja hatua ya Ofisi ya Mhasibu Mkuu wa Serikali kutumia kiasi cha sh bilioni 49 bila kuwepo kwa maelezo ya kueleweka.

Mkulo ambaye jana aliwashangaza wabunge baada ya kushindwa kuhudhuria kikao cha Bunge cha jioni, huku akitambua kuwa hoja iliyokuwa ikijadiliwa inamhusu, alianza kushambuliwa kwa tuhuma nzito za kulihujumu Shirika Hodhi la Mali ya Umma (CHC) kwa masilahi yake binafsi.
Mbunge wa Mwibara, Kange Lugora (CCM), akichangia taarifa za Kamati ya Bunge inayosimamia fedha za umma alimtuhumu Waziri Mkulo kwa kuingilia utendaji wa shirika hilo kwa masilahi yake binafsi.

"Waziri Mkulo aliingilia CHC katika uuzaji wa Plot namba 10 ya Mohamed Enterprises. Mkurungenzi wa CHC alikataa. Pia aliingilia uuzaji wa Tanzania Motors Company kwa Murad Sadic lililokuwa liuzwe kwa sh bil. 3.9, Katibu Mkuu, Ramadhani Kijjah alifanya mazungumzo na kuidhinisha malipo kwa sh milioni 900," alisema mbunge huyo.

Aliongeza kuwa kutokana na ubadhirifu huo, Mkulo aliwasilisha azimio bungeni la kutaka shirika hilo kufutwa, ili kuficha madhambi aliyoyafanya.

"Alimsimamisha kazi Mkurugenzi Mkuu wa CHC na kuvunja bodi ili kuficha madhambi aliyofanya na kisha kurudi bungeni na kusema wabunge wanaoitetea CHC wamehongwa.

"Zitto aliweka rehani ubunge wake na kumtaka Mkulo kuthibitisha madai hayo na kumtaka naye kuweka rehani uwaziri wake. Namtaka Waziri Mkulo afute hoja hiyo na kumsafisha Zitto," alisema na kuongeza kuwa Wizara ya Fedha inaangamiza nchi.

Zitto, Nyerere wailipua TANESCO, TBS

Wabunge, Zitto Kabwe (Kigoma Kaskazini - CHADEMA) na Vincent Nyerere (Musoma Mjini - CHADEMA), jana waliwalipua watendaji wa mashirika mawili ya umma kwa tuhuma nzito za ubadhirifu wa mabilioni ya fedha za Kitanzania.
Ufisadi huo uliibuliwa jana na Zitto wakati alipokuwa akiwasilisha taarira ya Kamati ya Bunge ya Hesabu za Mashirika ya Umma (POAC), kwa mwaka wa fedha unaoishia Juni 30, 2010 ambapo alisema kuwa katika hali ya kushangaza, watendaji wa TANESCO walifanya manunuzi ya sh bilioni 600 kinyume cha sheria.

Zitto alisema fedha zilizotumiwa na shirika hilo ni nyingi, hivyo, ametaka hatua za kisheria zichukuliwe dhidi ya TANESCO na mashirika mengine yaliyolisababishia taifa hasara kubwa.
"Mifano ya wazi kuhusu upotevu wa fedha za umma kutokana ama na kutozingatiwa kwa sheria za manunuzi ya umma inaweza kuelezwa kwa ufasaha katika mashirika mengi yaliyojihusisha na vitendo hivyo," alisema.

Mbali na kulishukia shirika hilo la umeme nchini, Zitto na kamati yake imeagiza kuwakamata na kuwafikisha mahakamani maofisa wa serikali walioingia mkataba wa ukodishaji wa ndege ya ATCL, Air Bus 420-214, mwaka 2007.

Zitto alisema ukodishaji huo wa ndege ni wa kutatanisha na uliojaa upungufu mkubwa ambao utaitia serikali hasara kubwa.
Alisema kamati ilibaini kuwa maofisa kadhaa wa shirika na serikali waliingia katika mkataba wa kukodisha ndege huku wakijua kuwa ingehitajika kwenda katika matengenezo nchini Ufaransa baada ya muda mfupi tangu itakapoanza kazi.
Alisema utata mwingine ni namna dhamana ya serikali ilivyotolewa, akibainisha kuwa Msajili wa Hazina kwa niaba ya serikali alitoa dhamana kwa ATCL mwaka 2007, ili ikodi ndege aina ya Air Bus 420-214 kutoka Kampuni ya Wallis Trading ya Lebanon kwa muda wa miaka sita, wakati dhamana ilitolewa mwaka uliofuata.

"Kamati ilikagua na kujiridhisha namna mchakato huo ulivyofanywa na kubaini mapungufu makubwa kuwa ukodishaji wa ndege hiyo ulifanywa Oktoba, 2007, wakati dhamana ya serikali kwa ATCL ilitolewa Aprili, 2008," alisema.
Alisema ni wazi ndege hiyo ilikodiwa kabla ya kutolewa dhamana ya serikali wakati ni kinyume cha sheria inayosimamia utoaji wa dhamana za mikopo serikalini.

