Bunge letu si bunge tukufu

BAK

JF-Expert Member
Feb 11, 2007
124,792
287,994
Haramu!?

Waungwana,

Kama tunavyofahamu bunge letu linajulikana kama ni bunge tukufu la Tanzania. Kwa maoni yangu ukipitia maamuzi mengi ndani ya bunge hili sioni utukufu wowote wa kustahili kuliita bunge letu ni Bunge tukufu la Tanzania.

Kipi walichokifanya tangu wateuliwe katika uchaguzi wa 2005 ambacho kinaonyesha utukufu wa Bunge hilo? Ukiondoa wabunge wachache wa CCM ambao hawafiki hata 10 na wabunge wote wa upinzani naweza kabisa kutamka kwamba Bunge hilo halina utukufu wowote.

Nasema kwamba Bunge letu halina utukufu wowote kwa sababu mbali mbali na nitazitaja hapa. Bunge hilo limeendelea kuwakumbatia mapapa mafisadi ndani ya Bunge hilo akiwemo Lowassa aliyehusika moja kwa moja na tuhuma za ufisadi wa Richmond/Dowans. Karamagi ambaye pamoja na bunge hili kufikia makubaliano kwamba mkataba wa kampuni yake ya TICTS na serikali uvunjwe tangu mwaka 2008 hadi hii leo hakuna ufuatiliaji wowote ndani ya Bunge ili kujua kwanini serikali hadi hii leo haijavunja mkataba huo pamoja na kushauriwa kufanya hivyo na Bunge. Na pia alihusika katika kuudanganya umma wa Tanzania kuhusu mkataba wa uchimbaji dhahabu wa Buzwagi.

Rostam Azizi ambaye ana tuhuma mbali mbali za ufisadi wa mabilioni kupitia Richmond/Dowans, Kagoda na pia inasemekama yumo pia kwenye Meremeta na Tangold. Chenge au kwa jina maarufu la "Mzee wa Vijisenti" ambaye pamoja na kugundulika kwamba alijipatia fedha haramu katika ununuzi haramu wa rada ambao ulipigiwa debe sana na mafisadi Mkapa na Mramba. Kama mtakumbuka kauli ya fisadi Mramba kwamba "Hata majani tutakula lakini Rada lazima inunuliwe" sina haja ya kuandika zaidi yaliyojiri katika ununuzi huo haramu wa rada. Fisadi Mkono ambaye alilipwa bilioni 8 na BoT ambazo hadi hii leo ameshindwa kuthibitisha alifanya kazi gani BoT kwa muda gani hadi kustahili kulipwa pesa nyingi kiasi hicho. Pamoja na Gavana kuunda tume ya kufuatilia uhalali wa Mkono kulipwa mapesa hayo yote, hadi hii leo Gavana Ndullu hajatwambia kuhusu hatma ya kazi aliyowapa kamati hiyo. Fisadi Mzindakaya ambaye alipatiwa mkopo wa mabilioni na BoT pamoja na kuwa bank hiyo haihusiki kutoa mikopo kwa watu binafsi kwani kazi hiyo hutakiwa kufanywa na mabenki ya biashara ambayo yako chungu nzima nchini.

Bunge hili pia hadi hii leo limeshindwa kufuatilia wizi uliofanywa na fisadi Mkapa na fisadi Yona wa kukupua Mgodi wa Kiwira ambao baada ya kufanyiwa tathmini na wataalamu ulionekana una tamani ya shilingi bilioni 7, lakini mafisadi hao waliamua kujiuzia mgodi huo kwa 10% tu ya thamani yake na ambayo ni sawa na shilingi milioni 700 kulipa 1% ya thamani ya mgodi huo ambayo ni sawa na shilingi 70 millioni.

Pia bunge hilo limeshindwa kufuatilia ukwapuaji wa nyumba ulioidhinishwa na fisadi Mkapa kwa kushirikiana na mafisadi wenziye katika awamu yake wa kuuza nyumba za serikali kwa bei ya kutupa. Ukwapuaji huo umesababisha serikali kuingia hasara ya shilingi bilioni 200.

Bunge hili pia hadi hii leo limeshindwa kufuatilia ahadi za Waziri Mkuu Pinda katika kutekeleza mapendekezo ya kamati ya Mwakyembe kuhusiana na ufisadi wa Richmond ambapo pia waliishauri serikali kuwaondoa Mkuu wa TAKUKURU Edward Hosea na Mwanasheria Mkuu Mwanyika

Bunge hili limeshindwa kufuatilia kelele za Watanzania kuhusiana na mikataba ya uchimbaji madini yetu ambayo haina maslahi yoyote kwa Watanzania ambayo mingi ilisainiwa katika awamu ya tatu. Mikataba ya uchimbaji wa dhahabu, Tanzanite na hata almasi zetu.