"Mkataba uliingiwa kinyume na ushauri wa wataalamu ambao katika taarifa yao walisema si sahihi kukodi ndege ambayo baada ya miezi sita itatakiwa kwenda Ufaransa kwa matengenezo makubwa, kamati ilibaini kuwa walioingia mkataba huo walijua ndege hiyo italazimika kufanyiwa matengenezo," alisema.

Nyerere afichua madudu mengine ya TBS
Kwa upande wake, Mbunge wa Musoma Mjini, Vincent Nyerere (CHADEMA), ameibua ufisadi mwingine mzito unaodaiwa kufanyika katika Shirika la Viwango Tanzania (TBS).

Akiuliza swali bungeni jana, Nyerere aliibua na tuhuma nzito akidai kuwa baadhi ya vigogo wa serikali na wale wa TBS wana uhusiano na kampuni saba zinazofanya ukaguzi wa magari nchini.
Alisema anao ushahidi wa kutosha na yupo tayari kuutoa iwapo wahusika watakuwa tayari kujiuzulu.
Nyerere ambaye kauli yake ilizua hali ya kutotulia kwa baadhi ya watendaji wa serikali, baadaye alizitaja kampuni hizo kuwa ni JK Jabal Kilimanjaro (Sharjah UAE), WTN-Utility Service ya UK, EAA ya Japan, Total Automative-Dubai UAE, Quality Garage-Hong Kong na Sime Darby-Hong Kong.

Alisema Septemba 25, 2007, vigogo hao wa serikali walifanya kikao katika hoteli moja maarufu jijini Dar es Salaam na kugawana kampuni bila kuzingatia sheria ya manunuzi ya mwaka 2004.
Shutuma hizo zilisababisha mawaziri wa viwanda kujichanganya katika majibu yao, kiasi cha kumlazimisha Mbunge wa Mwibara, Kange Lugora (CCM) kutaka mwongozo wa Spika.

Lugora alifanya hivyo, baada ya jibu la Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara, Lazaro Nyalandu aliyedai kuwa ripoti ya Mkaguzi wa Hesabu za Serikali (CAG) kuhusu suala hilo ipo wizarani na wahusika watachukuliwa hatua.
Wakati akijibu hivyo, juzi Waziri wa Viwanda na Biashara, Cyril Chami aliliambia Bunge kuwa ripoti hiyo ilikuwa bado haijakamilika.
"Juzi Waziri wa Viwanda alipokuwa akijibu swali linalofanana na hilo alisema bado ripoti haijakamilika, lakini leo Naibu Waziri, Lazaro Nyarandu anasema kuwa ripoti hiyo imeshatoka. Sasa hapa nashindwa kuelewa kati ya Waziri na Naibu Waziri nani anasema kweli?" alihoji Lugora.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu na Bunge), William Lukuvi, alisema Ofisi ya Waziri Mkuu itakusanya maelezo yote kuhusiana na suala hilo na baadaye kutoa taarifa bungeni.

"Tunaomba kupatiwa muda ili tuweze kukusanya maelezo yote na baadaye tutatoa taarifa bungeni," alisema.
Hata hivyo, majibu ya mawaziri hao yalizidi kuwakoroga wabunge, ambapo Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe, alisema suala hilo liliundiwa kamati maalumu na kulifanyia kazi kwa miezi minane.
"Tumeshakamilisha kazi hiyo na tumekabidhi taarifa kwa Spika ambaye pia amekabidhi ripoti hiyo kwa Waziri Mkuu. Tunachosubiri ni kwa serikali kutoa taarifa ya utekelezaji wa suala hilo ili liweze kumalizika," alisema Zitto ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Hesabu za Mashirika ya Umma.

Chami, Nyalandu wahaha
Majibu ya Zitto yalionekana kuwasha moto kwa wabunge wengi, ambapo baada ya kauli hiyo, Waziri Chami aliitwa na Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, ambaye alizungumza naye kwa takriban dakika saba huku Bunge likiwa linaendelea.

Wakati hayo yakiendelea Mbunge wa Ludewa, Deo Filikunjombe ambaye ni Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Mashirika ya Umma (POAC) alionekana akiteta na Lugora ambaye ndiye aliyeibua mjadala huo, kabla ya kwenda kwa Waziri Nyalandu na kuteta naye kwa dakika kadhaa.
Vincent Nyerere naye aliinuka na kwenda kwa Waziri Lukuvi na kuzungumza naye kwa muda.
Lugora kwa upande wake alieleza kushangazwa kuendelea kuwapo kwa shirika hilo huku bidhaa zilizopo chini ya kiwango kuendelea kuingizwa nchini.

"TBS mnasubiri nini? Watanzania wanakufa kutokana na kuingizwa kwa matairi yasiyo ya viwango, mafuta yanachakachuliwa, inawezekana hata ile ndege ya ATC iliyoanguka ilitokana na mafuta kuchakachuliwa. Mungu atuepushe na ndege ya rais isije ikawekwa mafuta ya kuchakachuliwa," alisema.