Pia kama mtakumbuka hivio karibuni tumeona juhudi kubwa za Sitta kuzuia mijadala mizito kuhusiana na mambo mbali mbali yenye maslahi makubwa kwa Watanzania kama ule mradi wa vitambulisho ambao inasemekana utagharimu shilingi 200 bilioni na kuchunguzwa kwa ufisadi mkubwa uliofanywa na makapuni ya Meremeta na Tangold labda na deep green ambapo at least shilingi 155 bilioni kama siyo zaidi zilikupuliwa na mafisadi.

Sasa kwa visingizio ambavyo havina kichwa wala miguu Sitta na Pinda wanadai kwamba Meremeta na Tangolod inalihusisha jeshi letu na hivyo hilo linagusa 'usalama wa Taifa' hivyo wizi huo mkubwa wa shilingi 155 bilioni haustahili kujadiliwa wala kuchunguzwa na yeyote yule nchini.

Kwa ushahidi niliotoa hapo juu mimi naamini kabisa Bunge letu ukiondoa wabunge wachache ambao hawafiki hata 10% ya Wabunge wote limepoteza mwelekeo na halistahili tena kuitwa "Bunge Tukufu la Tanzania" kwani utukufu huo umeshapotea miaka mingi sasa. Hili linastahili kuitwa Bunge la Mafisadi Tanzania maana siku zote liko mstari wa mbele kuficha madhambi ya mafisadi waliojaa tele katika serikali ya awamu ya tatu na hii iliyopo madarakani na pia wamejaa tele ndani ya Chama Cha .......

Hili Bunge letu sasa linastahili kuitwa Bunge Har........ la ....... mtajijua!

Mungu ibariki Tanzania

Tafakari!

SOURCE: BAK
 
Sitta analipeleka Bunge pabaya

TUMEKUWA tukifuatilia kwa makini mwenendo wa vikao vya Bunge la Bajeti vinavyoendelea mjini Dodoma, na kuingiwa na shaka na namna Spika wa Bunge, Samuel Sitta na wasaidizi wake, wanavyoliongoza Bunge hilo katika kutimiza wajibu kwa umma.

Tukizingatia kanuni zinazoliongoza Bunge, ni dhahiri kuwa Sitta amekuwa akipindisha baadhi ya kanuni, na wakati mwingine kuzitumia kwa usahihi kwa baadhi tu ya wabunge, lakini mara nyingi yeye ama wasaidizi wake huzipotosha au huzifumbia macho, hususan pale wanapoamua utata wa kauli zinazotolewa na wabunge wa vyama vya upinzani.

Mathalan, Mbunge wa Nzega, Lucas Selelii (CCM), alisema mawaziri wote walaaniwe, Mudhir Mudhihir (Mchinga - CCM) alimwita waziri mmoja ‘nyoka wa mdimu’, Richard Ndasa akawaita wabunge wanaomsema Mkapa, ‘ngiri’. Kauli zote hizi zinaudhi na ni kinyume na kanuni za Bunge zinazokataza lugha ya kuudhi, hata watoto hupigana kutokana na kauli kama hizo, lakini Spika na wasaidizi wake hawakuwataka wabunge hao kufuta kauli zao hizo.

Jana, Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe (CHADEMA), aliposema Naibu Waziri wa Fedha alitoa majibu ya hovyo hovyo, Mwenyekiti wa Bunge (msaidizi wa Sitta), alimlazimisha afute kauli yake hiyo, licha ya Zitto kumkumbusha maamuzi ya awali ya Spika kuhusu kauli kama hizo. Uonevu huu unadhalilisha sana Bunge letu.

Tukiwa chombo huru cha habari kinachojali heshima na uhuru wa Bunge kama chombo cha kuwakilisha maslahi ya umma, tunatahadharisha kwamba maamuzi mabovu ya Spika ya kuwapendelea wabunge wa CCM – chama ambacho yeye anatoka, hata wanapotukana au kutoa lugha za kuudhi, sasa yamefungua ukurasa mpya kwa kila mbunge kuwa na haki ya kutukana au kutoa lugha ya kuudhi, kwani wabunge wenzao walisharuhusiwa kufanya hivyo, kwa hoja ya kuelezea hisia zao.

Tukizingatia hoja hiyo hiyo potofu ambayo Sitta aliitumia kuwatetea akina Selelii, basi hata Zitto nae anaweza kujitetea kuwa alielezea hisia zake aliposema majibu ya waziri yalikuwa ya hovyo hovyo.

Tunasikitishwa pia na hoja ya Sitta aliposema kuwa hotuba ya Dk. Willbrod Slaa (CHADEMA) kuhusu bajeti ya ofisi ya Waziri Mkuu, ilikuwa na nia ya kutaka kumjadili Rais mstaafu Benjamin Mkapa, kwa tafsiri kuwa kinga ya rais si ‘absolute’, kwamba asingemruhusu kukisoma kipengele hicho kwani hayo ni mawazo yake tu wala hayajatoka mahakamani.

Tunahuzunishwa na hoja hiyo kwa sababu alichokuwa akifanya Dk. Slaa, kwa mujibu wa kanuni za Bunge, ni kuwasilisha maoni ya kambi ya upinzani, juu ya hotuba ya Waziri Mkuu, ambapo pamoja na mambo mengine, kambi hiyo inaona kuwa rais huyo mstaafu hana kinga ya kila kitu, kwamba anaweza kushitakiwa kwa baadhi ya makosa aliyoyafanya akiwa Ikulu.

Kwa mantiki hiyo, hatua ya Sitta kumkataza Dk. Slaa asisome kipengele hicho, ilikiuka kwa kiasi kikubwa kanuni za Bunge zinazotoa haki na uhuru kwa kambi ya upinzani kuwasilisha maoni yake (hata kama hayamvutii Spika).

Ieleweke kuwa hakuna kanuni yoyote ya Bunge inayotaka maoni ya upinzani yathibitishwe au yatokane na hukumu za mahakama kama Sitta anavyotaka umma uamini.

Aidha, alimkataza Dk. Slaa asizungumzie mwenendo wa rais kwani kufanya hivyo ni kukiuka kanuni ya 64 ya Bunge, lakini Spika huyo huyo mara kadhaa amekuwa akiruhusu wabunge wa CCM kuzungumzia mwenendo wa Rais Jakaya Kikwete, ambapo wamekuwa wakimsifia hususan kwa safari zake za nje ya nchi. Tungependa ieleweke kuwa, kumzungumzia rais kunaweza kuwa ni kwa kusifia mwenendo wa maamuzi na utendaji wake au kukosoa, kwa hiyo kama Sitta aliona ni haramu kwa wapinzani kuzungumzia mwenendo wa rais (kwa kukosoa), basi alipaswa pia kuzikataa kauli za wabunge wa CCM zilizomzungumzia rais kwa kumsifia, kwani kufanya hivyo nako ni kuzungumzia mwenendo wa rais, kinyume na kanuni hiyo aliyoitumia Sitta kumkandamiza Dk. Slaa. Kwa uonevu wote huu, tunasema kwa uchungu kwamba, Spika analipeleka Bunge letu pabaya, tunamtaka ajirekebishe sasa vinginevyo ajiuzulu cheo hicho haraka iwezekanavyo ili kunusuru heshima ya Bunge letu tukufu, ambalo ni kioo cha Watanzania wote.
 
Zito said it all, ni bunge la ovyo ovyo! BAK hii kitu umeicopy wapi kabla huja paste hapa? maana hujaweka source na sitaki kuamini umeandika wewe! Maana tunakujua style zako! Asante
 
hakuna bunge tukufu pale kuna bunge tukutu.



Arsene Wenger!

Nakushukuru wewe pamoja na Babu kwa kuanzisha hii Thread;lakini wale sio watukutu bali ni kwamba Wabunge wote wa CCM ni wezi na majambazi wanapaswa wkatwe mkono mmoja na mguu mmoja ili wapite mitaani wakiomba na mali zao wapewe masikini!! Ole wao wakifika Mogadishu!!!

Kwa mfano Bernad Membe hakuwepo Bungeni kumsikiliza Mudhihir lakini utakuta kachukua sitting allowance ya muda mzima wa Bunge la BAJETI Pamoja na Jambazi Kagasheki lakini spika huyo kawapa ruhusa wakatembee kwenye Kampeni za KUIGOMBEA jimbo la BIHARAMULO ambalo limekuwa chini ya ccm kwa miaka 45 kama sio ujambazi ni nini!!

98% ya wabunge wanaganga njaa au wanakinga maslahi yao wakiongozwa na Vijisenti! Karamagi na Rostam Azizi bila kumsahau John who is above 70years anafikiri ni ufalme kamchomeka mkewe ili mapato yawe mengi this is crazy!!

Hivi hakuna mwenye akili timamu akatembeza bakora hawa wapuuzi waktia akili kama wa kule kwa malkia yaani Paundi 2000 tu Mbunge out hapa !!!! MANENO yameniishia kwa hasira!!! Matonya anapanga kutumia Billioni moja na ushehe kutembea nyie watu wa rangi ya kijani mna akili au mbongo zimejaa mboji ahhhhhhhhhhh!!
 