Aidha, alisema walikwenda Hong Kong kukagua kampuni zinazodaiwa kukagua magari kabla ya kuingizwa nchini, lakini kampuni hizo zilikuwa hewa.
Alisema katika wizara hiyo wabunge wa kamati ya Bunge walitumia fedha za umma na kusema kuwa alikasirika na kutamani kumpiga ngumi Mkurugenzi Mkuu wa TBS, Charles Ekelege.

"Vitendo vya Wizara ya Viwanda na Biashara vinaonyesha kumlinda Ekelege. Alikiri kutudanganya kuwapo kwa kampuni hizo Hong Kong, lakini hakuna hatua zozote alizochukuliwa," alisema.
Katika hatua nyingine, Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali, John Cheyo, alisema kamati hiyo imebaini Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii, kutumia sh bilioni 1.1 katika maonyesho ya kimataifa kama Nanenane, Sabasaba na Utumishi.
Alisema fedha hizo zilitumika katika mwaka 2009/2010 na kwamba matumizi hayo hayakuwapo katika bajeti iliyopitishwa na serikali.

Joshua Nassari aunguruma

Naye Mbunge mpya wa Arumeru Mashariki, Joshua Nassari (CHADEMA) jana alimshambulia Waziri wa Fedha, Mustafa Mkulo kwa kuondoka bungeni wakati wa mjadala mzito wa ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali.
Akichangia kwa mara ya kwanza tangu kuchaguliwa kwake, Nassari akionekana kutokuwa mgeni kabisa na vikao vya Bunge, alisema Waziri Mkulo ameonesha kutojali mambo mazito ya ubadhirifu wa fedha na ndiyo maana hakuwa ndani ya Bunge, lakini juzi wakati wa kuchagua wabunge wa Afrika Mashariki alikuwapo.

Nassari ambaye kwanza alimshukuru Mungu kwa kumjalia kuwemo katika Bunge hilo, aliianika serikali alipodai kuwa inamiliki magari yenye thamani ya sh trilioni tano, huku ikishindwa kununua magari ya wagonjwa katika hospitali zake.
Alisema kuwa katika kilele cha ubadhirifu, baadhi ya viongozi wa serikali wamekuwa wakipandisha bei ya manunuzi ya magari hayo huko Japan, kwa kuwa kuna tofauti kubwa kati ya bei anayonunua mtu binafsi na ile ya serikali.

Mdee ataka Chavda akamatwe
Akichangia ripoti hiyo, Mbunge wa Kawe Halima Mdee (CHADEMA) aliitaka serikali kumkamata na kumfikisha mahakamani, mfanyabiashara aliyemtaja kwa jina moja la Chavda anayetuhumiwa kuchota fedha benki kwa kuweka dhamana mashamba aliyokodishwa na serikali na kisha kuyatelekeza.
Akizungumza kwa uchungu, Mdee alisema kuwa mawaziri wengi wamekuwa wakifanya uzembe wakijua kuwa hakuna hatua zozote watakazochukuliwa.
Aliwataka wabunge bila kujali itikadi za kisiasa kuchukua hatua za kinidhamu na kuwawajibisha mawaziri wote ambao wamefanya uzembe uliosababisha taifa kuingia katika hasara kubwa. Mjadala kuhusiana na ripoti hiyo unatarajiwa kuhitimishwa leo.

Chanzo:Tanzania daima
 
Mjadala umepamba moto, wabunge wamechachamaa, serikali haifanyi ipasavyo. Tune TBC.
 
Duh! Kumbe Madiwani huwa wanalipwa Sh 4000 kwasiku akiwa kikaoni! Ngoja niendelee kubangaiza.
 
Tatizo wakitoka kwenye hilo jengo wote kimyaaaaaaaa!!!!!!!!
Wanabaki wabunge wa CHADEMA wanahaha na harakati za kuwasaidia wananchi
 
halmashauri zetu wanatafuna pesa za walipa kodi kwa miradi hewa. Mishahara hewa ni miradi yao pia. Mungu twaomba utunusuru.
 
Aisee hii kali! Yaani gari la halmashauri ya wilaya serikali imelifanyia matengenezo kwa garama ya shilingi milioni 11 halafu jamaa akajiuzia gari hilo kwa shilingi milioni moja na nusu???:shock:
 
Aisee hii kali! Yaani gari la halmashauri ya wilaya serikali imelifanyia matengenezo kwa garama ya shilingi milioni 11 halafu jamaa akajiuzia gari hilo kwa shilingi milioni moja na nusu???:shock:
Mkuu unashanga mbona kuna kiongozi pale General Tyre (Arusha)alijiuzia gari kwa US$ 100
 
safi sana nawapata vema kuna mbunge anamwaga nondo kuhusu uuzwaji wa majengo kwa mohamed enterprises nk sijajua ni nani huyu.
 
Back
Top Bottom