Hili letu sio bunge ni kijiwe cha kishkaji cha kuwadanganya wadanganyika na ulimwengu, Sitta na wenzake wehu tuu, wanashikilia matawi ilhali shina la hoja wanaliweka pembeni kabisa, hatutafika namna hii, inabidi watz tuchague upinzani zaidi mwakani zaidi ya 50% then president awe J. K hapo patakuwa patamu kiasi, othewise haikatizi hoja. Naunga hoja bora bakora zitembezwe huko, kwanza ni watoro sana na wanajizungusha zungusha na chairs tu, loo! bunge la nchi maskini lipo confortable kuliko la uingereza? wao wanakalia mabenchi hapa hadi wanasinzia kulivo na uvono!!
 
Mimi nasema bunge linakosa muelekeo....hawa kina RA, Chenge,karamagi,Lowasa,Mramba.....hatuwezi kulilaumu bunge, tutaishtaki CCM...kwaninni waendelee kuwa na watu wachafu kwenye chama, tena ni viongozi wa juu kwenye kamati kuu ya chama, Unatarajia nini?? JK amseme Lowasa,RA, Chenge...kisa yeye ndo mwenyekiti? haitatokea, ila tusibiri tu uchaguzi wao wa chama...wale wachafu watakapochukua hatamu...

mimi namsupport dr. Slaa alipopendekeza kwamba spika akishachagulia basi ajiondoe kwenye kamati zote za Uongozi za chama chake, maana huwezi ukategemea upeleke hoja kinzani yeye aipokee bila kuangalia maslahi ya chama chake na Ugali wake...japo kuna wakati mi naona Spika anafanya kazi nzuri lakini kuna wakati anafungwa breki na chama...na pia nazani amepigwa mkwara safari hii...sio yeye..
 
Zito said it all, ni bunge la ovyo ovyo! BAK hii kitu umeicopy wapi kabla huja paste hapa? maana hujaweka source na sitaki kuamini umeandika wewe! Maana tunakujua style zako! Asante

Ha ha ha ha huwa naandika sana nafasi inaporuhusu. Pitia jumbe zangu nyingi nimeandika katika maada mbali mbali kwa kirefu na katika majukwaa mbali mbali. Hiyo article source ni BAK huwezi kuipata mahali popote pengine duniani ila JF, labda jamaa waichukue na kuipeleka katika mitandao mingine.

Have a great day :)
 
Tunakoelekea yatatukuta yaliyowakuta wenzetu katika nchi nyingine za ulimwengu wa tatu, Civil war.
 
Kitendo cha kumuadhibu Zitto Kabwe kwa kusema ukweli kwamba Mawaziri wanajibu hovyo hovyo tena kwa kiburi na kejeli kinathibitisha tena kauli yangu kwamba Bunge hili si Bunge Tukufu. Bunge hili halijawahi kuwaadhibu mafisadi mbali mbali ndani ya bunge hilo walioshiriki katika ufisadi wa mabilioni ya shilingi wakiwemo, Lowassa, Mramba, Chenge, Rostam, Mkono, Mzindakaya na wengine waliohusika na kusaini mikataba ambayo haina maslahi kwa nchi yetu, lakini kwa mara nyingine tena limepata sababu ya kumuadhibu Zitto Kabwe kwa kuwa mkweli. Kweli Bunge la Tanzania si bunge Tukufu.
 
Bunge halina utukufu wowote, ufisadi mtupu. Na asilimia kubwa ya hao fisadi ni wabunge wenyewe ambao wanajenga bunge.
 
  • Thanks
Reactions: BAK
Bubu Ataka Kusema, you have rendered to genuine patriots of Tz, great service by listing so succintly the shortcomings of our current Parliament.

Since I know quite a number of MPs read JFs, it is my prayer that God will direct them to that page so that they can read it and understand how miserably they have performed so far. They can then correct themselves, and bring some amelioration in the tough life being endured by the majority of our people.
 
Jamani uzuri wa jengo sio utukufu tosha?

Probably Shaw was right :Democracy ensures that we are governed no better than we deserve.
 
Ha ha ha ha huwa naandika sana nafasi inaporuhusu. Pitia jumbe zangu nyingi nimeandika katika maada mbali mbali kwa kirefu na katika majukwaa mbali mbali. Hiyo article source ni BAK huwezi kuipata mahali popote pengine duniani ila JF, labda jamaa waichukue na kuipeleka katika mitandao mingine.

Have a great day :)

Asante kwa fafanuzi anuani....wengi hapa wanahisi huna uwezo wa kuandika zaidi ya kile kipaji chako cha kukopy na kupaste kwa style yako ya kipekee...haya kaka nimekusoma!
 
3 Reactions
Reply
Back
Top Bottom